Kimataifa

UFISADI: Rais wa zamani wa Korea Kusini kuozea jela

August 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

PETER MBURU NA MASHIRIKA

Aliyekuwa Rais wa Korea Kusini kabla ya kung’olewa mamlakani Park Geun-hye Ijumaa alitupwa gerezani miaka 25 na mahakama ya rufaa nchi hiyo, kwa kupokea hongo kutoka kampuni ya Samsung alipokuwa uongozini.

Bi Park mwenye umri wa miaka 66 alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 24 na mahakama ya chini mbeleni kwa ufisadi, uongozi mbaya na makosa mengine ya jinai na akaamriwa kulipa pesa taslimu 18bilioni za nchi hiyo kama faini.

Lakini Ijumaa mahakama hiyo ya rufaa ikiketi eneo la Seoul ilimwongezea mwaka mmoja ndani na faini hadi 20bilioni won, ikisema hasara iliyosababishwa ilikuwa kubwa kuliko ilivyoamua mahakama ya chini.

Bi Park amekuwa akizuiliwa tangu mwaka uliopita na hakufika mahakamani wakati wa kusomewa hukumu Ijumaa.

Kitumbua cha uongozi wake kiliingia mchanga 2016 wakati maelfu ya waandamanaji walimiminika eneo la kati mwa Seoul wakitaka aondoke ofisini kwa miezi. Disemba mwaka huo, bunge la nchi hiyo lilimbandua kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi.

Machi 2017, Bi Park alikuwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kusini kuwahi kubanduliwa na bunge, wakati mahakama ya kikatiba ilishikilia uamuzi wa bunge hilo.

Wakati wa kumhukumu mnamo Aprili, mahakama ya chini ilisema Bi Park pamoja na mwandani wake wa miaka mingi Coi Soon-sil walipokea bilioni 23 won kama hongo kutoka kwa biashara tatu kubwa, ikihusisha karibu bilioni 7.3 kutoka kampuni ya Samsung.

Agosti mwaka uliopita, mkuu wa Samsung nchi hiyo Bw Lee Jae-yong alihukumiwa miaka mitano gerezani kwa kuwahonga Bi Park na Bi Choi lakini akatoka jela Februari baada ya mahakama ya rufaa kukata nusu ya kifungo chake kisha kukitupa ikisema kiwango cha hongo alichotoa kilikuwa kidogo.

Vilevile Ijumaa, rafikiye Bi Park Bi Choi alitupwa jela miaka 20.

Kifungo hicho cha miaka 25 sicho pekee ambacho Bi Park anakumbana nacho, kwani mwezi uliopita alihukumiwa jumla ya miaka minane kwa makosa mawili ya kuvunja sheria za uchaguzi na matumizi mabaya ya pesa za serikali.