Masaibu ya Sofapaka yaipa Gor ushindi, ubingwa wanukia
NA CECIL ODONGO
NYOTA ya jaha ilirejea na kumulika kambi ya Mabingwa mara 16 wa KPL Gor Mahia baada ya kuwalaza mabingwa wa mwaka wa 2009, Sofapaka mabao 3-0 katika mechi ya KPL iliyosakatwa Agosti 22 kwenye uga wa Narok.
Mabingwa hao walifunga mabao yao kupitia kiungo Joakim Onyango katika dakika ya 33 kisha beki wa kushoto Innocent Wafula akatia msumari moto kwenye kidonda cha Sofapaka kwa kuyafunga mabao mawili safi yaliyozamisha kabisa chombo cha wapinzani katika dakika ya 63 na 84 kipindi cha pili.
Bao la pili la K’Ogalo lilifungwa kupitia penalti baada ya kipa wa Sofapaka Wycliffe Kasaya kumchezea rafu mshambulizi wa Gor Lawrence Juma kwenye boksi.
Kosa hilo liliwaponza mabingwa hao wa zamani kwa kuwa Kasaya alipokezwa kadi nyekundu na ikawalazimu Sofapaka kumaliza mechi wakiwa watu tisa uwanjani.
Masaibu zaidi yaliandama Sofapaka dakika ya 15 baada ya kocha John Baraza kumwingiza kipa Mathias Kigonya na kumwondoa kiungo Justin Mico.
Mlinzi Mohamed Kilime aligongana na mlinzi wa Gor Mahia Samuel Onyango na kushindwa kuendelea na mechi dakika kumi za mwisho wa mtanange huo.
Vijana wa Kocha Dylan Kerr sasa wamefungua mwanya wa alama 20 na wanahitaji sare ya aina yoyote katika mechi zao zilizosalia ili kutwaa ubingwa wa KPL kwa mwaka wa pili mfululizo.
Ushindi huo unawapa matumaini mashabiki wa K’Ogalo ambao walikuwa wakiendelea kuomboleza kichapo cha Jumapili Agosti 19 mikononi mwa mibabe wa soka ya Rwanda, Rayon Sports kwenye mechi ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika, CAF.
K’Ogalo sasa watalazimika kurejelea mazoezi kabambe siku ya Alhamisi na Ijumaa kuyanoa makali yao dhidi ya mechi kubwa ya debi ya Mashemeji itakayowakutanisha na watani wao wa jadi AFC Leopards Jumamosi Agosti 25 katika uga wa MISC, Kasarani kuanzia saa tisa jioni.
Sofapaka walilazimika kumaliza mechi hiyo wakiwa wachezaji kumi
Kichapo hicho sasa kinazima kabisa azma ya Sofapaka ya kuwa wagombezi halisi wa ubingwa wa KPL msimu wa 2017/18. Batoto ba Mungu wanaonolewa na kocha John Baraza wanaendelea kushikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la ligi kwa alama 44 baada ya kujibwaga uwanjani mara 27.
Kocha Dylan Kerr alifanya mabadiliko kadhaa kwa kikosi kilichoicharaza Sofapaka ikiwemo kumpumzisha kipa Shaban Odhoji na kumtumia Fredrick Odhiambo katika nafasi yake.
Mnyakaji huyo alidhihirisha umahiri wake na kuwanusuru vijana wa K’Ogalo dhidi ya kufungwa goli la mapema alipookoa penalti iliyozawidiwa Sofapaka na kuchanjwa na mshambulizi matata Kepha Aswani.