#MashemejiDerby: Ingwe yalenga kuigwara Gor bila kucha za Odera
Na GEOFFREY ANENE
AFC Leopards itakosa mfumaji wake hodari Ezekiel Odera itakapokuwa ugenini dhidi ya mahasimu wa tangu jadi Gor Mahia kwenye Ligi Kuu uwanjani Kasarani hapo Agosti 25, 2018.
Mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 30 anatumikia marufuku ya mechi mbili, dhidi ya Gor Mahia (Agosti 25) na Wazito (Agosti 29), kutokana na kadi tano za njano na moja nyekundu.
Odera, ambaye alifungia Ingwe mabao mawili katika mechi mbili zilizopita ikipepeta Nakumatt 4-2 Agosti 12 na goli moja iliponyuka Thika United 2-0 Agosti 18, ameona lango mara 11 kwenye ligi hii ya klabu 18 msimu huu.
Yuko mabao manne nyuma ya Elvis Rupia na magoli mawili nyuma raia wa Rwanda, Jacques Tuyisenge.
Ingwe huenda ikakosa huduma za Moses Mburu, Salim Abdalla, Robinson Kamura, Jafari Owiti na Dennis Sikhayi. Wachezaji hawa wanauguza majeraha mbalimbali.
Kiungo mvamizi Whyvonne Isuza ni mmoja wa wachezaji ambao kocha kutoka Argentina, Rodolfo Zapata atategemea kutafuta matokeo mazuri dhidi ya Gor, ambayo itahifadhi taji ikishinda gozi hili maarufu kama ‘Mashemeji Derby’.
Maadui hawa wamekutana mara 83 ligini. Leopards imeshinda Gor mara 27, ikapoteza 25, huku mechi 31 zikitamatika sare. Ingwe itakuwa mawindoni kutafuta ushindi wake wa kwanza dhidi ya Gor katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili. Mara ya mwisho Ingwe ililemea Gor ni 1-0 Machi 6 mwaka 2016.
Timu hizi zilikutana ligini msimu huu mnamo Julai 22 Gor ikiibuka mshindi 2-1 kupitia mabao ya Tuyisenge na George ‘Blackberry’ Odhiambo. Isuza alifungia Ingwe bao la kufutia machozi.
Gor inaongoza kwa alama 68 kutokana na mechi 27 nayo Leopards inashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 48.
Ratiba:
Agosti 25, 2018
Nakumatt na Posta Rangers (11.00am, Camp Toyoyo), Chemelil Sugar na Ulinzi Stars (3.00pm, Chemelil), Kakamega Homeboyz na Wazito (3.00pm, Bukhungu), Sofapaka na Kaiobangi Sharks (3.00pm, Narok), SoNy Sugar na Tusker (3.00pm, Awendo), Gor Mahia na AFC Leopards (4.00pm, Kasarani);
Agosti 26, 2018
Bandari na Nzoia Sugar (3.00pm, Mombasa), Thika United na Vihiga United (3.00pm, Thika), Zoo na Mathare United (3.00pm, Kericho)