SHANGAZI AKUJIBU: Nilienda ng’ambo kurudi nikapata amesonga

Na SHANGAZI SIZARINA

Vipi shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 21 na nimekuwa na uhusiano na mwanamume fulani kwa miaka saba. Miaka miwili iliyopita nilipata safari ya ghafla ya kwenda ng’ambo kwa miaka miwili. Mpenzi wangu alinihakikishia kuwa angekuwa mwaminifu kwangu kwa muda ambao sikuwepo. Nilishangaa sana niliporudi majuzi nikapata ashapendana na msichana mwingine na tayari wamezaa pamoja. Sasa anadai eti bado ananipenda. Nishauri.
Kupitia SMS

Ni ajabu kwamba bado unahitaji ushauri kuhusu mwanamume kama huyo ilhali umehakikisha kwamba hana msimamo na hawezi kuwa mwaminifu kwako. Ukisafiri alikuhakikishia kuwa atakuwa mwaminifu kwako. Muda si mrefu akamhadaa msichana wa wenyewe kuwa anampenda akampa mimba. Sasa anataka kumuacha arudi kwako. Utamruhusu aendelee na karata yake hiyo? Utaamua mwenyewe!

 

Alinitema bila sababu,sasa anitaka
Vipi shangazi? Nilikuwa na uhusiano na mwanamume fulani na nilimpenda kwa moyo wangu wote. Lakini siku moja mwaka uliopita alinipigia simu akaniambia tuachane tu bila sababu yoyote. Nilikubali uamuzi wake wala sikumuuliza hata swali moja. Sasa ameanza kunitafuta kwa simu nafikiri anataka turudiane na mimi sitaki hata kumuona. Nishauri.
Kupitia SMS

Ninaunga mkono kwa dhati msimamo wako kuhusu mwanaume huyo. Ni dharau na ujeuri mkubwa kwa mtu anayedai kumpenda mwenzake kuamka siku moja na kukatiza uhusiano bila sababu. Inaonekana amegundua hawezi kupata mwingine kama wewe na ndiyo maana ameanza kukutafuta. Muondoe kabisa katika mawazo yako kwa kubadilisha nambari yako ya ama kufunga simu zake.

 

Alinichukia alipopata mimba yangu
Kwako shangazi. Kuna msichana tuliyependana sana na nilikuwa nimepanga kumuoa. Lakini alipopata mimba yangu alinichukia hata akanifungia kumpigia simu. Nampenda sana na sijui nitafanya nini. Nishauri.
Kupitia SMS

Kitendo cha msichana huyo ni ishara kwamba hakuwa ameamua moyoni mwake kwamba utakuwa mumewe. Hiyo ndiyo sababu alitoweka maishani mwako licha ya wewe kumhakikishia kuwa utamuoa na pia kupata mimba yako. Haina maana uendelee kuhangaisha moyo wako kuhusu mtu ambaye hana shughuli nawe na ameamua kuishi bila wewe.

 

Aliniahidi kunipeleka kwao, miaka minne sasa imeisha
Shangazi nilipata mpenzi na kwa bahati nzuri au mbaya nikapata mimba yake. Aliahidi kunipeleka kwao akanitambulishe kwa wazazi wake kisha anioe lakini huu sasa ni mwaka wa nne na bado hajatimiza ahadi yake hiyo. Amekuwa akiniambia nisubiri tu hadi umefika wakati nahisi kuwa ananichezea akili. Lakini pia nampenda sana sidhani ninaweza kumuacha. Nishauri.
Kupitia SMS

Ni hali ya kusikitisha sana kwamba baadhi yetu sisi wanawake huzuzuliwa na mapenzi tukawa hatuoni, hatusikii wala hatufikirii. Ni ajabu sana kuwa mpenzi wako huyo amekuhadaa kwa miaka minne kuwa atakuoa na bado unaendelea kusubiri ilhali tayari una mtoto wake. Na kama kwamba hayo si kitu si chochote, unasema huwezi kumuacha! Mimi sitasema zaidi, endelea kuubiri.

 

Rafiki ameniambia mpenzi wangu anamtongoza
Shikamoo shangazi. Nimegundua kuwa mwanamume mpenzi wangu amekuwa akimuandama msichana rafiki akitaka wawe na uhusiano wa pembeni. Rafiki yangu ameamua kuniambia kwa sababu hawezi kunisaliti kwa njia hiyo tena amemchukia sana mwanamume huyo kwa tabia yake hiyo. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Bila shaka sasa umejua kuwa mpenzi wako huyo si mwaminifu kwako na mkiendelea na uhusiano huo hatimaye atakucheza tu. Ni bahati nzuri kwamba amemjaribu rafiki yako ndipo ukajua tabia yake hiyo. Ushauri wangu ni kwamba umkabili ukiwa pamoja na rafiki yako umzome kisha umteme.

 

‘Si lazima ukate miti ndipo uchome makaa’

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA enzi hizi ambapo kumekuwa na uharibifu wa mazingira kwa sababu ya ukataji miti, anatoa suluhu kwa kuunda makaa kutokana na uchafu wa makaa na taka.

Ni kazi ambayo Stella Sigan, 35, amekuwa akiifanya kwa miaka mitatu sasa kupitia mradi wake wa Alternative Waste Technologies-AWT ambapo bidii yake imesaidia kukuza mazingira kwa kutumia uchafu vilevile kupunguza ukataji miti kutengeneza makaa.

Makaa haya kwa jina briquettes hutengenezwa kwa vumbi ya makaa na taka ambapo tangu waanze mwaka wa 2015, wametumia zaidi ya tani 600 za uchafu huo.

Mbali na kusafisha mazingira, yakilinganishwa na kuni, makaa haya yanawaka kwa muda mrefu na kutoa moshi mchache. Pia ni ya bei nafuu huku wateja wake wakiwa nyumba binafsi, taasisi za kielimu, hoteli na mikahawa

Kwa kawaida yeye hununua vumbi ya makaa kutoka kwa wakazi wa Kibera ambapo wanatengeneza kati ya mifuko 200 na 300 ya makaa haya kila mwezi.

Kwa sasa anafanya kazi na kikundi cha watu sita wanaohusika na shughuli za kuunda makaa haya na wengine takriban 100 wanaokusanya taka na uchafu wa makaa unaotumika katika shughuli hii huku wengine sita wakiyasambaza kwa wateja.

Alihitimu na shahada ya uundaji mavazi na mapambo ya nyumbani kutoka Chuo Kikuu cha Egerton. “Nikiwa chuoni, penzi langu la ujarisiamali lilijitokeza huku nikianzisha biashara ya ushonaji nguo na mapambo ya nyumbani, lakini kwa bahati mbaya biashara hiyo haikudumu,” asema.

Ili kuimarisha ujuzi wake kibiashara, alisomea shahada ya uzamili katika masuala ya kiuchumi na biashara na pia kujiunga na mpango wa Young African Leadership Program, mpango wa kutoa mafunzo ya biashara, ujarisiamali na uongozi miongoni mwa vijana kutoka mataifa 14 ya Afrika ambapo alipiga msasa ustadi wake wa kibiashara.

Penzi hili lilimjia alipokuwa akifanya kazi katika shirika la Carolina for Kibera, kama afisa anayesimamia masuala ya kiuchumi na ujarisiamali.

Ni hapa ndipo alipata wazo la kuanza kuunda makaa haya. Mwanzoni jitihada zake kuuza bidhaa hii hazikufaulu na akaamua kufanya utafiti zaidi kutuma maombi ya kupata ufadhili.

Mwaka wa 2016, alikuwa mmojawapo ya wajarisiamali 1,000 walionufaika na ufadhili wa Wakfu wa Tomy Elumelu ambapo alipokea mafunzo, unasihi wa kibiashara bali na kupokea mtaji wa shilingi laki tano alizotumia kuanzishia biashara hii.

Lakini ari yake kamili ilimjia kutokana na nia yake ya kutaka kuimarisha maisha ya raia wa kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Eneo hili huwa na idadi kubwa ya vifo vya mama na watoto kutokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na moshi wakati wa mapishi. Na nilipata taswira kamili ya masaibu yao baada ya kuingiliana na wakazi wa vitongoji duni na hasa Kibera,” aeleza.

Kabla ya kuanzisha biashara hii alifanya majaribio kwa kuyanunua kutoka kwa wafanyabiashara ambao tayari walikuwa wanayaunda na kuwauzia wakazi Kibera.

Kwa sasa nia yao ni kupanua huduma zao hadi magharibi mwa Kenya ambapo wanapanga kuanzisha kiwanda cha kutengeneza makaa haya.

PAMBO: Msaidie mchumba wako kupiga deki upate asali bila kipimo

Na BENSON MATHEKA

Unapomsaidia kazi za nyumbani bila shaka unampunguzia uchovu hivyo kumuacha katika hali mzuri ya kukupatia burudani tosha
-Alfred Ombati, Shirika la Love Care, Nairobi

IKIWA wewe ni mwanamume mzembe unayependa kuketi kwenye kochi mkeo akifanya kazi za nyumbani, unajinyima uroda kutoka kwake.

Wataalamu wanasema kwamba wanaume wanaosaidiana kazi za nyumbani na wake zao hupata shibe la uroda na pia ni magwiji wa shughuli chumbani.

Utafiti huo ulifichua kwamba wanaume wanaochangia kazi za nyumbani hawakaushwi na wake zao wanapotaka uroda. Na sio kukaribishwa kushiriki tendo lenyewe pekee, hukolezwa uhondo wa ngoma mara kwa mara.

Kulingana na mtafiti Dkt Matt Johnson, wa chuo kikuu cha Alberta, Canada aliyeshiriki katika utafiti huo uliochukua miaka mitano, kiwango cha kazi za nyumbani ambacho mwanamume hufanya huchangia kiwango cha burudani anachopata kutoka kwa mkewe.

Utafiti huo ulishirikisha wanandoa 1,338 kutoka Ujerumani na ulilenga kubaini iwapo kiwango cha kazi za nyumbani wanachofanya wanaume kina uhusiano na maisha ya uroda ya wanandoa.

“Katika uhusiano wa kimapenzi kiwango cha kazi hutegemea majukumu ya wachumba wenyewe. Kuna wanaume wanaoweza kupangusa meza na kuchochea hisia za mapenzi za wachumba wao na kuna wanaopiga deki na kukosa kusisimua watu wao,” aeleza Bw Johnson.

Hata hivyo Alfred Ombati wa shirika la Love Care jijini Nairobi anasisitiza kwamba mchango wa wanaume katika majukumu ya nyumbani huongeza joto la mahaba.

“Unapomsaidia mke au mchumba wako kwa kazi za nyumbani bila shaka unampunguzia uchovu. Kwa hivyo, mnapoingia chumbani atakuwa katika hali mzuri ya kukupatia burudani,” aeleza Bw Ombati.

Mwenzake wa shirika la Big Hearts Hellen Wanjiku anasema wanaume hujinyima uroda kwa kuwaachia wanawake kazi zote za nyumbani.

 

Asiwe mtumwa

“Unapomchukua mchumba wako kama mtumwa kwa kumuachia kazi za nyumbani huku ukitulia kochini na kutazama runinga, haufai kutarajia burudani faraghani,” aeleza.

Utafiti wa Johnson ulibaini kwamba wanawake wakihisi kuwa wachumba wao hawawachukulii kama watumwa, huwa wanawafungulia milango ya tendo la ndoa mara kwa mara na kuwa na maisha ya uroda ya kuridhisha.

Alisema matokeo ya utafiti huo ni muhimu kwa wanandoa wanaotaka kudumisha joto katika maisha yao ya uroda.

Bi Wanjiku asema wanandoa wanaposaidiana na kushirikiana katika majukumu ya nyumbani, mili yao hutulia na kuwa katika nafasi nzuri ya kulishana uroda.

“Ni suala la kisaikolojia na rahisi sana ambalo watu huwa wanapuuza na kwa kufanya hivyo wanaangamiza maisha yao ya tendo la ndoa,” asema na kukiri kwamba kuna vizingiti vya kitamaduni ambavyo watu wanafaa kuepuka iwapo wanataka kuboresha maisha yao ya uroda.

Utafiti huo unasema kwamba baadhi ya watu huwa wanaepuka kazi za nyumbani wakidhani kufanya hivyo kutawasaidia kuwa na maisha bora ya tendo la ndoa.

 

Kukaushwa

“Wanaofanya hivyo hujipata wameharibu uhusiano wao na wachumba wao na kukaushwa wanapohitaji burudani. Na hata wakipatiwa burudani huwa sio katika hali ya kuridhisha, wanapimiwa kama dozi,” aeleza Bw Ombati.

Anashauri watu kujukumika kwa kila hali iwapo wanataka kufurahia maisha ya uroda na wachumba wao. “Usipojukumika, usitarajie mchumba wako akukoleze mapenzi.

Mbali na kutekeleza majukumu yako kama kiongozi wa familia, msaidie mke wako kulea watoto, kupika, kupiga deki, kufua nguo na kupeleka watoto shuleni. Ukifanya hivi, tarajia mabadiliko makubwa katika maisha yenu ya burudani faraghani,” asema.

Utafiti mwingine wa Sharon Sassler mwanasaikolojia wa chuo kikuu cha Cornell, New York, unafichua kwamba kiwango cha uroda miongoni mwa wanandoa kote ulimwenguni kinaendelea kushuka, isipokuwa wale wanaogawana majukumu ya nyumbani kama kupika na kupiga deki.

“Siku hizi kujenga mapenzi ni mchango wa kila mtu. Ni wanaogawana majukumu ambao wanaendelea kufurahia tendo la ndoa kwa kiwango cha juu kinachowaridhisha,” aeleza.

 

FUNGUKA: Ninatumia Biblia kuwatafuna mabinti kanisani mwangu

Na PAULINE ONGAJI

“Mabinti hawa husikiza wahubiri sana kiasi cha kuwa hawawezi kutambua hata wanapotumiwa kuridhisha kiu cha mtu kimahaba. Wananiandalia maankuli ya kila aina ambapo baadaye wananipa mzinga wa asali chumbani na nikimaliza shughuli nitatoka bila kulipa hata senti. Kupitia rasilmali zao, nina furaha kutangaza kuwa nimeramba zaidi ya nusu ya mabinti kanisani mwangu”

KATIKA ulimwengu wa sasa ambapo kumekuwa na shaka kuhusu maadili ya baadhi ya viongozi wa kidini, Jeremy hajasazwa.

Kaka huyu mwenye umri wa miaka 36 ni mmojawapo wa mapasta wa vijana katika kanisa moja mitaani. Kimaumbile, Jeremy ameumbwa kiasi kwamba utadhani kuwa alichangia mawazo Maulana alipokuwa akimuumba.

Kaka huyu ana umbo la kupendeza huku mazoea yake ya kufanya mazoezi kila mara yakihakikisha kuwa misuli yake inajichora kwa kila vazi analovaa.

Rangi yake ya lami imemfanya kuwa kivutio cha mabinti wengi huku vibonyo vinavyojitokeza kidevuni mwake kila anapotabasamu zikiwaacha mabinti wachanga na akina mama waliokomaa kuduwaa.

Isitoshe, kataalumika ajabu. Jeremy amesomea udaktari lakini ameamua kuacha taaluma yake hiyo ya hali ya juu na kujitosa katika uhubiri. Kinyume na baadhi ya wanaojitosa katika huduma hii kama mwito, sababu zilizomsukuma Jeremy kwa uhubiri ni za kustaajabisha.

“Hii ni mojawapo ya sehemu ambapo una uwezekano mkubwa wa kurambaramba mabinti pasipo gharama. Kuanzia kwa wanakwaya, hadi kwa chama cha vijana na hata wake za watu umehakikishiwa uhondo.

Mabinti hawa husikiza wahubiri sana kiasi cha kuwa hawawezi kutambua hata wanapotumiwa kuridhisha kiu cha mtu kimahaba.

Nalenga hawa mabinti wasio na uhakika kuhusu maisha yao tena wasiojithamini. Hawa ni rahisi sana kuwanasa kwani ninachohitaji ni kuwaonyesha tabasamu na nia ya kuwapenda na sitakumbana na pingamizi yoyote.

Maumbile na sura yangu ya kupendeza pia ni kivutio kwa hao wanaojidai kuwa wa haiba ya juu. Naam wajua wale warembo kupindukia na maumbo ya kupendeza, vile vile taaluma za hali ya juu ambao nia yao huwa kujionyesha kanisani?

Lakini ukwasi wangu katika mahubiri pia kaniongezea alama kibao. Ni halua kwa wanaojifanya watakatifu sana. Ninachohitaji kufanya ni kuwapa deti kwa kisingizio kuwa tutajadili masuala ya dini na kabla hajatanabahi azma yangu, huwa nishamuingiza boksi na kumtafuna.

Kadhalika kuna wake za watu wanaovutiwa na sifa hizo mbili za utanashati na ukwasi wa kuhubiri ambapo mara nyingi mimi ndiye ninayenufaika hata baada ya kutafuna.

Ninachohitaji kufanya ni kumpigia mhusika simu na kumwambia kuwa siku hiyo nitamtembelea kwake kwa maombi. Mara nyingi nafanya hivyo siku za kazi kumaanisha kuwa sio rahisi kunaswa na waume au wapenzi wao.

Isitoshe, ninaposema kuwa naja mimi hupokea pesa za petroli au nikichukua teksi, inalipwa pindi ninapofika ninakoenda.

Nikifika nakutana na maankuli ya kila aina ambapo baadaye nitaandaliwa asali chumbani na nikimaliza shughuli nitatoka bila kulipa hata senti. Badala yake ni mimi nitakayepokea pesa za kunirejesha kwangu.

Kupitia rasilmali hizo, nina furaha kutangaza kuwa nimeramba zaidi ya nusu ya mabinti kanisani mwangu, na bado sikomi huku lengo langu likiwa kuacha alama kwa kila binti anayeingia kwenye jengo hilo”.

TAHARIRI: Miguna hakustahili kudhalilishwa JKIA

Na MHARIRI

SERIKALI inapaswa kushughulikia utata kuhusu uraia wa mwanaharati wa upinzani Miguna Miguna kwa kufuata sheria bila kuwasha tena joto la kisiasa nchini.

Matukio yaliyoshuhudiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumatatu ni ya aibu, izingatiwa kuwa mahakama ilikuwa imetoa maagizo wazi kuhusu urejeo wa Miguna.

Haikufaa kwa serikali kumlazimisha Miguna kuingia ndege iliyoelekea Dubai, kwa sababu ya kukataa kupeana pasipoti yake.

Miguna si mgeni Kenya, jamaa na familia yake wanajulikana. Kwa hivyo ni bayana wakili huyo ni raia wa Kenya kwa kuzaliwa.

Hatusemi kuwa hakuna kasoro kuhusu stakabadhi za usafiri za Miguna, lakini dosari zilizopo zinaweza kurekebishwa bila sarakasi zinazoharibia Kenya sifa, hasa katika uwanja wa ndege wa kimataifa.

Ukweli mchungu ni kuwa, Wakenya walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili katika uchaguzi uliopita na ni vyema tusifufue tena upepo huo. Nchi ilikuwa imeanza kutulia kisiasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga kusalimiana, lakini suala la Miguna linaturudisha hatua nyingi nyuma.

Miguna ni raia wakawaida na inashangaza jinsi serikali inamkabili kwa kutumia mamia ya GSU pamoja na jeshi ili kutatua suala dogo la uraia wake.

Bw Odinga alikuwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kujaribu kumuokoa Miguna, na ilishangaza wengi kuwa wakili huyo alifurushwa hadi kwenye ndege bila yeye (Odinga) kusaidia chochote.

Muafaka aliyotia saini unampa nafasi ya kumpigia simu Rais Kenyatta na kutatua suala la Miguna bila sarakasi nyingi za kisiasa.

Muafaka wa viongozi hao wawili hautakuwa na maana iwapo raia wataendelea kushuhudia raia wa kawada wakihangaishwa na serikali ambayo inafaa kuwalinda. Kuungana kwao kwafaa kuunganisha Wakenya wote na wala si jamii au familia mbili.

Mahakama iliagiza Miguna aachiliwe na tunatarajia serikali itii maagizo ya korti ili suala la Miguna lisuluhishwe bila kuzua wasiwasi usiofaa.

Ikiwa kweli serikali inataka nchi hii kuendelea mbele, na serikali ifanikiwe katika nguzo zake nne za maendeleo ilizojiwekea, basi lazima kuwe na mandhari tulivu ya kisiasa.

Kimya cha Raila kuhusu Miguna chashangaza wengi

Na BENSON MATHEKA

KINARA wa NASA, Raila Odinga ameshangaza wengi kwa kimya chake kuhusu masaibu ya wakili Miguna Miguna, ambaye alimuapisha kama “rais wa wananchi” Januari 30.

Kimya cha Bw Odinga kimefanya Wakenya na hasa wafuasi wake kutia kwenye mizani mwafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta hasa kwa kushindwa kumsaidia Bw Miguna kuingia nchini kutoka Canada.

Japo Odinga alifika katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), ambako Bw Miguna alizuiliwa tangu Jumatatu alasiri, hakusema chochote kuhusu hatua ya serikali kumhangaisha.

Bw Miguna alirejea Kenya mnamo Jumatatu, wiki nne baada ya kutimuliwa kwa kumuapisha Bw Odinga kuwa rais wa wananchi, na ilitarajiwa kuwa mwafaka wa wake na Rais Kenyatta ungemsaidia kurejea Kenya na kurudishiwa paspoti yake bila mushkil.

Juhudi za mawakili kushawishi maafisa wa uhamiaji kumruhusu kuingia Kenya hazikufua dafu japo walikuwa na agizo la mahakama.

Bw Odinga alifika katika uwanja huo mwendo wa saa tatu usiku mnamo Jumatatu. Muda mfupi baadaye Bw Miguna alikamatwa machoni pake na maafisa zaidi ya 40 wa polisi waliokuwa na maagizo ya kumwingiza katika ndege ya Emirates iliyokuwa tayari kuelekea Dubai. Bw Odinga hakusema chochote.

“Miguna alinyanyuliwa na maafisa wapatao 40 wa polisi mbele ya Bw Odinga na mawakili wake, kisha akaingizwa katika chumba kilichokuwa chini ya ulinzi mkali kabla ya kulazimishwa kupanda ndege ya kuelekea Dubai. Bw Odinga alitazama tu!” alisema aliyeshuhudia matukio JKIA.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM aliondoka uwanja huo punde tu Bw Miguna alipokamatwa bila kuzungumza na wanahabari, tofauti kabisa na ilivyokuwa mfanyabiashara Jimi Wanjigi na mwanamikakati wa NASA David Ndii walipokamatwa.

Hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii, Bw Odinga hakuwa ametoa taarifa kuhusu masaibu ya Bw Miguna.

Kufuatia ushirika wake mpya na Rais Kenyatta, wengi walitarajia kuwa angechukua hatua za kumuomba Rais Kenyatta aagize maafisa wa uhamiaji na usalama wa kumruhusu Bw Miguna kuingia nchini na kurejeshewa paspoti yake ili kuepuka kizaazaa kilichoshuhudiwa katika uwanja wa JKIA.

Wadadisi wanasema kwa kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta Bw Odinga alijifunga hivi kwamba hawezi kukosoa vitendo dhidi ya washirika wake wa kisiasa.

 

 

Miguna ni tisho kwa utawala wa Uhuru – Wadadisi

CHARLES WASONGA na WANDERI KAMAU

HISIA mseto zimetolewa kuhusiana na uzito ambao serikali imechukulia zogo kuhusu uraia wa Miguna Miguna huku baadhi ya wachanganuzi wakisema huenda serikali inahisi wakili huyo ni tishio kubwa kwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hata baada ya Rais Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga kuafikiana kutuliza joto la kisiasa, serikali inamkabili Miguna kwa mkono mzito hali ambayo huenda ikazua taharuki ya kisiasa nchini.

Wakili Bobby Mkangi anasema masaibu yanayomkumba Miguna ni ya kisiasa na huenda yakaathiri muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Baada ya Raila na rais kusalimiana, tulitarajia Miguna angerudi bila sarakasi lakini inaoenekana kuna mengi serikali inahofia kuhusu Miguna, kando na kisingizio cha sheria za uraia,” Bw Mkangi aliambia Taifa Leo kwa simu.

Kwa mujibu wa Bw Mkangi, masaibu ya Dkt Miguna yalianza baada ya kusimamia kiapo cha Bw Odinga mnamo Januari 31, na athari za kiapo hicho ndizo zinaendelea kumkumba.

“Bila shaka kuna baadhi ya viongozi serikalini na pia upinzani ambao mustakabali wao wa kisiasa unatishiwa sana na Miguna kuwa nchini,”aliongeza Bw Mkangi.

Mojawapo ya sababu zilizopelekea kuahirishwa kwa ziara ya Rais Kenyatta na Bw Odinga katika maeneo ya Nyanza ni marejeo tata ya Miguna.

Habari za kijasusi ziliashiria uwezekano wa viongozi hao wawili kutatizwa na baadhi ya wakazi wa Nyanza iwapo suala la kurejea kwa Miguna halitasuluhiswa bila kuzua joto la kisiasa.

Mchanganuzi wa siasa Dismas Mokua anasema huenda rais na Bw Odinga wakalazimika kuandamana na Miguna katika ziara ya Nyanza iwapo wanataka ziara hiyo ifanyike bila vurugu.

Wengine wanasema Bw Miguna wanaogopwa pia kutokana na uwezekano wake kutatiza ushirikiano wa Bw Odinga na Rais Kenyatta.

 

TAHARIRI: Siasa za 2022 haziwasaidii raia

Na MHARIRI

KILA baada ya uchaguzi mkuu kukamilika na hali ya kawaida kurejelewa, viongozi wa kisiasa huanza kujadili kuhusu uchaguzi unaofuata katika muda wa miaka mitano inayokuja. Mambo sio tofauti wakati huu kufuatia kukamilika kwa uchaguzi wa mwaka 2017.

Tumeanza kusikia mijadala ya viongozi wa kisiasa kuhusu ni nani anayefaa kuchaguliwa 2022, mikakati ya kuleta makabila tofauti katika makundi yapi na ni nani ambaye hafai na mengineo.

Ni makosa makubwa kwa viongozi kuweka nchi katika hali ya uchaguzi kila mara. Hii ni kwa sababu badala ya kutekeleza ahadi ambazo walitoa nao upinzani kuhakikisha walio madarakani wanafanya kazi yao ipasavyo, fikra za Wakenya zinawekwa mawazo ya uchaguzi usio na kikomo.

Ingawa ni haki ya wanasiasa kujipanga kwani azma yao kuu ni kuwa madarakani, ni jambo la busara zaidi kuafikia haya kwa kujishughulisha zaidi na utendaji kazi unaolenga kuinua maisha ya Wakenya na kuhakikisha demokrasia na utawala bora zinazingatiwa.

Lakini tabia ya kujadili siasa za ni nani atakayechaguliwa rais 2022 asubuhi hadi jioni kana kwamba zitaboresha maisha ya Wakenya ni ya kupotosha na iliyopitwa na wakati. Hii ni tabia ya kuelekeza nchi gizani badala ya mwangani.

Siasa ambazo Wakenya wanahitaji kwa sasa ni jinsi ugawaji wa raslimali za kitaifa unavyoweza kufanywa kwa uwazi ili kusaidia kila pembe ya nchi, kumaliza ufisadi, kuboresha elimu, kuzalisha chakula zaidi, uchumi, na mambo mengine yanayohusu ustawi wa nchi.

Siasa za wakati huu pia zinafaa kushirikisha masuala ya sheria zinazostahili kufanyiwa marekebisho ili kumfaa mwananchi.

Wanasiasa wanapasa kufahamu kuwa walichaguliwa kufanyia wananchi kazi wala sio kuwasumbua kwa mijadala isiyo na maana kwao kwani wakati wake haujafika.

Mikakati yao ya 2022 inaweza kuwa na manufaa zaidi iwapo itajengwa kwenye misingi ya yale ambayo watakuwa wamefanyia wananchi kufikia wakati huo.

Kelele za kila mara kuwa huyu analenga kumaliza yule asishinde kwenye uchaguzi wa 2022 ni siasa za kupoteza wakati ambao wengi wanahitaji kuweza kutafutia familia zao riziki na kujiimarisha maishani.

Wanasiasa wanapasa kukomesha mijadala ya 2022 na badala yake waheshimu wapigaji kura kwa kutekeleza waliyoahidi.

Biashara haramu ya makaa inayowafaidi Al-Shabaab msituni Boni yazimwa

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa usalama katika kaunti ya Lamu wamefichua kuwa biashara haramu ya makaa na upasuaji mbao unaoendelezwa kwenye msitu wa Boni inatumika kufadhili magaidi wa Al-Shabaab.

Akizungumza wakati alipozindua operesheni kali ya kuwasaka wachomaji makaa na wapasuaji wa mbao kwenye msitu wa Boni Jumanne, Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Bw Muchangi Kioi, alisema wanabiashara wa makaa na mbao wanaoendeleza shughuli zao ndani ya msitu wa Boni wamekuwa wakiwafadhili Al-Shabaab kwa chakula na maji kupitia mapato ya biashara yao.

Hapa ndipo makaa yamekuwa yakichomewa ndani ya msitu wa Boni. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Kioi alisema sehemu nyingi ambazo biashara ya makaa na mbao imekuwa ikiendelezwa ndani ya msitu wa Boni  na vijiji vinayokaribiana na msitu huo, ikiwemo Maleli, Pandanguo na Poromoko zimekuwa zikishuhudia uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa Al-Shabaab.

Wakati wa operesheni hiyo, jumla ya magunia 240 ya makaa na tani kadhaa za mbao zilinaswa kwenye maeneo ya Ziwa la Kengo, Ziwa la Taa na Maisha Masha ambayo yote yanayopatikana ndani ya msitu wa Boni.

Polisi wasimamia wakataji miti kupakia makaa ambayo wamekuwa wakichoma kwa gari lao. Picha/ Kalume Kazungu

Wachomaji makaa na wapasuaji mbao wanne pia walinaswa kwenye msako huo ilhali wengine wakifaulu kukwepa mtego wa polisi.

Bw Kioi alisema maafisa wa polisi wako macho na kwamba watashirikiana na vitengo vyote vya usalama vinavyoendeleza operesheni ya Linda Boni ili kumaliza biashara ya makaa na ukataji miti kwenye misitu yote inayopatikana Lamu.

Afisa ashtukia jinsi miti imekuwa ikikatwa kiholela katika msitu wa Boni kwa ajili ya uchomaji wa makaa kuwafaidi magaidi wa Al-Shabaab. Picha/ Kalume Kazungu

“Leo tumeamua kuzindua operesheni ya kuwasaka wachomaji makaa na wapasuaji mbao ndani ya msitu wa Boni. Tayari tumenasa magunia 240 na shehena kadhaa za mbao. Tumegundua kuwa biashara ya makaa na mbao ndani ya msitu wa Boni ndiyo inayotumiwa kuwanunulia magaidi wa Al-Shabaab chakula na maji.

Operesheni itaendelea hadi pale biashara hiyo itakapomalizwa kabisa ndani ya msitu wa Boni. Watu lazima wafahamu kwamba uchomaji makaa na ukataji mbao ni kinyume cha sheria. Marufuku ipo na lazima iheshimiwe,” akasema Bw Kioi.

Wakataji miti hawa walazimishwa kupakia magunia ya makaa ambayo wamekuwa wakichoma kwa gari la polisi. Picha/ Kalume Kazungu

Afisa huyo aidha alitoa onyo kali kwa maafisa wa usalama dhidi ya kushirikiana na wachomaji makaa na mbao katika kuendeleza biasahara hiyo kisiri.

Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Shirika la Uhifadhi wa Misitu (KFS) eneo la Witu, Bw John Mbori, aliwataka wakazi, viongozi na maafisa wa usalama kushirikiana vilivyo ili kufaulisha vita dhidi ya wachomaji makaa na wakataji mbao.

Wakataji miti hawa walazimishwa kupakia jumla ya magunia 240 ya makaa ambayo wamekuwa wakichoma kwa gari la polisi. Picha/ Kalume Kazungu

“Tukiwa na ushirikiano wa dhati, ninaamini marufuku iliyopo ya ukataji mbao na uchomaji makaa itafaulu,” akasema Bw Mbori.

Operesheni hiyo imezinduliwa mwezi mmoja baada ya serikali kupitia kwa Naibu wa Rais, William Ruto, kupiga marufuku ukataji miti na uchomaji makaa kote nchini kwa siku 90 ili kuzuia athari za ukosefu wa mvua na kuhifadhi chemichemi za maji ambazo zimekuwa zikihatarishwa na kuendelezwa kwa shughuli hizo hapa nchini.

Wakazi, viongozi na maafisa wa usalama wametakiwa kushirikiana vilivyo ili kufaulisha vita dhidi ya wachomaji makaa na wakataji mbao. Picha/ Kalume Kazungu

TAHARIRI: Tuongeze juhudi kuangamiza TB

Na MHARIRI

ULIMWENGU ulipoadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani Jumamosi, jambo moja lililojitokeza wazi ni kwamba Wakenya 29,000 walikufa mwaka jana kutokana na ugonjwa huo.

Hata takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonyesha kuwa TB ni ugonjwa wa pili kwa kuua watu duniani, ambapo 4,500 huaga dunia kila siku.
Ugonjwa huu umekuwa hatari zaidi, kutokana na kuzuka kwa Kifua Kikuu ambacho hakisikii dawa.

Tatizo kubwa linalowakumba Wakenya wengi ni kuwa, hata mtu anapoanza kukohoa mfululizo, huogopa kwenda kumwona daktari kutokana na itikadi isiyokuwa ya ukweli kuwa mtu akiugua TB bila shaka atakuwa ana virusi vya Ukimwi.

Ni kweli kwamba mtu anapokuwa na virusi vya HIV, huwa na kinga dhaifu na maradhi mengi humpata kikiwemo Kifua Kikuu. Lakini si lazima anayeugua Kifua Kikuu awe na Ukimwi.

Hapa Kenya, mojawapo ya mambo yanayochangia kwa kiwango kikubwa maambukizi ya TB ni watu kuwa kwenye mazingira yenye hewa isiyotosha. Ndani ya maduka ya jumla katika miji mingi, orofa za chini au juu hushuhudia msongamano wa wateja, lakini madirisha huwa machacho au wakati mwingine hayapo.

Ndani ya magari ya usafiri wa umma, abiria huamua kufunga vioo kwa kuhofia wachomozi ambao hunyakua simu au bidhaa nyingine za thamani kupitia madirishani.

Japokuwa wananchi wana jukumu katika suala hili, ipo haja kwa viongozi wa ngazi mbalimbali kuunga mkono juhudi za maafisa wa afya kuhamasisha raia kuhusu hatari ya kutokuwa na mzunguko wa kutosha wa hewa safi.

Kwa hivyo, kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni ‘Viongozi Wahitajiwa: Ili kuwa na Ulimwengu bila TB’ yafaa kuzingatiwa na viongozi wote, bila kujali tabaka au uwakilishi wao katika jamii.

Viongozi wan auchawishi mkubwa kwa wananchi. Tungependa kuona MCA, chifu, mzee wa kijiji, viongozi wa vijana na hata rais wa Jamhuri ya Kenya wakijitokeza na kuwaeleza wananchi madhara ya kutozingatia kanuni za kukabiliana na kusambaa kwa TB.

Kwa mfano wanapaswa kuhamasisha watu kwamba wakati mtu anakohoa katika eneo la umma, awe akiziba mdomo kwa kuwa vidudu vinavyosababisha TB hurukakupitia hewa tunayovuta.

Ni kupitia juhudi za pamoja tu, ndipo tutaangamiza Kifua Kikuu.

 

 

Mwaka mmoja baada ya Wamakonde kutambuliwa, bado ni kilio

KAZUNGU SAMUEL na FADHILI FREDRICK

Kwa ufupi:

 • Wamakonde walifika katika kaunti ya Kwale miaka michache baada ya Kenya kujinyakulia Uhuru
 • Wamekuwa wakifanya kazi katika mashamba ya makonge na sukari lakini walijikuta wakiwa na changamoto nyingi, hasa ile ya kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa, ambavyo vingewasaidia kupewa vitambulisho
 • Sherehe ya kuitambua jamii hiyo kuwa sehemu ya makabila ya Kenya, ilifanywa 2017 na Rais Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni zake za kutaka kuchaguliwa tena
 • Wanalia kuwa kumiliki ardhi kwao ni tatizo kuu huku wakitengwa na majirani zao licha ya kukubaliwa kama kabila la 43 nchini

MWAKA mmoja si kipindi kirefu katika maisha ya kawaida, hawa iwapo katika muda huo, mtu anasubiri kutimiziwa ahadi fulani.

Kauli hii ni sahihi zaidi kwa watu wa kabila dogo kutoka taifa la Msumbiji, ambao juhudi zao za kutaka kutambuliwa zilizaa matunda mwaka jana, wakati wa kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2017.

Jamii ya Wamakonde, ambao walifika katika kaunti ya Kwale miaka michache baada ya Kenya kujinyakulia Uhuru, ilijikuta ikiendelea kuzaana na kujazana katika kijiji cha Makongeni, kando mwa barabara kuu ya Likoni-Lunga Lunga, katika kaunti ya Kwale.

Taifa Leo ilipowatembelea wakazi hao mwaka mmoja tangu watambuliwe kuwa kabila la 43 la Kenya, wakazi wa kabila hilo walikuwa wengi wa matumaini kwamba labda walikuwa wamefikishiwa habari njema.

Kijiji hicho ambacho hakikuonekana kuwa na shughuli nyingi, ndiyo makao ya jamii hiyo ya Wamakonde.

Wamekuwa wakifanya kazi katika mashamba ya makonge na sukari maeneo ya Msambweni na Ramisi mtawalia lakini walijikuta wakiwa na changamoto nyingi, hasa ile ya kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa, ambavyo vingewasaidia kupewa vitambulisho.

Ingawa wamekuwa wakisoma katika shule za Kenya na kupata elimu na ujuzi, safari yao imekuwa ikifikia darasa la nane au kidato cha nne, kwa kuwa baada ya hapo wamekuwa hawapati ajira kwa vile hawakuwa na vitambulisho vya kitaifa.

Katikati ya kijiji hiki kuna kibao chenye ujumbe unaosema hivi ‘Kama kumbukumbu ya kukumbuka jamii ya Wamakonde ambao walikuja Kenya kama wafanyikazi katika mashamba ya makonge. Jamii hii ilipewa rasmi uraia wa Kenya mwaka wa 2016,’ kinasema kibao hicho.

Hata hivyo, sherehe ya kuitambua jamii hiyo kuwa sehemu ya makabila ya Kenya, ilifanywa mwaka jana Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni zake za kutaka kuchaguliwa kwa kipindi cha pili cha uongozi.

Kuna mti kando ya kibao hicho ambao ulipandwa siku ambapo jamii hiyo iliidhinishwa na serikali kuwa mojawapo ya jamii za Kenya.

Mwenyekiti wa jamii ya Wamakonde, Kwale, Mzee Thomas Nguli aelezea masaibu ya jamii hiyo alipohojiwa na Taifa Leo katika kijiji cha Makongeni. Picha/ Kazungu Samuel

Matumaini

Kwa hivyo, baada ya kutambuliwa, kulikuwa na matumaini makubwa kwamba sasa Wamakonde wangenufaika na miradi na mambo mengine ambayo jirani zao Wadigo na Wakamba wamekuwa wakinufaika nayo.

Hata hivyo msemaji wa jamii hiyo, Bw Thomas Nguli, anasema kuwa Wamakonde hawajaona yale matunda waliyokuwa wakitarajia kupata, ambayo yalifaa kuandamana na wao kufahamika rasmi Wakenya.

“Tunashukuru kwamba kwa sasa sisi ni Wakenya lakini bado tuko na changamoto nyingi ambazo zinatuathiri kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano sasa hivi sisi hatuna mashamba wala ardhi. Hatuna hati miliki za kijiji hiki ambacho sisi tumepaita nyumbani kwa miaka mingi,” akasema Mzee Nguli.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa jamii hiyo kwa sasa iko na zaidi ya watu 1,000 ambao wamepata vitambulisho vya kitaifa.

“Tunamshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kutuwezesha kupata uraia wa taifa hili, lakini hatuwezi kusema kwamba tumepata uhuru wetu wakati ambapo bado tunatatizika kumiliki ardhi. Hii ni shida kubwa,” akasema Mzee Nguli.

Wanawake wa jamii ya Wamakonde wakipiga soga nyumbani wakati Taifa Leo ilizuru kijiji cha Makongeni, kaunti ya Kwale. Picha/ Kazungu Samuel

Kutengwa

Alisema kuwa changamoto nyengine ambayo inawakabili ni kutengwa na majirani zao na hilo halijakuwa jambo jema kwao.

“Hapa wanatuita watoto wa Uhuru lakini tungeomba tu kama majirani zetu wanaweza kutambua kwamba sisi sasa ni Wakenya kama wao na wanafaa kututambua,” akasema Mzee Nguli.

Aliongeza kwamba jumla ya wakazi 1,875 kutoka kwa jamii hiyo tayari wamepata vitambulisho na hata wengine wakijisajili kama wapiga kura katika kaunti hiyo.

“Kutokana na mateso mengi tuliyopitia kama watu tusio na makao katika nchi hii ambayo tumeishi maisha yetu yote, tunadhani kwamba matakwa yetu sharti yaangaliwe kikamilifu na suluhisho la kudumu lipatikane,” akasema Bw Nguli.

Tutalala tu na amani ikiwa tutahakikishiwa kuajiriwa na serikali na kila aina ya jambo ambalo litatuwezesha kimaisha,” akaongeza.

Kitongoji cha Makongeni, Msambweni chenye watu wengi zaidi wa jamii ya Wamakonde waliohamia Kenya kutoka Mozambique. Picha/ Kazungu Samuel

Kupata kazi za serikali

Alisema kuwa kutambuliwa kwao hata hivyo kumewapatia faida kiasi kwani kuna watu sita miongoni wao ambao wamepata kazi baada ya kupewa uraia.

“Tuko na vijana wawili ambao wamejiunga na idara ya huduma za polisi na wane wameingia katika idara ya magereza. Zaidi ya vijana 200 sasa wameingia katika mradi wa huduma kwa taifa (NYS),” akasema Mzee Nguli.

Kulingana na Rose Boniface aliye na umri wa miaka 50, ilikuwa furaha kuu baada ya kupata kitambulsho tangu azaliwe. Hatua hiyo alisema ilimwezesha kushiriki katika uchaguzi wa wa mwaka 2017.

Alisema kabla ya kupata stakabadhi hiyo muhimu, maisha yalikuwa yamejaa usumbufu kwa vile hakuweza kupata huduma muhimu katika ofisi ya umma na vile vile alikuwa mara nyingi akisumbuliwa na polisi.

“Ilikuwa ni vigumu sana na tuliteseka sana miongoni mwetu ila sasa hali ni tofauti,” akasema.

Aliongeza kwamba mradi muhimu kama vile malipo kwa wazee walikuwa hawapati lakini sasa wamewekwa kaitka mpango huo.

Julieta Simenya, katibu wa kundi hilo alisema kuwa jamii bado inapitia changamoto kadhaa ambazo bila kuangaliwa vyema, zitatizika.

Katika eneo hili la Msambweni, Wamakonde huitwa watoto wa Uhuru na kutengwa na jamii zingine. Picha/ Kazungu Samuel

Kumiliki ardhi 

“Shida yetu kuu ilikuwa ni kupata uraia wa Kenya lakini pia tulikuwa na nyengine kama vile umiliki wa mashamba. Kwa sababu sasa tumepata vyeti vya kuzaliwa na kuwa raia kamili, serikali sasa haina budi kuangalia jinsi ambavyo itatusaidia tupate mashamba,” akasema Bi Simenya.

Jamii hiyo ina ukoo kutoka nchini Msumbuji na walikuja Kenya kupitia Tanzania Kusini ili kuja na kufanya kazi katika mashamba ya Makonge katika kaunti za Kwale na Kilifi.

Hata hivyo jamii hizo zilikumbana na hali ngumu baada ya kampuni za miwa na makonge kufilisika ambapo walijikuta wakiosa mahali pa kwenda.

Baada ya miaka mingi ya kutengwa, Bw Nguli alisema kuwa kwa kushirikiana na mashirika ya haki za kibinadamu, serikali iliwapatia uraia mwaka wa 2016.

“Tulianza safari hii mwaka wa 1995 na mimi sasa hata nikifa nitakuwa na furaha kwamba nilifanya kazi uyangu kubwa ya kufikisha watu wangu mahali walipotamani,” akasema Mzee Nguli.

 

Shule mbioni kupaka mabasi rangi ya manjano muda ukiyoyoma

KALUME KAZUNGU na WANDERI KAMAU

Kwa ufupi:

 • Dkt Fred Matiang’i alitoa agizo kwamba lazima mabasi ya shule zote za msingi na upili za umma yawe yamepakwa rangi ya manjano kufikia Machi 31
 • Kwa kuyapaka rangi hiyo ya manjano, inakuwa rahisi kwa mtu kugundua kuwa hayo ni magari ya shule
 • Katika maeneo mengiya nchi, mekanika wa kupaka rangi magari walionekana wakiwa katika hatua za mwisho, kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi
 • Kenya inaonekana kuiga nchi kama Amerika na Canada, ambako magari yote ya shule huwa yana rangi ya manjano

ZIKIWA zimesalia siku tano kabla ya kukamilika kwa makataa kwa shule zote nchini kupaka rangi magari ya kubeba wanafunzi, walimu wakuu na wamiliki wa shule wamo katika harakati za mwisho kutimiza agizo hilo.

Aliyekuwa Waziri wa Elimu, Dkt Fred Matiang’i alitoa agizo kwamba lazima mabasi ya shule zote za msingi na upili za umma yawe yamepakwa rangi ya manjano kufikia Machi 31.

Dkt Matiang’i alisema kwamba agizo hilo linalingana na Sheria ya Trafiki, ambayo ilipitishwa na Bunge mnamo 2016.

Hatua hiyo inaonekana kuchangiwa na ongezeko la ajali za barabarani, ambapo iligunduliwa kuwa baadhi ya magari yaliyokuwa yamekodishwa kusafirisha abiria, yalikuwa ya shule.

Kulingana na sheria hiyo, jina la shule husika linapaswa kuandikwa kwa rangi nyeusi.

 

Rahisi kutambulika

Kwa kuyapaka rangi hiyo ya manjano, inakuwa rahisi kwa mtu kugundua kuwa hayo ni magari ya shule, na kwa hivyo hatua za haraka zinaweza kuchukuliwa iwapo madereva wa magari hayo watapatikana wakiendeleza mambo yanayoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

Sheria hiyo pia inayahitaji mabasi hayo kuwa na mikanda ya usalama katika viti vyake vyote.

“Shule zote zinapaswa kuhakikisha kwamba zimetimiza kanuni hizo kufikia Machi 30, kama inavyohitajika kisheria. Hatutakubali visingizio vyovyote kuhusu suala hili,” akasema waziri.

Sheria hiyo pia inasema kuwa mabasi hayo yanapaswa kuendeshwa kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa.

Mwendo wa kasi umekuwa mojawapo ya mambo ambayo yamechangia ongezeko la ajali za barabarani. Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, kumekuwa na ajali kadha ambazo zimehusisha mabasi ya shule katika maeneo ya Nyanza na Kisii.

Kanuni nyingine ni kwamba yataruhusiwa kuhudumu kati ya saa 12 asubuhi na jioni pekee, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

Basi la Shule ya Msingi ya Twfiq Muslim mjini Malindi. Picha/ Hisani

Kuiga mataifa ya Magharibi

Kulingana na wadadisi wa masuala ya elimu, Kenya inaonekana kuiga nchi kama Amerika na Canada, ambako magari yote ya shule huwa yana rangi ya manjano.

Katika kaunti ya Lamu, shule zote za mzingi na za upili zinazomiliki mabasi zimetimiza amri hiyo.

Akizungumza Jumapili na Taifa Leo, Afisa wa Elimu wa Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi, Bw Josphat Ngumi, alisema ni shule mbili pekee za upili – ile ya wavulana ya Mpeketoni na shule ya sekondari ya Mokowe ambazo zinamiliki mabasi kati ya jumla ya shule 26 za umma zilizoko Lamu.

Alisema shule ya kibinafsi ya Tamani Junior Academy iliyoko Mpeketoni ndiyo shule ya msingi ya kipekee ambayo inamiliki basi kati ya shule 104 zilizoko eneo hilo.

Kwa mujibu wa Bw Ngumi, shule zote tatu kwa sasa zimehakikisha mabasi yao yamepakwa rangi ya manjano kama ilivyoamriwa.

“Hapa Lamu kuna shule mbili pekee za upili zinazomiliki mabasi ambazo ni Mpeketoni na Mokowe. Pia kuna shule moja pekee ya msingi ya kibinafsi ambayo ni Tamani Junior Academy iliyoko Mpeketoni ambayo ina miliki basi. Shule zote tatu zimetii sheria kwa kuhakikisha magari yao yanapakwa rangi ya manjano,” akasema Bw Ngumi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya wavulana ya Mpeketoni, Bw Macharia Kagutha alisema basi lao lilipakwa rangi takriban wiki tatu zilizopita.

 

Gharama ya kupaka rangi

“Tulisafirisha basi letu hadi Mombasa ambako lilipakwa rangi na kampuni ya Assosiated Motors. Tulitumia Sh127,000 katika kutekelezewa huduma hiyo. Kwa sasa liko sawa,” akasema Bw Kagutha.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mokowe, Bw Thaddeus Mogute, alisema shughuli ya kulipaka rangi gari hilo tayari ishaanza na itakamilika juma hili.

“Tunalenga kutumia kati ya Sh 130,000 na Sh 150,000 ili kupaka rangi ya manjano basi letu na pia kulikarabati. Tayari niko Mombasa na shughuli itakuwa imekamilika kufikia mwishoni mwa wiki hii,” akasema Bw Mogute.

Katika maeneo mengine ya nchi, mekanika wa kupaka rangi magari walionekana wakiwa katika hatua za mwisho, kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi ya kupaka rangi hiyo ya manjano kwenye magari yaliyopelekwa katika gereji zao.

Kulingana na kanuni zilizotolewa na serikali, hata matatu na magari ya kibinafsi yatakayotumiwa kuwabeba wanafunzi wa shule, yatahitajika kuwa na rangi hiyo ya manjano.

Mapuuza ya sheria huleta ufukara, aonya Maraga

Na BENSON MATHEKA

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga amesema kwamba kupuuzwa kwa utawala wa sheria na ufisadi barani Afrika kumechangia umaskini na kulemaza maendeleo.

Kwenye hotuba yake katika kongamano kuhusu maendeleo barani Afrika lililoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Harvard, Amerika, Bw Maraga alisema ni vigumu kutenganisha utawala wa sheria na maendeleo ya dhati.

“Utawala wa sheria na maendeleo vimeunganishwa na vinatiliana nguvu. Utawala wa sheria unatoa mazingira bora ya kushamiri kwa vitendo vyote vya binadamu na ni nguzo ambayo ustawi hujengwa,” alisema Bw Maraga.

“Hata hivyo, katika nyanja ya maendeleo Afrika, haki na utawala wa sheria havichukuliwi kwa umakinifu unaofaa,” aliongeza Bw Maraga.

Alisema kwamba ripoti kadhaa za Umoja wa Mataifa zimetambua kuwa utawala wa sheria na maendeleo haviwezi kutenganishwa.

Bw Maraga alisema kwamba kuimarishwa kwa utawala wa sheria katika viwango vya kitaifa na kimataifa ni muhimu kwa ukuaji na udumishaji wa uchumi, kupiga vita umaskini na njaa.

“Imetambuliwa kuwa utawala wa sheria huleta haki za binadamu ikiwemo haki ya maendeleo zote ambazo huwa zinaimarisha utawala wa kisheria,” alisema.

Alisema utawala wa sheria ni nguzo ya demokrasia. “Umehusishwa na upunguzaji wa mamlaka na nguvu za serikali, uhuru wa mahakama na usawa mbele ya sheria, kulinda haki za kimsingi ziwe za kijamii, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na haki ya mali,” alieleza.

Bw Maraga aliyealikwa kutoa hotuba kuu kwenye kongamano hilo alisema utawala wa sheria unahakikisha kwamba haki za binadamu zinapatiwa uhai kama njia moja ya kupiga vita ubaguzi, kutengwa kwa maeneo na jamii ambazo ni chanzo cha umasikini.

Alisema kwa kuelewa vibaya maana ya utawala wa sheria, sheria hutumiwa kukandamiza wananchi. Bw Maraga alisema Kenya imepiga hatua kubwa chini ya katiba mpya iliyopitishwa 2010 ambayo alisema ilisisitiza utawala wa sheria na jukumu lake katika maendeleo.

Alisema mahakama barani Afrika zinafaa kusaidia bara kufikia utawa bora na kutekeleza haki za kiuchumi na kijami.

“Mahakama ni asasi zinazotoa mchango muhimu katika utawala na hili ndilo jukumu ambazo zinafaa kutekeleza kulingana na sheria. Nchini Kenya, ugatuzi, fedha za umma, masuala ya jinsia zina jukumu muhimu katika kuimarisha utawala bora,” alisema.

Bw Maraga alisema ufisadi na kutekwa kwa asasi muhimu na wanasiasa na kumelemeza maendeleo.

“Ufisadi na vitendo vya ufisadi huendelezwa na wale ambao hawaheshimu sheria na kwa hivyo kupalilia umaskini. Kenya mhasibu mkuu wa serikali ameripoti kuwa thuluthi tatu ya bajeti ya taifa hupotea kupitia ufisadi,” alisema Bw Maraga.

 

 

JAMVI: Baada ya kumnasa Jumwa, Ruto sasa alenga kumkumbatia Sultan wa Pwani

Na WYCLIFFE MUIA

MUAFAKA wa kusitisha uhasama kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga unaendelea kuwaleta pamoja mahasimu wa kisiasa kwa matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Umoja wa viongozi hao wawili umempa Naibu Rais William Ruto mwanya wa kunyemelea ngome za upinzani ili kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa wandani wa Bw Odinga.

Na sasa, Bw Ruto anadaiwa kumlenga Gavana wa Mombasa Hassan Joho anayechukukuliwa kuwa ‘Sultan’ wa siasa za Pwani.

Washirika wa naibu rais walidokeza kuwa Waziri wa Utalii Najib Balala ametumwa na Bw Ruto kuwaunganisha kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Siku chache baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kukutana, Bw Ruto aliekea Pwani kwa ziara ya siku tatu ambapo alilakiwa kwa heshima na Wabunge wa chama cha ODM.

Baadhi ya wale waliomlaki Bw Ruto walidokezea Jamvi la Siasa kuwa naibu rais analenga kushirikiana na Bw Joho kuelekea siasa za 2022.

“Wakati Ruto alizuru Pwani, Joho alikuwa amesafiri nje ya nchi lakini naibu rais alitutuma tuongee na yeye ili tujipange kuhusu 2022,”mbunge mmoja wa Pwani asiyetaka kutajwa alisema.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema Joho amejikuza kisiasa kiasi cha kumnyima usingizi Bw Ruto kuhusu ndoto yake ya 2022.

 

Joho alivyong’aa

Mhadhiri wa chuo cha Pwani, Hassan Mwakimako anaamini kukosekana kwa Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses  Wetang’ula katika bustani ya Uhuru wakati Bw Odinga alikula kiapo mnamo Januari 31, kulikuwa kilele cha Joho kung’aa kisiasa.

“Kile Joho alifanya siku hiyo ni sifa wapigakura wengi hutafuta kwa kiongozi. Joho aliwapiku vinara wenza wa NASA na huenda akawa na umuhimu mkubwa wa kisiasa kuwaliko kuelekea 2022,”alisema Prof Mwakimako.

Kwa mujibu wa  Maimuna Mwidau, mchanganuzi wa siasa za Pwani, utiifu wa Joho kwa Bw Odinga umepandisha hadhi yake ya kisiasa na kando na kuwa ‘Sultan’ wa Pwani, huenda akadhibiti kura za Nyanza.

Ili kudhihirisha mandhari ya kisiasa eneo la Pwani ni tulivu kwa Bw Ruto kufanya urafiki na wapinzani wake, mwenyekiti wa wabunge wa Pwani  Suleiman Dori alifichua kuwa Bw Odinga aliwashauri wakomeshe kampeni za kujitenga hata kabla ya kukutana na Rais Kenyatta mnamo Machi 9.

“Alikuwa ashatuambia tuunge ajenda ya serikali na hivyo ndio tunafanya. Kama chama, ni sharti tufuate kile kinara wetu anatuambia,”alisema Bw Dori.

Zaidi ya wabunge 10 wa ODM walimlaki Bw Ruto katika ziara yake ya kaunti za Mombasa, Kwale na Taita Taveta  huku wengine wakiahidi kumuunga mkono ifikiapo 2022.

 

Kuzamisha ndoto ya Joho

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir aliliambia gazeti moja la humu nchini kuwa, kuna juhudi zinaendelea kumshawishi Bw Ruto apangue ndoto yake ya kuwa rais 2022 na badala yake amuunge mkono Joho.

Bw Nassir ambaye ni mwandani mkubwa wa gavana huyo alisema hatua hiyo itahakikisha Ruto amekumbatiwa kikamilifu na Wapwani.
“Msimamo wetu ni wazi. Tunamtaka Ruto amuunge Joho mkono ili awanie urais 2022,” akasema.

Bw Nassir alisema wabunge wa Pwani walijadiliana na Bw Ruto kuhusu mapendekezo hayo kabla ya kuambatana naye katika ziara yake Pwani.

Hata hivyo, msemaji wa naibu rais, David Mugonyi, alipuuzilia mbali kuwepo na mipango kama hiyo.

Ili kuhakikisha ushirikiano kati ya rais na Bw Odinga una maana kwa watu wa Pwani, wabunge wa ODM walisema sharti Bw Joho ashirikishwe.

“Karibu Pwani Bw Ruto, lakini ni vyema tukufahamishe kuwa eneo hili lina kiongozi wake,” alisema Asha Hussein alipomlaki naibu rais Ijumaa iliyopita, eneo la Jomvu Kuu-Rabai .

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa alijipata pabaya alipomuidhinisha Ruto kuwania urais 2022, lakini alijitetea kuwa huo ulikuwa uamuzi wake binafsi.

 

Asubiri 2022

Mbunge wa Kaloleni  Paul Katana alidinda kumuidhinisha Ruto  na badala yake akamshauri angoje hadi 2022. Haya yanajiri huku ikifichuka kuwa Bw Joho kwa ushirikiano na mwenzake wa Nairobi walichangia pakubwa kuja pamoja kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Mbunge wa  Makadara George Aladwa alinukuliwa akisema kuwa, magavana hao wawili walikutana siku chache kabla ya rais na kiongozi wa ODM kufanya mazungumzo.

“Nilifanya mkutano na Sonko afisini mwake Machi 8, kabla ya rais na Raila kukutana na akanifichulia kuwa vinara hao wawili wako tayari kufanya kazi pamoja,”alisema Bw Aladwa.

Sonko anaonekana kuwa mwandani wa rais huku Joho ambaye ni naibu kinara wa chama cha ODM, akionekana kuwa mtiifu kwa Bw Odinga.

Inadaiwa Joho anaendela kumshawishi mwenzake wa Kilifi Amason Kingi kupuuzilia mbali juhudi zake za kuanzisha chama cha Pwani na badala yake amuunge mkono katika chama cha ODM.

Eneo la Pwani lenye takriban wapigakura 1.7 ni ngome ya NASA na litakuwa muhimu sana katika siasa za 2022.

JAMVI: ‘Jenerali’ kutua nchini bila gwaride wala fataki…

Na LEONARD ONYANGO

MWANASIASA wa Upinzani Miguna Miguna atarejea humu nchini Jumatatu huku kukiwa na dalili kwamba hatalakiwa kwa mbwembwe na wafuasi wa National Super Alliance (Nasa).

Umaarufu wa Dkt Miguna ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Jubilee ulididimia mara tu baada ya kinara wa NASA Raila Odinga kutangaza kuwa atafanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta wiki mbili zilizopita.

Dkt Miguna ambaye amejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la NASA, National Resistance Movement (NRM), alifurushwa na serikali kwa nguvu kutoka Kenya hadi Canada mwezi jana kutokana na madai kuwa hakuwa Mkenya.

Kabla ya kufurushwa, mwanaharakati huyo wa NASA alikamatwa na kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi katika kaunti za Kiambu na Nairobi na kisha kufikishwa katika mahakama ya Kajiado baada ya siku tatu ambapo alifunguliwa mashtaka ya uhaini.

Bw Miguna ndiye aliapisha Bw Odinga kuwa ‘Rais wa Wananchi’ uwanjani Uhuru Park mnamo Januari 30, mwaka huu. Hata hivyo, serikali ilisisitiza kuwa kiapo hicho kilikuwa haramu na kisha kuwapokonya bunduki, paspoti na walinzi baadhi ya wanasiasa wa NASA huku vuguvugu la NRM likiharamishwa.

Tangu kusafirishwa nchini Canada kwa lazima, Dkt Miguna amekuwa akizunguka katika mataifa ya Amerika, Uingereza na Ujerumani ambapo amekuwa akihutubia makundi mbalimbali kuhusiana na hali ya kisiasa ya Kenya na yaliyojiri wakati wa uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26, mwaka jana.

“Machi 24, 2018, vuguvugu la NRM litakuwa jijini London, Uingereza kabla ya kutua jijini Nairobi Machi 26,” akasema Dkt Miguna.
Mwanaharakati huyo alitangaza kurejea wiki mbili baada ya Mahakama ya Rufaa kumwondolea vikwazo huku ikisema kuwa yuko huru kurejea.

Wafuasi wa NASA walimkumbatia DktMiguna na kumtaja shujaa alipojitokeza kukabiliana na serikali ya Jubilee huku akidai kuwa uchaguzi wa mwaka jana uligubikwa na dosari chungu nzima.

Lakini tangu Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, wafuasi wa NASA wameonekana kumtelekeza Miguna huku wengi wakiunga mkono hatua ya kiongozi wa Upinzani kukubali kushirikiana na serikali.

Wengi wa wafuasi wa NASA wamemchukulia Bw Odinga kama mpenda amani huku baadhi wakimwona kama msaliti kwa kuamua kushirikiana na serikali.
Bw Odinga pia ameonekana kujitenga naye tangu Miguna alipopasua mbarika kuwa baadhi ya maafisa wa NASA walipokea fedha za hongo kutoka kwa Jubilee kabla ya kuapishwa kwa Bw Odinga Januari 30.

Tangu Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta, Dkt Miguna amekuwa mkosoaji mkubwa wa kiongozi wa Upinzani huku akimtaja kuwa msaliti kwa wafuasi wake.

Amesisitiza kuwa vuguvugu la NRM litandelea kupigania haki katika masuala ya uchaguzi licha ya Bw Odinga ‘kujiunga’ na serikali.

“Kwa kukubali kufanya kazi na Rais Kenyatta ‘aliyemwibia’ ushindi wake, Bw Odinga amesaliti mamia ya Wakenya waliouawa na kuhataraisha maisha yao baada ya uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26,” akasema Dkt Miguna.

Mwanaharakati huyo pia alitangaza kuongoza maandamano katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia kesho ili kushinikiza kufanyika kwa mageuzi katika mfumo wa uchaguzi huku akisema kuwa: “ushindi haupatikani kwa kusalimiana (kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga) katika chumba cha mikutano katika afisi ya rais kwenye Jumba la Harambee.”

Dkt Miguna ambaye alibwagwa na Mike Sonko katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi wa Agosti 8, huenda akajizolea maadui zaidi; kutoka upande wa Jubilee na chama cha ODM atakaporejea kesho humu nchini.

Kulingana na aliyekuwa waziri na mwaniaji wa urais 2013, James Ole Kiyiapi, Dkt Miguna atakabiliwa na upinzani kutoka kwa Jubilee na ODM kutokana na mtindo wake wa kutaka kusema ukweli.

“Miguna Miguna anasema mambo ambayo wanasiasa hawataki kusikia uwe upande wa Jubilee au NASA. Miguna ni mwaminifu na ndiye kiongozi anayefaa kuongoza Kenya,” alisema Prof Kiyiapi.

JAMVI: Uhuru afanikiwa kupunguza makali ya vinara wa upinzani kwa utawala wake

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta hatimaye amefaulu kudhoofisha upinzani dhidi ya serikali yake kwa kumshawishi kiongozi wa ODM Raila Odinga kuunga ajenda zake.

Wadadisi wanasema, japo viongozi hao wawili walisema nia yao ni kuunganisha Wakenya,  Rais Kenyatta ndiye mshindi kwa sababu hatakuwa na upinzani wenye nguvu wa kukosoa serikali yake.”

Jubilee ilijaribu kusambaratisha upinzani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana lakini ikashindwa. Kwa kukutana na Bw Odinga na kufikia muafaka, Rais Uhuru amefaulu kulemaza upinzani,” asema Bw Godfrey Aliwa, mdadisi wa masuala ya siasa na wakili jijini Nairobi.

Anaeleza kuwa waliopanga mazungumzo hayo walielewa kuwa upinzani bila Raila ni butu. “Raila ndiye nguzo ya upinzani Kenya na kwa kumleta karibu na serikali ni kusambaratisha upinzani.

Lengo hapa ni kuhakikisha Rais Kenyatta hatakuwa na upinzani wenye nguvu kumsumbua katika kipindi chake cha pili na cha mwisho uongozini,” alisema Bw Aliwa.

Mbali na upinzani kuwa na wabunge wachache, wengi wao ni wa chama cha ODM cha Bw Raila ambao tayari wameanza kuchangamkia muafaka wake na Rais Kenyatta.

Washirika wa Bw Raila katika NASA, Kalonzo Musyoka wa Wiper Democratic Movement, Moses Wetang’ula wa Ford-Kenya na Musalia Mudavadi wa Amani National Congress hawakuhusishwa katika muafaka huo.

Baadhi ya washirika wa kisiasa wa Bw Musyoka, Bw Wetangula na Bw Mudavadi wamenukuliwa wakitaka chama cha ODM kuondoka NASA ili wachukue nafasi ya upinzani rasmi. Hata hivyo, kulingana na Bw Aliwa, hata kama wangeachiwa NASA, hawataweza kukosoa serikali alivyokuwa akifanya Bw Raila.

“Aliyenufaika pakubwa ni Rais Kenyatta kwa sababu atakuwa na mteremko kwa kukosa upinzani thabiti katika kipindi chake cha mwisho mbali na Raila kumtambua kama rais,” alisema.

Chini ya Bw Raila na wanasiasa wake wa ODM, upinzani uliongoza maandamano yaliyong’oa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) chini ya aliyekuwa mwenyekiti Isaack Hassan.

Ni Bw Odinga ambaye alifichua kashfa mbali mbali serikalini ikiwa ni pamoja na ile ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS na Eurobond. “Sidhani kama kuna anayeweza kufuata nyayo za Raila kati ya Musyoka, Wetangula na Mudavadi. Kumbuka ni Raila aliyekuwa akisukuma kubuniwa kwa mabunge ya wananchi yaliyokuwa yakikosesha Jubilee usingizi,” asema Bw Geff Kamwanah, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Anasema masuala ambayo NASA imekuwa ikipigania kama haki katika uchaguzi ni mazito na yanahitaji kiongozi mwenye ujasiri kama Raila.

Bw  Musyoka, Bw Wetang’ula na Bw Mudavadi wanasema wako tayari kusukuma ajenda za NASA bila Bw Odinga lakini hii ni kama mzaha,” asema mwanahabari na mdadisi wa masuala ya siasa Macharia Gaitho kwenye makala yaliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation.”

“Wamekasirika kwa sababu Bw Odinga alizungumza na Bw Kenyatta bila kuwahusisha,” alisema Bw Gaitho.

Bw Kamwanah anasema ishara kwamba Musyoka, Wetangula na Mudavadi hawana ujasiri wa kukabiliana na serikali ni kujitenga kwao na Raila alipokula kiapo kama rais wa wananchi.

“Huo ulikuwa mtihani waliofeli. Raila amejaribiwa mara nyingi kwa moto, ameteswa na kutupwa jela na kuibuka jasiri zaidi. Kwa kuzika tofauti zake na Rais Uhuru ni kama kuua upinzani,” aeleza.

Raila amesisitiza kuwa hajahama NASA akisema muafaka wake na Rais Kenyatta ni wa watu wawili na sio mirengo ya kisiasa. Hata hivyo, matamshi yake na washirika wake wa kisiasa, wakiwemo wabunge wa chama cha ODM, yanatoa ujumbe tofauti. Kulingana na mbunge wa Lugari Ayub Savula, Wiper, ANC na Ford Kenya viko tayari kuunda upinzani rasmi bila ODM.”

ODM ikioana na Jubilee tuko tayari kuunda upinzani rasmi,” alisema. Hata hivyo, wadadisi wanasema wanachotaka wabunge hao wapatao 40 bila ODM ni vyeo vya upande wa upinzani bungeni.

“Kenya imerejea ilipokuwa 1997 upinzani ulipodhoofishwa Raila alipojiunga na serikali ya Kanu. Jukumu la kukosoa serikali lilichukuliwa na vyombo vya habari na mashirika ya kijamii na yasiyo ya Serikali.

Jinsi hali ilivyo wakati huu, uhuru wa wanahabari na mashirika ya kijamii umedidimizwa. Kwa ufupi, hakutakuwa na upinzani Kenya iwapo Raila atamezwa na Jubilee,” asema Bw Kamwanah.

Hisia za wadadisi ni kuwa, muafaka wa Raila na Uhuru ulipangwa ili  kupangua upinzani ukose makali ya kukosoa Serikali.

Takwimu: Siaya yaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya vifo nchini

Na DOROTHY OTIENO na JOSHUA MUTISYA

IKIWA unaishi Siaya, una uwezo mkubwa zaidi kufariki kabla ya muda wako ikilinganishwa na yeyote anayeishi katika kaunti nyingine nchini Kenya, utafiti wa Nation Newsplex umebaini.

Kulingana na utafiti huo, idadi ya vifo ni asilimia 20 miongoni mwa wananchi 1,000 mwaka wa 2016, huku mkazi wa Siaya akiwa na uwezo mara tatu wa kuaga dunia akilinganishwa na mkazi wa Nairobi.

Jiji la Nairobi lina idadi ndogo zaidi ya watu wanaoaga dunia, ambapo ni watu sita kati ya 1,000. Hali hiyo imeshuhudiwa Siaya tangu 2011 ambapo kila mwaka huongoza kwa idadi ya vifo.

Kwa kipindi hicho, Nairobi imeorodheshwa miongoni mwa kaunti tatu ambazo zina idadi ndogo zaidi ya vifo nchini katika kipindi hicho.

Kwa kuzingatia visa vya watu wanaoua wengine, Kaunti ya Siaya iliorodheshwa ya saba. Kitaifa, visa hivyo ni 14 kati ya 100,000.

Kaunti zingine tatu Nyanza zimo miongoni mwa kaunti 10 za mbele zilizo na idadi kubwa ya vifo kwa watu 1,000.

Kisumu imeorodheshwa ya tano ambapo ina viwango vya vifo kuwa asilimia 14.1, Homabay ni ya saba kwa asilimia 13.5 na kufuatwa na Migori kwa asilimia 13.
Kaunti ya pili ni Vihiga ambayo idadi ya vifo ni 17 kwa watu 1,000 na kufuatwa na Elgeyo-Marakwet(15) na Taita Tavet(14.7).

Vihiga imekuwa nambari hiyo tangu 2011. Kaunti ya Turkana imo katika nafasi ya sita(14) na Bungoma imo nambari tisa(12.4).

Kaunti ya Kakamega ni nambari 10 (12). Idadi ya mauaji kwa watu 100,000 katika Kaunti ya Vihiga ni 11, ambapo kaunti hiyo ni miongoni mwa kaunti 10 zilizo na visa vingi zaidi vya mauaji.

Viwango hivyo vilikadiriwa kwa kuzingatia idadi ya watu wanaoishi katika maeneo ya kaunti, idadi ya vifo vilivyoripotiwa katika ripoti ya takwimu za kitaifa miaka ya 2015 na 2017.

Idadi ya vifo ilizingatiwa katika utafiti huo kwa sababu sio vifo vyote vilivyoripotiwa katika sajili ya kitaifa. Kwa mfano, asilimia 76 ya vifo vyote viliripotiwa na kusajiliwa 2016, idadi ya juu Zaidi nchini. Hata hivyo, idadi ya vifo iliyoripotiwa Mandera na Wajir ilikuwa chini ya asilimia 10.

Kaunti iliyo nambari mbili kwa viwango vya chini vya vifo kati ya watu1,000 ilikuwa Isiolo(6.8) na kufuatwa na Narok(6.9), Kajiado(7.3) na Embu(7.9).
Isiolo ndio kaunti ya pekee ambayo hakuna kisa hata kimoja cha mauaji kiliripotiwa mwaka wa 2016.

Kaunti za Garissa, Mandera na Wajir hazikuzingatiwa katika utafiti huo kwa sababu makadirio ya idadi ya watu 2011 na 2015 yalilandana na hesabu ya watu wote katika uchunguzi wa hesabu ya watu nchini (KNBS) wa 2009.

Hivyo, ni kaunti 44 ambazo zilijumuishwa katika utafiti wa Nation Newsplex.

 

Vifo jijini Nairobi

Ingawa Nairobi ina idadi ndogo zaidi ya vifo nchini, kifo kimoja kati ya 14 mwaka wa 2016 kilitokea jijini, idadi ya juu zaidi.

Hata hivyo, mmoja kati ya watu 10 nchini wanaishi Nairobi, kumaanisha ikilinganishwa na kiwango cha watu cha kitaifa, idadi hiyo ilikuwa ya chini zaidi.

Mwaka wa 2016, jumla ya vifo 189,930 vilisajiliwa, ambavyo vilikuwa takriban asilimia 42 ya vifo vyote mwaka huo ambavyo viliripotiwa bila kusajiliwa(452,214).

Katika miaka sita, Kaunti ya Nyeri iliripoti upungufu mkubwa zaidi wa vifo katika muda wa miaka sita, hadi 2016. Idadi hiyo ilipungua kwa thuluthi moja, hadi tisa, kutoka 14 kwa watu 1,000.

Idadi ya vifo iliongezeka zaidi katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet kutoka 11 hadi 15 kati ya watu 1,000. Kitaifa, idadi ya vifo iliongezeka kwa asilimia 10 hadi 10 kwa watu 1,000 katika kipindi hicho.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO), uwezekano wa mwanamke Mkenya kuishi hadi miaka 65 ni asilimia 72, kiwango kilichoshuka kwa asilimia 10.

 

Mauaji

Wakati wa kuzingatia kiini cha vifo, Kaunti ya Lamu ilikuwa na idadi ya juu zaidi ya mauaji huku Nakuru na Isiolo zikuwa na viwango vya chini zaidi.

Hii ni kumaanisha kuwa una uwezo mara 58 kufa kutokana na mauaji katika Kaunti ya Lamu ikilinganishwa na Isiolo au Nakuru.

Kulingana na ripoti ya polisi, visa 76 vya mauaji viliripotiwa Lamu, ambapo ni watu 59 kati ya 100,000.

Visa vinane pekee vya mauaji viliripotiwa Nakuru, ambavyo ni chini ya asilimia moja pekee.

Idadi ya mauaji ya kaunti hizo mbili ilikuwa chini zaidi ikilinganishwa na viwango vya kitaifa, cha asilimia sita pekee kwa watu 100,000.

Viwango hivyo kwa kaunti 23 vilikuwa chini ya viwango vya kitaifa vya 6 kati ya watu 100,000.

 

Viini vikuu vya vifo nchini
Pneumonia-vifo 21,295,
Malaria -vifo 16,000
Kansa- vifo 15,762
Ukimwi -vifo 9,471
Ukosefu wa damu mwilini -vifo 8,165

TAHARIRI: Muafaka usiwe kifo cha upinzani

Na MHARIRI

MALUMBANO ndani ya vyama tanzu vya upinzani unaendelea kupandisha joto la kisiasa ambalo lilikuwa limezimwa na mkutano wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga.

Jumanne, Seneta wa Bungoma Moses Wetangula alivuliwa wadhifa wake wa kiongozi wa wachache bungeni hatua ambayo ilivikera sana vyama vya Wiper, ANC na Ford Kenya.

Chama cha ODM kilimfurusha Bw Wetangula licha ya vinara wa NASA, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Wetangula na Bw Odinga kutoa maagizo ya kukomesha hatua hiyo.

Japo vyama vya kisiasa vina demokrasia ya kuadhibu wanachama waasi, ni vyema mizozo ya ndani ilisuluhishwe kimya na viongozi bila kuchochea uhasama wa kisiasa haswa miongoni mwa jamii.

Mabadiliko yanayoshuhudiwa NASA katika usimamizi wa bunge yalianza baada ya mkutano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Tungetaka kusisitiza umuhimu wa kuwa na chama cha upinzani bungeni ili kukosoa maovu ya serikali.

Bw Odinga alichukua hatua ya busara sana kuweka kando tofauti zake za kisiasa na kukutana na rais, lakini ni vyema Waziri huyo Mkuu wa zamani awape nafasi viongozi wengine wanaotaka kuendelea kuwa kwa upinzani.

Hatua ya ODM kumtimua Seneta Wetang’ula katika wadhifa huo imechukuliwa na wengi kama usaliti wa kisiasa hatua ambayo huenda ikaanzisha siasa za 2022.

Siasa zina ushindani mkubwa na ingekuwa vyema kutoanzisha mjadala wa uchaguzi wa 2022 ili kutoa nafasi kwa serikali kuu na zile za kuanti kuwahudumia Wakenya kabla ya kuingia katika mchakato mwingine wa kisiasa.

Bw Musyoka na wenzake walimuomba Rais Kenyatta awape sikio na tunasisitiza umuhimu wa kufanyika kwa mdahalo wa viongozi wote.
Japo mkutano wa rais na Bw Odinga umewapa wengi matumaini ya kutuliza joto la kisiasa nchini, ni vyema kutopuuza mchango wa vinara wenza katika upinzani.

Madhumuni ya kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga yawe kuunganisha Wakenya wote na wala si kuua upinzani ambao mchango wake ni muhimu sana kuhakikisha mali ya umma imelindwa na kutumika ipasavyo.

Bw Odinga anapaswa kujitokeza wazi kuelezea iwapo chama chake kimemezwa na Jubilee ili kutoa nafasi kwa vyama vingine vyenye uwezo wa kuikosoa serikali.

MAKALA MAALUM: Siasa za kuviziana zadhihirika katika uteuzi wa Uhuru kwenye Mahakama ya Rufaa

JAJI Paul Kihara Kariuki aliyeteuliwa na Rais Kenyatta kuwa Mwanasheria Mkuu. Picha/ Maktaba

Na RICHARD MUNGUTI

KINYANG’ANYIRO cha kuteua rais wa mahakama ya rufaa na mwakilishi wake katika tume ya Idara ya Mahakama (JSC) kilitifua vumbi kali wiki chache zilizopita, huku komeo za kudhibiti idara ya mahakama zikikosa kushikilia kama ilivyotarajiwa.

Siasa za kuviziana zilielekezwa katika mahakama hiyo ya pili kwa ukubwa nchini baada ya ile ya Juu na wadau wenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha Jubilee, lakini kura zilipopigwa, dau lao lilienda mrama.

Wale ambao hawakutarajiwa kushinda ndio walitwaa ushindi na sasa mahakama hiyo na JSC itafanyakazi na walioteuliwa.
Mahakama hiyo inayotarajiwa kuwa na majaji 30, kwa sasa ina majaji 18 baada ya baadhi yao kustaafu na wengine hawajateuliwa.

Kuna nyadhifa 12 katika mahakama hiyo kufuatia kuondoka kwa Jaji Paul Kihara Kariuki na kuwa Mwanasheria Mkuu.
Waliotazamiwa kutwaa nyadhifa hizo mbili zenye ushawishi mkubwa walilambishwa sakafu, na ndoto ya waliowatumainia kuwa na usemi katika Mahakama ya Juu kuambulia patupu.

Ushindani mkali ulizuka kujaza nafasi ya Jaji Kariuki alipoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta katika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu baada ya Prof Githu Muigai kujiuzulu.

 

Kivumbi
Nyavu za kuwavua rais na mwakilishi katika JSC wa Mahakama ya Rufaa zilitandazwa na kampeni zikaanza kushika kasi.
Kilele kilikuwa wiki iliyopita wakati kura zilipopigwa na kivumbi kikatulia.

Waliomenyana kutwaa urais walikuwa Majaji Alnashir Visram, William Ouko na Martha Koome.

Watatu hao walifanya kila juhudi kuridhisha wenzao kuwateua, lakini Jaji Koome aliyekuwa anatazamiwa kushinda alijiondoa na kuwaacha Majaji Visram na Ouko wapimane nguvu.

Baada ya kura kupigwa, Jaji Ouko alimshinda Jaji Visram kwa kupata kura 16 kati ya kura zilizopigwa naye Jaji Visram akapata kura nne. Sasa Jaji Ouko ndiye rais wa Mahakama ya rufaa. Ametwaa wadhifa uliokuwa umeshikiliwa na Jaji Kariuki kwa miaka kadhaa.

Uteuzi wa Jaji Kariuki kuwa Mwanashera Mkuu utajadiliwa na kamati ya bunge inayohusika na masuala ya haki, upelekwe bungeni kuidhinishwa kisha jina lipelekwe kwa Rais Kenyatta.

Kamati ya bunge ya masuala ya haki inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini, Bw William Cheptumo itajidili suala hili la Jaji Kariuki na kupokea maombi  kutoka umma.

Katika kinyang’anyiro cha kumteua mwakilishi wa JSC, Jaji Mohammed Warsame alimshinda Jaji Wanjiku Karanja kwa kuzoa kura 16 kwa 4 na kupata kipindi kingine katika JSC.

Matokeo hayo ya kura yalituliza siasa za pembeni za Jubilee ambapo baadhi ya wanasiasa waliona idara ya mahakama kuwa iliyo na majaji wengi walioegemea mrengo wa Nasa.

Ili kutaka kudhibiti JSC, wanasiasa hao walimshauri Rais Kenyatta kuteua aliyekuwa Msimamizi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) Profesa Olive Mugenda, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Felix Koskei na aliyekuwa karani katika bunge la kitaifa Patrick Gichohi kuwa wanachama wa tume hii ya kuwaajiri majaji na mahakimu (JSC) ndipo Jubilee iwe na usemi mkuu katika idara ya mahakama.

Lakini uteuzi wao ulipigwa breki Kituo cha Katiba Institute kilipowasilishwa kesi kortini na maagizo yakatolewa yakisitisha kuapishwa kwa watatu hao (Mugenda, Koskei na Gichohi) hadi kesi iamuliwe.

 

Sheria ilikiukwa

Mamlaka ya Rais Kenyatta ya kuwateua watatu yanahojiwa katika kesi hii kwani Katiba Institute inadai sheria ilikiukwa.

Nafasi nyingine katika JSC ilitokea baada ya Rais Kenyatta kumteua Bi Winnie Guchu kuwa naibu ajenti mkuu wa kampeni na uchaguzi wake Agosti na Oktoba 2017 ambaye alimteua kuwa  Waziri msaidizi.

Kuchaguliwa kwa Jaji Ouko, kutoingia kwa Jaji Karanja na kutoapishwa kwa wateule watatu katika JSC kumepunguza kasi ya Jubilee kuthibiti mahakama ya rufaa na JSC.

Sasa ni wazi historia itajirudia katika uteuzi AG kwa vile nyakati za utawala wa rais mstaafu Daniel arap Moi aliyekuwa wakati mmoja Jaji wa Mahakama ya Rufaa marehemu Mathew Guy Muli alimteua kuwa mwanasheria mkuu.

Na baadaye Jaji Muli akastaafu kama Mwanasheria Mkuu na kuteuliwa tena kuwa Jaji wa Mahakama ya rufaa wadhifa aliohudumu hadi akahitimu miaka 74 na kustaafu. Jaji Muli alifungua afisi ya uwakili na alikuwa akihudumu kama wakili wa kibinafsi hadi alipopungia dunia mkono wa buriani.

Kuteuliwa kwa Jaji Kariuki kutakuwa ni kama kuhamisha huduma zake hadi kwa afisi ya AG ambayo katiba inasema anayeteuliwa kuutekeleza lazima awe amehitimu kuteuliwa kuwa jaji katika mahakama ya rufaa.

“Kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Kifungu 156(2) cha Katiba nimemteua Jaji Kariuki kuwa Mwanasheria mkuu mpya wa nchi hii. Nimepeleka jina lake kwa bunge la kitaifa kuidhinishwa,” alisema Rais Kenyatta alipomteua.

 

Haijabainika

Wakati tangazo hilo lilipopeperushwa hakuna chochote kilisemwa iwapo Jaji Kariuki amejiuzulu na kufikia sasa haijabainika ikiwa amejiuzulu au la kwani JSC haijatoa habari.

Hiki ni kinyume na ilivyokuwa aliyekuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Keriako Tobiko alipong’atuka afisini.

Bw Tobiko alijiuzulu kisha Rais Kenyatta akatangaza amekubali kujiuzulu kwake kisha akamteua kuwa Waziri wa Misitu. Sivyo hivyo kwa Jaji Kariuki.

Kabla ya kuteuliwa kuwa jaji, Jaji Ouko alikuwa Msajili wa Idara ya Mahakama na kutokana kazi yake alikuwa akitangamana na majaji na mahakimu wote.

Alikuwa akihusika na maslahi yao ya kila siku na hivyo basi kipindi chake kama rais hakitakuwa na ugumu kutokana majukumu yake alipokuwa msajili.

Kazi ya rais wa mahakama ya rufaa ni kushughulikia masuala ya usimamizi na uteuzi wa majaji wanaosikiza rufaa mbalimbali. Pia huwa anafanya mikutano na Jaji Mkuu kuhusu korti hiyo.

 

Msimamo mkali

Duru zasema Jaji Warsame alishinda kuwa mwakilishi wa mahakama hiyo katika JSC kutokana na msimamo wake thabiti wakutopendelea upande wowote.

Msimamo wake mkali ulidhihirika alipokuwa akihudumu kama Jaji wa Mahakama kuu.

Wakati mmoja akiamua kesi aliwahi kumlaumu rais mstaafu Mwai Kibaki kwa kutotekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kutia saini vibali vya kuwanyonga wa wahalifu waliokuwa wamehukumiwa kutiwa vitanzi.

Hata wakati wa mahojiano ya Jaji Mkuu, Jaji Warsame alikuwa anapasua mbirika kwa waliowania kwa sababu ya maamuzi yao kwenye kesi mbali mbali.

Wakati mmoja alimhoji vikali Jaji Jackton Ojwang wa Mahakama ya Juu hata jaji huyo akasema “nipe fursa nipumue”
Wanachama wengine wa JSC ni Jaji Mkuu (CJ) David Maraga (mwenyekiti), naibu wake DCJ Philomena Mwilu (mwakilishi wa

Mahakama ya Juu ), Mwenyekiti wa Tume ya Kuajiri Watumishi wa Umma (PSC), Katibu ni Msajili wa Idara ya Mahakama (sasa ni Ann Amadi)

Wengine ni wawakilishi wawili kutoka Chama cha wanasheria nchini (LSK) ambacho wawakilishi ni Profesa Tom Ojienda na wakili Mercy Deche. Uanachama wao utatamatika mnamo Februari 1, 2019.

 

TAHARIRI: KEBS na ACA zimeshindwa kukabiliana na bidhaa feki?

Na MHARIRI

TANGU mvua ya msimu ilipoanza kunyesha wiki mbili zilizopita, mijengo kadhaa imeporomoka Kiambu, Nairobi na Mombasa. Sababu kuu ya kuporomoka kwa mijengo hii ni utumizi wa vifaa duni vya ujenzi.

Katika taarifa ya kina tuliyochapisha majuzi, utumizi wa bidhaa ghushi ulitajwa na wataalamu kama sababu kuu ya mijengo kuporomoka.

Mbali na mijengo tuliangazia pia athari kwa afya ya binadamu kutokana na utumizi wa bidhaa ghushi, ambazo kwa kawaida huwa zimetengenezwa kwa tekinolojia duni, kemikali hatari na hazijafikia viwango vinavyokubalika.

Kulingana na wataalamu, biashara hii inaendelea kuimarika kila uchao na inaendelezwa na wafanya biashara ambao nia yao pekee ni utajiri wa haraka.

Na kweli wengi wao wamekuwa mamilionea katika muda mfupi, lakini madhara ya biashara yao yamekuwa ni maelfu kupata magonjwa hatari yasiyo na tiba, vifo, hasara ya ajali na mijengo kuporomoka na kiwango cha ushuru kushuka.

Kinachosikitisha ni kuwa kuna taasisi ambazo zimepewa jukumu la kukabiliana na biashara feki na kuhakikisha bidhaa zinazowekwa sokoni zinafikia viwango vya ubora uliowekwa.

Lakini taasisi hizi zimeonekana kulemewa na kazi ama zinafungia macho watengenezaji na wauzaji wa bidhaa feki.

Imekuwaje kwa watengenezaji bidhaa hizi feki kuzipenyeza hata katika maduka ya rejereja bila taasisi husika kama vile KEBS na Anti Counterfeit Agency (ACA) kufahamu ama kuchukua hatua zifaazo?

Ni makosa ya uhalifu kwa waliopewa jukumu la kuhakikisha Wakenya wanatumia bidhaa za ubora wa juu kukosa kufanya hivyo, kwani hatua hii inaweka maisha ya taifa lote katika hatari kubwa.

Wasimamizi wakuu wa mashirika husika wanapasa kung’atuka ama waondolewe katika nyadhifa zao kwa kuhatarisha maisha ya Wakenya milioni 45 kwa kukosa kufanya kazi yao kikamilifu.

Huenda wakuu hawa wakadai hawana uwezo wa kukabiliana na wahalifu wanaotengeneza na kuuzia Wakenya bidhaa ghushi.

Lakini hatua mwafaka kwa afisa yeyote ambaye anajali hata maisha yake mwenyewe na ya familia yake ni kusema wazi ameshindwa kutokana na sababu hii ama ile.

Makundi ya kutetea watumiaji bidhaa pia yana jukumu kubwa la kuendeleza kampeni ya kitaifa ya kupigana na bidhaa hizi na kuhamasisha kuhusu hatari zake.

Kwa ujumla wajibu wa kukabiliana na bidhaa feki ni wa kila mmoja.

JAMVI: Wimbi la ‘minjiminji’ layeyuka kama mvuke huku wakazi wakimkosoa Waiguru

Na WANDERI KAMAU

Kwa ufupi:

 • Baadhi ya changamoto zinazomwandama Bi Waiguru zinatokana na tofauti zake na viongozi wengi wa eneo hilo ambao, awali, walikuwa washirika wake wakuu.
 • Upungufu ya uongozi wa Bi Waiguru ni kutopatikana kwa urahisi, kutoshirikiana na viongozi wengine, kutenga baadhi ya maeneo katika masuala ya maendeleo, kuongeza ada za biashara na magari
 • Waendeshaji magari Kerugoya walilalamikia “kupendelewa” kwa baadhi ya kampuni za matatu, kiasi cha mmoja wa wawakilishi wake kuteuliwa Waziri wa Fedha na Bi Waiguru
 • Endapo kutakuwa na uchaguzi mpya, kutakuwa na ushindani mkali kati ya Bi Waiguru na Bi Karua, na huenda Bi Waiguru “akasombwa” na ghadhabu za wakazi dhidi ya uongozi wake

UTAWALA wa gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru umo kwenye darubini baada ya wakosoaji wake kudai kuwa anatenga maeneo ambayo hayakumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu uliopita..

Kwa muda wa chini ya miezi miwili, wakazi wa Kerugoya na Ngurubani wameandamana wakidai kupuuzwa na kutoshirikishwa katika maswala ya maendeleo katika kaunti hiyo.

Mbali na hayo, uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba kesi ya kupinga kuchaguliwa kwake iliyowasilishwa na Bi Martha Karua isikizwe tena, imetajwa na wadadisi kama kisiki kwamustakabali wake wa kisiasa.

Na ingawa Bi Waiguru amewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Mahakama ya Juu, wadadisi wanasema kibarua kigumu kwake, ni ikiwa patakuwepo na marudio ya uchaguzi wa ugavana.

Kulingana na Wahome Kiruma, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za ukanda wa Mlima Kenya, baadhi ya changamoto zinazomwandama Bi Waiguru zinatokana na tofauti zake na viongozi wengi wa eneo hilo ambao, awali, walikuwa washirika wake wakuu.

“Kibarua kinachomkabili gavana (Waiguru) ni kikubwa, ikiwa mahakama itaamua kuwe na uchaguzi mpya. Hii ni kwa sababu wakazi na viongozi wengi wamepoteza imani na uongozi wake, ikilinganishwa na matumaini waliyokuwa nayo kabla ya Agosti 2017,” asema Bw Kiruma.

Kwenye matokeo ya ugavana, Bi Waiguru alishinda kura 161, 343 huku mpinzani wake wa karibu Bi Karua, akizoa kura 122,091.

Hata hivyo, wachanganuzi wamekuwa wakitaja matokeo hayo kuwa kinyume na tafiti zilizotolewa na mashirika mbalimbali kuonyesha Bi Waiguru alikuwa kifua mbele kwa mbali.

Kwa mfano, siku kadhaa kabla ya uchaguzi huo, shirika la TIFA lilionyesha Bi Waiguru akiongoza kwa asilimia 55 ya kura dhidi ya Bi Karua, ambaye angepata asilimia 35 pekee.

Hata hivyo, hali ilikuwa kinyume, kwani Bi Karua alipata asilimia 42 ya kura kwenye uchaguzi huo, naye Bi Waiguru akazoa asilimia 54.

 

Si rahisi kumpata Waiguru

Kulingana na wakazi, baadhi ya mapungufu ya uongozi wa Bi Waiguru ni kutopatikana kwa urahisi, kutoshirikiana na viongozi wengine, kutenga baadhi ya maeneo katika masuala ya maendeleo, kuongeza ada za biashara na magari kati ya mengine.

Kwenye maandamano ya Ngurubani wiki iliyopita, waendeshaji wa magari aina ya Probox waliandamana wakilalamikia hatua ya kiongozi huyo kuongeza ada zao hadi Sh450, kinyume na ada za sasa ambapo huwa wanalipa wastani wa Sh200 kila siku.

Katika maandamano ya Kerugoya majuzi, baadhi ya waendeshaji magari walilalamikia “kupendelewa” kwa baadhi ya kampuni za matatu, kiasi cha mmoja wa wawakilishi wake kuteuliwa Waziri wa Fedha katika serikali yake.

Kwa hayo, wachanganuzi wanaeleza kuwa mojawapo ya sababu zinazowakasirisha uongozi wake ni kutokana na matumaini makubwa waliyokuwa nayo kwake, hasa baada ya kuraiwa kumpigia kura na Rais Uhuru Kenyatta.

“Wakazi wametamaushwa sana na uongozi wa Bi Waiguru, ikizingatiwa kwamba walipewa msukumo mkuu kumchagua na kampeni kali alizofanyiwa na Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto. Hivyo, ghadhabu yao huenda ikaashiria kutofurahishwa kwao na uongozi wa Serikali  Kuu,” asema Bw Linford Mwangi, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

 

Kutowajali wakazi 

Aidha, anasema kwamba, katika hali ambapo kutakuwa na uchaguzi, huenda mojawapo ya sababu kuu zikawasukuma watu kutomuunga mkono ni dhana ya kutoshughulikia matakwa yao, licha ya kuungwa mkono na serikali ya kitaifa.

Tangu kuchaguliwa kuwa gavana, Bi Waiguru ametofautiana na viongozi wengi, akiwemo mwandani wake wa muda mrefu Bi Wangui Ngirichi, mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo.

Baadhi ya wabunge na madiwani pia wameeleza kutoshirikishwa vilivyo naye, kwenye uongozi wa kaunti hiyo.
Kwa wakati mmoja, mbunge wa Mwea, Kabinga Thayu, alimkosoa vikali Bi Waiguru hadharani kwa madai ya kulitenga eneo hilo, licha ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya wapigakura.

“Ni masikitiko kwamba tumepewa waziri mmoja pekee, licha ya eneo hili kuwa na zaidi ya wapigakura 200,000. Hiki ni kinaya kikubwa, ikizingatiwa kwamba gavana mwenyewe anatoka katika eneo hili,” akalalama Bw Thayu.

 

Waiguru hatarini

Endapo kutakuwa na uchaguzi mpya, wachanganuzi wanatabiri ushindani mkali kati ya Bi Waiguru na Karua, huku wengine wakisema kwamba huenda Bi Waiguru “akasombwa” na ghadhabu za wakazi dhidi ya uongozi wake.

“Kuna uwezekano wa Bi Karua kupata uungwaji mkono zaidi ya ilivyokuwa Agosti 2017, kwani baadhi ya wakazi wanaonekana kujutia uamuzi wao,” asema wakili Mwangi Tharau, ambaye ni mkazi wa Mwea.

Licha ya malalamishi hayo, watetezi wa Bi Waiguru wanapuuzilia mbali mengi ya madai hayo, wakiyataja kama njama za mahasimu wake wa kisiasa.

“Bi Waiguru anapigwa vita kutokana na maono yake makubwa katika kustawisha eneo hilo. Haya ni mawimbi tunayoamini yatapita tu,” asema Naibu Gavana Peter Ndambiri.

JAMVI: Wabunge waonekana kutoelewa makubaliano ya Uhuru na Raila yanakoelekea

Na CHARLES WASONGA

HUKU mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga ukiendelea kuibua hisia mseto imebainika kuwa wabunge wa pande zote mbili hawaelewi mwelekeo utakaochukua.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa sasa wanaelezea hofu kwamba huenda hali hii ikalemaza juhudi za kuafikiwa kwa masuala muhimu yaliyoangaziwa katika taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na viongozi hao.

Akiwasilisha hoja ya kuhimiza wabunge kukumbatia maelewano hayo Jumatano, kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi alisema wawili hao walikubaliana kuhusu masuala yenye umuhimu kwa maendeleo ya nchi.

Lakini akaeleza: “Sisi kama wafuasi wao tumekubali kuunga mkono mipango ya kuchochea maendeleo nchini. Kwa hivyo, tunasubiri mapendekezo hayo ili tuyajadili na kuyaelewa kabla ya kuyapitisha.

 

Mambo muhimu

Bw Mbadi, hata hivyo, alioorodhesha masuala amabayo yamekuwa yakiibuliwa na muungano wa upinzani, NASA, tangu 2017 kama vile, haki katika uchaguzi, uhuru wa idara ya mahakama, ukabila, ridhaa kwa wahasiriwa wa fujo za kisiasa, vita dhidi ya ufisadi na kupigwa jeki kwa ugatuzi, kama yatakayoangaziwa katika mazungumzo hayo.

Mwenzake upande wa Jubilee, Aden Duale naye alionekana mwenye ufahamu finyu kuhusu misingi na muundo wa mwafaka huo.

Kiongozi huyo wa wengi akasema: “Wakati huu muafaka huo ungali mchanga. Tungali kushuhudia mengi. Tumeonyeshwa ukurasa mmoja tu.”

Kiranja wa wachache Junet Mohammed ambaye aliandamana na Bw Odinga kwa mkutano na Rais Kenyatta katika jumba la Harambee, Nairobi Machi 9 pia hakutoa mwanga kuhusu yaliyojiri katika mkutano huo.

“Katika bungeni hili mimi niliyepewa nafasi ya kipekee ya kuandamana na kinara wetu katika mkutano huo. Nilisikiza yote na nikaridhika kabisa,” akasema bila kuelezea wenzake yale aliyoyasikia.

Bw Martin Andati sasa anasema kauli za wabunge hao, wandani wa karibu wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, zinaonyesha wazi kuwa wao pia hawaelewi mambo mengi kuhusu muafaka huo.

“Hii ni kwa sababu ya maandalizi ya mkutano huo yalifanywa kwa siri kubwa, hali iliyopelekea vinara wengine wa NASA kulalamika walidai walifaa kuhusishwa,” anasema.

“Japo Wakenya wote wanakubali mkutano kati ya Raila na Uhuru ulipoesha joto la kisiasa nchini kufuata utata uliotokana na pande zote mbili zinafaa kutoa mwongozo utakaotumiwa kuendeleza mazungumzo kuhusu masuala yaliyoorodheshwa kwenye taarifa yao ya pamoja,” Bw Andati anasema.

 

Vioja bungeni

Ukosefu wa mwongozo mahususi kuhusu mwelekeo ambao ushirikiano kati Rais Kenyatta na Bw Odinga utachukua kutimiza malengo yao ndio ulichangia kioja kilichoshuhudiwa bungeni Jumanne alasiri.

Mbunge wa Mavoko Patrick Makau (Wiper) aliamua kuketi kwenye kiti kilichotengwa mahsusi kwa kiongozi wa wachache, Bw Mbadi. Alisema alichukua hatua hiyo baada ya kile alichodai kuwa “hatua ya ODM  kujiunga na Jubilee baada ya Raila kama kiongozi wake kuelewana na Rais Kenyatta.”

“Baada ya ODM kujiunga na Jubilee chama change cha Wiper ambacho ndicho cha tatu kwa ukubwa kimeniteua kuwa kiongozi wa wachache. Hii ndio maana niliketi katika kiti hicho,” aliwaambia wanahabari baada ya Spika Justin Muturi kumfurusha nje kwa kukaidi amri ya kumtaka ampishe Bw Mbadi.

Mwenzake wa Makueni Daniel Maanzo pia aliamua kukalia kiti cha Bw Junet (kiranja wa wachache) kwa sababu hiyo hiyo ya ODM kujiunga na Jubilee. Hata hivyo, aliondoka upesi kabla ya kuadhibiwa na Spika Muturi.

“Kwa sababu Raila, kama kiongozi wa ODM, hakuwahusisha wenzake; Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya) katika mkutano wake na kiongozi wa Jubilee, Rais Kenyatta, tunaamini kuwa amejiunga na Jubilee. Hii ndio maana niliketi katika kiti cha Junet na mwenzao Makau akaketi katika kiti cha Mbadi,” anaeleza Mbunge huyo ambaye ni wakili.

Bw Maanzo anasema Wiper itaunga mkono mazungumzo yatakayoendeshwa chini ya mpangilio “unaoeleweka na kuwekewa mihimili ya kesheria” na kujumuisha wadau wote.

 

‘Hakuna nusu mkate’

Ni  ufasiri aina hii uliomsukuma Bw Duale kufafanua kuwa mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga haumaanishi kwamba kuna mipango ya kubuniwa kwa serikali ya mseto kati ya Jubilee na ODM.

“Hakuna nusu mkate hapa. Na chama cha ODM hakijamezwa na Jubilee kama inavyodaiwa. Sisi kama Jubilee tunataraji ODM kupiga msasa utendakazi wa serikali huku ikishirikiana nasi kusukuma ajenda ya maendeleo kwa manufaa ya Wakenya,” anasema.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini anashauri vyama tanzu katika NASA kukoma kumkaripia Bw Odinga kwa kufuatua uamuzi wake wa kufanyakazi pamoja na Rais Kenyatta.

“Viongozi hawa wawili wameamua kuzika tofauti zao kwa ajili ya kuliunganisha taifa. Wiper, Ford Kenya na ANC ambao ni wenye hisa wadogo katika NASA wanapaswa kuheshimu uamuzi huu wa ODM,” anasema.

Kwa upande wake mchanganuzi wa masuala ya kisaisa Bw Odoyo Owidi anasema kukanganyikiwa huku kwa wanasiasa kunaweza tu kuondolewa ikiwa afisi kuu iliyobuniwa kushirikisha mazungumzo hayo itaanza kufanya kazi na kwa uwazi.

“Wakili Paul Mwangi na Balozi Martin Kimani walioteuliwa kuongoza afisi hiyo, kwa ushirikiano na washauri wengine, wanafaa kuanza kazi. Na watatekeleza majukumu yao kwa uwazi la sivyo hali hii ya wanasiasa kuendelea kurusha cheche za maneno huku na kule bado itaendelea,” anasema, akionya kuwa huenda hali hiyo ikavuruga malengo ya muafaka huu.

“Huu mkutano wa jumba la Harambee ulikuwa ni wa watu wawili. Sisi kama Wiper hauutambui wala kufahamu yaliyojadiliwa,” anasema.

Kauli yake inaungwa mkono na naibu kiongozi wa ANC Bw Ayub Savula ambaye anasema vyama tanzu ndani ya NASA viko tayari kuipa ODM “talaka” kwa kushirikiana na Jubilee.

JAMVI: Tetesi za vinara wa NASA kukutana kisiri na Ruto zilivyoyeyusha misimamo mikali

MKUTANO wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga wiki iliyopita ulianza kuandaliwa hata kabla ya hafla ya kumuapisha Bw Odinga kama “rais wa wananchi” mnamo Januari 30.

Imefichuliwa kuwa wawili hao walianza kuzungumza moja kwa moja  kwa simu na kukutana mara kadhaa kwa siri kuweka mikakati ya kuzika tofauti zao.
Duru zinasema kuwa mazungumzo ya wawili hao kushirikiana yalianza punde tu baada ya uchaguzi wa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26 mwaka jana ambao Bw Odinga alisusia.

Juhudi za kuwapatanisha wawili hao ziliendelezwa na mabalozi, viongozi wa kidini na Umoja wa Mataifa, japo baadhi ya washirika wa kisiasa wa viongozi hao walishikilia misimamo mikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, alikiri kwamba shirika hilo lilimtuma aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obassanjo kuwapatanisha viongozi hao.

Imefichuliwa kuwa muafaka wao ulicheleweshwa kwa kuwa awali, kulikuwa na kutoaminiana.

“Kulikuwa na kutoaminiana hasa baada ya Bw Odinga kujiapisha kama rais wa wananchi. Hata baadhi ya washauri wa rais ambao hawakuwa wakifahamu mazungumzo hayo walitaka akamatwe kwa kujiapisha nao wale wa Bw Odinga hawakutaka mazungumzo.

Baadhi walitaka aunde serikali mbadala. Hii iliweka breki mazungumzo ambayo yangekamilika mapema Januari,” alisema mmoja wa waliohusika  kwenye mazungumzo hayo ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Inasemekana kuwa, wawili hao walikuwa wakizungumza kwa simu na hata kukutana usiku mara kadhaa baada ya marudio ya uchaguzi wa urais kufuatia shinikizo za jamii ya kimataifa.

 

Walivyozika tofauti

Kabla ya mkutano wa Ijumaa wiki iliyopita, walikutana katika nyumba ya afisa mmoja mkuu wa Mahakama ambapo waliamua kutangaza kuzika tofauti zao.

Watu wa familia zao na wazee wa jamii za Waluo na Wakikuyu pia walitekeleza wajibu muhimu kwenye mazungumzo hayo hadi viongozi hao wawili wakaamua kuacha tofauti zao za kisiasa na kushirikiana.

Mchango wa balozi wa Amerika Robert Godec pia ulitajwa kuwa mkubwa kupatanisha mahasimu hao wa kisiasa ambao tofauti zao zilizidi baada ya uchaguzi wa mwaka jana ambapo Raila anadai alipokonywa ushindi.

“Kwamba walitangaza kupatana saa chache kabla ya aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Amerika, Rex Tillerson kuwasili Kenya ilichukuliwa kwamba Amerika na jamii ya kimataifa ilihusika kuandaa muafaka huo,” asema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Geff Kamwanah.

Anasema muafaka huo ulimfaidi Bw Odinga ambaye uhusiano wake na jamii ya kimataifa ulikuwa umedorora tangu alipojiapishwa kuwa rais wa wananchi.

Duru zinaeleza kuwa, ni walipokutana kisiri mara ya mwisho katika nyumba ya afisa mmoja wa mahakama mtaani Karen ambapo waliafikiana kushirikiana na kukubaliana kuweka wazi uamuzi wao.

 

Kuepuka kulemaza mazungumzo 

Waliopanga mikakati ya kuwapatanisha wawili hao walihisi kwamba kuwashirikisha washauri wao wa kisiasa walio na misimamo mikali kungekwamisha mazungumzo.

Waliamua kuacha nje wanasiasa wenye misimamo mikali wakiwemo  vinara wenza wa Bw Odinga na naibu rais William Ruto. Hata hivyo, japo vinara wenza wa NASA Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula wamesema wazi kwamba hawakuhusishwa kwenye mazungumzo hayo, Bw Ruto hajasema wazi hakuyafahamu.

Wanamikakati hao walihisi kwamba,  mvutano kati ya serikali na upinzani ulikuwa hatari kwa uchumi na usalama wa nchi, hasa serikali ilipoanza kuwaandama viongozi wa upinzani.

Raila aliandamana na binti yake Winnie, wakili Paul Mwangi na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed naye Rais Kenyatta aliandamana na balozi Martin Kimani.

 

Siri

Imebainika kuwa mazungumzo ya simu kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta yaliwekwa siri chini ya usimamizi wa mkurungenzi wa ujasusi Philip Kameru ambaye inasemekana alitekeleza wajibu muhimu kupatanisha wawili hao.

Kulingana na duru za kuaminika, ni Bw Kameru aliyemshauri Rais Kenyatta kutomkamata Bw Odinga alipojiapishwa kuwa rais wa wananchi.

Kukubali kwa Bw Odinga kushirikiana na Rais Kenyatta kulichochewa na tetesi kwamba, vinara wenza katika NASA, ambao walisusia hafla ya kumuapishwa, walikuwa wakizungumza na Bw Ruto kuunda muungano wakilenga uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya kuhisi kwamba chama cha ODM cha Bw Odinga kilipanga kujitenga na muungano huo.

Wadadisi wasema hatua ya wawili hao kupatana itabadilisha mwelekeo wa kisiasa nchini katika siku chache zijazo.

“Kwa sasa, huenda ni vinara wenza wa NASA wanaolalamika lakini ukweli ni kwamba,  muafaka wa Raila na Uhuru utayumbisha Jubilee,” alisema Bw Sila Tirop, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

JAMVI: Mkataba wa Raila na Uhuru wazalisha mayatima wa kisiasa

Na WYCLIFFE MUIA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga kutangaza ushirikiano mpya inatishia mustakabali wa wanasiasa wengi walionuia kufaidi na mzozo wa mara kwa mara kati ya viongozi hao wawili.

Wachanganuzi wanakubaliana kuwa, mkutano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulipangua pakubwa mipangalio ya sasa ya kisiasa na italazimu baadhi ya viongozi katika pande zote kujitathmini upya la sivyo, watakufa kisiasa.

Kwa mujibu wa wataalamu wa kisiasa, waathiriwa wa kwanza kabisa wa umoja wa vinara hao ni Naibu Rais William Ruto na vinara wenza wa upinzani Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

Juhudi za Bw Musyoka kutaka rais kumpa sikio zinaonekana kugonga mwamba huku matumaini yake ya kupata uungwaji mkono wa Bw Odinga kuwania urais 2022 yakisalia kitendawili.

Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga tayari kimethibitisha ushirikiano wake na serikali ya Jubilee na kumtaka kiongozi wao (Bw Odinga) asiyumbishwe na walio na azma ya kuwania urais 2022.

Wakili Kamotho Waiganjo anasema, kuna kila sababu ya Bw Musyoka na Bw Mudavadi kuwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu ni bayana macho yote yako 2022 na mkutano wa rais na Bw Odinga unazika Mkataba wao wa kisiasa wa 2017 ambapo chama cha ODM kilikubali kutoteua mgombeaji wa urais 2022 na badala yake, kuunga mmoja wa wagombeaji wa vyama tanzu.

“Iwapo mkutano wa rais na Bw Odinga ni mwanzo wa serikali nyingine ya muungano, bila shaka vigogo kadhaa wa kisiasa wanaathiriwa. Kuna uwezekano wa kuchipuka kwa miungano mingine ya kisiasa inayohusisha wanasiasa ambao hawadhirishwi na umoja wa vinara hao wawili,”anasema Bw Waiganjo.

Bw Waiganjo anahisi kuwa, japo Bw Ruto ana uungwaji mkono wa 2022 wa chama cha Jubilee, anapaswa kufuatilia kwa makini uhusiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Kulingana na mhadhiri wa masuala ya kisiasa Herman Manyora, shida kubwa ya kisiasa inayorudisha taifa hili nyuma, ni usaliti wa kisiasa na rais pamoja na Bw Odinga wanaweza kuleta suluhu.

 

Historia ya usaliti

“Shida kuu hapa ni usaliti wa kihistoria. Shida hii ilianza pale Mzee Jomo Kenyatta alipomruka Jaramogi Odinga, mtindo huu ukaendelea baada ya Mwai Kibaki kusaliti maafikiano yake na Raila.

Kisha Uhuru akaonekana kukandamiza demokrasia ambayo ingemwezesha Raila kutimiza ndoto yake ya kuwa rais. Mkutano wao uliashiria mwisho wa usaliti huo,”anasema Bw Manyora.

Kulingana na Bw Manyora, ili kutatua shida hii, sharti wanasiasa kadhaa watolewe kafara pamoja na ndoto zao za kisiasa.

Bw Manyora anahisi kuwa umoja huu utampa rais mandhari mazuri ya kutekeleza ahadi zake za maendeleo pamoja na kuunda wosia wake wa kisiasa naye Bw Odinga huenda akagawiwa mamlaka.

“Inawezekana kuwa si kweli lakini nahisi kuwa kuna mpango wa kuhakikisha Raila ameonja urais. Huu mjadala unasikia kuhusu mabadiliko ya katiba ni kuhakikisha Bw Ruto hajaachwa nje,”anasema Bw Manyora.

Katika miaka mitano iliyopita, Bw Ruto amekuwa akiunda himaya yake ya kisiasa, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kumrithi Rais Kenyatta mnamo 2022.

 

Mke mwenza’ 

“Lazima Bw Ruto atambue sasa ndoa yao na rais imepata mke mwenza hali ambayo huenda ikabadilisha kabisa mipango ya urithi wa urais,”anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Edward Kisiang’ani.

Prof Kisiang’ani anahisi kuwa, Bw Ruto ni yatima mkubwa wa Jubilee na mustakabali wake wa kisiasa utategemea jinsi atakavyohusiana na Bw Odinga.

Kwa upande wa NASA, MaBw Musyoka, Mudavadi na Seneta Wetangula huenda wakalazimika kusahau ndoto zao za kuwa rais, iwapo  Bw Odinga atasisitiza kuwania urais tena 2022.

“Tayari umesikia baadhi ya viongozi wa Jubilee wenye misimamo mikali kama (Adan) Duale na Seneta (Kipchumba) Murkomen, wakimsifu Bw Odinga na kumtaja kama kiongozi mwenye uzalendo mkubwa. Wanafahamu vyema kuwa yeye ndiye atakayeunda siasa za 2022,” anaongeza Prof Kisiang’ani.

Kando na Duale na Murkomen, Prof Kisiang’ani anahisi kuwa Seneta wa Tharaka Nithi Kindiki Kithure vilevile ni yatima wa umoja huu ikizingatiwa kuwa alikuwa ametangaza wazi kuwa anataka kuwa mgombea mwenza wa urais wa Bw Ruto ifikiapo 2022.

 

Onyo

Tayari Prof Kindiki ameonya kuhusu uhusiano wa Bw Odinga na Jubilee akisema Waziri huyo Mkuu wa zamani ni ‘mtaalamu’ wa kisiasa na huenda akavuruga kabisa mpangilio wa 2022 wa chama hicho.

Iwapo Bw Musyoka na wenzake katika NASA watajumuishwa katika mkataba wa rais na Bw Odinga, viongozi walioazimia kuwania urais 2022 wataathiriwa sana kisiasa.

Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho na mwenzake wa Machakos Dkt Alfred Mutua watalazimika kutathmini upya mipango yao ya kisiasa ya 2022 kwa sababu hawatawania ugavana kwa awamu ya tatu.

Wengine ambao hatima yao haijulikani iwapo Bw Odinga atajiunga na serikali ni Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na mwenyekiti wa chama cha Jubilee Raphael Tuju.

Dkt Matiang’i amekuwa akitoa maagizo yaliyoonekana kuwahangaisha viongozi na wafuasi wa upinzani huku Bw Tuju akitunukiwa nyadhifa zilizolenga kujumuisha jamii ya Luo.

Kando na wanasiasa, wanablogi, mabwenyenye wanaofadhili wanasiasa na vyombo vya habari vitakuwa na wakati mgumu baada ya joto la kisiasa kutulia kufuatia umoja wa rais na Bw Odinga.

TAHARIRI: Mafuriko ya sasa yawe funzo kwa umma na serikali

Na MHARIRI

MAAFA na uharibifu wa mali unaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa humu nchini.

Kufikia Jumamosi, zaidi ya watu 20 walikuwa wameripotiwa kufariki kutokana na mafuriko katika kaunti tofauti tofauti.

Aidha, hiyo Jumamosi magari saba ya kifahari yaliharibiwa baada ya kuangukiwa na miti katika hoteli ya Serena.

Japo Gavana wa Nairobi Mike Sonko aliomba radhi kutokana na hali hiyo, kunahitajika juhudi zaidi ili watu wasiwe wakitatizika wala kupoteza maisha au mali yao wakati wa mvua.

Katika taarifa yake ya kuomba msamaha, Gavana Sonko alimlaumu mtangulizi wake Dkt Evans Kidero kwa matumizi mabaya ya Sh10 bilioni zilizotengwa kutengeneza mabomba ya njia za maji jijini.

Ni vyema Bw Sonko aelewe kuwa huu si wakati wa kulaumiana. Anapaswa kufanya kazi na fedha alizo nazo na kuachia taasisi husika kuchunguza ubadhirifu anaodai ulitekelezwa.

Serikali za kaunti na wakazi wa maeneo mengine ambako mvua inaendelea kunyesha, wanapaswa kuhifadhi maji ya mvua ili kuepuka upungufu wa maji baada ya misimu ya mvua kuisha.

Itakuwa aibu sana kwa wakazi kuanza kuhangaika wakitafuta maji, wakati mamilioni ya tani za maji zinaendelea kupotea wakati wa mvua.

Mbali na mafuriko, ni vyema wananchi wawe makini kwa sababu mvua inayoendelea kushuhudiwa inaweza kusababisha maradhi kutokana na uhaba wa maji safi na salama pamoja na kuwapo kwa mfumo hafifu wa majitaka hususan katika miji.

Ni vyema serikali itoe tahadhari kwa wadau wa sekta ya uvuvi, kilimo, mifugo, chakula na wanyamapori wafuate maagizo ya watabiri wa hali ya hewa. Kuwa na ufahamu wa mapema kutasaidia kujipanga kukabiliana na hali hiyo bila kukurupushwa.

Tahadhari hiyo pia inapaswa kutolewa kwa wachimbaji madini katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Tunaamini kwamba pamoja na kuomba Serikali na taasisi zake kuchukua tahadhari, wananchi nao pia wanapaswa kuacha kufanya shughuli kwenye mikondo ya maji kama vile ujenzi.

Aidha, ni muhimu ikumbukwe kwamba Idara ya Hali ya Hewa imesema kuwa mvua itaendelea kunyesha na hivyo basi ni muhimu kwa wananchi pamoja na serikali kuhakikisha wameshirikiana ili kupunguza maafa ya watu na uharibifu wa mali.

Je, ni nembo ya ‘usaliti’ kwa Raila kumkumbatia Uhuru?

Na BENSON MATHEKA

Kwa ufupi:

 • Kuna hisia kuwa Bw Odinga ni mtu mbinafsi, asiyeweza kuaminika na lengo lake ni kuwatumia watu kuafikia malengo yake ya kisiasa na kisha kuwatema
 • Wanaodai Bw Odinga aliwasaliti vinara wenzake wanasema kwamba, matukio ya hivi punde ni historia inayojirudia katika maisha yake ya kisiasa
 • Mkutano wake na Bw Kenyatta umefananishwa na 2001 alipounganisha chama chake cha NDP na KANU ambapo aliingia serikalini kwa mara ya kwanza 
 • Peter Mathuki anasema japo Odinga amepigania demokrasia, uamuzi wake wa kujitenga na vinara wenza na kuzungumza na Rais Uhuru unamsawiri kama msaliti

HATUA ya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, ya kujitenga na vinara wenza katika muungano wa NASA na kuamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, imeibua tena nembo ya “msaliti” ambayo imekuwa ikimuandama katika vipindi tofauti vya maisha yake ya kisiasa.

Hisia za wanasiasa na wafuasi wa vyama vya Wiper, Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya ni kuwa, Bw Odinga ni mwanasiasa mbinafsi, asiyeweza kuaminika na lengo lake ni kuwatumia watu wengine kuafikia malengo yake ya kisiasa na kisha kuwatema.

Kwa baadhi yao, Bw Odinga alichukua hatua hiyo ili kukwepa mkataba wa maelewano wa NASA, kwamba hatagombea urais 2022 na badala yake angeunga mmoja wa vinara wenzake.

“Usinitaje jina, lakini unaweza kuweka amana kauli hii; Bw Odinga anataka kukwepa mkataba wa NASA kwa sababu hakuwa, na hana nia ya kuunga vinara wenza 2022. Hivyo ndivyo alivyo na ndivyo amekuwa kwa miaka mingi,” anasema mbunge mmoja wa chama cha ANC na mshirika wa miaka mingi wa Bw Odinga.

Hata hivyo, wafuasi wa Bw Odinga wanaamini Bw Odinga ni mzalendo na kila hatua anayochukua ni kwa manufaa ya Wakenya. Wakereketwa wa chama cha ODM wanamtaja kama kiongozi jasiri asiyekosea katika kila hatua anayochukua na wameapa kumuunga mkono katika ushirikiano wake mpya na Rais Kenyatta.

“Nimesema mara nyingi kwamba, baba hawezi kukosea na nitarudia kusema hivyo.  Raila amejitolea mhanga kupigania demokrasia na haki za binadamu katika nchi hii na anajua afanyalo,” asema mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Homa Bay, Gladys Wanga.

Hata hivyo, wanaodai Bw Odinga aliwasaliti vinara wenzake, Kalonzo Musyoka ( Wiper), Musalia Mudavadi ( ANC) na Moses Wetangula( Ford Kenya) wanasema kwamba, matukio ya hivi punde ni historia inayojirudia katika maisha yake ya kisiasa.

Wanasema hatua yake kumbukumbu ya alivyotofautiana na aliyekuwa makamu wa rais Michael Kijana Wamalwa 1994 muda mfupi baada ya kifo cha baba yake, Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa wakati huo kiongozi wa chama cha Ford Kenya.

Bw Wamalwa alirithi uongozi wa chama hicho kutoka kwa Jaramogi lakini kwenye uchaguzi wa viongozi, alimshinda Bw Odinga ambaye alihama na kujiunga na chama cha National Development Party (NDP).

 

1997

Kushindwa kwake na Bw Wamalwa kulimnyima tiketi ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 1997. Katika NDP, alipata tiketi na kugombea urais lakini akawa wa tatu nyuma ya Rais Daniel Moi wa KANU na Mwai Kibaki wa chama Democratic Party.

Kutofautiana kwake na Bw Wamalwa ambaye alikuwa mwanasiasa muungwana kulimsawiri kama mwanasiasa mwenye tamaa ya uongozi ambaye hangekubali kuongozwa hata katika chama cha kisiasa na ndivyo ilivyo hadi wakati huu.

Mkutano wake na Bw Kenyatta umefananishwa na uamuzi aliochukua 2001 wa kuunganisha chama chake cha NDP na KANU ambapo aliingia serikalini kwa mara ya kwanza alipoteuliwa waziri wa Kawi.

Kulingana na wadadisi, japo lengo lake lilikuwa ni kupata tiketi ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2002 Moi alipokuwa akistaafu, yeye na wanasiasa wengine walipigwa kumbo Moi alipoamua kumuunga Uhuru Kenyatta.

Aliungana na wanasiasa wengine wa Kanu akiwemo Bw Musyoka, marehemu George Saitoti na Joseph Kamotho kupinga uamuzi wa Moi wa kuwataka wamuunge Bw Kenyatta ambaye walimchukulia kuwa limbukeni wa kisiasa wakati huo.

 

‘Kibaki Tosha’

Alivikwa nembo ya msaliti 2002 kwa kumtangaza Mwai Kibaki kuwa mgombea urais wa muungano wa upinzani  wa Narc siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo bila kushauriana na wanasiasa wenzake kwenye tamko maarufu la “Kibaki Tosha.”

Mdadisi wa siasa George Okwaro asema kwa kutamka Kibaki tosha, Odinga hakuwashauri wenzake na alionyesha kuwa mtu asiyetegemewa katika miungano ya kisiasa.

“Tamko hilo liliwakasirisha baadhi ya wanasiasa waliokuwa kwenye upinzani  na ukikumbuka baadhi yao, akiwemo Simeon Nyachae waliamua kujitenga na Narc na kugombea urais,” alisema Bw Okwaro.

“Kumbuka wakati huo, Bw Musyoka pia alikuwa na azima ya kugombea urais na kama wanasiasa wengine alihisi kusalitiwa,” aliongeza.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2007, Raila alikuwa ametofautiana na Bw Kibaki na akaungana na wanasiasa wengine, akiwemo Bw Musyoka, Musalia Mudavadi na William Ruto kuunda chama cha ODM ambacho kilisajiliwa na watu wengine na wakalazimika kusajili ODM-K. Chama hicho kilikumbwa na misukosuko

 

Siasa si urembo

Bw Musyoka alitaka akabidhiwe tiketi ya urais ambayo Bw Odinga alimezea mate. Walitengana na Bw Odinga alipomweleza Bw Musyoka kwamba, siasa sio mashindano ya urembo mtu akabidhiwe tiketi kwa sababu ya kuwa na sura nzuri.

Kupitia juhudi na weledi wa siasa wa Bw Ruto, Raila alikomboa ODM alichotumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 uliokumbwa na utata naye Bw Musyoka akagombea kwa tiketi ya chama cha ODM- K ambacho alibadilisha kuwa Wiper Democratic Movement.

Kwenye  uchaguzi mkuu wa 2013, aliungana na Bw Musyoka na Bw Wetang’ula kuunda  muungano wa Coalition for Restoration of Democracy (CORD) na akateuliwa mgombea urais huku wakikubaliana kuwa angemuunga Bw Musyoka kwenye uchaguzi wa 2017. Hata hivyo, mambo yalibadilika Bw Mudavadi alipojiunga nao kubuni muungano wa NASA na Odinga akakabidhiwa tiketi kwa ahadi kuwa ingekuwa mara yake ya mwisho kugombea urais.

Kulingana na mkataba wa maelewano, kama NASA ingeshinda, Odinga angeongoza kwa kipindi kimoja na kumuunga Bw Musyoka au Bw Mudavadi. Hata hivyo, baada ya kushindwa na Rais Uhuru Kenyatta inaonekana alibadilisha nia na kuamua kwenda kinyume na matarajio ya wenzake.

Katibu mkuu wa chama cha Wiper Peter Mathuki anasema japo Odinga amepigania haki na demokrasia katika nchi hii, uamuzi wake wa kujitenga na vinara wenza na kuzungumza na Rais Uhuru unamsawiri kama msaliti.

 

SHAIRI: Siasa nimekuacha, kwaheri tutaonana

Ni tafakari ya babu, au kichwa cha gazeti?

Nayatafuta majibu, kwalo hili swali nyeti,

Kenya ina maajabu, ukifanya utafiti, 

Siasa nimekuacha, kwaheri tutaonana.

 

Majuzi mulisikika, mukifoka kwa hasira,

Sote tukaghadhibika, kuitaka haki bora,

Kumbe hadithi za paka, kukimbizana na chura,

Siasa nimekuacha, kwaheri tutaonana.

 

Tulowaamini ndio, watudandanya mchana,

Walivileta vilio, wenyewe tukatengana,

Leo hii hao hao, mikono wanapeana!,

Siasa nimekuacha, kwaheri tutaonana.

 

Wapiganapo fahali, nyasi huikosa kinga,

Ulipozuka muhali, tulicharazwa mapanga,

Amani ikawa ghali, sawa na bei ya unga,

Siasa nimekuacha, kwaheri tutaonana.

 

Mpendwa dada na kaka, keti chini tafakari,

masikio toa taka, wasije tena tughuri,

Sote tuipe talaka, siasa iso na Kheri,

Siasa nimekuacha, kwaheri tutaonana.

 

Na KHASIM AHMED, Mombasa

DOMO KAYA: Muacheni Bahati na ya kwake, hayawahusu ndewe wala sikio

Na THOMAS MATIKO

ACHA niwaambieni kitu leo. Simpendi Bahati hilo nalo siwezi kukuficha. Ila sina kinyongo wala chuki naye.

Simpendi kwa nini? Kwa sababu dogo kalewa ustaa. Ana dharau na majivuno sifa ambazo sikutegemea kabisa angelikuwa nazo. Ila naelewa zilipomkutia, mara tu baada ya kuwa staa na kuanza kushika pesa.

Zamani wakati akiwa hana kitu, akiwa ni yatima, akiwa anaishi kwenye makao ya Childrens Home, naambiwa hakuwa hivi, alikuwa ni mnyenyekevu na mstaarabu.

Nilitokeaje kutompenda lakini? Pengine kwako wewe itakuwa ni kwa sababu ndogo tu ila kwangu hali ni tofauti.

Mara kadhaa nimejaribu kumhoji, hasa kwa simu lakini jamaa mara zote aniyeyusha, au atanikatia simu au ataahidi kupiga lakini haijawahi tokea.

Mpaka wa leo mahojiano hayo hatujawahi kuyafanikisha na niliishia kukataa tamaa, sio lazima nimwandike. Dogo ana dharau sana mwanzo kama hamna mazoea.

Nakumbuka akininyima nukuu ya stori fulani niliyokuwa nikimbizana nayo na keshoye akawapa masela wake tofauti wakachapisha. Ila haina neno acha tuishi hivyo.

Licha ya masaibu yangu na huyu dogo, sijawahi kumtakia mabaya katika maisha yake. Juzi kumeibuka tetesi kwamba huenda yule mtoto Heaven aliyempata majuzi na mkewe aliyemzidi umri kinoma Diana Marua, sio wake.

Tetesi zimedai kuwa Bahati alishuku yule mtoto atakuwa ni wa mchepuko na hivyo kuamua kumfanyia vipimo vya DNA chini ya maji na baada ya kupata majibu, nyumbani kwao kukawa hakukaliki.

Bahati baadaye alijitokeza na kucharukia kinoma mabloga waliochapisha hiyo stori. Aliwaomba wamwache yeye na mke wake na mwanawe. Kikweli japo simpendi huyo dogo, katika hili la familia nimejikuta nikisimama naye.

Hata kama ni lazima ‘headlines’ ziuze sio kwa dizaini hii jamani. Nazungumza kama mwandishi na pia mwanafamilia. Unapozuga kwa stori kama hizi ili uuze ‘headlines’ wakati huna ushahidi wa unachokiandika maana yake nini?

Tujifunzeni kuheshimu familia za mastaa hawa jinsi nasi tunavyopenda zetu ziheshimiwe. Hata kama kweli yule mtoto sio wa kwake, nafahamu ni stori tamu lakini kama huna ushahidi mbona uchapishe uvumi kwa malengo ya kumuumiza mtu?

Sisemi kwamba sio kweli lakini mpaka sasa hamna ushahidi wa uhakika au udokezi unaoashiria hivyo jamani.

Diana sio kwamba naye mzuri kwa sababu nafsi yangu inanifanya kusadiki kuwa ni muhuni. Ndiye aliyemtongoza Bahati, wajua.

Wakaja wakaanza kuitana ‘prayer partner’ Lakini kikubwa zaidi Diana toka mahusiano yake ya zamani ameonekana kuwapenda watu maarufu, watu ambao sura zao hazikosekani kwenye TV.

Kabla ya Bahati, alikuwa akitoka na mtangazaji wa michezo wa runingani ndio akaja kuangukia huyu dogo na sasa unacheki anavyompelekesha mbio.

Lakini pamoja na yote, naamini naye anahitaji amani yake amlee huyo mtoto mchanga ambaye ndio mwanzo ana wiki tatu. tujifunzeni kuwa na utu hata kwa maadui wetu jamani.

Uandishi mwingine wa kizushi kama huo unachomea picha waandishi wengine wanaojielewa. Kama mimi hivi. Ama ni namna gani my frens’!