• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Maskwota kunufaika na ekari 250 za ardhi

Maskwota kunufaika na ekari 250 za ardhi

Na LUCY MKANYIKA

MATUMAINI ya maskwota wa eneo la Singila-Majengo kupata maelfu ya ekari za ardhi ya shamba la makonge la Teita yalididimia juzi baada ya serikali kukubaliana na wamiliki kutoa ekari 250 pekee.

Naibu waziri wa Ardhi Bw Gideon Mung’aro, alisema maskwota hao watapata vyeti vya umiliki chini ya siku 30 na kwamba, maafisa wa usoroveya wanashughulikia suala hilo.

Bw Mung’aro alisema ripoti ya usoroveya inaonyesha kampuni hiyo haikunyakua ardhi ya wananchi.

“Tunataka kuhakikisha tunamaliza swala la uskwota nchini,” akasema.

Maskwota hao chini ya chama chao cha Mwasima Mbuwa wamekuwa wakipigania maelfu ya ardhi yanayomilikiwa na kampuni hiyo ya makonge.

Wakiongozwa na katibu wao Bw Mnjala Mwaluma, walikosoa mpango huo na kudai kutohusishwa kwa shughuli hiyo.

Bw Mwaluma aliitaka wizara ya Ardhi kuwaeleza maskwota hao kuhusu swala hilo kwani walitarajia kampuni hiyo kutoa ardhi kubwa zaidi.

“Tumekuwa tukipigania ardhi hii kwa muda mrefu sana. Inashangaza wakuu serikali wanapanga mipango bila kutuhusisha,” akasema.

Alisema kundi hilo litaelekea mahakamani kupinga zoezi hilo.

You can share this post!

Wafungwa wasusia chakula siku ya pili wakidai kuteswa

Ajinyonga kutotaka wazazi wagharimie matibabu

adminleo