KINA CHA FIKIRA: Ujeuri wa mpapai hujeruhi na udhalili wa unyasi huokoa

Na WALLAH BIN WALLAH

KILA mwanadamu ana hulka au tabia tofauti.

Wapo wenye tabia za upole, unyenyekevu na heshima.

Pia wapo wenye tabia za ujeuri, ukali, hasira na kiburi!

Watu wenye sifa za ujeuri na kiburi hujisifu wakidhani ati ujeuri ni ushujaa!

Wanasahau kwamba kujisifu au kusifiwa kwa kufanya vitendo vya ujeuri, ukatili na kiburi ni kashfa wala si sifa njema!

Hawakumbuki methali zisemazo, ‘Kwa shujaa huenda kilio, kwa mwoga huenda kicheko; na kiburi si maungwana?’

Unyenyekevu na heshima huambatana na woga! Mtu mtiifu mwenye nidhamu huwa mwoga!

Kamwe hajipigi kifua hadharani na kujigamba au kujionyesha kiburi chake kama sokwe dume!

Chunguza nukuu za vitabu vya dini zote wanasema, ‘Ogopa Mungu wako!’

Yaani uwe mnyenyekevu na mtiifu kwa Mungu wako! Woga ni heshima! Hapo ndipo nilipopata ari na hamasa ya kuandika kauli ya leo katika Kina cha Fikira!

Babu yangu Mzee Majuto alikuwa mkulima na mfugaji maarufu.

Shambani kwake kulikuwa na mpapai mkubwa uliozaa mapapai mengi makubwa! Karibu na mpapai huo kulikuwa na nyasi ndefu zilizostawi kuwa chakula cha ng’ombe wake!

Siku moja jioni mawingu mazito meusi yalitanda ghafla angani! Mara upepo mkali ukaanza kuvuma na ngurumo za radi kurindima kuashiria mvua kubwa!

Hatimaye mvua kubwa ya theluji ikaanza kumwagika! Watu wote wakajifungia ndani ya nyumba zao. Nyasi zile ndefu zilizokuwa karibu na mpapai zikalala chini ardhini kwa kuogopa hasira za upepo na kani za mvua kubwa! Lakini mpapai ule mkubwa ulisimama tu kwa kiburi na ujeuri bila kuogopa wala kuinama kuepuka dhoruba ya mvua!

Mvua ilipozidi kumwagika na upepo kuvuma zaidi, mpapai ulivunjika matunda yake yote yakapukutika chini!

Asubuhi kulipokucha kulikuwa shwari baada ya mvua kupusa. Nyasi zile zilianza kunyanyuka taratibu na kusimama kuendelea kuishi kama kawaida!

Mpapai uliovunjika ulipoona nyasi zikisimama tena, mpapai ukafoka, “Mbona nyinyi nyasi na unyonge wenu hamkuvunjika kama mimi mpapai ilhali nina nguvu na thamani zaidi yenu?”

Nyasi zilijibu kwa upole, “Wewe mpapai umeanguka ukavunjika kwa sababu ya ujeuri wako na kiburi chako! Sisi nyasi na unyonge wetu tuliogopa upepo mkali na mvua kubwa tukanyenyekea tukalala chini kwa heshima mpaka tufani ilipoisha! Tumenusurika!”

Ndugu wapenzi, tuwe watu wanyenyekevu wenye nidhamu ili tuepuke majanga tuishi maisha marefu!

Ujeuri hujeruhi na unyenyekevu huokoa maisha! Unyenyekevu wa unyasi ndio usalama wa unyasi! Nimewaambia!!!!!

SAUTI YA MKEREKETWA: Sekta ya elimu nchini itafaidi iwapo walimu watakubali mafunzo

Na HENRY INDINDI

MJADALA umekuwepo nchini kuhusu mafunzo ya kisarifu kwa walimu ilivyopendekezwa na mwajiri wao, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).

Mwanzoni walipoitangaza nia ya kutekeleza mafunzo haya asilimia kubwa ya walimu walilalamikia hilo na kuahidi kutoshiriki.

Kilio chao kilikuwa kwenye ada za mafunzo, haja ya mafunzo yenyewe na vyuo vikuu vilivyoteuliwa kuyatekeleza. Kusema la kweli, wengi hawakujua mwanzoni kwamba hayo yaliyotangazwa yalikuwa katika sheria ya TSC.

Waliikemea Tume kwa kufanya uamuzi bila kushauriana na walimu kupitia kwa vyama vyao na kufikia sasa ni dhahiri kwamba walimu wanapinga wazo hilo.

Tutangulize kwa kusema hapa kwamba mafunzo ya kujiimarisha na kujisarifu ni muhimu hasa ikichukuliwa kwamba ulimwengu unabadilika kila uchao na mahitaji na matarajio yake vilevile.

Kwa maana hii, kila mwanataaluma katika taaluma yake anahitajika kufanya kozi mbalimbali muda baada ya muda ili aweze kuenda na uchao katika taaluma husika.

Hadharauliwi mwanataaluma yeyote anapokumbushwa kuhusu haja ya kujinoa hata zaidi ili aifae taaluma vyema zaidi katika umbo la mabadiliko yake.

Teknolojia hivi sasa ni sehemu ya maisha na ni hakika kwamba baadhi ya walimu wanahitaji kunolewa upya katika masuala haya ya teknolojia na jinsi tunavyoweza kuitumikisha kazini.

Fursa zinapopatikana kama hizi za mafunzo ya kujinoa, tuzichangamkie kama njia ya kudhihirisha kwamba tunataka kuenda na uchao katika taaluma yetu.

Isitoshe, tumeingia katika mtaala mpya wa elimu, CBC, unaowahitaji walimu kuelekezwa hata zaidi kuhusu jinsi ya kuufanikisha.

Malalamishi tuliyokuwa nayo baadhi yetu kwamba hatukuwa tumefunzwa vyema kuuwezesha mtaala huu mpya, yatashughulikiwa kwa kukubali kupokea mafunzo haya ya kisarifu.

Changamoto

Ila ninayoiona mimi itakuwa katika mchakato wa kulitekeleza hili la mafunzo.

Inawezekana litatikisa baadhi ya asasi za jamii kama ndoa hasa iwapo wanandoa hao wote ni walimu na wameenda kwa mafunzo pande mbalimbali.

Pili, ingekuwa vyema zaidi ikiwa tume ingejihimu kufanyia walimu tathmini ili kutambua udhaifu wao.

Huenda kuna walimu wanaohitaji kunyanyuliwa katika mbinu za kufundishia masomo yao pekee na pakawa na wengine ambao huenda mahitaji yao yakawa katika masomo mahususi wanayofundisha.

Tume haifai kuchukulia kwamba udhaifu na mahitaji ya walimu wote ni sawa na hivyo kuwasukumizia kila kitu katika mafunzo. Hapo hawatakuwa wamewafaa walimu.

Kuhusu vyuo vikuu vilivyoteuliwa, kuna haja ya kushauriana zaidi kuhusu ikiwa inawezekana walimu wakayapate mafunzo hayo katika vyuo vikuu vilivyo karibu nao.

Kingeteuliwa angalau chuo kikuu kimoja katika kila eneo (katika mikoa ya zamani) ili walimu wanaotoka katika mkoa huo wayapate mafunzo yao huko.

Aidha, kwa kuwa vyuo vikuu vya umma vimekuwa na kilio kuhusu uhaba wa pesa, labda hii ingekuwa mojawapo katika fursa za kuviwezesha kupata pesa.

Hata hivyo, ibainike kwamba katika Sheria hiyo ya TSC, tume ina mamlaka ya kuteua vyuo na haigizwi popote kushauriana na yeyote kulihusu suala hilo.

NDIVYO SIVYO: Ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu ‘ni’ ni ‘si’ wala si ‘sio’!

Na ENOCK NYARIKI

SIO si ukanushi wa kitenzi ‘ni’.

Tazama jinsi nilivyolitumia neno “si” baada ya “sio”.

Vinginevyo, ningeshawishika kusema: ‘…kitenzi kikanushi sio ‘sio’ ukanushi wa kitenzi’.

Nitairejelea kauli hii ili kuifafanua zaidi ila kwanza ni muhimu kueleza kuwa ‘ni’ ni kitenzi kishirikishi kipungufu.

Dhana vitenzi vishirikishi hutumiwa kwa maana ya vitenzi vinavyoshirikisha vitu mbalimbali kihali, kitabia au kimazingira.

Navyo vitenzi vishirikishi vipungufu haviwezi kuchukua viambishi vya wakati ingawa hakika vinaweza kuchukua viwakilishi nafsi-viambata na viambishi ngeli.

Kinyume cha vitenzi vishirikishi vipungufu ni vitenzi vishirikishi vikamilifu. Mahali fulani hapa juu tumetaja dhana ‘viwakilishi nafsi-viambata’.

Dhana hii itaeleweka vyema baada ya kufafanua maana ya ‘viwakilishi nafsi’.

Viwakilishi nafsi ni maneno kamili au viambishi vinavyosimamia nomino za viumbe vyenye uhai hususan binadamu.

Mimi, wewe, yeye ni viwakilishi nafsi huru kwa kuwa ni maneno yanayojisimamia na yanayoleta maana ilhali ‘ni-’, ‘u-’, ‘a-’ ni viwakilishi nafsi-viambata kwa sababu haviwezi kuleta maana mpaka vitumiwe au kufuatwa na maneno mengine.

Ukanushi wa sentensi “Mimi ni daktari wa mifugo” si “*Mimi sio daktari wa mifugo”.

Tena tazama matumizi ya ‘si’ – ambayo imetangulia kiwakilishi nafsi huru ‘mimi’. ‘Sio’ ni wingi wa ‘siye’. Maneno yote mawili yaani; siye na sio, yako katika hali kanushi.

Siye ni ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu ndiye.

Kwa mfano, ukanushaji wa sentensi, “Yeye ndiye aliyetuletea habari hizo’’ ni “Yeye siye aliyetuletea habari hizo’’.

Ningependa kueleza kwamba si kosa kutumia ndi- pamoja na O-rejeshi katika sentensi moja.

Kosa hilo litatokea iwapo mzizi amba- utatumiwa pamoja na O-rejeshi katika sentensi moja.

Hata hivyo, pasi na kutumia kiwakilishi nafsi huru katika sentensi tuliyoitaja hapa juu, bado maana itajitokeza wazi.

Pengine athari ya pekee itakayojidhihirisha ni kuondolewa kwa msisitizo. Kwa njia nyingine, tunaweza kusema: ‘Ndiye aliyetuletea habari hizo’ – sentensi hii ikawa na maana sawa na ile tuliyoitaja hapo juu.

Siyo nao ni wingi wa silo. Kwa mfano, sentensi “Jambo hili silo nililolitarajia’’ katika wingi itakuwa “Mambo haya siyo tuliyoyatarajia.”

‘Sivyo’ ni neno linalotumiwa kupinga kilichosemwa. Mfano: ‘Hivi sivyo ulivyotuambia jana’.

Neno hilo pia ni wingi wa ‘sicho’. Alhasili, ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu ‘ni’ ni ‘si’ bali si ‘sio’ jinsi baadhi ya watu wanavyokitumia.

Tunasema: Yeye si mjinga; Mimi si daktari; Hili si jibu sahihi; bali si: *Yeye sio mjinga; *Mimi sio daktari na kadhalika.

GWIJI WA WIKI: Dennis Mwima

Na CHRIS ADUNGO

MAISHA huisha. Kabla yaishe, yaishi yaishe. Usiishi kuisha.

Maisha ni safari ambayo mwisho wake ni siri kubwa isiyojulikana kwa binadamu!

Japo utajikwaa, kuteleza na mara nyingine kuanguka katika safari ya maisha, usiogope kitu! Jinyanyue upesi, futa vumbi, pangusa tope na utimke tena. Kuanguka ndiko kuinuka!

Nidhamu, bidii na uvumilivu huchangia pakubwa mafanikio ya mtu. Huwezi kabisa kujiendeleza maishani au kitaaluma iwapo hujiamini. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta!

Usitamauke unapokosa kufaulu. Mtangulize Mungu, endelea kukazana na hatimaye milango ya heri itajifungua yenyewe!

Huu ndio ushauri wa Bw Dennis Mwima almaarufu ‘Mwalimu wa Ulimwengu’ – mwandishi mzoefu wa vitabu ambaye kwa sasa anafundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Providence Academy, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Dennis alizaliwa na kulelewa katika eneo la Butere, Mumias, Kaunti ya Kakamega. Ndiye mwanambee katika familia ya Bw Washingtone Mwima na Bi Sarah Faluma.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Shinamwenyuli, Butere mnamo 1996. Ni katika shule hiyo ambapo hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ilianza kujikuza ndani yake.

Mara si haba, alijipata akiiga sauti za wanahabari maarufu na akapendwa na watu kutokana na ‘sauti yake ya utangazaji’.

Baadhi ya wanahabari aliowaiga ni Jilani Wambura, Leonard Mambo Mbotela na marehemu Billy Omalla.

Kati ya walimu waliotambua utajiri wa kipaji cha Dennis katika utangazaji wa habari na kumpa majukwaa maridhawa ya kukuza na kupalilia talanta yake ni Bw Atita, Bi Susan Kageha na Bw Andrew Were Nyangweso waliomfundisha katika shule ya msingi.

Wengine waliopanda na kuotesha mbegu za utashi wa Kiswahili ndani yake ni Bi Stella Angufu na Bi Agnes Sungu waliotangamana naye kwa karibu sana katika Shule ya Upili ya Musanda, Butere.

Baada ya kufanya mtihani wa KCPE mnamo 2005 kisha KCSE mnamo 2009, Dennis alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Meru (2011-2012).

Alihiari kusomea ualimu baada ya ndoto yake ya kujiunga na chuo cha uanahabari kuyeyushwa na mawimbi ya ufukara yaliyotishia kumzimia mshumaa wa elimu. Hata hivyo, anaishi kwa imani kwamba mvuto wa kipekee uliomo ndani ya mrindimo wa sauti yake utakuja kuwa kitambulisho chake atakapokuwa mwanahabari katika siku za usoni.

UALIMU

Dennis alianza kufundisha mnamo 2013 baada ya kuajiriwa na Kakamega Hill School Junior. Akiwa huko, alikutana na walimu wazoefu wa Kiswahili – Zadock Amakoye na Bw Masika – waliomkuza pakubwa kitaaluma. Alihudumu huko hadi 2015 kabla ya kuhamia Ruai Junior Schools, Nairobi.

Kutua kwake jijini Nairobi kulikuwa mwanzo wa mkoko kualika maua. Alipata fursa za kuhudhuria makongamano mbalimbali ya Kiswahili, akapevuka zaidi kitaaluma na akawa mwalimu bora.

Kabla ya kuajiriwa na Shule ya Msingi ya Providence Academy Ruaraka mnamo Januari 2021, Dennis aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Msingi ya Anas Academy (Eastleigh), Clara Academy (Ruaraka) na Total Care Academy (Pangani).

UANDISHI

Dennis alikuwa mwepesi wa kuandika hadithi bunilizi za watoto alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Insha nyingi alizozitunga chini ya uelekezi wa walimu wake zilimzolea sifa sufufu na kumfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Kufikia sasa, ameandika kitabu cha kiada ‘Kichocheo cha Kiswahili KCPE’ kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Jalada la ‘Kichocheo cha Kiswahili’. Picha/ Chris Adungo

Ametunga pia hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika diwani mbalimbali. Baadhi ya hadithi hizo ni ‘Kuku Mfanyabiashara’ katika mkusanyiko wa ‘Kasuku wa Salome na Hadithi Nyingine’, ‘Udongo wa Hekima’ katika ‘Mtoto wa Dhahabu na Hadithi Nyingine’ pamoja na ‘Ibilisi Mweupe’ katika ‘Kilele cha Mambo na Hadithi Nyingine’.

Dennis ameandika miswada mingi ya hadithi fupi na vitabu vya kiada kwa minajili ya Mtaala wa Umilisi (CBC). Nyingi za kazi hizo zipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu nchini Kenya.

‘Shauku ya Kuishi’ ni novela ambayo Dennis anaiandaa sasa kwa matarajio ya kuchapishwa hivi karibuni.

Miongoni mwa waandishi waliomshika mkono, kumpa motisha ya kujitosa ulingoni kikamilifu na kupiga mbizi katika bahari pana ya uandishi wa vitabu vya Kiswahili ni Ali Hassan Kauleni, Benard Simiyu Mkuyuni, Mathias Momanyi, Tom Nyambeka na Timothy Omusikoyo Sumba.

Wengine waliomshajiisha kukichangamkia Kiswahili kama kiwanda kikubwa cha ajira na maarifa ni Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, marehemu Profesa Ken Walibora, marehemu Sinjiri Mukuba na marehemu Eliud Shihanda Murono.

JIVUNIO

Dennis anaazimia kuvikwea vidato vya taaluma na kuwa miongoni mwa walimu na waandishi maarufu wa Kiswahili. Sawa na alivyoshikwa mkono hadi akafika alipo, naye anajitahidi kuwainua chipukizi katika sanaa ya uandishi.

Mbali na kufanya tafsiri na ukalimani, Dennis huendesha masimulizi na mijadala mingi ya kitaaluma kupitia kumbi mbalimbali za Kiswahili mitandaoni na YouTube (MwalimuTv).

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo sasa inatawala wanafunzi, wanahabari na walimu wengi ambao wametangamana naye katika makongamano anuwai ya kupigia chapuo Kiswahili.

Kwa pamoja na mkewe, Bi Violet Alividza, wamejaliwa watoto wawili – Mishie Nadia Neema na Zarina Zawadi Pendo.

CAPTION 2: Baadhi ya kazi za Mwalimu Dennis Mwima

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Lelwak

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Lelwak (CHAKILE) kiliasisiwa mwaka huu na walimu wapenzi wa Kiswahili katika shule hiyo iliyoko Kapsabet, Kaunti ya Nandi.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa CHAKILE ni kuimarisha na kuweka wazi umuhimu wa lugha ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Chini ya ulezi wa Bw Richard Ondoli Amunga, CHAKILE kwa sasa kiko chini ya uongozi wa Walter Aunga (Mwenyekiti). Vinara wengine wa chama hiki ni Steven Mwololo (Naibu Mwenyekiti), Leon Kiprop (Mhariri), Claudius Kipchirchir (Mhazini) na Ian Kipkurui (Afisa wa Uhusiano Mwema).

Madhumuni mengine ya CHAKILE ni kuboresha matokeo ya somo la Kiswahili katika KCSE, kubadilisha mtazamo hasi kwa Kiswahili, kuleta pamoja watetezi wa Kiswahili, kukuza talanta za wanafunzi katika kazi za kubuni, kustawisha matumizi ya Kiswahili Sanifu shuleni, kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kushirikiana na vyama vingine ili kuimarisha juhudi za makuzi ya Kiswahili.

Chama kwa sasa kina mikakati ya kushiriki makongamano mbalimbali ya Kiswahili kwa malengo ya kuwakutanisha wanafunzi na walimu, wanahabari na waandishi maarufu wa Kiswahili ambao watawaamshia hamu ya kukichapukia Kiswahili.

Aidha, kimetenga vipindi maalumu kila siku ya Jumatano ili kupitia gazeti la Taifa Leo hasa kijarida cha Lugha na Elimu kwa madhumuni ya kujifunza mengi kuhusu taaluma ya Kiswahili.

Katika juhudi za kufanikisha baadhi ya malengo yake, chama kimewapa wanafunzi jukwaa la kukuza vipawa vyao katika ulingo wa uanahabari. Wanachama hutafiti kuhusu baadhi ya matukio na masuala ibuka na kusoma habari hizo gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Chama pia kimezamia uchapishaji wa jarida la ‘Lelwak Times’ ambalo hutoa fursa kwa wanachama kuchangia makala ya kitaaluma na kazi bunilizi mara moja kwa mwaka.

CHAKILE pia huandaa kongamano la Kiswahili kila muhula ili kuwapana wanafunzi nafasi ya kujadili masuala mbalimbali katika somo la Kiswahili. Walimu wa Idara ya Kiswahili wakiwemo Amunga, Rosemary Jepkurgat, Aaron Lang’at, Nehemiah Kirui na Edwin Magut wanazidi kushirikiana na usimamizi wa shule kuhakikisha kuwa kuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili na nakala za magazeti ya Taifa Leo maktabani.

Wanachama wa CHAKILE hukutana mara kwa mara kujadili masuala mbalimbali kuhusu uandishi wa insha, sarufi na matumizi ya lugha, fasihi simulizi, ushairi na kuchambua vitabu vya fasihi andishi.

Chama pia kina huandaa vikao maalumu mara mbili kila muhula kwa lengo la kushirikisha wanachama katika mashindano yanayolenga kubaini upekee wa vipaji vyao katika kughani mashairi, kutamba hadithi, kutunga mashairi na kuigiza.

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Upili ya Lelwak, Kapsabet, Kaunti ya Nandi. Picha/Chris Adungo

Mlezi wa CHAKILE hutumia fursa hiyo kutuza washindi wa vitengo mbalimbali na kutoa nasaha za kuwatia wanachama motisha kuhusu safari ya usomi kwa jumla.

Kufikia sasa, manufaa ya chama hiki yameonekana kwani wanachama wengi wameendelea kufaulu vyema katika somo la Kiswahili na kuwapiku wenzao wanaodunisha Kiswahili na kuchapukia masomo mengine.

Licha ya kwamba hakijakomaa vilivyo, chama kimefaulu kufanya mengi shuleni chini ya kipindi kifupi ikiwa ni pamoja na kuandaa makongamano ya ndani kwa ndani, kuingia mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) na kuwapa wanafunzi fursa ya kuendesha midahalo wazi ili kuangazia masuala mbalimbali yanayofungamana na maendeleo ya jamii.

Uwapo wa chama hiki shuleni umeamsha ari ya mapenzi ya Kiswahili miongoni mwa wanachama ambao kwa sasa ni wazalendo na mabalozi wa Kiswahili na wasomaji wakuu wa magazeti ya Taifa Leo.

Changamoto zinazokabili CHAKILE ni pamoja na baadhi ya wanafunzi kutokionea fahari Kiswahili na ukosefu wa fedha za kuendesha baadhi ya shughuli ili kufanikisha maazimio mbalimbali ya wanachama.

Aidha, baadhi ya wanafunzi wana kasumba kuwa Kiswahili ni lugha duni na hakina umuhimu hivyo kupendelea zaidi masomo mengine kama vile Hisabati, Kemia na Fizikia. Wanafunzi wengine huchukulia Kiswahili kuwa somo rahisi lisilohitaji kutengewa muda zaidi kwa minajili ya mazoezi na marudio.

WASONGA: Vijana wahimizwe kujisajili kwa miradi ya kuwanufaisha

Na CHARLES WASONGA

NI jambo la kusikitisha kuwa ni wakati kama huu ambapo uchaguzi mkuu unakaribia ndipo wanasiasa wametambua umuhimu wa vijana katika taifa hili.

Wanasiasa hao, haswa wale wanaotaka kiti cha urais, wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kuwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kujisajili kuwa wapiga kura ili washiriki uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii ni kwa sababu inakadiriwa kuwa kati ya wapiga kura wapya 6.3 milioni ambao Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inalenga kusajili, 5.2 milioni ni vijana ambao walitimu umri wa miaka 18 kati ya 2017 na sasa.

Idadi hii ni muhimu zaidi katika kuamua mshindi katika uchaguzi wa urais katika uchaguzi huo utakaofanyika mnamo Agosti 9, 2022.

Lakini wanasiasa hawa wamedhihirisha ubinafsi katika miito yao kwa vijana wajiandikishe kuwa wapiga kura.

Hii ni kwa sababu sijawasikia wanasiasa wanaowahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi huo.

Sijawahi kuwasikia Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na wengine wanaomezea mate kiti cha urais wakiwahimiza vijana kuwania viti katika uchaguzi huo.

Hii ina manaa kuwa wanasiasa hawa wanawachukulia vijana katika watu ambao wajibu wao ni kuwapigia kura pekee na wala sio watu wanaostahiki kushikilia nyadhifa za uongozi.

Huu ni ubinafsi mkubwa.

Vijana wanafaa kushikilia nyadhifa za uongozi ili waweze kushiriki katika mpango wa utungaji sera na maongozi ya taifa hili.

Hii ni kwa sababu wao ndio huathirika pakubwa na makali ya uongozi mbaya kizazi cha sasa cha viongozi, hali ambayo imechangia wengine wao kupotoza matumaini maishani.

Ningehimiza kwamba huku wanasiasa wanapowahimiza vijana kujitokeza kwa wingi wajiandikishe kuwa wapiga kura, pia wawahimize kujiandikisha katika mipango ya serikali inayolenga kuboresha maisha yao.

Kwa mfano, vijana wahimizwe na waelekezwe kujiandikisha katika mipango ya kuwapa nafasi za ajira kama vile; Kenya Youth Employment Opportunities (KYEOP), Ajira Digital Youth Empowerment Programmes (ADYED), Presidential Digital Talent Development Youth Programmes, miongoni mwa mingine.

Mipango kama hii, inayodhaminiwa na serikali kuu, ndio inaweza kuwasaidia vijana kujiendeleza kimaisha kando na kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Wanasiasa wakome kuendeleza dhana kwamba umuhimu wa vitambulisho vya kitaifa kwa vijana ni katika kushirikisha shughuli za kisiasa pekee.

Vijana, haswa wale wanaoishi mashambani, watambue kuwa wanaweza kutumia stakabadhi hizo za utambulisho kwa shughuli nyingine nyingi za kuboresha maisha yao kando na kupiga kura.

WANGARI: Mikakati yahitajika kupunguza mzigo wa matibabu nchini

Na MARY WANGARI

IDADI ya watu wanaoandaa hafla za uchangishaji pesa za kugharamia matibabu imeongezeka pakubwa katika siku za hivi majuzi, huku mzigo wa gharama ya afya ukizidi kuwalemea Wakenya.

Iwe ni katika sehemu za ibada, kazini, makazi, mitandao ya kijamii na kwingineko, imekuwa kama ada kila uchao kupata matangazo ya kuomba msaada kuchangisha mamilioni ya fedha kugharamia malipo ya hospitali.

Uhalisia uliopo unajitokeza bayana hasa katika kizazi hiki cha utandawazi ambao umeufanya ulimwengu kuwa kijiji.

Si ajabu siku hizi mtu kujipata katika kundi zaidi ya moja katika mitandao ya kijamii anapotakiwa kusaidia kuchangisha mradi tu kusaidia familia, jamaa au marafiki waliolemewa baada ya wapendwa wao kulazwa hospitalini.

Kwa muda mrefu, mzigo wa kugharimia matibabu nchini umekuwa kero ambayo imewafilisisha raia wengi.

Familia nyingi zimelazimika kuuza mali yao yote na kutumia kila walicho nacho katika juhudi za kugharamia matibabu ya wapendwa wao hasa wanaougua maradhi sugu.

Hali pia imevurugika zaidi kutokana na janga la Covid-19 ambalo limesababisha madhara yasioelezeka kijamii na kiuchumi.

Katika baadhi ya visa vya kuvunja moyo, familia zimegubikwa na majonzi maradufu baada ya kupatwa na msiba, kisha usimamizi wa hospitali walimolazwa hasa katika hospitali za kibinafsi, kukatalia miili ya wapendwa wao.

Ndiposa umuhimu wa kuwepo mikakati kabambe ya kuwapunguzia Wakenya gharama ya matibabu hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Japo hospitali za kibinafsi huwa ghali, Wakenya hujipata hawana hiari ili kwenda huko kutafuta huduma bora za matibabu ikilinganishwa na hospitali za umma, katika juhudi za kuokoa wapendwa wao.

Serikali imepiga hatua katika juhudi za kuboresha sekta ya afya nchini kuambatana na malengo ya Afya kwa Wote (UHC).

Mfano mzuri ni kupitia mswada mpya wa NHIF unaoagiza kila mwananchi mwenye umri kuanzia miaka 18 kujisajilisha na Hazina ya Afya Nchini.

Ingawa mswada huo una vipengele kadhaa vinavyohitaji kupigwa msasa ili kuwafaidi Wakenya kikamilifu, bila shaka ni ishara njema.

Isitoshe, wiki chache zilizopita, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa ilani kwa hospitali za kibinafsi zinazotoza ada ghali kupindukia na kukatalia miili ya wagonjwa wanapoaga kabla ya kukamilisha malipo.

Ili kutoa afueni kwa Wakenya, Bunge linapaswa kubuni sheria zitakazoweka ada mahsusi inayostahili kuzingatiwa na hospitali za kibinafsi kuhusu utowaji huduma mbalimbali.

Serikali pia inafaa kutumia vyema ushuru unaokusanywa kutoka kwa wananchi kuimarisha huduma za afya katika vituo vya umma.

Hii ni kupitia ukarabati wa miundomsingi, kuboresha utowaji huduma za afya, kuhakikisha kuwepo kwa dawa za kutosha na vifaa vya kisasa vya matibabu.

TAHARIRI: Vijana wapewe vitambulisho upesi

KITENGO CHA UHARIRI

SHUGHULI ya usajili wa wapigakura kitaifa ilianza jana ambapo Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inalenga kusajili zaidi ya Wakenya milioni nne.

Usajili huo ukifanikiwa, Kenya itakuwa na jumla ya angaa wapigakura milioni 24 bila kuzingatia awamu nyingine ya usajili inayotarajiwa kufanyika Januari 2022.

Je, idadi hiyo itafikiwaje bila kuwawezesha vijana ambao ndio wengi wanaolengwa katika usajili huu?

Zaidi ya asilimia 90 ya wanaotazamiwa kusajiliwa ni vijana.

Changamoto kuu ambayo imejitokeza kuhusu kufaulisha azimio la kusajili angaa wapigakura milioni nne wanaolengwa mwezi huu wa Oktoba ni ukosefu wa vitambulisho.

Hii ni kwa sababu shughuli ya vijana kupewa vitambulisho imeanza siku chache zilizopita, hali inayomaanisha kuwa haitakuwa rahisi kusajiliwa kama wapigakura katika usajili wa mwezi huu kwa sababu shughuli hizo zote mbili zinaenda sambamba.

Vitambulisho huchukua angaa mwezi mmoja kabla ya kuwa tayari kuchuliwa na waliotuma maombi ya kupewa.

Katika muda huo wa kusubiri, vijana hupewa stakabadhi ya kuonesha kuwa wanangoja kupewa vitambulisho kamili.

Haieleweki ni sababu gani serikali, katika enzi hii ya kidijitali bado inajikokota katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama vile kuwapa vijana na raia wake vitambulisho.

Wengi wao wanaoshika vitambulisho sasa wataweza tu kujisajili kama wapigakura kwenye mkumbo wa Januari.

Maadamu IEBC imelenga jumla ya wapigakura milioni saba katika mikumbo hii miwili ya usajili, basi itakuwa vigumu kufikisha idadi hiyo iwapo wengi hawatapata vitambulisho hivi kwa sasa ndipo wajisajili.

Inapozingatiwa kuwa upigaji kura ni haki ya kidemokrasia ya kila Mkenya, iwapo vijana hao hawatakuwa wamepata vitambulisho vya kuwawezesha kujisajili kwa madhumuni hayo, basi watakuwa wamenyimwa haki yao; jambo ambalo si zuri.

Mbali na vijana, IEBC inahitajika kujitahidi kuhakikisha kuwa shughuli nzima ya usajili wa wapigakura imeendeshwa vyema bila hila zozote zinazoweza kutokea.

Kwa mfano, wapo baadhi ya watu ambao tayari wameanza kulalamika kuwa kuna wanasiasa fulani ambao wameanza kuhamisha wapigakura kutoka maeneo wanakostahili hadi kwenye maeneo yao kwa nia ya kujipa ushindi katika uchaguzi wa 2022.

Sharti njama kama hizo zizimwe.

PATA USHAURI WA DKT FLO: Kwa nini mjamzito huvuja damu puani?

Mpendwa Daktari,

Ni nini kinachosababisha kuvuja damu kutoka puani na kwenye ufizi ukiwa mjamzito?

Christine, Nairobi

Mpendwa Christine,

Wanawake wengi hukumbwa na shida ya kutokwa na damu puani wakati wa ujauzito na mara nyingi hali hii ni kawaida.

Lakini baadhi ya wanawake hukumbwa na wasiwasi wasijue la kufanya.

Sababu zinazochochea hali hii hutegemea na mtu binafsi.

Wanawake wajawazito kwa kawaida huwa na asilimia 30 hadi 50 zaidi ya mzunguko wa damu mwilini ikilinganishwa na watu wa kawaida.

Hii huhitajika ili kudumisha afya ya mtoto tumboni.

Baadhi ya masuala yanayochochea hali hii wakati huu ni kupanuka kwa mishipa ya kupitisha damu kwani damu inayosukumwa huongezeka wakati wa ujauzito.

Aidha kuna mafua yanayosababisha utandio kuwa mkavu na hivyo kusababisha mwasho.

Pia kuna ongezeko la homoni za estrogen na progesterone wakati wa ujauzito ambazo huongeza mzunguko wa damu mwilini.

Ongezeko hili husababisha damu kuvuja kutoka puani.

Mbali na hayo, hali hii yaweza sababishwa na kuchanua pua kwa nguvu, kwani hii husababisha mwasho na hata kutokwa na damu.

Wanawake wajawazito kwa wingi hushuhudia kufungamana kwa pua.

Ili kukabiliana na hali hii, tumia mbinu mbalimbali ili kudumisha unyevu chumbani hasa unapolala.

Pia, usichanue pua kwa nguvu hasa ukiwa na mafua. Tumia karatasi ya shashi yenye unyevu.

Kunywa maji au viowevu kwa wingi wakati wa mchana ili kunyoosha utando puani.

Aidha, tumia dawa maalum inayonyunyizwa kwenye pua au mafuta ya kujipaka ya petroli ikiwa unakumbwa na hali hii kwa wingi.

Hii itazuia kukauka kwa utando puani.

Pia usichokore pua na acha mdomo wazi unapopiga chafya ili kupunguza msukumo puani.

Pia ongeza kiwango cha virutubisho vya vitamini C kwenye mlo kwani huharakisha kupona kwa seli iwapo kuna majeraha.

Mpendwa Daktari,

Mwanangu wa kiume mwenye miaka miwili amekuwa akivuja mkojo kwa mwezi mmoja sasa.

Nimejaribu aina tofauti za dawa kutoka dukani lakini tatizo halitoweki.

Napaswa kufanya nini?

Jennifer, Mombasa

Mpendwa Jennifer,

Katika umri wa miaka miwili, watoto wengi hawajajua kwenda choo vilivyo na hata kwa wale wanaojua, ni kawaida kushindwa kujidhibiti mara kwa mara.

Masuala mengine ambayo yanaweza chochea tatizo hili ni pamoja na wasiwasi; mabadiliko ya kimazingira au matatizo ya kifamilia; dhuluma (matusi, kimwili, kimapenzi au kutelekezwa); tumbo kuvimba; kisukari; maambukizi kwenye mfumo wa mkojo; matumizi ya kafeini; usingizi wa pono au ikiwa ana matatizo ya kibofu.

Mpeleke mwanao akaguliwe na daktari kuthibitisha hali yake ya kiafya. Kuna dawa ambayo hupewa watoto wenye umri mkubwa (wa zaidi ya miaka sita).

Kumbuka kwamba dawa hii haipaswi kupewa mtoto wa miaka miwili, na unashauriwa kuipata kutoka hospitalini baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kutosha.

SHINA LA UHAI: H. pylori: Bakteria hatari wanaotesa mamilioni ya Wakenya

Na LEONARD ONYANGO

JE, umekuwa ukihangaishwa na maumivu makali tumboni kwa kipindi kirefu na kuhisi kushiba hata bila kula, kuna uwezekano mkubwa kwamba unasumbuliwa na ugonjwa wa Helicobacter pylori, al-maarufu H.pylori.

Bakteria hao wanapoingia tumboni, hushambulia ‘ukuta’ wa tumbo ambao huilinda dhidi ya kuharibiwa na asidi (nyongo) inayotumika kusaga chakula tumboni.Bakteria hao hatari hufanya tumbo kuwa na asidi nyingi hivyo kusababisha vidonda tumboni (ulcers), kuwasha kwa ‘ukuta’ wa tumbo na kansa ya tumbo (gastric cancer).

Mnamo 2015, wataalamu wa afya kutoka nchi mbalimbali duniani waliafikiana kwamba kuangamiza H.pyroli kutasaidia pakubwa katika kupunguza visa vya kansa ya tumbo ulimwenguni.

Kansa ya tumbo huchangia asilimia 6.3 ya vifo 32,000 vinavyotokana na saratani kila mwaka humu nchini.

Hiyo inamaanisha kuwa huua takribani watu 2,000 humu nchini kila mwaka.

Kati ya visa vipya 47,800 vya kansa ambavyo hubainika hospitalini kila mwaka nchini Kenya, kansa ya tumbo huwa asilimia 4.4, kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Afya.

Kansa hii ilisababisha vifo vya 769 000 kote duniani, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mnamo 2019, watu 1,058,327 walitibiwa H. pylori humu nchini, kulingana na takwimu za wizara ya Afya.

Kevin Ochola, mkazi wa mtaa wa Kibra jijini Nairobi, anasema kwamba amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo tangu 2019.

“Baada ya kuhisi maumivu tumboni kwa takribani mwezi mmoja, niliamua kwenda hospitalini lakini ugonjwa haukupatikana. Nilipewa dawa za kutuliza maumivu lakini sikupata nafuu. Januari 2020, nilirudi hospitalini ikabainika kwamba nilikuwa na H. pylori. Nilipewa tembe za kumeza kwa siku 15 na nilipopimwa tena bakteria hao walikuwa wametoweka,” anaeleza.

Mapema mwaka huu 2021, Bw Ochola alianza kuumwa na tumbo tena. Maumivu yalizidi mwezi uliopita na alipoenda kupimwa, ilibainika kwamba anasumbuliwa na H. pylori.

Naye, Alice Kariuki anasema kuwa alisumbuliwa na tumbo kwa miezi kadhaa mwaka jana hadi pale alipopimwa na kupatikana na bakteria hao.

“Nilipewa dawa nyingi na nilinunua kwa bei ghali. Nilimeza dawa chache tu maumivu yakaisha na ninashukuru Mungu nilipona,” anasema.

Dkt Christopher Opio, mtaalamu wa afya ya tumbo katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi, anasema kuwa H.pylori huenezwa kwa kula chakula ambacho hakijasafishwa vyema na kunywa maji machafu.

Anasema kinyesi au matapishi ya mwathiriwa yanaweza kusababisha mtu kupata baketria hao.

Kulingana na Dkt Opio, wapenzi au wanandoa wanapopigana busu mdomoni na mate yao kukutana, wanajitia katika hatari ya kuambukizana H.pylori ikiwa mmoja wao atakuwa na bakteria hao.

“Hiyo ndiyo maana mwanaume akipatikana na H.pylori ni vyema mke wake pia apimwe ili tuthibitishe ikiwa ana bakteria hao au la. Mke akiwa na bakteria hao bila kupewa dawa, itakuwa kazi bure kutibu mumewe,” anasema Dkt Opio.

Dalili nyingine za ugonjwa huo ni kuhisi tumbo ‘kuchomeka’, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula na tumbo kufura.

Wataalamu wanaonya kuwa mtu anapohisi ugumu wa kumeza chakula au kukojoa na kutoa kinyesi cha rangi nyeusi, anafaa kukimbia hospitalini haraka kwani hizo ni dalili kwamba ugonjwa huo umefikia pabaya.

Utafiti uliofanywa mnamo 2015 humu nchini, ulibaini kwamba takribani asilimia 67 ya Wakenya wanaugua H.pyroli.

Dkt Opio anasema kuwa japo mamilioni ya Wakenya wana bakteria hao, ni baadhi tu ambao huwa na dalili kama vile maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kufura kwa tumbo kati ya nyinginezo.

Dkt Kimang’a Nyerere, mtaalamu wa viini na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), anasema kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanaokunywa maji machafu wako katika hatari ya kupatwa na H.pylori.

“Mnamo 2016, mimi na wenzangu tulitafiti uwepo wa H.pylori katika mito mitatu jijini Nairobi – mto Nairobi, Ngong na Mathare. Tulibaini kwamba kulikuwa na bakteria hao kwenye maji ya mito hiyo. Asilimia 90 ya watu wanaoishi karibu na mito hiyo tuliowapima, walipatikana na bakteria hao,” anasema Dkt Nyerere.

Anatabiri kwamba idadi ya visa vya H.pylori jijini Nairobi itaongezeka zaidi katika miaka ijayo.

“Hii ni kwa sababu idadi ya watu, haswa katika mitaa ya mabanda inaendelea kuongezeka. Ikiwa hatua mwafaka hazitachukuliwa kuboresha mazingira, hali itakuwa mbaya zaidi katika siku za usoni,” anasema.

Dkt Nyerere anaonya kwamba baadhi ya wagonjwa hawamalizi dawa walizopewa na daktari hivyo bakteria hao hawaishi tumboni.

“Usipomaliza dawa, kuna hatari ya kuambukizwa tena. Kutomaliza dawa si tatizo la Kenya pekee bali ni changamoto ambayo imeripotiwa kote duniani. Kutomaliza tiba kunamaanisha kwamba bakteria hao wanazoeana na dawa hivyo hazitakusaidia wakijitokeza tena,” anaeleza.

Matibabu

Dkt John Kiiru wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu nchini (Kemri), anasema kuwa si bakteria wote wa H.pylori ni hatari.

“Baadhi ya bakteria hao wanaishi tumboni bila kusababisha madhara yoyote. Mara nyingi watu wanaoenda hospitalini wakipimwa kinyesi na kupatikana na ugonjwa huu, wanapewa tembe za kukabiliana na bakteria hao. Lakini baada ya kumaliza dawa maumivu yakiendelea tu, inamaanisha kuwa huenda mgonjwa anasumbuliwa na maradhi mengine na wala si H.pylori,” anasema.

Anasema kuwa vifaa vilivyoidhinishwa kupima bakteria hao nchini Kenya, havina uwezo wa kubaini ikiwa bakteria hao wana madhara au la.

“Wataalamu wa Kemri walifanya utafiti katika hospitali za Nairobi na wakabaini kwamba kati ya wagonjwa 100 waliokuwa wanatibiwa H.pylori ni watano tu ndio walikuwa na bakteria hatari.

Hiyo inamaana kwamba wengine walikuwa na magonjwa mengine lakini wakapatiwa dawa ya H.pylori kwa sababu bakteria hao walipatikana kwenye kinyesi chao,” anaeleza.

H.pylori hutibiwa kwa kutumia viua vijasumu (antibiotics) na tembe za kupunguza asidi tumboni (antacids).

Mgonjwa hutakiwa kumeza tembe hizo kwa kati ya siku 10 na 15.

Japo vipimo na dawa za H.pylori katika hospitali za umma hutolewa bila malipo, ni ghali katika hospitali za kibinafsi.

Kwa mfano, katika hospitali ya Aga Khan, kipimo hugharimu Sh6, 000 na dawa pia zinagharimu kiasi sawa na hicho.

Kujilinda dhidi ya H pylori

Dkt Nyerere anasema kuwa usafi ni njia mojawapo ya kuepuka ugonjwa wa H.pylori“Kunawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kula ni muhimu katika kuzuia maambukizi. Epuka kula vyakula ambavyo hali yake ya usafi inatiliwa shaka na kunywa maji machafu. Kula vyakula ambavyo vimepikwa vyema,” anashauri Dkt Nyerere.

ODONGO: Kanu ina kibarua kurejelea umaarufu wake wa awali

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha Kanu bado kina safari ndefu kurejelea umaarufu wake wa enzi za utawala wa chama kimoja na miaka ya 90 hata baada ya kumteua mwenyekiti wake Gideon Moi kuwania Urais mwakani.

Wajumbe 3,000 wa Kanu mnamo Alhamisi wiki jana waliandaa Kongamano katika ukumbi wa Bomas ambapo seneta wa Baringo aliidhinishwa kugombea Urais mwaka 2022.

Wengi walinasibisha kongamano hilo na lile la 2002 ambalo liliidhinisha Uhuru Kenyatta kuwania kiti cha Urais wakati Daniel Arap Moi alikuwa akistaafu baada ya miaka 24 uongozini. Rais wa Pili wa Kenya alifariki Februari 2020.

Hata hivyo, ni jambo lisilofichika kuwa chama hicho kimesalia kigae na itabidi kijikaze kisabuni iwapo kina nia ya kurejelea umaarufu huo.

Ni vyema ifahimike kwamba wakati wa utawala wa Mzee Moi, ngome ya Kanu ilikuwa eneo la Bonde la Ufa japo chama hicho pia kilikuwa kikifanya vyema hata katika baadhi ya ngome za upinzani.

Hili lilikuwa dhahiri katika matokeo ya uchaguzi wa 1992 ambao ulikuwa wa kwanza baada ya mfumo wa vyama vingi kukumbatiwa nchini.

Bonde la Ufa lilichangia nusu ya kura ambazo Mzee Moi alipata katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa.Katika uchaguzi huo, Mzee Moi alijizolea kura milioni 1.9 huku karibu kura milioni moja zikitoka Bonde la Ufa.

Vivyo hivyo, kwenye kura ya kutetea wadhifa wake 1997, Bw Moi alijizolea asilimia 70 ya kura za bondeni huku mpinzani wake wa karibu Mwai Kibaki akipata asilimia 20 pekee.

Hata hivyo, jinsi ilivyo kwa sasa, Seneta Moi hana ushawishi mkubwa Bondeni akilinganishwa na Naibu Rais William Ruto anayeonekana kuwa kigogo wa siasa za jamii ya Wakalenjin.

Ushawishi

Ni kutokana na ushawishi wa Dkt Ruto ambapo eneo hilo lilimpigia Kinara wa ODM Raila Odinga kura kwa wingi mnamo 2007 kisha Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2013 na 2017.

Kwa hivyo, Bw Moi ana mlima mrefu wa kukwea kuhakikisha kuwa Kanu inasalia hai katika Bonde la Ufa kisha maeneo mengine ila kwa sasa itakuwa vigumu kutokana na ushawishi wa Dkt Ruto katika jamii ya Wakalenjin.

Aidha, kumezuka vigogo wa kieneo ambao wana ushawishi katika maeneo yao na kuifanya iwe vigumu sana kwa Kanu kupenya maeneo hayo kama zamani.

Kwa mfano, Kanu enzi hizi ina nafasi finyu sana ya kushinda kiti cha ubunge Nyanza au Pwani kwa kuwa wakazi wengi wanaegemea ODM.

Vivyo hivyo, ilikuwa vigumu kwa chama hicho kushinda viti eneo la Kati au Bondeni mnamo 2017 kutokana na ushawishi wa Jubilee.

Mwanzo wa kupungua kwa umaarufu wa Kanu ulikuwa baada ya uchaguzi 2002 ambapo aliyekuwa Waziri na mwandani wa Mzee Moi, Nicholas Biwott alikihama chama hicho baada ya kushindwa kumbandua Uhuru Kenyatta kama mwenyekiti 2005.

Kabla ya uchaguzi wa 2007, Dkt Ruto alikihama chama hicho na viongozi wengi kisha kujiunga na ODM huku Rais Uhuru Kenyatta pia akibanduka mnamo 2012 na kubuni TNA kisha kuacha chama hicho kigae tu.

Katika uchaguzi mkuu ujao, Kanu inaweza kuongezea idadi ya wabunge wake 10, maseneta wawili na gavana ila kurejelea umaarufu wake wa enzi za utawala wa chama kimoja na miaka ya 90 ni kibarua kigumu.

FAO yahimiza vijana wawe mstari wa mbele katika shughuli za kilimo

Na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Chakula na Kilimo (FAO-UN) limewahimiza vijana kukumbatia shughuli za kilimo-biashara ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt Qu Dongyu amesema changamoto zinazozingira sekta ya kilimo zitaangaziwa ipasavyo endapo nguvu mpya itajumuishwa katika mtandao wa uzalishaji chakula.

Alisema hayo wakati akizungumza kupitia kikao cha mtandao, kufuatia kongamano la Kimataifa la Chakula linaloendelea na lililoanza Ijumaa, Oktoba 1.

Dkt Qongyu alisema maendeleo katika sekta ya kilimo yatashuhudiwa kwa kuzindua mikakati tofauti, ikiwemo kushirikisha vijana katika shughuli za kilimo na ufugaji.

Aidha, alieleza haja ya kuwa na ubunifu ili kuboresha sekta ya kilimo na uzalishaji wa chakula, kila familia ulimwenguni iwe na maisha bora.

“Athari za janga la Covid-19, mabadiliko ya tabianchi, wadudu na magonjwa zimechangia uhaba wa chakula unaotukumba. Tunapaswa kutathmini masuala kwa kina.

“Kwa kujumuisha nguvu mpya, vijana watasaidia kuleta mabadiliko makubwa,” Dkt Dongyu akafafanua, akisema mkondo huo utasaidia kuimarisha mambo.

Huku vijana wengi ulimwenguni wakilalamikia kutohusishwa katika maamuzi ya maendeleo ya nchi wanazotoka na pia katika uongozi, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema haja ipo kuwapiga jeki, akitaja mchango na ubunifu wao hasa katika masuala teknolojia na kidijitali kama vigezo na nguzo muhimu kuboresha sekta ya kilimo na uzalishaji wa chakula.

“Vijana ndio matumaini ya siku zijazo. Wana mtazamo wa kuleta maendeleo,” Dkt Dongyu akasisitiza.

Kikao hicho kilichopeperushwa kupitia mtandao wa Zoom pia kilihudhuriwa na wadauhusika, akiwemo Bi Fabiana Dadone ambaye ni Waziri wa Masuala na Mikakati ya Vijana Italia.

Bi Dadone alieleza Imani yake kwa vijana kusaidia kulinda mazingira na kuangazia mabadiliko ya tabianchi.

Kongamano la Chakula Duniani (World Food Forum) linaloendelea na la kwanza kushirikisha vijana, pia linatumia sanaa kufanya hamasisho na kutoa mchango na ubunifu kuboresha sekta ya kilimo.

Limeandaliwa Rome, Italia na linaendelea hadi Oktoba 5, 2021.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo yameibuka na mikakati maalum kushirikisha vijana katika sekta ya kilimo, ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula.

“FAO – Kenya tunatambua mchango wa vijana katika kilimo. Tumezindua miradi mbalimbali kwa ushirikiano na serikali, na kuwapa vijana motisha kushiriki na kuendeleza shughuli za kilimo.

“Hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kufufua mpango wa 4K Club shuleni ni afueni kwa taifa ili kukuza na kushirikisha vijana katika sekta ya kilimo. Utasaidia kuiboresha na kuongeza chakula,” akasema Hamisi Williams, Naibu Mwakilishi FAO-Kenya.

Juni 2021, Rais Kenyatta alifufua mpango wa 4K Club, kuanza kutekelezwa katika shule zote za msingi na upili nchini.

Mwezi Julai, Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya aliongoza hafla ambapo shule 10 katika Kaunti ya Nairobi zilipokea miche 10, 000 ya mboga kutoka kwa Ubalozi wa Israili hapa Kenya.

WASONGA: Chiloba, wenzake wasaidie IEBC kufanikisha kura 2022

Na CHARLES WASONGA

UTEUZI wa waliokuwa maafisa wanne wa ngazi za juu katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kushikilia nyadhifa kuu katika asasi zitakazohusika na uchaguzi mkuu wa 2022 ni mtihani mkubwa kwao.

Ezra Chiloba, Emmaculate Kassait, James Muhanji, na Anne Nderitu watahitaji kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi mkubwa ili kuondoa lawama zilizoelekezwa kwao kuhusiana na dosari zilizokumba chaguzi za 2013 na 2017, waliposhikilia nyadhifa za juu katika IEBC.

Bw Chiloba, ambaye alikuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mawasiliano Nchini (CA).

Anatarajiwa kutekeleza wajibu mkubwa katika uchaguzi huo kwa sababu asasi hiyo inatwikwa jukumu la kuhakikisha kuna mawasiliano ya masafa ya 3G na 4G katika vituo vyote vya kupiga kura nchini na hivyo kuiwezesha IEBC kutuma, haswa matokeo ya uchaguzi wa urais hadi kituo cha kitaifa cha ujumuishaji bila matatizo yoyote.

Tayari mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amelalamika kuwa kuna maeneo ya humu nchini ambayo hayajafikiwa na masafa ya 3G ambayo watategemea kupeperusha matokeo ya uchaguzi.

Ikumbukwe kwamba hitilafu katika upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais kutoka jumla ya vituo 11,500 vya upigaji kura ndio mojawapo ya sababu zilizochangia kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo 2017.

Hatua hiyo ilitumbukiza taifa hili katika lindi la taharuki ya kisiasa na hasara baada ya IEBC kuamuriwa irudie uchaguzi wa urais.Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Wapigakura katika IEBC Emmaculate Kassait ambaye aliteuliwa kuwa Kamishna wa Data Novemba 2020, anasimamia data muhimu kuhusu uchaguzi mkuu kama vile idadi ya watu nchini.

Ni wajibu wa Bi Kassait kuhakikisha kuwa data zote kuhusu Wakenya ni salama na haziingiliwi wala kuvurugwa kwa njia yoyote.

Kwa upande mwingine, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika IEBC James Muhati ndiye Afisa Mkuu Mtendaji wa Huduma Kenya.

Katika idara hii, Bw Muhati anasimamia miongoni mwa mengine data zilizoko katika stakabadhi za utambulisho kama vile vitambulisho vya kitaifa vitakavyotumika katika shughuli za usajili wa wapiga kura wapya unaoanza leo na upigaji kura mnamo Agosti 9, 2022.

Kwa upande wake Bi Anne Nderitu ambaye zamani alihudumu kama afisa wa mafunzo kuhusu Masuala ya Uchaguzi katika IEBC ndiye Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Afisi yake ina wajibu mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu ndiyo inasajili vyama vipya na kuidhinisha miungano ya kisiasa.

Miungano hiyo ambayo inaendelea kubuniwa itakuwa kiunga muhimu katika kuamua mgombeaji wa urais atakayeshinda katika uchaguzi.

Bi Nderitu pia ndiye anasimamia orodha ya wanachama wa vyama vya kisiasa na ambayo itatumika katika michujo ya vyama hivyo kuelekea uchaguzi huo mkuu.

Kwa hivyo, kwa mtazamo wangu, ufanisi wa uchaguzi mkuu ujao utategemea zaidi utendakazi wa maafisa hawa wanne ambao zamani walihudumu katika IEBC.

Japo wengine wao walielekezewa lawama kuhusiana na dosari mbalimbali zilizotokea walipokuwa wakihudumu katika tume hiyo, sasa wanayo nafasi ya kujitakasa kwa kufanya kazi mzuri katika asasi hizi muhimu wanazozisimamia wakati huu.

TAHARIRI: Vijana wajisajili wasikike 2022

KITENGO CHA UHARIRI

IDADI kubwa ya watu wanaolengwa katika shughuli ya usajili wa wa wapigakura kwa wingi inayoanza leo, ni vijana.

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya 2019, takribani vijana milioni 6 wamehitimu umri wa miaka 18 kuanzia Agosti 2017 hadi sasa. Hiyo inaamana kwamba vijana waliokuwa watoto waliokuwa na kati ya umri wa miaka 13 na 17 katika uchaguzi wa 2017 sasa wamehitimu kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Katika uchaguzi wa marudio wa urais wa Oktoba 26, 2017, Rais Kenyatta alishinda kwa kura milioni 7.4 milioni. Hiyo inamaana kwamba iwapo vijana hao wote milioni 6 watajitokeza kusajiliwa kuwa wapigakura na kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao, watakuwa na usemi mkubwa katika kuamua kiongozi wa tano wa Kenya.

Takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zilionyesha kuwa asilimia 51 ya wapigakura katika uchaguzi wa 2017, walikuwa vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 35. Iwapo vijana hao wote milioni 6 watajisajili basi asilimia ya wapigakura vijana itaongezeka hadi asilimia 65.

Kati ya vijana 3,428 waliowania viti mbalimbali vya kisiasa ni 314 tu walioshinda ilhali wao ndio wapigakura wengi.

Kwa miaka mingi, vijana wamekuwa wakilalama kwamba wameachwa nje katika masuala ya uongozi. Vijana wamekuwa wakilalamika kwamba wamechoka kuambiwa kuwa wao ni viongozi wa kesho.

Ikiwa kweli vijana wamechoka kuambiwa kwamba wao ni viongozi wa kesho, hawana budi kujitokeza kwa wingi na kusajiliwa kuwa wapigakura.

Inasikitisha kusikia baadhi ya vijana wakiapa kwamba hawatapiga kura kwa sababu hawajaona viongozi waliochaguliwa awali wakileta mabadiliko. Wakati wa kuleta mabadiliko ambayo vijana wanahitaji ni sasa. Mabadiliko hayaji kwa kulalamika bali kwa kupigakura ambayo ni haki ya kidemokrasia kwa kila Mkenya ambaye amehitimu umri wa miaka 18 na zaidi.

Vijana wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha watu ambao hawajasajiliwa kuwa wapigakura kwenda kujisajili.

Vijana wanafaa kuongoza juhudi za kuhakikisha kuwa vitambulisho vya kitaifa ambavyo havijachukuliwa katika afisi za usajili wa watu vinapelekewa wenyewe ili wasajiliwe kuwa wapigakura.

WARUI: Wazazi watumie fursa ya likizo kunasihi watoto wao

Na WANTO WARUI

VISA vya utovu wa nidhamu na vile vya wanafunzi kutaka kujitoa uhai vimekuwa vingi sana siku hizi.

Huku visa vya kujitoa uhai kwa watu wazima vinasababishwa na mambo mawili makuu: umaskini na mapenzi, kwa wanafunzi huenda ni matatizo tofauti kabisa.

Baadhi ya mambo yanayopelekea wanafunzi kujipata katika hali hizi mbaya ni pamoja na kujiunga na vikundi vya marafiki wabaya, kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kutokuwa na kazi maalum nyumbani na zaidi ni kukosa ushauri nasaha kutoka kwa wazazi wao.

Wanafunzi wengi hasa walio katika shule za malazi huwa na muda mfupi sana wa likizo wa kuwa na wazazi wao.

Kuna wale wazazi ambao huwa wanaenda kazini asubuhi na mapema kisha kurudi jioni au usiku kabisa.

Hawa hawapati muda mwafaka wa kuweza kuzisoma tabia za wana wao hasa zile geni.

Wanafunzi wanapokuwa pamoja hushiriki katika mambo tofauti shuleni au popote pale walipo.

Kuna mambo mema na mengine yasiyo mema ambayo huwa wanajadiliana.

Miongoni mwa wanafunzi hao, kuna wale huathirika na mambo mabaya na hatimaye kujipata wakiyatenda.

Haya ni pamoja na kujikuta wakianza kutumia dawa za kulevya, kutazama filamu mbaya ama hata kujiingiza katika mapenzi ya kiholela.

Ni jukumu la kila mzazi kuweza kutenga muda maalum ili ajadiliane na mwanawe kuhusu mambo ambayo yanaweza kumharibia maisha yake ya baadaye.

Kwa mfano, mwanafunzi anaporudi nyuma katika matokeo yake ya masomo mwisho wa muhula, haitoshi tu mzazi kuambiwa kuwa mtihani ulikuwa mgumu.

Kuna sababu nyingi tu ambazo husababisha matokeo mabaya kwa mwanafunzi.

Baadhi ya mambo ya utovu wa nidhamu yanaweza kuonekana madogo tu na kupuuziliwa mbali hatimaye yawe mwiba usiong’oleka.Hii ndiyo sabau wazazi wanastahili kuwa macho sana na yale yote yanayoendelea katika maisha ya wana wao.

Wakati mwingine visa vya utovu wa nidhamu vinaweza kuibuka kutoka shuleni.

Endapo tabia mbaya zipo shuleni na hazijakabiliwa na uongozi wa shule ipasavyo, patakuwa na uwezekano mkubwa zikaenea hata kwa wale wanafunzi wazuri wasio na kinga ya ushauri kutoka kwa wazazi.

Ni muhimu sana kwa kila mzazi ambaye ana mtoto shuleni kuchukua fursa hii ya likizo aweze kumhoji mwanawe na kuchunguza kama ameingilia mienendo isiyofaa ili kama atagundua mambo yasiyofaa kwa mtoto aweze kukabiliana nayo mapema.

Matatizo mengi yanayowapata watoto siku za baadaye hutokana na wazazi kukosa kurekebisha makosa madogo madogo mapema yanapojitokeza nyumbani ama kukosa muda wa kujadiliana na watoto ili wawajue vyema.

Bila shaka usipoziba ufa utajenga ukuta.

UDAKU: Jicho kali la nje laponza kocha mwenye tamaa ya fisi

Na CHRIS ADUNGO

IMEFICHUKA kwamba jicho kali la nje ndicho kiini cha kocha Paul Riley kupoteza posho aliyokuwa akipokezwa na klabu ya North Carolina Courage.

Riley, 58, alipigwa kalamu wiki iliyopita kwa madai ya kuwadhulumu kimapenzi vipusa wa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake Amerika (NWSL).

Madai dhidi ya mkufunzi huyo raia wa Uingereza yaliwekwa wazi kupitia taarifa iliyochapishwa na gazeti la The Athletic Alhamisi iliyopita.

Kufichuka kwa habari hizo kulichochea Shirikisho la Soka Amerika kumpokonya Riley leseni ya ukocha na kupendekeza atimuliwe mara moja.

Riley alizaliwa jijini Liverpool, Uingereza, na akaanza taaluma ya ukufunzi nchini Amerika mnamo 1986.

Anatuhumiwa kulazimisha wanasoka wa kikosi chake kumfungulia mizinga ya asali nyakati mbalimbali.

Ripoti ya The Athletic ilichapisha maelezo ya baadhi ya wachezaji walioungama kuwahi kudhulumiwa kimapenzi waliponolewa na Riley, ambaye alihudumu katika ligi ya NWSL tangu 2014.

Miongoni mwa vipusa hao ni Mana Shim na Sinead Farrelly, aliyewahi kutiwa makali na Riley kambini mwa Philadelphia Independence (2011), New York Fury (2012) na Portland Thorns (2014-2015).

“Riley alivutiwa sana na warembo wenye ghuba kubwakubwa na maziwa yaliyosimama tisti vifuani. Ilitokea kwamba nilikuwa katika kundi la vidosho hao, na alilimenya tunda kwa lazima kwa mara ya kwanza mnamo 2011,” akaeleza Farrelly kwenye mahojiano na The Athletic.

Riley amesimamia vikosi kadhaa vya soka ya wanawake nchini Amerika tangu 2006.Ingawa amekana madai hayo, Shim ameungama kuwa kocha huyo aliwahi pia kumtambalia mara kadhaa kati ya 2019 na 2020.

“Ilinichukua muda kugundua kwamba alikuwa akiwania buyu la karibu kila mchezaji kikosini, na kila aliyemnyima aliozea benchi,” akasema.

Kidosho mwingine aliyeviziwa na Riley kambini mwa North Carolina Courage aliripoti tukio hilo kati ya Aprili na Julai mwaka huu, japo alitaka isalie kuwa siri.

“Tumebana jina lake sababu tunaheshimu haki zake na tunatambua kwamba suala hili limemwathiri kisaikolojia,” ikasema The Atheltic na kukiri kuwa Riley alimbaka mchezaji huyo katika hoteli moja ya kifahari jijini Los Angeles.

“Alinijia baada ya juhudi za kumlaza kipusa mwenzangu kikosini kuambulia pakavu. Alichovya asali kwa lazima na muda haukupita kabla yake kudandia mwanafasheni mwingine maarufu raia wa Amerika,” aliungama kichuna huyo.

Kikosi cha North Carolina Courage kimepongeza wanasoka wake kwa ujasiri wa kufichua uozo wa Riley na kuahidi kushirikiana na vinara wa NWSL kuendeleza uchunguzi zaidi.

MBWEMBWE: Guu la kushoto la Mahrez linazidi kumvunia dhahabu

Na CHRIS ADUNGO

RIYAD Karim Mahrez, 30, ni winga matata raia wa Algeria ambaye kwa sasa anasakata soka ya kulipwa kambini mwa Manchester City – mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Alijitosa katika ulingo wa soka akivalia jezi ya kikosi cha AAS Sarcelles nchini Ufaransa, kabla kusajiliwa na klabu ya Quimper mnamo 2009.

Alichezea timu hiyo msimu mmoja pekee akahamia Le Harve kwa miaka mitatu.Ilikuwa hadi Januari 2014 ambapo Mahrez aliingia katika sajili rasmi ya Leicester City.

Akawa sehemu ya kikosi kilichoshindia klabu hiyo taji la Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship) mwishoni mwa mwaka huo, na hivyo kufuzu kwa kipute cha EPL.

Mwishoni mwa msimu 2015-16, Mahrez alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka nchini Algeria. Alituzwa pia taji la PFA la Mchezaji Bora wa Mwaka na akatiwa katika Kikosi Bora cha Mwaka cha PFA, baada ya kuongoza waajiri wake kunyanyua ubingwa wa EPL.

Mwaka 2018 sogora huyo mwenye guu kali la kushoto alijiunga na Man-City. Alisaidia klabu hiyo kushinda ufalme wa EPL, Kombe la FA na taji la EFL Cup katika msimu wake wa kwanza ugani Etihad.

Ingawa alizaliwa Sarcelles nchini Ufaransa, Mahrez aliteua kuchezea timu ya taifa ya Algeria iliyomwajibisha kwa mara ya kwanza mnamo 2014.

Aliwakilisha kikosi hicho kwenye Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil kisha Kombe la Afrika (AFCON) 2015, 2017 na 2019.

Algeria walinyanyua ubingwa wa AFCON mnamo 2019 nchini Misri chini ya unahodha wa Mahrez, aliyetawazwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuwa Mchezaji Bora wa Afrika 2016.

Babake Mahrez, Ahmed, alikuwa mzawa wa Algeria wa eneo la Beni, Snous katika wilaya ya Tlemcen naye mamake ana usuli wa Algeria na Morocco.

Babake Mahrez aliwahi kucheza soka nchini Algeria na aliaga dunia kutokana na mshtuko wa moyo Mahrez akiwa na umri wa miaka 15 pekee.

UKWASI

Mahrez yuko katika kundi la tatu la masogora wanaodumishwa kwa mshahara mnono zaidi ugani Etihad.

Ujira wake wa Sh78 milioni kila mwezi unawiana na ule wa Rodrigo Hernandez na Aymeric Laporte.

Wanasoma kwa karibu migongo ya Ilkay Gundogan, Bernardo Silva na Fernandinho Luis Roza.

Wanasoka wanaotia mfukoni kiasi kikubwa zaidi cha mshahara kikosini Man-City ni Kevin De Bruyne, Raheem Sterling na Jack Grealish.

Akiwa Leicester, Mahrez alikuwa akitia mfukoni mshahara wa Sh10 milioni. Kufikia mwisho wa Juni 2021, thamani ya mali ya Mahrez ilikadiriwa kufikia kima cha Sh4.6 bilioni.

Winga Riyad Mahrez wa Man-City katika mechi ya awali ugani Etihad. Picha/Maktaba

Jarida la Forbes lilimweka nambari 72 miongoni mwa masogora wanaovuna hela nyingi zaidi ulingo wa soka.

Ilivyo, fowadi huyu hupokea ujira wa takriban Sh1 bilioni kwa mwaka pamoja na nyongeza ya Sh365 milioni kwa kuwa balozi wa mauzo ya bidhaa na huduma za kampuni ya Nike.

Isitoshe, hujirinia marupurupu na bonasi tele akisajili sare au ushindi mechi za klabu na timu ya taifa au kuvuna ushindi katika vibarua tofauti kwenye ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Mahrez pia hufanya matangazo mengi kwa ajili ya kuvumisha huduma na bidhaa za kampuni mbalimbali ambazo humlipa kitita kinono kwa mujibu wa maelewano.

MAGARI

Kwa mwanasoka wa kiwango na haiba yake, Mahrez huvutiwa zaidi na michuma ya kisasa inayohusishwa na mwendo wa kasi.

Baadhi ya magari anayoyamiliki ni pamoja na Aston Martin, Ferrari F12 TDF, Audi Q9 Ferrari, Porshe na Lamborghini Gran-Turismo ambayo kwa pamoja yanakisiwa kumgharimu kima cha Sh106 milioni.Mchumba wake kwa sasa, Taylor Ward, huendesha magari aina ya Wrangler S-SUV na Range Rover ambayo yanakisiwa kumgharimu Mahrez Sh70 milioni.

MAJENGO

Moja kati ya makasri yanayomilikiwa na Mahrez nchini Uingereza ni la Sh620 milioni jijini Manchester anakoishi na familia yake. Mnamo 2017, alijinunulia jengo jingine la Sh540 milioni jijini Algiers, Algeria ambako amewekeza sana katika sekta ya kilimo, vipuri vya magari na bidhaa za utabibu.

FAMILIA NA MAPENZI

Mahrez alizaliwa katika mnamo Februari 21, 1991.

Alifunga pingu za maisha na kipusa Rita Johal mnamo 2015 na wakajaliwa mtoto wa kike mwaka uliofuata. Mnamo Juni 2019, wakiwa na watoto wawili wa kike, Mahrez na Rita walipatikana na hatia ya kutomlipa yaya wao wa awali na wakaagizwa na mahakama moja nchini Uingereza kumfidia Sh562,000.

Mahrez alianza kutoka kimapenzi na Taylor mnamo Oktoba 2020 baada ya kutemana na Rita naye kipusa huyo kutengana na mwanasoka Sergio Aguero ambaye sasa anachezea Barcelona.

Ili kudhihirisha ukubwa wa kiwango cha kukomaa kwa penzi kati yake na Taylor, 23, Mahrez alimvisha kidosho huyo pete ya almasi ambayo thamani yake inakadiriwa kuwa Sh62 milioni mnamo Juni 21, 2021.

Nyota huyo aliyepatikana na virusi vya corona mnamo Septemba 7, 2020, alipoteza vito vya thamani kubwa pamoja na kiasi kisichojulikana cha pesa mnamo Mei 2020 baada ya kasri lake jijini Manchester kuvamiwa na majambazi waliompora.

Kwa mujibu wa Rita ambaye ni mwanamuziki, hatua ya Mahrez kujiunga na Man-City ilichangia kusambaratika kwa ndoa yao.

“Mahrez ambaye awali alikuwa mnyenyekevu kiasi cha hata kuwa radhi kutumwa sokoni kununua mboga akiwa Leicester, alibadilika ghafla na kuwa jeuri baada ya kiburi cha kuvalia jezi za Man-City kumuingia kichwani,” akaungama.

“Mahrez hakuwa tena akishikika baada ya Man-City kuanza kumpokeza mamilioni yasiyohesabiki kila baada ya wiki,” akaongeza Rita, 28.

“Mahrez alikubali umaarufu umtawale. Alibadilika sana akawa haambiliki hasemezeki. Alisahau kwamba nilisilimu na kuacha maisha ya anasa – ya kunywa pombe na kutoka kimapenzi na mabwanyenye zaidi yake kwa ajili ya kudumisha uhusiano wangu naye.”

Japo walidumu katika ndoa kwa miaka saba, Rita ameshikilia kwamba Mahrez alianza kuwa na mienendo isiyoelekewa pindi baada ya kuhamia Man-City kwa Sh8.4 bilioni mnamo 2018.

Rita ambaye amewahi kuigiza katika filamu za Kingsman: The Secret Service na Cinderella alianza kumfungulia Mahrez mzinga wake wa asali mnamo 2014.

UDAKU: Ma’ Rashford mbioni kupatanisha mwanawe na mrembo Lucia Loi

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI mahiri wa Manchester United, Marcus Rashford, yu mbioni kurudiana na mchumba wake wa tangu utotoni, Lucia Loi.

Videge hao walitemana mwezi Mei baada ya kudumu katika uhusiano wa kimapenzi kwa kipindi cha miaka minane.

“Rashford hajawahi kupata utulivu tangu atengane na Lucia. Anaumia sana kimawazo tangu wakati huo. Kinachomkoroga nyongo ni hatua ya Lucia kufuta picha zao zote mitandaoni baada ya kufunganya virago kwenda zake,” akatanguliza msemaji wa familia ya Rashford, 23.

“Bila shaka walitofautiana kuhusu mambo fulani. Lakini kutengana kwao hakukuhusisha mtu yeyote. Waliachana kwa amani na sasa wanapania kurudiana sababu mamake Rashford, Melanie Maynard, amejitolea kuwapatanisha. Bado wanawasiliana. Walipendana na kustahiana sana. Wangali wachanga na walikuwa katika mwanzo wa safari ambayo ingeishia kwa ndoa,” aliongeza.

Lucia, 23, ni afisa wa mahusiano mema katika kampuni moja ya sukari nchini Uingereza.

Alikuwa nguzo muhimu katika safari ya kuimarika kwa Rashford kitaaluma hadi akawa mshambuliaji tegemeo kambini mwa Man-United na timu ya taifa ya Uingereza.

Kwa mujibu wa Melanie, ambaye amekuwa akimhimiza mwanawe kufunga pingu za maisha na Lucia, kiini cha kusambaratika kwa uhusiano wao ni presha iliyochangiwa na masharti makali, hasa ya ‘lockdown’ nchini Uingereza katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Lucia, ambaye amefanya kazi nyingi za hisani nchini Zambia na Sri Lanka, amekuwa akiunga mkono miradi mingi ya Rashford, ambaye amekuwa akipigana dhidi ya umaskini na kutetea haki za watoto kupata mlo na elimu.

Hisani hiyo ilimfanya staa huyo kupewa tuzo ya Member of the Order of the British Empire (MBE) mnamo Oktoba 2020, na akatiwa kwenye orodha ya waheshimiwa watakaokuwa wakihudhuria maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Malkia wa Uingereza.

“Japo wametengana bado kuna mapenzi ya dhati kati yao. Wanastahili kuzungumziwa na mtu atakayewaelewesha kuhusu pandashuka za kawaida maishani,” akasema mmoja wa marafiki wakuu wa Rashford aliyenukuliwa na gazeti la The Sun.

Aliongeza rafiki huyo: “Ni vizuri kwamba juhudi hizo za kuwapatanisha zimeshika kasi. Tutarajie makuu hivi karibuni kisha harusi baadaye mwaka huu au mapema mwakani.”

Rashford alianza kutoka kimapenzi na Lucia mnamo 2013 wakiwa wanafunzi Shule ya Mersey, eneo la Ashton jijini Manchester.

Sogora huyo ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto watano waliolelewa na mzazi mmoja – Melanie, katika eneo la Wythenshawe jijini Manchester.

Alianza kuvalia jezi za kikosi cha kwanza cha Man-United mnamo 2016 akiwa na umri wa miaka 18 pekee na akafunga mabao mawili dhidi ya Arsenal katika mchuano wake wa kwanza.

Miaka miwili baadaye, alitiwa kwenye kikosi kilichotegemewa na Uingereza katika fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mnamo 2018.

Lucia alihudhuria mechi zote zilizosakatwa na Uingereza kwenye fainali hizo huku akivalia jezi zilizoandikwa jina Rashford mgongoni.

Rashford alifungia Man-United jumla ya mabao 19 katika mapambano yote msimu jana.

Aliwaongoza waajiri wake kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya pili na kutinga fainali ya Europa League dhidi ya Villarreal ya Uhispania.

Rashford alirejelea mazoezi kambini mwa Man-United kwa mnamo Ijumaa iliyopita baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye bega.

Hajawajibishwa katika mchuano wowote tangu aletwe uwanjani katika kipindi cha pili kwenye fainali ya Euro 2020 iliyokutanisha Uingereza na Italia mnamo Julai 11.

DOUGLAS MUTUA: Mnyanyaso wa ngono kazini ukabiliwe

Na DOUGLAS MUTUA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limeapa kuwaadhibu maafisa wake waliowanyanyasa wanawake kimapenzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Manyanyaso hayo ya ngono yalifanyika wakati ambapo maafisa hao walikuwa katika shughuli ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kati ya mwaka 2018 na 2020.

Yaani watu walioaminiwa kuiepushia dunia nzima maafa walikuwa na muda wa kufanya mambo mengine kando na dharura iliyokuwepo! Uhayawani, au maradhi ya akili hayo?

Ripoti ya wachunguzi huru inaonyesha maafisa wa kigeni walishirikiana na wenzao wenyeji kuajiri na kufuta watu kazi kutegemea huduma ya ngono.

Mkuu wa shirika hilo, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, amekuja juu baada ya kupokea ripoti hiyo na kuapa kuwachukulia hatua kali wote waliohusika. Ameomba na msamaha.

Wapo waliofutwa kazi kwa kukataa kulala na wakuu wao kazini, na vilevile wapo walioajiriwa kwa kukubali kutoa huduma hiyo kwa wasimamizi wa mradi huo wa WHO.

Labda umezoea kusikia mambo kama haya hivi kwamba huoni kama ni hoja, ati anayetoa huduma kataka mwenyewe, lakini ni makosa makubwa sana katika dunia ya wastaarabu.

Manyanyaso ya ngono na ubakaji yapo kwenye kiwango sawa kwa kuwa katika hali zote mbili hamna hiari bali shinikizo na matumizi ya nguvu ambayo humdhalilisha mhanga.

Unapoanza kuyachukulia kuwa jambo la kawaida, basi jua ama umepotoka kupindukia au una tatizo fulani la akili linalopaswa kuchunguzwa.

Inaudhi sana unapotambua kuwa katika jamii yetu, hasa Afrika, ngono imetokea kuwa kigezo kikuu cha kuwapa watu kazi au kuwashusha madaraka kiasi cha kuzoeleka.

Hatuwezi kuendelea kuishi kama wanyama katika enzi hii ambapo dunia imeunganishwa na teknolojia na kuwa kijiji kimoja. Ni sharti tujiheshimu kwanza ili tuheshimiwe.

Ni maudhi kwa kuwa maafisa hao waliotoka mataifa ya kigeni, hasa Uropa na Marekani, hawawezi kuthubutu kufanya mambo hayo kwao kwani watafungwa jela.

Lakini walijasiria kuyafanya nchini DRC kwa kuwa walichukulia huko ni porini, mbali sana na ustaarabu waliozoea, hivyo watakwepa sheria.

Na walijua ni rahisi kufanya mambo hayo Afrika kwa maana imekuwa desturi yetu kuwadharau wanawake, si ajabu madume wenyeji walikuwa radhi kushirikiana nao.

Hili si jambo geni kwetu Kenya; wawekezaji kutoka Asia na Uropa wanajulikana kwa utundu wa kutumia ngono ili kuwatenga na kuwatawala wafanyakazi wao Wakenya.

Ngono imetumika kwa njia hiyo hata katika ofisi kubwa-kubwa. Watu waliofuzu kikamilifu wamenyimwa kazi kwa kuwa wanaowania fursa nao wamekubali kulazwa!

Hii ni kashfa ambayo inaendelea kuanzia viwandani, hasa vinavyozalisha bidhaa za kuuzwa nje, hadi ofisi kubwa zaidi nchini.

Waulize wanaume watakwambia mara nyingi tu wamenyimwa fursa na wanaume wenzao, wanawake wakapendelewa. Hawatangazi hadharani wasikose kazi kwingineko.

Ajabu akidi ni kwamba kwa jumla wanaume wengi waliowahi kuathirika hivyo huchukulia kuwa wanawake wanapenda sana kutumika hivyo. Si kweli!

Kwanza tuelewane hapa: Kuna wanawake wengi mno ambao wana heshima zao, wanapata kazi kwa sababu wamehitimu na hawapendi masihara hata kidogo.

Lakini pia kuna wengi wanaolazimika kukubali masharti hayo magumu na maovu ya kazi, ambayo kwa hakika si rasmi, bila kujua wananyanyaswa.

Wanadhani wanapendwa. Na wanataka kutoa ‘ahsante’ yao kwa kupewa fursa ya kupata unga.

Ukweli huwapambazukia baada ya kuajiriwa kwa njia hiyo, kisha baada ya kitambo kidogo wengine wanaotamanisha zaidi wanaajiriwa hivyo-hivyo na kuwahatarishia kazi.

Swali kuu: Mbona jamii imewaruhusu wanaume waovu kuendelea kuwanyanyasa wanawake na wanaume wenzao namna hii?

Ama unadhani mwanamume anayenyimwa kazi kwa kuwa mwanamke amependelewa hakunyanyaswa?

Vita dhidi ya manyanyaso ya ngono vinapaswa kuwa vya kila mtu, tena jinsia zote mbili, kwa kuwa uovu huo unaathiri jamii nzima.

mutua_muema@yahoo.com

Ni makosa UN kuzitenga nchi zilizo na misukosuko

Na WANDERI KAMAU

MIONGONI mwa masuala makuu yanayoonekana kuendelea kuangaziwa pakubwa katika Kongamalo Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), nchini Amerika, ni jinsi janga la virusi vya corona lilivyoiathiri dunia.

Wajumbe wengi waliohutubu kufikia sasa kwenye kikao hicho, kikichopangiwa kumalizika Jumatatu ijayo, wameangazia kuhusu haja ya nchi mbalimbali duniani kuungana pamoja ili kukabili athari za janga hilo.

Hata hivyo, suala kubwa ambalo kikao kimeonekana kulisahau ni kutathmini mustakabali wa kiusalama katika nchi zinazokumbwa na misukosuko ya kisiasa kama Afghanistan, Syria, Somalia, Ethipoia kati ya mengine.

Ingawa suala la corona limetikisha chumi za nchi nyingi duniani, kuna haja kubwa washiriki kutathmini mielekeo ya mataifa hayo.

Kwa mfano, taharuki iliyo nchini Afghanistan ilidhihirika wazi baada ya mjumbe aliyekuwa amepangiwa kumwakilisha aliyekuwa rais wa taifa hilo, Ashraf Ghani, kujiondoa katika dakika za mwisho mwisho kwenye orodha ya watu ambao wangelihutubia kongamano hilo.

Mtafaruku huo ulizidishwa na UN kuwanyima nafasi wajumbe wa utawala mpya wa Taliban kuhutubu.Kwenye taarifa kufuatia hatua hiyo, UN ilisema bado haiutambui utawala wa Taliban kama serikali halali iliyochukua mamlaka kwa taratibu zinazokubalika kimataifa.

Bila shaka, tofauti hizo zinaonyesha wazi kuwa kinyume na dhana zilizopo, hali nchini humo si shwari hata kidogo, licha ya wanajeshi wa Amerika kuondoka mwishoni wa Agosti.

Tayari, Taliban wameanza kurejelea baadhi ya masharti ya kiutawala waliyokuwa wakitekeleza katika serikali yao awali, kama kuwanyima wanawake nafasi za kuendelea na masomo yao.

Ikizingatiwa Afghanistan imekuwa likionekana kama ngome kuu ya makundi hatari ya kigaidi kama vile Al-Qaeda, Islamic State (IS) kati ya mengine, kuna haja kubwa UN kuangazia hali ya usalama nchini humo, badala ya kuitenga kwenye shughuli zake muhimu.

Mwelekeo uo huo ndio unaopaswa kuchukuliwa kwa nchi zote zinazokumwa na changamoto za kiusalama.Sababu ni kuwa kwa kuyatenga, UN haijifaidi hata kidogo, bali inahatarisha usalama katika nchi hizo na majirani wake.

Katika mataifa kama Somalia na Ethiopia, changamoto za kiuslama zinazoyaandama zinahatarisha uthabiti wa kisiasa katika nchi kama Kenya, Uganda au Tanzania, kwani ni majirani wake wa karibu.

Hatungependa kuona janga la ugaidi likirejea tena kwa makali yaliyoshuhudiwa awali, kutokana na ukosefu wa umoja na mikakati bora miongoni mwa nchi wanachama wa UN.Umoja pekee ndio utaiwezesha dunia kulishinda janga hilo.

akamau@ke.nationmedia.com

WANDERI KAMAU: Ughaibuni si mbinguni, huko pia kuna magumu

Na WANDERI KAMAU

DHANA kuu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu katika nchi zenye chumi za kadri ni kuwa, maisha katika mataifa yaliyostawi kiuchumi huwa bora.

Ni taswira aliyochora marehemu Prof Ken Walibora, kwenye novela ‘Ndoto ya Amerika’, inayorejelea ndoto ya kijana mmoja aliyetamani sana kwenda Amerika ili kutimiza ndoto zake maishani.

Ingawa malengo yake hayakutimia kama alivyotarajia, simulizi kuu iliyo kwenye novela hiyo ni picha halisi iliyo katika vijiji tunakotoka.Wale waliofanikiwa kusafiri na kukaa ughaibuni huonekana kama ‘miungu wadogo.’

Huwa wanachukuliwa kama watu waliopiga hatua kubwa maishani, kiasi kwamba kila mmoja anayewazunguka hutamani kusafiri ng’ambo “kuchuma mazuri yaliyo huko”.

Imani hiyo imejenga dhana mbaya miongoni mwa vijana katika mataifa hayo, kiasi kuwa wengi wao wamepoteza kabisa uzalendo kuhusu nchi zao.

Kwa sasa, kila kijana anatamani kusafiri ughaibuni kutokana na hali ngumu ya maisha iliyo katika nchi nyingi zenye chumi za kadri, hasa barani Afrika.

Hata hivyo, kile ambacho wengi wanasahau ni kuwa, kinyume na dhana hizo, maisha ya ughaibuni si rahisi kama ambavyo imekuwa ikielezwa kupitia majukwaa mbalimbali.

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya raia kutoka nchi hizo wanaosafiri Ulaya imeongezeka sana, ambapo hilo limegeuka kuwa janga kuu linaloyakabili mataifa hayo.

Mataifa kama Italia yamependekeza sheria kali ili kudhibiti idadi ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini humo kutoka Afrika na kwingineko duniani, hasa kupitia Ziwa Mediterranean.

Kila mwaka, imekuwa kawaida kwa ripoti kuibuka kuhusu mamia ya Waafrika wanaofariki katika ziwa hilo wakitumia njia za mkato kujaribu kuingia Ulaya kujiendeleza kimaisha.

Hapa Kenya, si jambo la kusikitisha tena kuhusu idadi kubwa ya Wakenya wanaotesekea katika nchi za Arabuni mikononi mwa waajiri wakatili.

Wengi wanaojipata kwenye masaibu hayo ni mabinti wachanga wanaoenda katika nchi hizo kutafuta kazi za kuwa vijakazi katika makazi ya watu matajiri.

Katika mataifa kama Amerika na Ujerumani, watu wengi wamekuwa wakilalamikia kubaguliwa kwa misingi ya rangi zao.Ni katika nchi hizo ambapo visa vya watu kuuana kwa kufyatuliana risasi huwa vinaripotiwa mara kwa mara. Wakenya wamejipata kuwa waathiriwa wa maovu hayo.

Kutokana na uhalisia huo, imefika wakati kwa vijana katika mataifa hayo kuzinduka na kufahamu kuwa maisha ya ughaibuni si “mbinguni” kama wengi wanavyoamini.Si rahisi, bali yanaandamwa na mahangaiko ya kawaida kama ilivyo katika nchi zao.

Hata hivyo, ubora uliopo katika nchi nyingi ni kwamba nyingi huwa na mifumo bora ya kiutawala, inayodhibiti sekta muhimu kama elimu, afya na masuala ya ajira.Hata hivyo, hilo halimaanishi wenyeji huwa hawafanyi kazi.

La. Wao hujituma kama kawaida ili kupata riziki zao.Hivyo, badala ya kuendelea kuhamia ughabuni “kutafuta mazuri’ yasiyokuwepo, ni wajibu wao kuamka na kuzishinikiza serikali katika nchi zao kuboresha mifumo ya uongozi na usimamizi wa sekta muhimu.

Ni kupitia hilo pekee watakapochangia uboreshaji wa nchi zao, badala ya kuendelea kuhamia ughaibuni bila kufanikiwa kutimiza ndoto zao.

akamau@ke.nationmedia.com

Chanjo ya corona ilivyo changamoto kwa wazee

NA PAULINE ONGAJI

Alipopata dozi ya kwanza ya chanjo ya virusi vya corona mnamo Aprili 23, 2021, Anne Musanga, 70, mkazi wa eneo la Makina katika kitongoji duni cha Kibera, Kaunti ya Nairobi, alidhani kwamba baada ya majuma manane kama ilivyo matarajio, angepokea chanjo yake ya mwisho na hivyo kujihakikishia usalama dhidi ya maradhi haya.

Lakini hilo halikutendeka. Kulingana naye, pindi baada ya kuchanjwa, alikumbwa na tatizo la shinikizo la damu na kuagizwa na daktari kuanza kutumia dawa mara moja.

Ripoti yake ya matibabu inaonyesha kwamba presha ya damu ilikuwa 171 dhidi ya 83 (171/83 mmhg), ishara kwamba alikuwa katika awamu ya pili ya tatizo la shinikizo la damu.Hali hii ilichelewesha dozi ya pili ambayo alifaa kupokea Juni 26, na tangu wakati huo, bado hajapata idhini ya daktari.

“Nilishauriwa kwamba nikamilishe dawa na kufanyiwa uchunguzi wa kila mara wa kimatibabu kabla ya kupata dozi ya ya pili,” aongeza.

Kwa upande mwingine, Molly Aluoch Oloo, 73, kutoka eneo la Katwekera, Kibera, asema kwamba mwanzoni alihofia kudungwa sindano hiyo kutokana na taarifa za kupotosha sio tu kuhusiana na chanjo hiyo, bali maradhi hayo kwa ujumla.

“Nusura nisipokee chanjo kabisa lakini nikabadili msimamo baada ya kushiriki katika vikao kadhaa vya uhamasisho,” aongeza.

Kwa bahati nzuri, asema, hakushuhudia athari zozote za kiafya kutokana chanjo, suala lililomfanya kujitwika jukumu la kuhimiza wazee wenzake pia kuchanjwa.

Wallace Gachau, 71, kutoka Lang’ata, Kaunti ya Nairobi, asema, kilichomsukuma zaidi kuchanjwa ni kufahamu umuhimu wake, hasa ikizingatiwa kwamba, kabla ya kustaafu mwaka wa 2006, alikuwa mfanyakazi msaidizi hospitalini.

“Aidha, nilikuwa nimejifunza mengi kuhusiana na maradhi haya, ambapo nilielewa hatari zake hasa kwa watu walio na umri kama wangu,” asema.

Naye Macfidensio Mureithi, 69, mfanyabiashara kutoka eneo la Makina, mtaani Kibera, asema ngano kibao kuhusu matatizo ya kiafya, vilevile vifo kutokana na maradhi haya, vilimhimiza kupokea chanjo.

Yeye pia alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuchanjwa nchini mwezi Machi. Hata hivyo, ari yake ya kupokea dozi ya pili mwezi Juni ilisitishwa baada ya serikali kutangaza kwamba kulikuwa na upungufu.

“Wakati wa dozi ya pili ulipokaribia, nilipokea ujumbe kutoka Wizara ya Afya nchini ukiniarifu kwamba chanjo hazikuwepo,” aeleza.

Hata hivyo, mwezi Julai serikali ilipotangaza kwamba bidhaa hii inapatikana, alienda hospitalini na akachanjwa.Kulingana na Wizara ya Afya, kufikia Septemba 1, 2021, dozi 2,807,945 za chanjo zilikuwa zimetolea nchini kote, ambapo jumla ya dozi za kwanza zilizotolewa ilikuwa 2,000,285, huku jumla ya dozi za pili zilizokuwa zimetolea ikiwa 807,660.

Dozi ya kwanza ya chanjo kwa watu waliozidi umri wa miaka 58 ilikuwa 424, 919 ambayo ni sawa na zaidi ya 21% ya jumla ya dozi za kwanza za chanjo zilizotolewa.Kwa upande mwingine, watu walio katika mabano haya ya umri waliokuwa wamepokea dozi ya pili walikuwa 240, 293, takriban 30% ya jumla ya dozi zote za pili zilizotolewa.

Aidha, kufikia wakati huo, takwimu zinaonyesha kwamba 56.6% ya walio na umri wa zaidi ya 58 waliokuwa wamepokea dozi ya kwanza, walipokea pia ya pili.Lakini japo takwimu hizi ni za kutia moyo, ni 9.3% pekee ya watu wenye umri huu waliokuwa wamepokea chanjo kamili dhidi ya maradhi haya.

Ni suala linaloibua swali kwa nini asilimia hii ni ya chini hivi? Wataalamu wanahoji kwamba kuna masuala kadha wa kadha ambayo yamesababisha watu wa umri wa zaidi ya miaka 58 kususia chanjo.Kulingana na Jude Otogo, mwakilishi shirika la HelpAge International nchini, shirika linalopigania haki za wazee, mojawapo ya sababu kuu ni umaskini.

Takwimu za shirika la HelpAge zinaonyesha kwamba ni watu wanne pekee miongoni mwa 100, wanaopokea malipo ya uzeeni hapa nchini. Hii inawaacha wengi bila mbinu yoyote ya mapato katika umri wa uzeeni.

Kulingana na Dkt Stephanie Hauck, mshauri katika kitengo cha kuzuia maambukizi hatari katika Shirika la Afya Duniani, eneo la Afrika Mashariki na Mediterania, wazee wamo katika hatari kubwa wakati huu wa janga la corona, kutokana na sababu kwamba wanawategemea wengine kimaisha.

“Hasa hali ni mbaya zaidi kwa mukadha wa Afrika ambapo wengi wao wanawategemea watoto na wajukuu zao ili kupata mahitaji ya kila siku, huku suala la marufuku ya usafiri na kujitenga yakitatiza mambo hata zaidi,” aeleza.

Bw Otogo asema kwamba hali si hali hasa kwa wanaoishi katika mitaa ya mabanda. Kwanza kabisa asema, kwa wanaoishi mbali na vituo vya kiafya, changamoto ni kupata nauli ya kusafiri ili kwenda kupokea chanjo.

“Lakini pia, wanaokumbwa na changamoto ya kiuchumi hawana muda wa kupanga foleni katika vituo vya afya kwani wakati mwingi wako katika harakati za kujitafutia mapato,” aeleza.

Hili ni tatizo ambalo limemkumba Edward Nyundo, 75, kutoka eneo la Kibera 42. Bw Nyundo ambaye ni mlinzi wa usiku hajapokea chanjo yoyote akidai anachokipa kipaumbele kwa sasa ni kufanya kazi ili kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

“Mimi hufanya kazi kama mlinzi wa usiku ambapo wakati wa mchana inanibidi nilale ili kujiandaa kuingia kazini jioni. Endapo nitachukua nafasi kwenda kupanga foleni na pengine ichukue muda mrefu, nitashindwa kwenda kazini jioni. Nitakula nini?” ahoji.

Kulingana na Dkt Willis Akhwale, Mwenyekiti wa jopokazi la usambazaji wa chanjo nchini, mwanzoni wazee hawakuwa miongoni mwa makundi yaliyopewa kipaumbele katika upokeaji chanjo, hadi wimbi la tatu lilipojiri. Lakini aongeza kwamba hili ni suala dogo.

“Tatizo kuu ni kwamba wazee hawaji hospitalini kwa sababu wanahofia wataambukizwa maradhi haya. Kumbuka kwamba hiki ni kikundi cha watu walio na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na matatizo mengine ya kiafya kama vile kisukari. Hali inakuwa mbaya hata zaidi kutokana na dhana potovu kwamba kupokea chanjo kutafanya hali yao ya kiafya kuwa mbaya hata zaidi,” aongeza.

Ni changamoto ambayo Yasmin Abdulrahman Aboyo, msimamizi msaidizi katika kituo cha wazee cha Kibera Day Care Center For The Elderly, asema, imetatiza kampeni zao za kuhimiza watu kuchanjwa.

“Tumeshuhudia visa vingi vya kuenezwa kwa hofu miongoni mwa baadhi ya watu ambao baada ya kupokea dozi ya kwanza au zote, pengine walishuhudia athari kidogo, na wametumia matatizo hayo kama visingizio vya kuwatahadharisha wenzao dhidi ya kudungwa sindano hii,” aeleza.

Dkt Hauck, asema huenda hii ikawa na athari baadaye. “Huenda mambo yakawa mabaya hata zaidi ikiwa pia vijana watasusia chanjo hii kwani wanaweza wakawaambukiza, na hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kiafya,” aongeza.

Dkt Akhwale asema hii ni changamoto ambayo itakabiliwa vilivyo kupitia elimu. “Watu wanapaswa kuelewa kwamba mara nyingi chanjo huwa na athari zake.

Lakini je, hii inamaanisha kwamba tunapaswa kususia? La hasha,” asema.Hata hivyo, kuna matumaini kwani takwimu zaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la watu zaidi ya umri wa miaka 58, wanaoendea dozi ya kwanza ya chanjo. Kwa nini?

“Mwezi Mei tulikuwa tumesitisha shughuli za kuwapa watu dozi ya kwanza, hadi waliopokea awali kukamilisha dozi zote mbili. Lakini baada ya kupokea chanjo za kutosha, shughuli hii iliendelea na imechangia ongezeko hili. Aidha, awali tulikuwa na vituo vichache vya kutoa chanjo ikilinganishwa na sasa,” aongeza Dkt Akhwale.

Pia asema kwamba hii ni kutokana na ongezeko la kampeni za uhamasishaji, suala ambalo limefanya iwe rahisi kufikia taarifa kuhusiana na corona vilevile chanjo.Bw Otogo asema pia ukosefu wa shughuli za uhamasishaji na kampeni kuwalenga wazee vimekuwa kizingiti.

“Shughuli za kiafya na kampeni kuwasaidia wazee hazipo, ikilinganishwa na makundi mengine kama vile akina mama wajawazito, watoto na walemavu. Hii ni licha ya kwamba wanajumuisha asilimia kubwa ya idadi ya watu,” asema.

Dkt Akhwale asema kwamba ili kufikia watu katika mabano ya umri huu, jopokazi la chanjo limetoa mapendekezo fulani.

“Tumependekeza matumizi ya wahudumu wa kiafya. Aidha, tumelenga shughuli za uhamasishaji miongoni mwa kikundi hiki kupitia wahudumu wa kijamii. Aidha, wanapaswa kupokea chanjo katika kliniki maalum wanapoenda kufanyiwa ukaguzi wa kawaida wa kiafaya,” aongeza.

 

|Makala haya yamefadhiliwa na mradi wa Code for Africa’s WanaData kama sehemu ya the Data4COVID19 Africa Challenge chini ya l’Agence française de développement (AFD), Expertise France, na The GovLab|

TAHARIRI: Serikali isilazimishe walimu kusoma tena

NA MHARIRI

WAKUU wa vyama vya kutetea walimu nchini ni wasaliti kwa kukubali kuingia katika mkataba ya kuwataka walimu waongezee masomo yao kila baada ya miaka mitano na kujigharimia fedha zinazohitajika kufaulisha mpango huo.

Chama cha Walimu wa Shule ya Upili na Vyuo Anuwai (Kuppet) na kile cha Knut, vimewasaliti walimu kwa kuwa mkataba huo unasema walimu wenyewe watajilipia karo.

Pia Tume ya Kuwaajiri Walimu ambayo iliingia katika maelewano hayo na Knut ilipendekeza kuwa leseni au nambari ya TSC itarefushwa kila baada ya miaka mitano baada ya kila mwalimu kukumbatia masomo hayo. Si vibaya kwa kila mwalimu kujiongezea elimu ambayo ni hazina isiyokwisha.

Kila mtu anafaa kujifahamisha mambo mapya wala si kusubiri hadi miaka mitano pekee.Hata hivyo, Knut na Kuppet zinaonekana kama vyama visivyozingatia maslahi ya walimu tena.

Kwa kuingia mkataba huo, vyama hivyo havikuzingatia kuwa walimu wanafamilia na majukumu mengine ya kimsingi ambayo yanawahitaji kuwajibikia kifedha.

Je, mwalimu ambaye atakuwa na watoto wake shule au vyuoni ataweza kugharimia karo yao kivipi iwapo wakati huo yeye pia atakuwa akitakiwa awe shuleni kwa gharama yake mwenyewe?

Walimu hawajaongezwa mshahara wowote. Hata makubaliano ya mwaajiri wao pamoja na vyama hivyo ya nyongeza ya mishahara bado hayajatekelezwa. Itakuwa vigumu kupata pesa za masomo hayo ikizingatiwa kuwa wengi wao pia huwa wana mikopo mikubwa ya kulipa kila mwezi.

Taaluma ya ualimu vyuoni huchukua miaka minne au miwili kuisomea. Je, ina maana kuwa muda huu wote utakuwa umepotea iwapo mwalimu hatajisajili katika masomo haya mapya na leseni yake kutorefushwa ?Pia kumekuwa na malalamishi kuwa mkataba huu haukuwashirikisha walimu kupitia matawi ya vyama vyao.

Kwa hivyo, kuna uwezekano TSC na Kuppet na Knut zilipuuza hitaji la ushirikishaji walimu kuhusu suala hili linalowaathiri.

Walimu walifaa kusikizwa na maoni yao kutiliwa manani. Ni vyema iwapo TSC na uongozi wa vyama hivi uwazie upya mpango huu wa masomo na kutumia mbinu ambayo itakubalika na walimu. Viongozi wa Knut na Kuppet nao wamefeli na wanaonekana kutokuwa na ari ya kutetea walimu dhidi ya serikali.

JAMVI: Nyota ya kisiasa ya Karua inaingia doa?

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya kutangazwa kwa kiongozi wa Narck-Kenya, Bi Martha Karua, kama kaimu msemaji wa ukanda wa Mlima Kenya, imeibua maswali kuhusu ikiwa ametia doa sifa yake kama kiongozi wa kitaifa.

Bi Karua alitwikwa jukumu hilo kwenye kikao maalum cha viongozi wa ukanda huo, kilichofanyika mwanzoni mwa wiki hii, mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru.

Waliokuwepo kwenye kikao hicho ni Bi Karua, aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo na mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini).

Bw Kabogo ni kiongozi wa chama kipya cha Tujibebe Wakenya Party (TWP) huku Bw Kuria akiwa kiongozi wa Chama cha Kazi (CCK).

Viongozi hao walisema walifanya uamuzi huo baada ya kushauriana na viongozi wenzao kutoka sehemu mbalimbali katika ukanda huo.

Vile vile, walisema kuwa uamuzi wa kumtawaza Bi Karua kushikilia nafasi hiyo ulitokana na hali kuwa yeye haegemei mrengo wowote wa kisiasa.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wameeleza kuwa, ingawa huenda hatua hiyo inaonekana kumkweza Bi Karua kisiasa katika ukanda huo, kuna uwezekano ikampaka tope na kushusha nyota yake kitaifa kama mwanamageuzi anayeheshimika.

Kulingana na Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, kukwezwa kwa Bi Karua kama kaimu msemaji wa ukanda huo kutamwingiza kwenye “siasa chafu” za ushindani wa yule anayepaswa kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

“Ni wazi kuwa kuna ushindani mkubwa ambao umejitokeza miongoni mwa wanasiasa wanaolenga kumrithi Rais Kenyatta. Ikizingatiwa Bi Karua amekuwa kwenye ligi ya kisiasa ya kitaifa, kuna uwezekano mkubwa akaanza kupigwa vita na wanasiasa wanapania kuchukua nafai hiyo,” akasema Prof Njoroge.

Bi Karua ni miongoni mwa viongozi wa eneo hilo ambao wamekuwa kwenye ulingo wa siasa kwa muda mrefu.

Alijitosa kwenye ulingo wa siasa katika miaka ya tisini, alipowania ubunge katika eneo la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga na kuibuka mshindi.

Alihudumu kama waziri wa Maji na Haki na Masuala ya Katiba katika serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki, hadi alipojiuzulu mnamo 2009.

Vile vile, alikuwa miongoni mwa viongozi walioshiriki katika Mazungumzo ya Serena baada ya ghasia za uchaguzi tata wa 2007, kumtetea Bw Kibaki.

Bi Karua alikuwa katika upande Bw Kibaki na chama cha PNU, akiwa pamoja na maseneta Moses Wetang’ula (Bungoma) na Prof Sam Ongeri (Kisii).

Kiongozi huyo pia aliwania urais mnamo 2013, ingawa hakuibuka mshindi.

Mnamo 2017, aliwania ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga ingawa alishindwa na Gavana Anne Waiguru.

Wadadisi wanasema kuwa Bi Karua amejijengea sifa nzuri ya kiongozi anayeheshimika sana nchini na kimataifa, kwani kando na siasa, amekuwa akitumia taaluma yake ya uwakili kuwatetea wananchi.

“Hata ingawa Bi Karua analenga kurejea nyumbani kisiasa kama livyofanya mnamo 2017, nadhani kuna njia mbadala ambayo angetumia badala ya kukubali uteuzi wa kuwa msemaji wa Mlima Kenya. Kuna uwezekano mkubwa akajitosa kwenye vita na makabiliano ya kisiasa ambayo tumekuwa tukishuhudia baina ya mirengo mbalimbali katika ukanda huo,” asema Bw Ochieng’ Kanyadudi, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Baada ya uteuzi wake, Bi Karua alijitenga na madai ya kuwa mwanachama wa mrengo wowote wa kisiasa, akishikilia nia yake ni kuhakikisha eneo hilo limeungana ili kuwa na sauti moja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mimi si mwanachana wa mrengo wowote. Ni mwanasiasa huru, anayelenga kuhakikisha watu wetu wamezungumza kwa sauti moja, kinyume na ilivyo sasa. Tunapaswa kuungana na kubuni njia tutakayofuata kwa wawaniaji wote wanaofika katika eneo letu kutuomba kuwaunga mkono,” akasema Bi Karua.

Mwanasiasa huyo amekuwa kiongozi wa Narc-Kenya kwa muda mrefu, akikitaja kuwa chama huru chenye misimamo yake kisiasa.

Kufikia sasa, viongozi waliotangaza ama kuonyesha nia ya kumrithi Rais Kenyatta ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, magavana Mwangi wa Iria (Murang’a), Francis Kimemia (Nyandarua), Waiguru (Kirinyaga) kati ya wengine.

Hata hivyo, nia zao zimeandamwa na migawanyiko mikali, ambapo kwa sasa, kuna mirengo ya kisiasa ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga.’

Mrengo wa ‘Kieleweke’ umekuwa ukimtetea Rais Kenyatta huku ‘Tangatanga’ wakimtetea Naibu Rais William Ruto, kwenye nia yake kuwania urais 2022.

Bw Kanyadudi anasema kuwa kukubali nafasi hiyo, huenda Bi Karua analenga kuimarisha nafasi yake kuwania ugavana Kirinyaga, ikizingatiwa anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirichi.

“Ilivyo sasa, Bi Karua ana kibarua kigumu kuwakabili Bi Ngirichi na Gavana Waiguru, ambao washatangaza azma ya kuwania ugavana. Kwa upande mmoja, nafasi hiyo itamsaidia kuinua nyota yake kisiasa, ila ajajipata tope ikiwa hatajiepusha na mizozo ya urithi ambayo huenda ikaibuka,” akasema mdadisi huyo.

Jifunze kuoka keki ya kakao na vanilla

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa mapishi: Dakika 50

Walaji: 5

Vinavyohitajika

  • siagi robo kilo
  • sukari robo kilo
  • unga robo kilo
  • mayai 6
  • arki ya vanilla kijiko 1
  • kakao yaani cocoa vijiko 3
  • baking powder 1
  • chungwa 1
  • maganda ya chungwa kijiko 1
  • chumvi

Maelekezo

Chekecha unga kwenye bakuli kisha weka chumvi na baking powder na uchanganye vizuri kwa mwiko.

Osha chungwa vizuri kisha lipare kwa kipario ili upate maganda yake kijiko kimoja. Weka maganda ya chungwa kwenye unga na uchanganye tena vizuri.

Weka sukari na siagi kwenye bakuli jingine.

Saga mchanganyiko wako kwa muda wa dakika tatu (3).

Weka Vanilla endelea kusaga kwa muda wa dakika mbili (2).

Weka mayai yako moja baada ya jingine mpaka uyamalize huku ukiendelea kusaga.

Weka juisi ya chungwa kisha saga tena kidogo.

Malizia kuweka unga kidogo kidogo mpaka umalize wote huku ukisaga.

Chukua bakuli gawa mchanganyiko wako kisha weka kakao (cocoa) kwenye bakuli ul’oweka mchanganyiko wako halafu changanya vizuri kwa kijiko kikubwa.

Washa ovena nyuzi joto sentigredi 160. Chukua chombo chako cha kuokea, kisha anza kuweka mchanganyiko mweupe na kati weka wa cocoa kisha malizia mweupe.

Oka kwa dakika 50 kisha fungua jiko na tazama keki yako.

Ingiza kijiti au kisu safi kwenye sehemu mbali mbali – tofauti – za keki yako kuangalia kama imeiva.

Ikiwa kijiti kitatoka na umaji maji basi keki yako bado rudisha kwenye ovena.

Ikipoa toa kwenye trei na ikate vipande tayari kuliwa na kinywaji upendacho.

TAHARIRI: Sakata ya Kemsa inakatisha tamaa

KITENGO CHA UHARIRI

KAMATI ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) iliyokuwa ikichunguza sakata ya wizi wa mabilioni ya fedha kupitia kandarasi zilizotolewa kiholela na Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Tiba nchini (Kemsa), janga la corona lilipovamia Kenya mwaka jana, haikufanya kazi ya kuridhisha.

Katika ripoti yake, kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, haikutoa mapendekezo ya kushtakiwa kwa baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi serikalini waliotajwa wakati wa uchunguzi.

Sh7.8 bilioni zilitengwa na serikali kupambana na virusi vya corona lakini takribani Sh3.2 bilioni zinaaminika kuishia katika mifuko ya mabwanyenye wachache licha ya hospitali kukosa mitungi ya oksijeni na mavazi ya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya virusi.

PIC ilipendekeza kampuni zilizopata kandarasi hizo zilizokuwa zikitolewa kiholela, zirejeshe fedha.

Wakati kamati hiyo ilipokuwa ikihoji wakurugenzi wa kampuni 102 zilizofanya biashara na Kemsa, walionufaika na kandarasi hiyo walikiri kukiuka sheria.

Wakenya walistaajabishwa kusikia baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo wakidai kwamba waliomba Mungu kuwapa kandarasi.

Wengine walidai kwamba walikuwa wakipita karibu na jumba la Kemsa wakaitwa na kupewa kandarasi hiyo.Ukweli ni kwamba, ni vigumu kwa raia wa kawaida kupata kandarasi bila kuwa na ushawishi serikalini.

Kulikuwa na dalili kwamba kampuni hizo zilimilikiwa na watu wenye ushawishi serikalini waliojificha nyuma ya wakurugenzi hao.Sakata hiyo ilipoibuka, Rais Uhuru Kenyatta, mnamo Agosti 2020, aliagiza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufanya uchunguzi na kuukamilisha ndani ya siku 21.

EACC ilikamilisha uchunguzi wake baada ya siku 21 kupita na kuwasilisha ripoti yake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Bw Haji, hata hivyo, alikataa faili ya uchunguzi huo huku akiitaka EACC kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ushahidi wa kutosha.

EACC ilikuwa imependekeza kushtakiwa kwa wakurugenzi wa kampuni za Accenture Kenya, Gadlab Supplies, Meraky Healthcare, Steplabs Technical Services, Wallabis Ventures, Shop n Buy na Kilig Ltd ambayo Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe alikiri kuisimamia kuchukua mkopo katika Benki ya Equity.

Mbali na PIC, sakata hiyo imechunguzwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya pamoja na Seneti.

Inaonekana sakata hiyo imeingia kwenye orodha ndefu ya visa vya ufisadi ambapo walipa ushuru wamepoteza mabilioni ya fedha bila wahusika kuchukuliwa hatua.

Idata ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) haina budi kuingilia kati kuhakikisha kuwa fedha zote zilizopotea katika sakata hiyo zinarejeshwa na wahusika wanakamatwa.

TAHARIRI: Ripoti ya Kemsa inakatisha tamaa

KITENGO CHA UHARIRI

KAMATI ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) iliyokuwa ikichunguza sakata ya wizi wa mabilioni ya fedha kupitia kandarasi zilizotolewa kiholela na Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Tiba nchini (Kemsa), janga la corona lilipovamia Kenya mwaka 2020, haikufanya kazi ya kuridhisha.

Katika ripoti yake, kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, haikutoa mapendekezo ya kushtakiwa kwa baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi serikalini waliotajwa wakati wa uchunguzi.

Sh7.8 bilioni zilitengwa na serikali kupambana na virusi vya corona lakini takribani Sh3.2 bilioni zinaaminika kuishia katika mifuko ya mabwanyenye wachache licha ya hospitali kukosa mitungi ya oksijeni na mavazi ya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya virusi.

PIC ilipendekeza kampuni zilizopata kandarasi hizo zilizokuwa zikitolewa kiholela, zirejeshe fedha.

Wakati kamati hiyo ilipokuwa ikihoji wakurugenzi wa kampuni 102 zilizofanya biashara na Kemsa, walionufaika na kandarasi hiyo walikiri kukiuka sheria.

Wakenya walistaajabishwa kusikia baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo wakidai kwamba waliomba Mungu kuwapa kandarasi.

Wengine walidai kwamba walikuwa wakipita karibu na jumba la Kemsa wakaitwa na kupewa kandarasi hiyo.Ukweli ni kwamba, ni vigumu kwa raia wa kawaida kupata kandarasi bila kuwa na ushawishi serikalini.

Kulikuwa na dalili kwamba kampuni hizo zilimilikiwa na watu wenye ushawishi serikalini waliojificha nyuma ya wakurugenzi hao.

Sakata hiyo ilipoibuka, Rais Uhuru Kenyatta, mnamo Agosti 2020, aliagiza Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufanya uchunguzi na kuukamilisha ndani ya siku 21.

EACC ilikamilisha uchunguzi wake baada ya siku 21 kupita na kuwasilisha ripoti yake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Bw Haji, hata hivyo, alikataa faili ya uchunguzi huo huku akiitaka EACC kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ushahidi wa kutosha.EACC ilikuwa imependekeza kushtakiwa kwa wakurugenzi wa kampuni za f Accenture Kenya, Gadlab Supplies, Meraky Healthcare, Steplabs Technical Services, Wallabis Ventures, Shop n Buy na Kilig Ltd ambayo Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe alikiri kuisimamia kuchukua mkopo katika Benki ya Equity.

Mbali na PIC, sakata hiyo imechunguzwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya pamoja na Seneti.

Inaonekana sakata hiyo imeingia kwenye orodha ndefu ya visa vya ufisadi ambapo walipa ushuru wamepoteza mabilioni ya fedha bila wahusika kuchukuliw hatua.Idata ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) haina budi kuingilia kati kuhakikisha kuwa fedha zote zilizopotea katika sakata hiyo zinarejeshwa na wahusika wanakamatwa.

DINI: Unahitaji hekima kucheza karata zako vyema maishani na usikubali hofu ikuwekee vikwazo

FAUSTIN KAMUGISHA

 

KULINGANA na Edward de Bono, kuwekeza ni suala la namna unavyocheza karata ulizopewa.

Mwalimu aliwaeleza wanafunzi wake kwamba atawauliza swali na na atampa simu atakayelijibu.

Lakini pia akasema kuwa, mwanafunzi ambaye angemuuliza swali na yeye ashinde, basi atamrudishia simu yake.

“Yesu alilisha wanaume wangapi chakula?” aliuliza.

Naye mwanafunzi alijibu kuwa walikuwa 5,000.

Alipewa simu. Naye mwanafunzi alimuliza mwalimu alimtaka mwalimu kutaja majina ya watu hao, jambo ambalo hakuweza na akapoteza simu hiyo. Kutokana na hali hii, basi tunasema kuwa ilikula kwake.

Mwalimu hakucheza vizuri karata zake.Katika Biblia kuna masimulizi juu ya watu watatu waliopewa talanta na bwana wao aliyesafiri. Aliyepewa talanta tano alitengeneza faida nyingine tano.

Aliyepewa talanta mbili alitengeneza faida ya talanta mbili. Aliyepewa talanta moja aliizika.

Alimwambia bwana wake, “basi nikaogopa, nikaenda nikaficha talanta yako katika ardhi” (Mt. 25 : 25).

Aliyepewa talanta moja hakushughulika, ilikula kwake. Jitahidi katika maisha isile kwako. Ukiogopa kuwekeza inakula kwako.

“Ole wao ambao hawaimbi kamwe, lakini wanaaga dunia muziki wao wote ukiwa ndani mwao,” alisema Oliva W Holmes.

Kuna hatua saba za kushindwa kifedha. Kinyume chake ni hatua saba za kushinda kifedha.

Kwanza ni kuwa na hofu. Kuwa na hofu ni hatua ya kwanza ya kushindwa. Kuwa na ujasiri ni hatua ya kwanza ya kushinda. Fikiria una ndugu ambaye amezaliwa bila mkono wa kulia na nusu ya mguu wa kulia. Fikiria akiwa na umri wa miaka sita anakuuliza, “Unafikiri nitaweza kushiriki michezo shuleni? Utamwambia nini? Au utamweleza hali halisi?’ Fikiria siku moja mnatazama mechi kwenye runinga naye anakuuliza, “Unafikiri nitawahi siku moja kucheza mpira?’ Utamwambia nini? Fikiria, siku moja anakuona unafungua kurasa kwenye kitabu cha rekodi cha ligi za mpira. Anakuuliza, siku moja nitacheza mpira vizuri na jina langu kuingizwa kwenye kitabu hicho? Utamwambia nini?

Mwaka 1953, mtoto mwenye umri wa miaka sita aitwaye Tom Dempsey alikuwa anauliza maswali kama haya kama ndugu yako wa kufikirika naye alizaliwa bila mkono wa kulia na nusu ya mguu wa kulia.

Tom alienda shule na kucheza mpira wa Marekani. Alicheza timu ya Junior College California. Badaye alisajiliwa kwenye timu ya New Orleans Saints.

Novemba 8 1970, timu ya Saints ilikuwa imechapwa 17 kwa 16 na Detroit. Zilibaki sekunde mbili mchezo kumalizika. Kocha J. D Roberts alimgusa Tom na kumwambia, “Ipe timu yako shuti nzuri sana.” Tom alitoa shuti nzuri sana na timu yake ilishinda kwa 19 – 17.

Alitumia kipaji kimoja alichokuwa nacho kufanya maajabu. Tom hakuwa na hofu na hali aliyokuwa nayo.

Aliyepewa talanta moja alisema, “niliogopa’ (Mt. 25: 25).

“Kila kitu unachohitaji kipo upande mwingine wa hofu.”

Jack Confield aliwahi kusema. Ilipo hofu yako ndipo yalipo mafanikio yako. Unaogopa kupeleka ndizi Ulaya, huko ndipo yalipo mafanikio yako. Unaogopa kumiliki duka, huko ndiko yapo mafanikio yako. Kulingana na Gandhi, “Adui ni hofu. Tunafikiri ni chuki kumbe ni hofu.” Ili kuvumbua bahari mpya lazima uende mbali lazima ufanye kitu. “Mtu ambaye hajiweki katika hali ya hatari, hafanyi lolote, hana chochote, na si chochote na atakuwa si chochote. Anaweza kukwepa mateso na huzuni, lakini hawezi kujifunza kuishi na kubadilika na kukua na kupenda na kuishi,” alisema Leo F. Buscaglia (1924 – 1998)Marekani anayetambulika kwa kuhimiza kuhusu upendo.Kama kila mtu angejitahidi kufanya lolote zuri duniani ingekuwa mahali pazuri pa kukalika (Itaendelea wiki ijayo).