FUNGUKA: ‘Yote kwa raha zangu’

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA ulimwengu wa uhuru wa kuchagua na kufurahia chochote kinachochochea mahaba, bila shaka hakuna nafasi ya kustaajabu.

Lakini hata ikiwa siku hizi ni vigumu kushangazwa na yanayojiri, bila shaka ukikumbana na ya Abe, 49, hutakuwa na budi ila kuachwa kinywa wazi.

Abe ni mhasibu mkuu katika shirika moja lisilo la kiserikali, kazi aliyoipata huenda kutokana na kisomo chake cha hali ya juu.

Ana shahada mbili za uzamili katika masuala ya uhasibu na ukaguzi wa mahesabu kutoka vyuo viwili vya haiba ya juu nchini Amerika.

Ajira hii imemsaidia kuwekeza katika nyanja mbalimbali na katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili akihudumu katika nafasi hii, amejizolea mali kibao.

Mbali na majumba yake mawili mitaani Karen na Runda, anamiliki majumba ya watu kuishi huku wakilipa kodi katika mitaa kadhaa jijini Nairobi.

Kimaumbile, Abe pia ana mengi ya kumshukuru Mungu. Utanashati wake unaakisiwa kutoka utosini hadi miguuni, suala ambalo limemfanya kung’ang’aniwa na takriban kila binti anayekutana naye kwa mara ya kwanza.

Lakini kwa mabinti wengi, mvuto huisha pindi wanapopata fursa ya kumfahamu kwa undani.

“Kwangu, mahaba huchochewa na maumivu kwenye sehemu nyeti. Namaanisha kwamba nafurahia kupigwa na kupondwa sehemu hii kama mbinu ya kujiridhisha kimahaba. Pindi tunapoingia chumbani, bila shaka masuala ya mahaba kama vile kuvua mavazi, kupapapasana na kubusiana yatazingatiwa. Lakini ni hapo tu yatakapokomea kwani kitakachofuatia ni vita.

Vita hivi vinahusisha binti kunitandika makonde na mateke na hata kunifinya na kunikanyaga sehemu hii. Binti anapotekeleza haya sharti awe amevalia viatu vya visigino virefu.

Shughuli hii huendelea kwa muda wa saa kadhaa tukiwa mle ndani hadi nitakapolemewa kabisa na uchungu, ambapo atakuwa huru kuondoka na kuendelea na shughuli zake.

Sio kwamba nina kasoro ya kimaumbile, la, nina uwezo kama mwanamume yule mwingine. Tatizo ni kwamba sifurahishwi kamwe na tendo la ndoa. Hata nikioa, itakuwa tu kwa sababu ya kumpata mtu wa kuzungumza naye kila siku, na sio kwa sababu ya kushiriki tendo la ndoa.

Nina pesa na hivyo niko tayari kukufanyia kila kitu mradi ukubaliane nami kwamba hata tukioana, hakuna tendo la ndoa. Tamaa na uchu wetu wa kimahaba vitakuwa vikimaliziwa tu chumbani unaponipiga na kuniumiza. Hii inamaanisha kwamba hata suala la kuwa na mtoto usiliwazie. Ni suala ambalo wengi hujaribu kulikubali mwanzoni pengine kutokana na maisha ya kifahari ninayowapa.

Wengi huja wakiwa na imani ya kwamba pengine baada ya miezi kadhaa nitabadili msimamo, lakini wanapoingia na kugundua kwamba hilo halitafanyika, hutoweka ghafla”.

Shirika la kutafutia wakulima soko lawahimiza kukuza mimea inayostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi

Na SAMMY WAWERU

SHIRIKA moja la kutafutia wakulima soko la mazao yao nje ya Bara Afrika limewahimiza kukumbatia ukuzaji wa mimea inayostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Janga la ukame, mkurupuko wa magonjwa na wadudu ni miongoni mwa athari zinazojiri kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Shirika la Fairtrade Africa (FTA) limesema wakulima wakikuza mimea yenye ustahimilivu wa hali ya juu kwa athari hizo, mataifa yanayohangaishwa na kero ya baa la njaa yatakuwa na usalama wa chakula.

“Tunahimiza wakulima wafanye utafiti na kutambua mimea inayoweza kustahimili makali ya athari za mabadiliko ya tabianchi,” akashauri Bw Chris Oluoch, Mkurugenzi wa Mikakati FTA, katika hafla iliyoandaliwa jijini Nairobi na kuleta pamoja kampuni na mashirika ya yanayochangia uzalishaji wa chakula, maua na pamba nchini.

Kwenye mahojiano, afisa huyo aliambia Taifa Leo kwamba shirika hilo limeweka mikakati kabambe kuona wakulima na mashirika wanachama wake, wanakabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

“Tumeweka mipango na sheria kuona wanaboresha shughuli za kilimo,” akasema.

“Isitoshe, tunawapiga jeki waweze kukumbatia vigezo vya kilimo bora, katika mchakato mzima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” Bw Oluoch akaelezea.

Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha hali ya anga kubadilika kwa kiasi kikubwa, kaunti zinazoshuhudia kiangazi mara kwa mara nchini (ASAL), zikiendelea kuhangaishwa na ukame na njaa.

Kaunti zipatazo 24 zina mamilioni ya wakazi ambao serikali isipotafuta suluhu ya kudumu dhidi ya ukame, huenda wakafa njaa.

KAMAU: Ni aibu kuwatelekeza mashujaa waliopigania uhuru

Na WANDERI KAMAU

KULINGANA na majarida mbalimbali ya historia, vita vya Maumau ni miongoni wa harakati zinazotambulika duniani kote kutokana na jinsi Wakenya walivyojitolea kuukabili utawala wa kikoloni wa Waingereza.

Wasomi wa historia wanasema kuwa kwa namna moja, kujitolea kwa Wakenya kwenye vita hivyo ndiko kulikowapa msukumo Waafrika wengine katika nchi kama Algeria, Msumbiji, Angola na Afrika kusini.

Nchini Algeria, vita vya ukombozi wa taifa hilo vilidumu kati ya mwaka 1954 hadi 1962, wakati taifa hilo lilijinyakulia uhuru wake kutoka kwa Ufaransa.

Vikosi vya Ufaransa vilijipata taabani, wakati raia wa Algeria walijitokeza kwa ujasiri kuwakabili kutokana na dhuluma ambazo walikuwa wakiwafanyia.

Nchini Msumbiji, vita vya ukombozi vilidumu kati ya 1964 hadi 1974, wakati taifa hilo lilipata uhuru wake kutoka kwa Ureno, kupitia kubuniwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Nchini Angola, harakati hizo zilidumu kati ya 1961 hadi 1974.Bila shaka, ni wazi kuwa vita vya Maumau vilibuni msingi mzuri wa harakati hizo, kwani vilidumu kati ya 1952 hadi 1958.

Licha ya vita hivyo kubuni msingi thabiti kuhusu jinsi Afrika ilipigania uhuru wake, inasikitisha kuwa hadi sasa, Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo zimewatelekeza mashujaa hao.

Hadi sasa, wapiganaji wa Maumau wamekuwa wakilalamikia jinsi serikali nyingi zimekosa kushughulikia maslahi yao tangu miaka ya sitini.

Hii ni licha ya Uingereza kutoa mabilioni ya fedha kwa wapiganaji hao kulipwa kama ridhaa, kutokana na mateso na dhuluma ambazo walipataSerikali ya Mzee Jomo Kenyatta, marehemu Daniel Moi na Rais Mstaafu Mwai Kibaki zilifumbia macho vilio vyao vyote.

Hata hivyo, Bw Kibaki alijaribu jinsi awezavyo kushughulikia maslahi yao, ingawa juhudi hizo hazikuzaa matunda sana.

Ni wakati wa utawala wa Mzee Kibaki ambapo minara ya mashujaa kama Dedan Kimathi na mwahaharakati Tom Mboya ilijengwa, kama njia ya kukumbuka michango waliyotoa kwenye harakati za ukombozi wa nchi.

Inasikitisha kuwa wapiganiaji wengi wamekuwa wakidai kiwango kikubwa cha fedha walizopaswa kulipwa ziliporwa na maafisa na mawakili waliosimamia taratibu za kuwalipa.

Je, Kenya kwelininawajali wazalendo wake?

Imefika wakati tujifunze kutoka kwa nchi kama Afrika Kusini, kuhusu njia bora za kuwathamini mashujaa na wanaharakati waliopigania uhuru.

akamau@ke.nationmedia.com

MUTUA: Wakenya walio ng’ambo wana haki ya kupiga kura

Na DOUGLAS MUTUA

NILICHEKA kidogo kisha nikakereka kweli-kweli hivi majuzi kutokana na matamshi ya mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw Wafula Chebukati.

Akiongea na makundi ya kidini, Bw Chebukati aliahidi kwamba angewapa haki za kupiga kura, katika uchaguzi ujao, Wakenya wanaoishi nje ya nchi.

Wanaoishi kwenye mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Afrika Kusini walishiriki chaguzi kuu za 2013 na 2017.

Kwa walio kwingineko Afrika, Marekani, Uropa, Asia, Mashariki ya Kati na kadhalika, hiyo imesalia ndoto isiyoagulika – hadaa baada ya hadaa, na hadaa zaidi.

Serikali ikidai haina uwezo wa kifedha kuendesha shughuli hiyo kokote waliko Wakenya milioni 3.5, lakini ikipokea kwa pupa ushuru wanaolipa kwa mamilioni.

Sikwambii mfuko mnono unaotengewa tume ya uchaguzi huishia kuwa kitoweo cha watu wabadhirifu wanaoitafuna nchi kana kwamba kiyama chaja kesho.

Sasa Bw Chebukati anadhani amefanya kitu cha maana sana kutangaza huenda wanaoishi Marekani, Canada, Sudan Kusini, Uingereza, Qatar na Muungano wa Mataifa ya Kiarabu (UAE) wakamchagua rais mwaka 2022.

Nilicheka kwa kuwa nilidhani hiyo ni danganya-toto ya kawaida ambayo tumeisikia tangu mwaka wa 2010 tulipoipitisha Katiba ya sasa.

Huwa raha ukihadaiwa ukajua.

Yaliyoniudhi hadi ya kuniudhi ni matamshi ya ‘kuwapa haki ya kupiga kura Wakenya wanaoishi ughaibuni’.

Yangetolewa na kabwela wa watu ningemmpuuza tu, hazidishi hapunguzi! Lakini Bw Chebukati ndiye mkuu wa uchaguzi hasa, tena wakili anayeielewa Katiba sawasawa.

Anajikweza sana mtu wa kiwango chake anapodai atawapa haki Wakenya walionyanyasika miaka yote hii ilhali anajua ni haki yao ya kikatiba.

Hata heri angetanguliza kwa kuomba msamaha kwani amekiuka Katiba miaka mingi tu kwa kutoweka mikakati ya kuwawezesha Wakenya kupata haki hiyo.

Hii si mara ya kwanza kwa ahadi kama hiyo kutolewa, lakini kila uchaguzi unapokaribia vinavyoandamana ni visingizio.

Hata baada ya makundi kadha ya Wakenya kuishtaki serikali mahakamani wakidai haki hiyo, wasimamizi wa uchaguzi wametokea kushupaa shingo na kupuuza kilio hicho.

Kupanga mikakati ya Wakenya kupiga kura kokote waliko hakuigharimu serikali kama miradi ambayo imeishia kufyonzwa na kupe wanono wanatao kwenye nundu ya umma.

Tatizo ni ukosefu wa utashi wa kisiasa; wanasiasa hawaoni tija katika kuwawezesha Wakenya walio ughaibuni kushiriki upigaji kura.

Hakika, wanasiasa wanawaogopa watu hao kwa kuwa wanadhani wamepambazukiwa na dunia kwa kuishi nchi za watu ambako mambo hufanywa tofauti na kwa uwazi.

Kwa makadirio ya wanasiasa, watu milioni 3.5 walioonja ubora wa maisha nje ya nchi ni hatari ikilinganishwa na ‘kondoo’ wa mtaani waliozoea kupelekwa machinjioni kimyakimya kila baada ya miaka mitano.

Wanasiasa huhofia kuwa watu hao, kutokana na mtagusano wao na watu wa asili nyingine, wanaweza kuukiuka ukabila wakamchagua mwaniaji aliye na sera bora.

Na kwa kuwa wanasiasa wetu ni wakora wasiojiamini, hawana hakika sera zao zinaweza kuwashawishi Wakenya hao, hivyo ni heri waliwe njama, watulize boli huko waliko.

Ukiwaona waambie wasihofu kwa kuwa huku nje tumetengana kishenzi tu, tumeshindwa kuuacha ukabila, hata makundi ya WhatsApp tunaunda kwa misingi ya makabila yetu!

Wanasiasa pia huogopa uwezo wa kifedha wa wanaoishi ughaibuni kwani, kinyume na wanavyofanya nchini, wanasiasa hawawezi kwenda kuwagawia vihela vyao huko nje.

Kwa jumla, Wakenya tumelimatia sana kudai haki zetu za kimsingi kama hii ya kupiga kura.

Tumezembea kuwawajibisha wanasiasa wetu, wakatugawa mafungu, sasa wanacheza nasi kama mwanasesere.

Wataanza kutuheshimu tutakapoacha uzembe na upofu wa kupanga tuliojitwika, tudai haki zote za kimsingi hata zisizotufaa moja kwa moja.

mutua_muema@yahoo.com

FATAKI: Komesheni tabia ya kutia mkono chunguni kabla mboga kuchemka

Na PAULINE ONGAJI

MAPEMA wiki hii nilikutana na chapisho fulani la kuchekesha kwenye mtandao mmojawapo wa kijamii.

Chapisho hilo la binti fulani liliandamana na picha iliyoonyesha vyakula vilivyopakiwa vizuri kwenye vifaa vya plastiki na kuwekwa kwenye friji.

Chini yake kulikuwa na maandishi… “kila wiki ninapomtembelea mpenzi wangu, lazima nihakikishe kuwa nampikia na kumhifadhia chakula cha kumtosha juma nzima…”

Ni picha iliyosababisha hisia mseto kutoka kwa wanamitandao. Hasa nakumbuka maoni fulani ya kudhihaki kutoka kwa binti fulani yaliyosema… “juma lililopita uliweka chumvi nyingi….”

Japo naamini kwamba ulikuwa utani, yaliakisi hali halisi ya yanayowakumba mabinti wanaojitoa kijasho kwa kuyashughulikia mahitaji ya madume ambao hawajawaoa wala kuwachumbia rasmi, wakidhani kwamba hayo ni mapenzi.

Hii yanikumbusha kisa cha kaka mmoja miaka kadhaa iliyopita aliyekuwa akinung’unika kwa sababu binti mmoja alikuwa “amevamia” nyumba yake na kutaga mayai.

Yaani kipusa huyo alikuwa amejileta nyumbani mwa kaka huyo na kwa wiki tatu mfululizo hakuwa anaonyesha dalili za kurejea alikotoka.

Naelezwa kwamba ni mojawapo ya sababu kuu ambazo zimewafanya akina kaka wengi siku hizi kuzembea inapowadia wakati wa kufuata utaratibu unaohitajika kabla ya kupata mke.

Nasikia kwamba madume siku hizi hufurahia kila wanapotembelewa na vipusa wikendi kwani wanajua watapiga deki, kuwapikia na kuwapa huduma nyingine muhimu bila malipo.

Dhana hii ni sababu tosha ya kuonyesha jinsi kuna baadhi ya mabinti wanaojishusha thamani wakidhani hii ni ishara ya mwanamke bomba.

Ya nini uchubue mikono yako ukimfulia na kumpikia kaka ambaye huna uhakika kwamba atakuoa?

Ya nini kumpa burudani na hata hajathibitisha uhusiano wenu?

Najua wanasema sehemu hiyo si sabuni eti itaisha lakini mbona kumpa mtu asiyestahili?

Ujumbe huu ni kwa wale warembo unaowapata kila wikendi wakiharibu kucha wakiwafulia madume huku wakijua sio wao pekee wamo mpangoni.

Kumbuka kuwa wengine hawapewi hata nauli. Nakumbuka binti mmoja akilalama jinsi baada ya wikendi zima akipiga deki na kumpa mahaba kaka, hata hela za P2 (kinga mimba) hakupata ng’o!

Japo wanayofanya baadhi ya madume hawa ni makosa, utawalaumu vipi?

Wengi wao hujiuliza, ya nini nimnunue ng’ombe ilhali ninaweza nikapata maziwa ya bure?

UMBEA: Jinsi unavyoweza kuwasha moto hisia tena hadi mwenzio apagawe

Na SIZARINA HAMISI

MAISHA ya ndoa yamewatumbukia nyongo wengi.

Kwa wengine yamekuwa machungu mfano wa shubiri. Jambo lililonishtua ni jinsi ndoa nyingi zilivyo hatarini kuvunjika. Pia kwa wanandoa niliozungumza nao, wote walikuwa wakiishi pamoja sababu ya watoto na wala sio sababu ya upendo.

Haya nayasema baada ya kushiriki usuluhishi wa ndoa kadha. Usuluhishi wa ndoa hizi ulikuwa na jambo moja linalofanana, kwamba wanaume wengi huachana na wake zao kutokana na utofauti wa mambo chumbani.

Kuna wanaume wanaopenda wafanyiwe mambo fulani na wake, kuna wengine hawataki mambo fulani na kuna wengine waliogubikwa na masharti mengi.

Kuna muda ambao mke anaweza kukuwekea ngumu, hadi uone dunia imekuinamia. Zile siku unaporudi nyumbani na kupata mke ameweka sura ya kazi. Yaani unakuta kafura, hazungumzi, hacheki, hakuangalii wala hataki kukusogelea. Na wewe labda umejitayarisha, umetafuna njugu, pilipili na umekunywa supu ya samaki na damu inachemka. Unaweza ukajaribu mbinu zako hapo za kumchekesha labda ama kumwuliza, lakini mambo yakashindikana. Utafanya nini?

Ni vyema kuelewa pale mkeo anapokuwa amepoteza hisia za mahaba. Na jinsi unavyoweza kuziwasha moto hisia hizo hadi mwenzio apagawe.

Kuna mambo unayoweza kuyajua haraka kwa mwenzako.

Kwanza yale mambo ama vitendo vinavyoweza kumpunguzia hamu ya mapenzi.

Wengine hupungukiwa hamu wanapokaribia siku za hedhi, wakiwa na mambo yanayowasumbua akili na wengine kama umeanza kurudi nyumbani usiku wa manane.

Na kuna vile vijimambo vinavyomkirihisha na kumtia kichefuchefu, kama unanuka mdomo, kama jasho lako linatoa harufu kali ama kama una tabia ya kumvamia, kumpanda, kumaliza na kulala usingizi.

Lakini pia unaweza kujua hisia zake za mapenzi ama hamu yake ya kuoshwa roho. Wapo akina kaka ambao anapoingia nyumbani tu, anajua kama leo mambo yatakuwa shwari. Unaweza kumkuta mkeo ameoga vizuri, amejiremba, ametandika vizuri kitanda na ananukia vizuri. Ujue hii ni dalili kwamba leo mkeo anakutaka, nawe pia usizubae.

Lakini kuna akina dada tunaweza kuwatunuku shahada kwa kuweka sura ya kazi. Kaka hapa itabidi uanze uchunguzi wa siri ili ujue kulikoni? Cha kufanya, kama mlikuwa na mazoea ya kuketi pamoja, basi siku utakayoanza uchunguzi, ukifika nyumbani, mwite aketi karibu yako na aketi upande wako wa kulia tayari kwa kuanza upelelezi.

Mfanyie kitu ambacho hujawahi kukifanya kama vile mshike sehemu yoyote ambayo huna mazoea ya kumshika.

Akifurahia ujue kuna matumaini, lakini ukiona anachukia kitendo hicho na anajisogeza kutoka ulipo na kwenda pembeni kidogo, kaka yangu ujue una kazi ngumu mbele yako.

Kama mna watoto na ukiona anapenda sana kuwa karibu na wanawe kuliko kuwa na wewe, kaka anza kukaza mshipi.

Na unapoongea naye kama hapendi kukutanisha sana macho yenu na kukwepa kuangalia macho yako moja kwa moja… nakupa pole.

Kama mkeo anapenda kusonya kila wakati mnapokuwa pamoja, anapenda kujadili mambo ya shari zaidi furaha na ukifanikiwa kuingia naye kitandani akaonekana kama anatimiza wajibu badala ya kufurahia rusha roho, kuna shida.

Ufahamu kabisa kwamba mwanamke anakuwa katika tabaka kuu tatu, kwanza anakuwa na mapenzi ya ugeni, kisha anatafuta faraja yaani kumpa raha inayostahili, hasa ikizingatiwa kwamba ni wewe uliye karibu naye na unayestahili kumpa kila anachotaka na cha tatu anatakiwa awe na kitu cha kukukumbuka kila unapokuwa mbali naye.

sizarinah@gmail.com

TAHARIRI: Usimamizi wa soka umedorora

KITENGO CHA UHARIRI

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Soka (KPL) unaanza hii leo ukigubikwa na sintofahamu kubwa jinsi ligi itafadhiliwa, baada ya kampuni ya Odibet kuwa ya hivi punde kuondoa udhamini wake.

Wiki hii Odibet ilitangaza rasmi kuagana na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kwa kile kinachosemekana ni kutoridhishwa na juhudi za shirikisho kukuza soka mashinani.

Kampuni hiyo ya kamari ilikuwa ikitoa ufadhili wa Sh127 milioni katika mkataba wa miaka mitatu uliotangazwa Desemba 2019. Ufadhili huo ulikuwa kwa Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza, Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili na Ligi ya Kaunti.

Madhumuni yalikuwa kuimarisha kandanda mashinani ili kuwa na timu thabiti zinazokuza chipukizi watakaowika kesho na mtondogoo.

Kujiondoa kwa Odibet kunakujia miezi kadha baada ya wafadhili wa Ligi Kuu, Betking, kukatiza uhusiano wake na FKF kuelekea mwisho wa msimu jana Agosti.

Betking, kutoka Nigeria, ilikuwa imetoa ufadhili wa Sh1.2 bilioni katika mkataba wa miaka mitano kuanzia Julai 2020.Kwa sasa ni kampuni moja pekee iliyosalia ya Betika, inayofadhili Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Hata huko mambo ni hatihati huku kukiwa na minong’ono kwamba pia inawazia kuondoa ufadhili wake wa Sh45 milioni kwa miaka mitatu, ulioanza Novemba 2019.

Ni wazi kwamba wafadhili hawana imani tena jinsi Rais Nick Mwendwa anavyosimamia soka ya Kenya.Kinara huyo amejawa na kiburi, haambiliki hasemezeki. Hataki kuwajibikia mabilioni ya fedha ambazo FKF inapokea kuendesha soka.

Isitoshe, amekuwa kama dikteta – alilazimisha klabu za soka kutia saini mkataba wa kupeperusha mechi kupitia Star Times, la sivyo zinyimwe posho la ufadhili wa Betking.

Akajipata katika mvutano na vigogo wa soka nchini, Gor na AFC, kuhusu Sh3 milioni za kombe la Betway Cup ilhali siku chache tu alizindua mnara wa KPL la Sh5 milioni.

Juzi aliibuka na jipya alipotangaza kocha mpya wa timu ya taifa Harambee Stars kwa mkataba wa miezi miwili! Ni matukio ya kushangaza jinsi usimamizi wa soka unavyozidi kudorora kila uchao. Je, nani atawaondolea mashabiki madhila haya?

Wanachama wa Baraza Simamizi la Kitaifa (NEC) ndio wenye kuamua jibu la swali hili. Wako na uwezo wa kupiga kura ya kumuondoa Mwendwa ofisini kwani hatokubali kubanduka. Wataweza?

Tunasubiri kuona iwapo watatimiza wajibu huo ipasavyo ili kuokoa soka ya Kenya.

TAHARIRI: Midahalo endelevu itachochea ustawi

KITENGO CHA UHARIRI

NYAKATI za kampeni za kisiasa husheheni matumizi tele ya propaganda za kisiasa ambapo washindani mbalimbali huzitumia kuwaumbua wenzao, hasa uchaguzi unapokaribia.

Ni mtindo ambao umekuwepo kwa muda mrefu tangu mwanzo wa tawala zilizojikita kwenye mfumo wa kidemokrasia katika maeneo kama Ugiriki na falme ya Roma.

Nchini Ugiriki, washindani wa nyadhifa mbalimbali za uongozi katika miji ya Athens na Sparta walitumia majarida maalum kuelelezea mikakati ambayo wangetumia kuboresha uongozi.

Kando na kujumuisha mikakati yao, walikosoana, japo kwa njia ambazo zilizua midahalo ya kuvutia miongoni mwa wenyeji wa miji hiyo miwili mikuu.

Mfumo huo ndio uliokua na kupanuka kabisa kiasi cha kuigwa na nchi kama Amerika na Uingereza.

Lengo kuu la tathmini hii ni kubuni msingi kuhusu chimbuko na athari za matumizi ya propaganda kwenye siasa.

Nchini Amerika, midahalo ambayo hufanyika miongoni mwa washindani wa urais huwa ni kuumbuana na kukosoana, ingawa huendeshwa kwa njia ya kuwazindua wafuasi wa kila upande.

Hapa Kenya, tumeona majaribio kadhaa ya maandalizi ya mdahalo wa kitaifa miongoni mwa wawaniaji wakuu wa urais.

Jaribio la kwanza lilikuwa mnamo 2013 huku zoezi la pili likiwa 2017.

Kwenye mdahalo uliofanyika 2013, Wakenya walipata nafasi ya kufuatilia kwa kina mipango ambayo wawaniaji husika walikuwa nayo ili kuiboresha nchi.

Jambo lilo hilo lilifanyika mnamo 2017, ingawa halikufaulu kama 2013 kutokana na migawanyiko ya kisiasa iliyokuwepo nchini, hasa kati ya mrengo wa Jubilee, ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Nasa, ulioongozwa na Raila Odinga.

Tunapokaribia uchaguzi mkuu wa 2022, Baraza la Wahariri Kenya (KEG) limetangaza Julai 12 na 26 kuwa tarehe ambapo midahalo hiyo itafanyika. Hata hivyo, swali ni: Midahalo hiyo itafaulu kutokana na migawanyiko ya kisiasa iliyopo nchini?

Kosa kubwa ambalo vigogo wakuu wa kisiasa nchini wanafanya ni kuumbuana na kukosoana isivyofaa. Wengine hata wanatusiana hadharani kwa kisingizio cha kushindana.

Matumizi yafaayo ya propaganda hukitwa kwenye sera za mgombea husika wala si mwenendo wake, familia, marafiki au jamaa zake.

Nchini Amerika, wawaniaji hukosana kwa misingi ya sera na manifesto zao wala si sifa au familia zao.

Kosa hilo ndilo hujenga taharuki na migawanyiko ya kikabila isiyofaa.

Ni wakati wanasiasa wafahamu kuwa propaganda huwa njia ya kuzua midahalo endelevu wala si kutusiana.

KIKOLEZO: Kapochi ka Tik ToK

Na THOMAS MATIKO

TIK TOK ilipozinduliwa 2018, suala la kutengeza mkwanja kupitia mtandao huo wala halikuwa katika mawazo ya wengi.

Lakini mwaka 2020, jarida maarufu la Forbes lilichapisha orodha ya mastaa wa Tik Tok waliotengeneza mkwanja mrefu 2020 kwenye mtandao huo.

Addison Rae Easterling, binti mwenye umri wa miaka 19, ndiye aliongoza kwa dola 5 milioni (Sh545 milioni).

Rae ambaye ana ufuasi wa zaidi ya watu 84 milioni kwenye akaunti yake ya Tik Tok, alitengeneza pesa hizo kupitia dili za matangazo alizosaini na kampuni ya Eagle na Spotify. Pia aliingiza fedha zaidi kupitia brandi yake ya vipodozi, Item Beauty.

Nafasi ya pili na ya tatu ilimwendea mtu na mdogo wake. Tineja Charlie Dámelio mwenye umri wa miaka 17, aliunda dola 4 milioni (Sh436 milioni) huku dadake mkubwa Dixie Dámelio akitengeneza dola 2.9 milioni (Sh316 milioni).

Mwanamuziki chipukizi ambaye pia ni mwanamitindo Loren Gray mwenye miaka 19 alikuwa wa nne akiunda dola 2.6 milioni kupitia dili alizosaini na Virgin Records, Hyundai, Burger King na Revlon.

Michael Le, 21, alichukua nafasi ya sita kwa kuunda dola 1.2 milioni kutokana na dili yake na Bang Energy Drinks. Spencer X alikamilisha listi hiyo kwa kuunda kiasi sawa na cha Le kupitia dili zake za Oreo, Uno na Sony.

Hapa nchini vilevile, kuna mastaa wa Tik Tok ambao wameanza kufuata mkondo huo, wafuatao wakiwa ni baadhi tu.

Azziad Nasenya, 21

Pengine ndiye staa maarufu zaidi wa Tik Tok. Azziad ana zaidi ya wafuasi milioni moja kwenye Tik Tok na Instagram.

Nyota yake ilianzia Tik Tok Aprili 2020 alipoposti video akinengua hiti ya Femi One Utawezana ingawaje alikuwa tayari ameshajiunga na App hiyo 2019 baada ya kushawishiwa na mpenzi wake.

Tangu awe maarufu, Azziad amepokea dili za kutosha za biashara matangazo akishirikiana na kampuni mbalimbali kama vile Bic, Phillips, Cortez, na hata kampuni za usafiri.

Kulingana na mtu aliye karibu sana naye, mrembo huyu hutengeneza zaidi ya nusu milioni kwa mwezi kazi ikiwa nzuri.

“Kiwango hicho ujue bado hujaongeza na mshahara anaopata kutokana na kazi yake ya redioni,” anasema mdokezi wetu.Kando na dili za biashara matangazo, anatengeneza hela zaidi kupitia chaneli yake ya Youtube, Shoe Game With Azziad.

Ajib Gathoni, 22

Janga la Covid-19 lilipozuka Machi mwaka jana, Ajib ambaye ni mwanafunzi wa Computer Science alilazimika kukatiza masomo yake chuoni baada ya uamuzi wa serikali vyuo vifungwe.

Alijikuta akitumia muda mwingi nyumbani. Kupitisha muda akawa anashinda Tik Tok kucheki video za ucheshi za watu wengine. Ni pale wazo la kuanza kupakia video lilimshika.

“Kila mtu alikuwa akiizungumzia Tik Tok na nilipoingia na kuona video wanazotengeneza, nikaona mbona na mimi nisitengeneze za kwangu,” asema.

Ubunifu wake ukaishia kuzifanya video zake maarufu na taratibu akaanza kupata wafuasi kila kukicha. Video zake nyingi huwa ni za kudensi. Alifanya hivyo kwa muda kabla ya kugundua kwamba anaweza pia kutengeza pesa kupitia shughuli hiyo.

“Kwa miezi kadhaa sikujua kabisa kwamba ninaweza kuunda pesa hadi wakati mmoja jamaa fulani alinitaka nishiriki kwenye kampeni ya kuhamasisha mabinti kuhusu masuala ya hedhi. Alinilipa kiasi fulani cha pesa na hapo ndipo niligutuka,” afunguka.

Baada ya kuulizia mastaa wenzake alioona wakifanya vizuri, Ajib akapata ujanja na kutoka kipindi hicho, amekuwa akipiga biashara.

Wasanii wengi wamemlipa kupromoti nyimbo zao mpya kama vile Dufla na Mutahi Kigawe. Naye pia kalamba dili kadhaa za matangazo akiwa amefanya kazi na Bata, LG na Safaricom.

“Siwezi kupa idadi kamili ya fedha ninazotengeneza ila huwa ni kati ya Sh50,000 hadi Sh100,000 kwa kutegemea na aina ya dili,” Ajib anasema.

Alma Mutheu, 23

Mapenzi yake ya uigizaji ndiyo yaliyomsukuma kujiunga na Tik Tok 2019.

“Napenda kuigiza na Tik Tok ilipozinduliwa, nikaona hii ni fursa nzuri ya kuonyesha uwezo wangu sababu mfumo wa App hiyo ni video tu,” asema.

Kama tu Ajib, hakuwa na wazo kuwa anaweza kutengeneza pesa kupitia App hiyo. Hata hivyo baada ya kupata ufuasi mkubwa, alianza kutokea na kampuni kadhaa zilizotaka kushirikiana naye kutangaza bidhaa zao.

“Lengo langu lilikuwa ni kuonyesha kipaji changu na kuwafurahisha watu. Ila nilipopata habari kuwa naweza kupata fedha kupitia sanaa yangu, nikawa makini kujua mengi,” atupia.Kwa Alma mwenye wafuasi zaidi ya 280,000, huwa hakosi kiasi kisichopungua Sh30,000 kutokana na dili za biashara matangazo.

Mr Mbilimbili, 23

Gideon Musau anafahamika zaidi kwenye Tik Tok kama Mr Mbilimbili.

Video zake huwa ni za vichekesho. Alianza kutengeneza video zake za ucheshi 2017 na akawa anazipakia YouTube.

Agosti 2020 baada ya Tik Tok kuwa maarufu, aliamua kujiunga nayo na ikawa ndio mwanzo wa raha kwake.

“Toka zamani nilipenda kuigiza na nd’o sababu nilianza kupakia mizigo YouTube ila haikuwa ikifanya vizuri hadi nilipoanza kuposti Tik Tok,” anasema.

Akiwa na zaidi ya wafuasi 483,000 Mr Mbilimbili ni mmoja kati ya mastaa wa Tik Tok waliofanikiwa kusaini dili kadhaa za biashara matangazo na kampuni mbalimbali.

“Kwa mwezi ninaweza kutengeneza hadi Sh400,000 ila huwa inategemea na aina ya dili ninazopata,” anaongeza.

Ana timu ya wasanii wabunifu watatu ambao kwa pamoja hushirikiana kupiga mzigo.

MATHEKA: Kuongezeka kwa mapinduzi Afrika ni hatari kwa ustawi

Na BENSON MATHEKA

KUNA hatari ya hatua ambazo bara la Afrika limepiga katika kukuza demokrasia, kuporomoka kufuatia msururu wa mapinduzi ya kijeshi ya hivi majuzi katika nchi kadhaa.

Katika muda wa mwaka mmoja, wanajeshi wametwaa mamlaka katika nchi tatu kusini mwa jangwa la Sahara.

Wanajeshi wa kikosi maalumu walipindua serikali ya kiraia ya Mali ambapo Kanali Assim Goita alijitangaza rais.

Miezi michache baada ya Kanali Goita kuongoza mapinduzi Mali, wanajeshi walitwaa mamlaka Chad baada ya kifo cha Rais Iddris Derby.

Mwanawe Derby, Jenerali Mahamat Derby alitangazwa rais wa nchi hiyo kwa usaidizi wa Ufaransa iliyotawala nchi hiyo enzi za ukoloni.

Mapema mwezi huu Septemba, Kanali Mamady Doumbouya aliongoza wanajeshi wa kikosi maalum, kupindua serikali ya kiraia ya Guinea na kumzuilia Rais Alpha Conde.

Mapema Jumanne, serikali ya mpito ya Sudan ilitangaza kuwa ilizima jaribio la mapinduzi mwaka mmoja baada ya kuondolewa mamlakani kwa Rais Omar el Bashir.

Msururu wa mapinduzi haya unazua kumbukumbu ya hali iliyokumba nchi kadhaa za kusini mwa jangwa la Sahara miaka ya kwanza baada ya kupata uhuru.

Wimbi la mapinduzi miaka ya sitini na sabini lilisababishwa na ukosefu wa usawa, utawala wa kiimla na wanajeshi vijana waliotaka kuonja mamlaka baada ya kupata mafunzo ng’ambo.

Watawala wa kijeshi waliua na kuwazuilia wapinzani wao, walikandamiza haki za raia wao, wakapora rasilimali na matokeo yakawa ni bara la Afrika kudumaa kimaendeleo.

Katika baadhi ya nchi hasa zilizo na utajiri wa madini na mafuta, mapinduzi yalichochewa na mataifa yenye nguvu yaliyotaka kuweka viongozi waliojali maslahi yao.

Katika miaka ya themanini, mapinduzi yalififia huku nchi nyingi za Afrika zikikumbatia demokrasia na kuruhusu raia kuchagua viongozi.

Wale walioingia mamlakani kupitia mapinduzi waliruhusu ushindani wa kisiasa kupitia uchaguzi na baadhi wakashinda na kuwa viongozi wa kiraia.

Kwa miaka ambayo demokrasia ilinawiri Afrika, bara hili lilipiga hatua kimaendeleo.

Raia walichangia katika ujenzi wa nchi zao, watoto walisoma na miundomisingi ikaimarika kwa sababu ya uthabiti wa kisiasa.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi walikwamilia mamlakani huku wakibadilisha katiba za nchi zao wapate kuendelea kutawala, kutumia mamlaka kuiba kura wakati wa uchaguzi na kukasirisha raia wengi ambao ni vijana wanaotaka mabadiliko.

Ingawa mapinduzi ya kijeshi si tiba ya utawala mbaya, si ajabu wanaoongoza mapinduzi hayo ni vijana wanaotwikwa majukumu ya kulinda nchi zao na marais wanaowapindua na si waasi wanaopigana msituni.

Kuzuka upya kwa mapinduzi ya kijeshi, kunaweza kurejesha Afrika enzi za giza kwa kufuta demokrasia na ustawi.

WASONGA: Wabunge wapiganie kurejea kwa bei nafuu

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi na wabunge wameamua kuwachezea shere Wakenya kuhusiana na suala muhimu la bei ya mafuta wakijifanya kuwa watetezi wao.

Lakini ukweli ni kwamba Bw Muturi na wabunge wote 349 ndio wamewasababishia Wakenya madhila yanayowakumba wakati huu kutokana na ongezeko la bei ya mafuta kwa kiwango cha juu kupita kiasi.

Ni unafiki mkubwa kwa Bw Muturi, ambaye ametangaza azma ya kuwania urais 2022, kuamuru Kamati ya Fedha kuchunguza ikiwa kuna sababu nyinginezo zilizochangia hatua hiyo mbali na msururu wa ushuru ambao hutozwa bidhaa za mafuta.

Aidha, ameitaka kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay kuandaa mswada wa marekebisho ya sheria za ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kukinga bidhaa za mafuta kutokana na ushuru huo.

Bw Muturi aliamuru kamati hiyo kuwasilisha ripoti, na mswada huo bungeni baada ya siku 14 kuanzia Jumanne, Septemba 21, 2021.

Kabla ya Spika kutoa amri hiyo mjadala mkali ulishamiri bungeni huku wabunge wakielekeza ‘mishale’ ya lawama kwa serikali, Rais Uhuru Kenyatta na muafaka kati yake na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kwa kuwa nyongeza ya kati ya Sh7.5 na Sh12 kwa bei za petroli, dizeli na mafuta taa itaendelea kutekelezwa hadi Oktoba 14, agizo la Bw Muturi kwa wabunge halitawakinga wananchi dhidi ya makali ya bei hizo mpya zilizotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia sekta za Kawi na Mafuta (EPRA).

Kamati ya Bi Wanga itakapokuwa ikiwasilisha ripoti yake, na kielelezo cha mswada wa marekebisho ya sheria za ushuru, hapo Oktoba 7, tayari zitakuwa zimesalia siku saba kabla ya Epra kutangaza bei zitakazotumika kati ya Oktoba 14 hadi Novemba 14, 2021.

Isitoshe, hata ingawa Bw Muturi atatumia mamlaka yake kulingana na kanuni za Bunge kufupisha muda wa kushughulikiwa kwa mswada huo wa marekebisho ya sheria hiyo ya VAT, muda huo unaweza tu kupitshwa mapema mwezi Desemba.

Kwa mtazamo wangu, spika huyu na wabunge hawajawasaidia Wakenya kwa njia yoyote kwa hatua waliyochukua ya kuanzisha mchakato wa kuondoa ushuru huo ulioanza kutekelezwa baada ya wao kupitisha Mswada wa Fedha wa 2018.

Kadhalika, tayari kiongozi wa wengi Amos Kimunya na mwenzake wa upande wa wachache John Mbadi wamepinga kuondolewa kwa ushuru wa VAT wa kiwango cha asilimia nane kwa mafuta.

Bw Kimunya, ambaye ni waziri wa zamani wa Fedha, alisema kuondolewa kwa ushuru huo kutavuruga bajeti ya serikali na kuinyima mapato ya kiwango cha Sh35 bilioni kwa mwaka.

Ikizingatiwa kuwa Bw Kimunya ndiye mwakilishi wa Rais Kenyatta na serikali yake bungeni, uwezekano wa bunge kupitisha mswada utakaoandaliwa na kamati ya Bi Wanga ni finyu mno.

Pendekezo langu ni kwamba wabunge washinikize Serikali Kuu irejeshe afueni ya bei ya mafuta ili kudhibiti ongezeko la bei ya bidhaa hizo.

Hii ni kwa sababu mojawapo ya sababu zilizochangia ongezeko la bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa mwezi huu, kulingana na Epra, ni kuondolewa kwa nafuu hiyo ya kiwango cha Sh1.4 bilioni.

Pili, wabunge waandae sera ya kuihimiza serikali kuimarisha matumizi ya kawi mbadala kama vile mvuke na jua na upepo katika mahitaji ya kila siku badala ya kutegemea mafuta ambayo bei yake inapanda kila mara katika masoko ya kimataifa.

DOMO KAYA: Jamani nani kamkula fare?

Na MWANAMIPASHO

KUNA mjomba aitwaye Andrew Kibe.

Alianza kama utani kuchambua tabia za mademu wa Nairobi na jinsi wanavyowapa ugumu kina boy-child.

Kila kukicha lazima ungeamka kupata kaposti video akiwachambua mademu na tabia zao za kula fare na kisha kuwatoka watoto wa kiume.

Alipoanza posti zake, malengo ya Kibe yalikuwa ni kuwachanua watoto wa kiume namna ya kupambana na janja za mademu hasa wa Nairobi ambao kusema kweli ni wajanja ajabu. Usipokuwa makini nao, utalilia chooni.

Ghafla posti zake zikaanza kusambaa. Sio kwa sababu mara nyingi alisema vitu vya maana, hapana. Ila ni jinsi alivyokuwa akiwasilisha hoja zake kwa dizaini ambayo ilizua ucheshi sana.

Taratibu akaanza kuwa na ushabiki mkubwa. Mwenyewe nilikuwa shabiki wa Kibe sababu nyingi ya mada alizowahi angazia, binafsi zimewahi ‘nitokea. Jina lake lilipozidi kuwa kubwa, ghafla jamaa akawa ndiye gumzo mtaani. Akaanza kupata dili za ku-emcee shoo za mjini na klabuni.

Kabla mambo hayajakaa sawa, akapata dili kubwa ya kuajiriwa kazi NRG Radio. Kule aliunganishwa na mrembo Kamene Goro na kwa pamoja waliunda timu moja maridadi.

Walipiga shoo, wakavutia wateja na ushabiki mkubwa.

Kwa pamoja na Kamene, brandi yao ikawa kubwa na baada ya mwaka au miwili hivi kama sikosei, wakapata ulaji kujiunga na Kiss FM.

Shughuli iliendelea, Kibe aliendelea kutiririsha mawazo yake lakini ilifikia wakati akaanza kuonekana kama vile kazidi kwenye mashambulizi yake.

Kule Kiss ilifika wakati alizenguana na bosi na akaamua kuacha kazi. Ndio fursa hiyo ikapewa Jalang’o ambaye mpaka sasa anaendelea kupiga shughuli na Kamene.

Baada ya kuanza vizuri, ilifikia wakati alipoteza mwelekeo wake. Aliacha mada ya kuchambua tabia za mademu wa jiji na kuanza kumwingilia kila mtu.

Hata Kamene waliyekuwa na ukaribu naye kwa muda waliofanya kazi, sasa hivi wawili hao hawasikizani. Zile dili alizokuwa akipata za kuhosti mashoo, ghafla zikapotea.

Nakumbuka Kibe akimwingilia bloga Edgar Obare. Alimsimanga jamaa kwa kuchaji Sh5,000 kumtangazia mteja biashara kwenye mtandao wake wa kijamii. Jamaa alimcheka sana.

Kumbe muda wote alikuwa akimcheka kilema wakati kwake kipo. Alipoondoka Kiss FM, maisha yalimtandika na kumsukuma kuanzisha redio yake ya mtandaoni. Kwenye shoo yake hiyo aliyokuwa akipeperusha laivu, alikuwa akitoza Sh3,000 kumtangazia yeyote biashara.

Shoo yake haikudumu na nataka kuamini ni kwa sababu ya maongezi yake na tabia ya kushambulia chochote kile.

Nakumbuka miezi miachache tu kabla hajaondoka Kiss FM, alikutwa na kesi ya kushindwa kumlipa swahiba wake deni la nusu milioni ambalo lilikuwa limedumu kwa miaka saba. Mshikaji wake aliamua kumwitia maafisa wa usalama alipoanza kumzungusha. Baada ya kulala seli siku mbili-tatu, ni kama vile waliafikiana namna atakavyomaliza deni hilo. Nakumbuka bado akimchamba jamaa kwa kumdhalilisha.

Alikudhalilishaje wakati umeishi miaka na mikaka na deni lake na hutaki kulipa?

Siku hizi kila anapofungua mdomo wake, kila neno ni la kumkashifu mtu. Juzi kamwingilia Jalang’o kwa sababu ya kumsaidia yule muuza mtumba ambaye katrendi siku za hivi karibuni. Sijui kwa nini Kibe ana machungu.

Jalang’o kadai kuwa maisha ya jamaa hayamwendei poa na ndio sababu ana machungu kivile. Amejaribu vitu kadhaa lakini bado havijalipa. Kwa sasa kahamia Marekani lakini bado hajaacha kumtupia mtu yeyote cheche.

Haijalishi unachokifanya, ilimuradi unatrendi hata kwa uzuri, Kibe lazima aone ubaya na lazima akutemee maneno makali.

Nasadiki kabisa jamaa atakuwa ana machungu. Kama sio machungu ya maisha jinsi anavyodai Jalang’o labda pengine ni machungu ya kutendwa na demu. Hivi ni nani anaweza akawa amemkula Kibe fare?

KINYUA BIN KING’ORI: Masharti ya wandani kisiki kwa ‘handisheki’ ya UhuRuto

Na KINYUA BIN KINGORI

JUHUDI zilizoanzishwa na viongozi wa makanisa kupatanisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto, zinafaa kulenga maslahi ya Wakenya si binafsi ya viongozi hao wawili wenye mamlaka makuu serikalini.

Wandani wao wameanza kutoa masharti ambayo lazima yazingatiwe ili mapatano hayo kufanikiwa.

Aidha, wanalaumiana kwa kutoa vijisababu visivyo na maana, na huenda wakavuruga juhudi za viongozi hao kuridhiana.

Imebakia miezi 11 kwa serikali ya Jubilee kumaliza muda wake na kupisha utawala mpya baada ya uchaguzi mkuu 2022.

Lakini nyingi ya ahadi ambazo UhuRuto walitoa hazijatekelezwa.

Hakuna maendeleo ya kujivunia ambayo tumepata kipindi hiki cha pili, na katika kipindi hiki cha lala salama hatutarajii maendeleo yoyote ikiwa viongozi hao hawatazika tofauti zao.

Hivyo, kuna haja kubwa Wakenya kuunga mkono viongozi hao wapatane ili tuone ikiwa watasuka mipango ya haraka kuokoa wananchi na madhila ya uchumi mbaya sababu ya utendakazi duni wa serikali hii ya Jubilee.

Je, serikali ambayo viongozi wakuu wanatumia muda wao mwingi kulumbana, kuchimbana na kupigana kisiasa kwa manufaa yao, watarajia ipate muda lini kujua wananchi wamelemewa na ugumu wa maisha?

Je, wanaweza kupata suluhisho litakalohakikisha Wakenya wanaohangaika kwa makali ya njaa wamepata msaada wa chakula? Kushindwa kwa Jubilee kushughulikia matatizo yanayokumba Wakenya kumechochewa na uhasama kati ya Rais na Dkt Ruto.

Ajenda kuu ziliwekwa kando, miradi mingi kupuuzwa na mafaniikio waliyotuahidi ya maziwa na asali yamebakia kitendawili.

Badala yake, wamechochea chuki serikalini hadi bungeni ambako wabunge wanatekeleza wajibu wao kutegemea mrengo wao wa kisiasa wala si kwa manufaa ya wananchi walala hoi.

Leo hii tunaumizwa kwa bei ya juu ya mafuta baada ya wabunge kupitisha mswada wa kuongeza ushuru.

Maisha yataendelea kubakia magumu katika miezi michache inayokuja kabla uchaguzi, ikiwa Uhuruto hawatajitolea kumaliza uhasama wao.

Dkt Ruto ametangaza hadharani kwamba yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais bila masharti, naye Rais anafaa kujtokeza kukumbatia maridhiano ili juhudi za viongozi wa makanisa zifaulu.

Pia watumie nafasi hiyo kuelezea Wakenya kiini cha uhasama wao maana hatujui kilichoenda mrama baada ya uchaguzi wa 2017.

Rais na Dkt Ruto waweke kando maslahi ya binafsi na matamanio ya kisiasa ya 2022 ili kulenga msamaha na masikizano bila unafiki.

Taifa linahitaji mshikamano wao ili kumaliza baa la njaa, kuimarisha udhibiti wa corona na utoaji chanjo yake, kuunda nafasi za ajira kwa vijana, kuboresha elimu kwa kutatua changamoto zinazotishia ubora wa mtaala wa CBC, kupunguza gharama ya maisha, na kukamilisha miradi ya maendeleo kabla Agosti 2022.

Rais Kenyatta atafaulu kuacha nchi iliyo salama na yenye amani na umoja iwapo atapatana na naibu wake ili wamalize safari yao pamoja.

KAMAU: Mizozo UoN inatishia ndoto za vijana wetu

Na WANDERI KAMAU

MOJA ya ndoto zangu za utotoni ilikuwa kusomea katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Ingawa ndoto za utotoni hubadilika kadri mtu anapokuwa mkubwa, yangu haikubadilika kamwe. Ilibaki kwenye nafsi yangu.

Ulipofika wakati wa kuchagua kozi za kusoma nitakapoingia chuoni, karibu zangu zote zilikuwa katika chuo hicho.

Msukumo wa ndoto zangu ulitokana na sifa nzuri nilizosikia vijijini kuhusu taasisi hiyo, maarufu UoN.

Sifa hizo zilitokana na simulizi za wazee, walimu wangu na maelezo niliyosoma kwenye majarida kadhaa.

Watu wachache waliofaulu kujiunga na vyuo vikuu walikuwa wakialikwa katika shule za msingi kuwapa wanafunzi manufaa ya kujiunga na chuo kikuu.

Walitupa simulizi nyingi za kututia moyo, wakirejelea jinsi chuo cha Nairobi kilichangia uwepo wa watu maarufu kama Prof Ngugi wa Thiong’o, Prof Micere Githae Mugo.

Pia kuna Prof Arthur Obel (aliyeaminika kuvumbua tiba ya virusi vya HIV) na mwandishi Wahome Mutahi (maarufu kama Whispers) kati ya wengine wengi.

Binafsi, nilijipa msimbo wa ‘Whispers Junior’ – kwani nilimuenzi sana Wahome Mutahi na simulizi nilizopewa kumhusu.

Chuo Kikuu cha Nairobi kilikuwa na hadhi kubwa katika jamii kwa mchango wake katika kuendeleza nchi, hasa kupitia sekta ya elimu.

Hata hivyo, inasikitisha kuona taasisi hiyo ikiyumba.

Kwa sasa chuo kinakumbwa na mizozo si haba – hali inayozua wasiwasi kuhusu mustakabali wake.

Mzozo wa kwanza unatokana na tofauti kali ambazo zimezuka kati ya Naibu Chansela, Prof Stephen Kiama, na baadhi ya wasimamizi wakuu kufuatia pendekezo la kubadilisha utaratibu wa kiusimamizi wa UoN.

Mzozo wa pili umeibuka kati ya Prof Kiama na wanafunzi kutokana na hatua ya usimamizi wa chuo kuongeza karo maradufu na kodi ya malazi.

Kwenye malalamishi yao, wanafunzi wanadai hawakushirikishwa hata kidogo wakati maamuzi hayo yakiafikiwa.

Vivyo hivyo, malalamishi kama hayo ndiyo yametolewa na wasimamizi wa idara mbalimbali, ambao hawakuridhishwa na pendekezo la kuunganishwa kwa baadhi ya idara huku zingine zikifutiliwa mbali.

Kimsingi, ni kinaya kwa mizozo kama hii kushuhudiwa katika mojawapo ya taasisi muhimu sana ya elimu nchini.

Taasisi hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kupewa hadhi ya chuo kikuu nchini, baada ya Kenya kujinyakulia uhuru kutoka kwa wakoloni.

Kabla ya hapo, Wakenya wengi walioonyesha nia ya kuendeleza walikuwa wakienda katika vyuo vikuu vya nchi jirani, kama Makerere nchini Uganda na kile cha Dar es Salaam nchini Tanzania.

Inavunja moyo kuona mizozo, malumbano na mivutano inayozidi kuchipuka kwani inatishia kuzamisha na kupaka tope taasisi hiyo kubwa zaidi ya elimu ya juu nchini.

Madhara yake yatasambaa mbali kwani yatavunja ndoto za maelfu ya vijana vijijini wanaopania kusomea katika chuo hicho kwa wakati mmoja maishani mwao.

Wito wangu ni kwa usimamizi mkuu wa chuo kusuluhisha mizozo hiyo ili kurejesha hadhi yake tena kama ilivyokuwa awali.

akamau@ke.nationmedia.com

AKILIMALI: Magurudumu yanamvunia hela, ni kutia bidii tu!

Na WINNIE ONYANDO

BAADHI ya watu hutupa magurudumu baada ya matumizi ya muda ila kwake Joseph Mwaniki, 33, gurudumu lililotumika bado lina manufaa tele kwake.

Joseph alianza kazi hii ya kutumia magurudumu kuunda bidhaa tofauti mnamo 2012, alipoacha kazi kama ajenti wa kampuni moja ya bima.

“Mimi hukusanya magurudumu yaliyotumika, kuyasafisha na kutengeneza bidhaa tofauti. Pesa ninazopata kutoka kwayo ni nyingi hata mtu hawezi kuamini,” akaeleza Akilimali ilipozuru karakana yake katika soko la Kariokor, jijini Nairobi.

Yeye hutumia magurudumu hayo kutengeneza viatu, kanda, kamba za kufungia mizigo na pia zinazotumika katika uundaji wa makochi; sofa.

Hata hivyo, katika uundaji wa vitu tofauti, pia kuna vile ambapo hulazimika kujumuisha ngozi ya ng’ombe au ngamia, gundi na pia vitambaa pamoja na madoido mengine hasa kwa viatu ili kuvutia wateja.

Kwa siku, anasema, yeye hutengeneza zaidi ya jozi 50 za viatu na kujipatia faida ya takriban Sh5,000.

Kila jozi huwa anaiuza kwa kati ya Sh200 na Sh400.

“Mara nyingi mimi huuza viatu ninavyounda kwa wateja wa jumla, hasa kutoka jamii ya Wamaasai. Pia huwa ninawauzia wateja wa rejareja wanaofika kwa karakana yangu,” anaeleza.

Biashara hiyo anasema imemuwezesha kujiinua kimaisha kama kujenga nyumba nzuri na pia kumudu karo ya watoto wake wawili.

Hata hivyo, zipo changamoto na inayomkaba zaidi anasema ni ushindani mkubwa wa soko.

“Ubunifu ndio njia ya kujifaa katika biashara yoyote. Hii itakuwezesha kuwashinda washindani wako,” anashauri kuhusu mbinu anayotumia kuweza kukabiliana na changamoto hiyo.

TAHARIRI: TSC idhibiti zogo la shule haraka

KITENGO CHA UHARIRI

RIPOTI kuhusu uchomaji wa shule kubwa za upili humu nchini siku mbili zilizopita zinaibua hofu kuu kwa wazazi hasa ikikumbukwa kwamba mwaka huu wa masomo ni mfupi mno na wanafunzi, walimu wana kazi nyingi kukamilisha kabla ya Machi 2022.

Kando na miaka ya awali, wadau sasa wanahitajika kusomesha silebasi ya mwaka mzima katika wakati mfupi uliowekwa na wizara ya Elimu.

Katika hali hii, shule zinafaa kuwa na mazingira matulivu yatakayoyawezesha kufikia maazimio na malengo yao kimasomo, kama kupasi mitihani ijayo kwa alama za juu.

Serikali, walimu, wazazi, wanafunzi na wadau wote katika shule kwa jumla wanafaa kujukumika kufanikisha haya kwa ushirikiano.Matukio yalishuhudiwa katika Shule ya Upili ya Sigalame iliyoko kwenye Kaunti ya Busia ni kinyume cha matarajio haya.

Mojawapo ya mabweni ya shule hii iliripotiwa kuchomwa na wanafunzi kuagizwa kwenda nyumbani hadi uchunguzi kamili kuhusu tendo hilo la uhalifu huo ukamilike na suluhisho kamili na kudumu kupatikana.

Mbali na hasara kutokana na uharibifu wa vifaa vya wanafunzi katika bweni, hakuna madhara ya kiafya yalitoripotiwa kuwakumba wanafunzi.

Hali inayotamausha katika tukio hili ni kwamba, hii ni bweni la nne kuchomeka ndani ya mihula miwili pekee na bado kiini cha uhalifu huu hakijafichuliwa licha ya uchunguzi kufanywa kila wakati.

La wazi ni dai kwanza wanafunzi hawahusiki kabisa!Kulingana na Bodi ya Usimamizi (BOM) katika shule hii, tayari imewasilisha kwa Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC) malalamiko na ushauri kuhusu jinsi ya kukabili tatizo hilo lakini hatua ya dharura ilivyokatikana haikuchukuliwa na TSC kwa wakati uliofaa.

Kuna malalamiko chungu nzima ya usimamizi mbaya na ufisadi katika utoaji tenda ambapo kidole cha lawama kinaelekezewa Mwalimu mkuu na naibu wake.

Ni aibu pia kuona Shule ya Upili ya Ofafa Jericho katika Kaunti ya Nairobi ikijipata katika orodha hii ya uchomaji bweni siku moja baada ya wenzao wa Sigalame.

Tume ya TSC ikishirikiana na wizara ya Elimu inafaa kuingilia kati masuala ya kinidhamu kama haya kabla hayajaenea nchini ili kuhakikisha shule zinasimamiwa na walimu wenye maadili ya kipekee.

GWIJI WA WIKI: Fred Mutwiri

Na CHRIS ADUNGO

MSHUMAA hauzimiki kwa kuuwasha mwingine.

Maisha ni safari na safari ni hatua. Safari ya kitalifa kirefu huanza kwa hatua moja.

Kabla ya binadamu kupiga hatua yoyote safarini, huwa tayari ameipiga hatua hiyo akilini mwake. Kwa hivyo, ni dhahiri shahiri kuwa mtu afikirivyo ndivyo alivyo. Uko jinsi ulivyo leo kwa sababu wewe mwenyewe uliamini utakuwa hivyo tangu jana. Vyovyote vile uwavyo, jinsi utakavyokuwa kesho ni matokeo ya jinsi unavyoamini leo kuhusu hiyo kesho yako.

Jihisi kuwa mwenye thamani kwa sababu umeibeba sura ya Mungu aliyekuumba kwa mfano wake mwenyewe. Usikubali kushindwa na lolote maishani.

Katika kila ufanyacho au unachotarajia kutenda, ukitanguliza mawazo ya kushindwa, haitakuwa rahisi kufaulu.

Kama ambavyo neno litokalo kwa Mungu linavyoweza kuumba, ndivyo maneno ya kutoka vinywani mwetu pia yanavyoweza kutujenga au kutubomoa.

Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi. Kila tunachokiri ndicho hutokea. Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mawazo ya mtu na maneno ayanenayo. Ayazungumzayo mtu ndio yanayoujaza moyo wake.

Tofauti kati ya kuku na tai ni nia. Penye nia pana njia. Ni wajibu wa kila mja kuteua iwapo anataka kuwa kuku asiyepaa ama tai anayepaa upeo wa kupaa. Kufaulu kwako ni zao la juhudi. Bahati ni chudi na nidhamu ndiyo dira kamili katika maisha.

Azimia kutimiza ndoto zako kwa kuwa mafanikio hayaji kwa kulaza damu bali kwa kupinda mgongo na kujifunga kibwebwe.

Huu ndio ushauri wa Bw Fred Mutwiri – mwanafunzi wa shahada ya uzamifu na mwandishi mahiri anayefundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Lawrence Nziu Girls, Kaunti ya Makueni.

MAISHA YA AWALI

Mutwiri alizaliwa mnamo 1992 katika kitongoji cha Nkandone, Kaunti ya Meru. Ndiye mtoto wa sita katika familia ya Bi Martha Kabiro na Bw John Ngore.

Hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ilianza kujikuza ndani ya Mutwiri tangu utotoni. Alikuwa mwepesi wa kusoma habari shuleni na kanisani huku akiiga sauti za watangazaji maarufu wa redioni. Alistahiwa pakubwa na wanafunzi na waumini kwa upekee wa kipaji chake cha ulumbi.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Nkandone, Meru. Alisomea huko hadi darasa la saba kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Naathu, Meru. Nusura ndoto zake za masomo ziyeyushwe na pigo la kufariki kwa baba mzazi mnamo 2004.

Kwa imani kwamba penye mawimbi na milango ya heri i papo hapo, Mutwiri alianza kuishi kwa kumtegemea mama mzazi ambaye hakuwa na kazi yoyote ya staha na haiba.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) katika Shule ya Upili ya Igembe Boys, Meru mnamo 2009 na akajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Anakiri kuwa mapenzi yake kwa masomo ya lugha ni zao la kuhimizwa mara kwa mara na Bw Irai aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya upili. Wengine waliochangia ari yake ya kukichapukia Kiswahili ni Prof Rayya Timammy, Dkt Ongarora na marehemu Prof Ken Walibora.

UALIMU

Mutwiri alianza kufundisha mnamo 2013 akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Chuka kuanzia 2015. Alifuzu mwaka wa 2019 baada ya kuwasilisha tasnifu “Muundo wa Sentensi ya Kiigembe: Mtazamo wa Eksibaa” chini ya usimamizi wa Prof John Kobia na Dkt Allan Mugambi.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo 2017 na kumtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya St Lawrence Nziu Girls Makueni. Baada ya kukamilisha shahada ya uzamili, Mutwiri alirejea katika Chuo Kikuu cha Chuka mnamo 2020 kwa minajili ya shahada ya uzamifu (phD). Analenga kufuzu mnamo 2022.

UANDISHI

Mutwiri alikuwa na mazoea ya kuandika hadithi za kubuni pamoja na mashairi alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Utashi wake wa kuandika ulichochewa zaidi na wahadhiri wake wa shahada ya uzamili wakiwemo Prof Kobia, Dkt Erastus Miricho na Bw Bitugi Matundura.

Waliomhimiza aanze kuchapisha kazi zake ni marehemu Bernard Omwega Osano (Kaka Benosa) aliyekuwa mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi na Bw Timothy Omusikoyo Sumba – mwandishi stadi na mhariri mzoefu wa vitabu vya Kiswahili.

Kufikia sasa, Mutwiri amechapishiwa makala ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida ya kitaifa na kimataifa.

Mwalimu Fred Mutwiri. Picha/ Chris Adungo

Alishirikiana na Prof Miriam Mwita wa Chuo Kikuu cha Mashariki ya Afrika Baraton kuandika makala ‘Usawiri wa Wahusika wa Jinsia ya Kiume katika riwaya ya Chozi la Heri’ na yakafyatuliwa katika jarida Mwanga wa Lugha’.

‘Muundo wa Virai vya Sentensi ya Kiigembe’ ni makala aliyoandika kwa kushirikiana na Dkt Allan Mugambi na yakachapishwa na ‘East African Scholars Journal of Education, Humanities and Literature’.

Mbali na riwaya ‘Joka Kitandani’, Mutwiri ameandika kitabu ‘Fumbo la Fasihi’ na msururu wa vitabu vya mazoezi na marudio ‘Futari Njema ya Fasihi Simulizi’, ‘Futari Njema ya Isimujamii’, ‘Futari Njema ya Kigogo’, ‘Futari Njema ya Chozi la Heri’ na ‘Futari Njema ya Tumbo Lisiloshiba’.

Aidha, ametunga hadithi fupi ‘Sumu Tamu’, ‘Karakana ya Upatanisho’, ‘Ningali Hai’, ‘Fumbo la Fumba’, ‘Bibi wa Tajiri’, ‘Si Ndoto Tena’, ‘Joka la Baharini’ na ‘Nzige’.

‘Siri ya Insha’ ni kitabu ambacho Mutwiri aliandika kwa pamoja na Bw Steven Mativo na mwalimu Allan Babashi wa Starehe Boys Centre & School mnamo 2021.

Baadhi ya mashairi yake yamechapishwa katika diwani ‘Malenga wa Afrika’ iliyohaririwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Timothy Omusikoyo Sumba na Fatma Ali Mohammed kutoka Zanzibar.

Mutwiri anatarajia kutoa kitabu ‘Fumbo la Sarufi Mtindo wa KCSE’ mwaka huu 2021.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Mutwiri ni kuweka hai ndoto yake ya kuwa profesa wa Kiswahili na mhadhiri katika vyuo vikuu.

Anajivunia kuelekeza idadi kubwa ya chipukizi katika sanaa ya uandishi kupitia ‘YouTube’ (Mutwiri Fred).

Kwa pamoja na mkewe, Bi Ruth Kaimuri, wamejaliwa mtoto mmoja: Mellisa Gatwiri.

TAHARIRI: Sarakasi hazimfai raia anayeumizwa

KITENGO CHA UHARIRI

WANANCHI wanapoendelea kuumizwa na bei ya juu ya mafuta, kila mtu anajaribu kujiondolea lawama.

Maseneta, kwa kutaka kujipendekeza kwa wapigakura, jana Jumanne walijaribu kufurahisha umma kwa kutaka kuwahoji mawaziri wawili. Mawaziri hao John Munyes (Petroli) na Charles Keter (Kawi) walipuuza mwaliko huo.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, ambaye aliongoza Bunge mwaka 2018 kupitisha Mswada wa Fedha, safari hii amejitokeza kuwa mkosoaji.

Akizungumza wikendi eneo la Runyenjes, Embu, Bw Muturi aliwataka wabunge wawasilishe bungeni marekebisho ya sheria hiyo.Siku walipopitisha, Bw Muturi alionekana kusukuma wabunge waharakishe shughuli hiyo, bila kusikiza waliokuwa na pingamizi.

Maseneta, kwa kutaka kujipendekeza kwa wananchi, walichukua jukumu lisilo lao. Waliwaita mawaziri kujadili kuhusu Sheria ya Fedha (2018), ambayo ushuru uliopendekezwa umeanza kuonekana athari yake.

Wakenya wanapopambana na ugumu wa maisha kutokana na janga la Corona, ipo haja ya kuangalia upya sheria hiyo. Kwa sababu ya ushuru kupita kiasi kwenye bei ya mafuta, bidhaa hiyo ni ghali humu nchini kuliko ilivyo Uganda.

Taifa lisilokuwa na bandari, linalotoa mafuta yake kwenye bandari ya Mombasa na kuyapitishia nchini, linauza lita moja ya petroli Sh4300 za Uganda, sawa na Sh131 za Kenya.

Hiyo ndiyo bei ya juu zaidi Uganda, ikilinganishwa na Sh147 mjini Mandera.

Maseneta wanafahamu kwamba Katiba inalipatia Bunge la Taifa jukumu na mamlaka ya kuhusika na masuala ya fedha. Mswada uliopandisha ushuru wa mafuta unaweza tu kurekebishwa na wabunge.

Si maseneta wala mawaziri.

Ndio maana mawaziri Munyes na Keter ambao ni maseneta wa zamani, walikataa kufika mbele ya Seneti.

Walijua mwaliko huo ni sarakasi tupu.

Ingawa Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga aliamua kwamba sheria hiyo ya ushuru ni batili, Serikali imeonyesha siku za nyuma kuwa haiheshimu maamuzi ya korti.

Kinachohitajika sasa ni mbunge yeyote kuunda mswada wa marekebisho ya sheria hiyo.

Mswada huo ujadiliwe kwa haraka na kuondoa sheria inayotoza ushuru zaidi kwa mafuta.

Bila hivyo, agizo la Spika kwamba Kamati ya Fedha ichukue wiki mbili kuangalia suala hilo, ni sarakasi isiyowaondolea dhiki wananchi.

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya wavulana ya Mukaa (CHAKIMU)

Na CHRIS ADUNGO

CHAKIMU ni chama kinachochangia matumizi bora ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys’ iliyoko viungani mwa mji wa Salama, Kaunti ya Makueni.

Chama hiki kiko chini ya Idara ya Lugha inayoshughulikia Kiswahili na Kiingereza katika Shule ya Upili ya Mukaa.

Mwalimu Mkuu, Bw M. Tuke huhakikisha kuwa magazeti ya ‘Taifa Leo’ yamesomwa na wanafunzi wote kila siku. Pia anawanunulia vitabu vya kudurusu ili kuboresha matokeo ya somo la Kiswahili katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE).

Kwa mujibu wa Bw Deon Musau ambaye ni mlezi wa CHAKIMU, wanafunzi wake hudumisha umahiri wao katika Kiswahili kwa kujizolea alama nzuri katika mitihani ya KCSE. Siri ya mafanikio yao ni mazoea ya kusoma magazeti ya ‘Taifa Leo’ kila siku.

Isitoshe, lugha sanifu itumiwayo katika uandishi wa habari na makala katika gazeti la ‘Taifa Leo’ huwanufaisha sana wanafunzi. Wanachama huangazia masuala mbalimbali ya Kiswahili yaliyo na faida darasani na nje ya darasa.

Kufikia sasa, idadi ya wanachama wote ni mia nne. Watahiniwa wa KCSE ambao huwa wanachama wa CHAKIMU wameendeleza desturi ya kusajili matokeo bora zaidi katika somo la Kiswahili.

CHAKIMU kina vitengo mbalimbali vinavyosaidia wanachama umilisi wao katika Kiswahili. Vitengo hivyo ni pamoja na: kitengo cha ushairi, kitengo cha sanaa na uigizaji, kitengo cha sarufi, kitengo cha utangazaji na kitengo cha tafsiri na ukalimani.

Wanachama wengi huishia kutambua talanta zao kutokana na uwepo wa vitengo hivi kwa sababu madhumuni ya chama ni kuwapa wanafunzi jukwaa mwafaka la kukuza vipaji vyao vya utambaji wa hadithi, uchoraji, uigizaji, uanahabari na utunzi wa mashairi.

Chama kina wawakilishi kutoka kila kidato wakiongozwa na Calvin Mutoko (Mwenyekiti), Michael Muoki (Naibu Mwenyekiti), Abraham Kisua (Mhazini), Peter Njoroge (Mwakilishi wa Kidato cha Nne), Collins Kyengo (Mwakilishi wa Kidato cha Tatu), Geoffrey Kimeu (Mwakilishi Kidato cha Pili) na Daniel Mui (Msimamizi kitengo cha sarufi).

Chama huandaa vikao vya mara kwa mara kwa lengo la kuwashirikisha wanafunzi kikamilifu katika mashindano yanayolenga kubaini upekee wa talanta zao.

Chama kinapania pia kushiriki na kuchangia mijadala ya kitaaluma kuhusu Kiswahili kupitia vipindi vya lugha ambavyo huendeshwa katika vituo mbalimbali vya redio na runinga za humu nchini.

Kuwepo kwa CHAKIMU kumeamsha ari ya mapenzi ya Kiswahili miongoni mwa wanachama ambao kwa sasa ni mabalozi halisi wa Kiswahili na wasomaji wakubwa wa gazeti la ‘Taifa Leo‘ katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys.

Bw Musau anaamini kuwa chama hiki kitawabadilisha wanafunzi wengi na kuwapa uwanja mpana wa kuzamia taaluma zinazohusiana na Kiswahili katika siku za usoni.

NGILA: Teknolojia mpya ya mbegu sawa ila wapi hamasisho?

Na FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita nilihudhuria uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya kilimo barani Afrika ambapo matokeo ya utafiti kuhusu mbegu yalitolewa.

Habari njema ni kuwa matumizi ya teknolojia yamepelekea kuimarika kwa ubora wa mbegu wanazopanda wakulima wa humu nchini, hali inayochangia kwa juhudi dhidi ya ukosefu wa chakula nchini.

Ripoti hiyo iliyotangazwa na shirika la The African Seed Access Index (TASAI) ilionyesha kuwa visa vya mbegu feki kusambazwa mashambani vimepungua kutoka 36 mwaka wa 2013 hadi 12 mwaka wa 2019.

Pia, ilieleza kuwa jitihada za kampuni za mbegu nchini katika kutokomeza uuzaji wambegu feki umeimarika kutoka asilimia 39 mwaka wa 2013 hadi asilimia 70 mwaka wa 2019.

Lakini ni teknolojia gani hasa, ilitumika kupata matokeo haya?

Kimsingi, wakulima hununua mbegu katika maduka ya kuuza mbegu. Katika karatasi za kupakia mbegu hizo, kuna nambari 12 ambazo zimefichwa kwa stika.

Wakulima hukwaruza stika hizo na kufichua nambari hizo ambazo wanatuma bila malipo kupitia ujumbe mfupi wa SMS na kupokea ujumbe mara moja kuthibitisha kuwa mbegu hizo ni halali.

Kwa mara ya kwanza, nimeona sheria ambazo serikali imeweka kulinda wakulima zikifuatwa.

Katika sheria za kilimo, mbegu zote ambazo zinauzwa kwa mifuko ya chini ya kilo tano inatakiwa kuwa na stika za ithibati.Huu ndio uwezo mkubwa wa teknolojia.

Bila ubunifu huu, mbegu nyingi zinazopandwa Kenya zingetuletea mazao dhaifu tu na kuchangia baa la njaa ambalo hukumba nchi hii kila mwaka.

Hata hivyo, juhudi hizi zinahitaji kupigwa jeki kwani si wakulima wote wanatambua kuwa kuna stika katika mifuko ya mbegu wanayonunua.

Utafiti tofauti uliofanywa na Muungano wa Biashara ya Mbegu nchini (STAK) katika kaunti nane umefichua kuwa kiwango cha wakulima wanaojua kuwa kuna stika hizi ni asilimia 85 kwa wastani.

Hii inamaanisha kuwa asilimia 15 ya wakulima bado wamo katika hatari ya kupanda mbegu feki sababu kuu ikiwa ukosefu wa Habari kuhusu teknolojia hiyo.

Lakini katika utafiti mwingine, licha ya asilimia 85 kutambua stika hizo, ni asilimia 35 pekee kwa wastani ambao wanazikwaruza na kutuma nambari kupitia arafa kuthibitisha ubora wa mbegu.

Yaani, tunajua umuhimu wa teknolojia lakini hatuitumii kutufaa katika njia ambayo inastahili. Sasa basi inakusaidiaje iwapo matapeli watanunua au kuunda stika feki na kupachika kwenye mfuko wa mbegu?

Licha ya kupungua kwa visa vya mbegu feki, bado kuna hatari kuwa ya kuendelea kupata mazao duni hali ambayo katika miaka ya hivi majuzi imekuwa ikipandisha bei ya chakula nchini na kuumiza wananchi ambao tayari wamechoshwa na kupanda kwa gharama ya Maisha kila mwezi.

Ni wajibu sasa wa serikali, kupitia Wizara ya Kilimo, kueneza Habari kuhusu stika hizi katika kaunti zote. Uhamasisho kwa wakulima wadogo na wakubwa ndio utaifaa nchi hii iwapo tunataka kujitegemea katika uzalishaji wa chakula.

SAUTI YA MKEREKETWA: Wizara sasa ifanye uamuzi imara kuhusu vitabu teule vya fasihi

Na HENRY INDINDI

MOJA katika mambo yaliyozua mijadala mikali katika siku za hivi majuzi ni kusuasua kwa uamuzi kuhusu kuteuliwa kwa ama ‘Nguu za Jadi’ au ‘Paradiso’ miongoni mwa vitabu vingine vilivyoteuliwa vya fasihi.

Yamkini, kulikosekana uwazi katika uamuzi uliofanyika na kusema la haki kufikia sasa, walimu wananunua chochote katika vitabu hivi kwa matumaini ya kuteuliwa kimojawavyo.

Haya yameisawiri serikali kama isiyo na uwezo wa kufanya uamuzi bora au pengine inayokosa uwazi katika uamuzi muhimu kama huu.

Kadri tunavyoendelea kuchukua muda mwingi kuteua kitabu kitakachofunzwa na kutahiniwa ndivyo tunavyowakanganya wazazi na wanafunzi.

Tunaonekana kukiri peupe kwamba kweli huwa na au kulikuwa na mchezo mchafu katika uteuzi huo wa vitabu.

Taswira inayojengwa miongoni mwa wazazi, walimu na wanafunzi wetu kulihusu hili inatuacha na maswali mengi kuhusu ikiwa kweli tuna nia na tunaweza kupambana na ufisadi nchini.

Kwamba imepita miezi hii yote bila kutumwa rasmi kwa barua ya kulielekeza taifa, wazazi, walimu na wanafunzi kuhusu vitabu vilivyoteuliwa, ni dhahiri kwamba kuna tatizo kuhusu jinsi tunavyoiendesha elimu yetu.

Tusipohimiza na kujikumbusha kuhusu uwazi na haki katika usimamizi wa elimu, tutatoa wapi ujasiri wa kuwahimiza wanafunzi katika shule zetu kuujenga umilisi huo? Tutakuwa tukiwaeleza nini kimsingi kuhusu haja ya uaminifu na uwazi katika utendakazi wao maishani?

Mwelekeo

Hivi leo ningekuwa waziri wa elimu, baada ya kubaini kwamba mchakato huo ulikuwa na walakini mahali, ningechukua hatua ya kimakusudi kuukita msimamo wa wizara kulihusu hilo.

Ni ama ningeagiza mchakato huo kurudiwa na kuuhakikishia uwazi au ningechukua vitabu kutoka kwa mashirika ya serikali vilivyoshiriki katika mchakato huo wa uteuzi na kuuzima mjadala huu kwa msimu mzima.

Haiwezekani kukaa kwa kipindi hiki chote bila mwelekeo imara kulihusu suala hili.Uamuzi wa kuchukua vitabu kutoka kwa mashirika ya serikali ungetokana na ukweli uliopo kwa sasa kwamba serikali hununua vitabu na kuwapa wanafunzi shuleni.

Itakuwa picha ya aina gani kwa serikali kugharimika kusambaza vitabu vya mashirika ya kibinafsi kwa pesa ambazo si ufadhili kutoka nje?

Ufadhili kutoka kwa mashirika ya nje ni raslimali za kuwafaa wote kwa hivyo ufadhili huo ni haki ya kila shirika na kila mwananchi.

Ni katika ufadhili kama huo tu ambapo serikali inaweza kusambaza vitabu kutoka kwa mashirika ya kibinafsi.

Vitabu vinavyosambazwa shuleni kama vya mfumo wa umilisi na utendaji (CBC) ni zao la ushirikiano na wafadhili na hii ni haki ya kila mmoja.

Lakini kuchukua pesa za serikali kununua vitabu kutoka kwa mashirika ya kibinafsi huku kukiwa na vitabu vya kutoka kwa mashirika ya serikali ni moja tu katika hatua za kuuendeleza uozo huo.

Vinginevyo, kwa vitabu vya fasihi na vya kiada ambavyo havina ufadhili kutoka nje, serikali ijiondoe katika mchakato huo na kuyaachia mashirika uwanja huru wa kufanya biashara.

KINA CHA FIKIRA: Asilan usimchape na kumtesa punda akubebeaye mizigo

Na WALLAH BIN WALLAH

WAJIBU wa wanadamu ni kufaana na kusaidiana katika kuishi.

Unifae nikufae; unisaidie nikusaidie.

Huo ndio utu na uungwana kwa watu wenye hekima na busara isiyoleta hasara maishani. Hekima na busara husaidia sana katika utekelezaji wajibu kuboresha maisha duniani.

Kwa hakika binadamu tumeumbwa kufaana wala si kufanana!

Tunaishi kwa kutegemeana na kuegemeana kama mafya au mafiga ya mekoni ndipo tupate mafanikio! Kila mtu anahitaji ushirikiano wa mwenzake katika kuishi.

Mara nyingine, hutokea mwanadamu akahitaji huduma na uwezo wa wanyama wengine pia ili kuwasaidia kufanya kazi.

Viongozi wa serikali nchini huhitaji juhudi za raia au wananchi wachapakazi wajitoleao kujenga taifa lipate maendeleo.

Taifa lisilokuwa na wananchi wachapakazi haliwezi kuendelea! Raia ndio watumishi wa kuitumikia nchi.

Ni bora watunzwe vyema na wahudumiwe vizuri kwa kuwa wao ndio wamejitwisha na kutwishwa mizigo ya kuijenga nchi. Wananchi ndio nguvukazi na uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Kwa hivyo, wasiteswe wala kunyanyaswa kulihali!!Wakuu na waajiri wote wenye miradi ya uzalishaji mali huhitaji wafanyakazi wa kuwasaidia kuinua viwango vya mapato kazini.

Kampuni zote au mashirika na viwanda vya uchumi na biashara huwategemea pakubwa wafanyakazi wao!

Mwajiri na mwajiriwa, wote wanafaana na kutegemeana sawasawa kama sahani na kawa katika kuleta faida kazini.

Muhimu tuelewe kwamba mfanyakazi si mtu duni. Bila huyo mfanyakazi, kazi haifanyiki! Mwajiri naye asipokuwapo, mwajiriwa hana kazi. Lakini mwajiri hawi mtenda yote bila nguvu za mfanyakazi!

Mkondo huu wa kutumikiwa na kutumikia ndio unaoitwa kutumikiana au kufaana!

Mtumikiwa asimpuuze na kumnyanyasa mtumikiaji kwa kumchukulia kuwa ni punda mbeba mizigo tu! Mara nyingi Babu yangu Mzee Majuto aliniambia, ‘Mjukuu wangu, mtu yeyote anayekusaidia kufanya kazi ya kuzalisha mali, anakuongezea mchango adhimu na ufanisi katika kukuza mali yako! Umtunze vizuri kwa mchango wake wa kukusaidia kufanya kazi. Wafanyakazi wowote wale: walimu, wakulima, wavuvi, askari, madaktari, mawakili, madereva, waandishi, wanahabari, wachuuzi, marubani, wapagazi, matopasi na wengineo ni wadau wakuu wa kuzalisha mali na kuboresha uchumi nchini! Watukuzwe!’

Ndugu wapenzi, mtu yeyote anayekufanyia kazi, anakusaidia kubeba mzigo wa uchumi na maendeleo!

Mtu huyo ni sawa na punda ambaye amekubebea mizigo mizito ya mali ambayo labda usingebeba peke yako! Umheshimu! Usimpige! Umlipe vizuri na kumtunza tu! Usimnyanyase! Usimtese na kumchapa punda anayekubebea mizigo! Unamchapia nini ilhali amekusaidia kukubebea mizigo????

Kwake, fursa ya kumsalimia Mzee Jomo Kenyatta ilikuwa ni ya kipekee

Na SAMMY WAWERU

MZEE Jomo Kenyatta alikuwa kiongozi aliyethamini bidii katika kazi.

Kulingana na Moses Gitonga, ambaye amewahi kuhudumu katika kikosi cha jeshi la Kenya, chini ya utawala wa Rais huyo mwanzilishi wa taifa hili, aliyepata fursa kutangamana naye lazima angekuwa mhudumu mchapakazi.

Gitonga alihudumu katika kikosi cha jeshi kwa muda wa miaka mitano pekee.

Ni mwalimu kitaaluma, ila aliacha gange hiyo kujiunga na jeshi la Kenya.

“Nilikamilisha kozi ya mafunzo ya ualimu mwaka wa 1974, nikafunza mwaka mmoja pekee,” adokeza.

Alijiunga na kikosi cha jeshi mwaka wa 1975, na akafuzu tayari kuhudumia Kenya.

Chini ya kipindi cha muda wa miaka mitano aliyochapa kazi, mengi yalitokea.

Moses Gitonga wakati akiwa afisa wa kikosi cha jeshi la Kenya alipata fursa ya kukutana na Mzee Jomo Kenyatta, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya ambapo alimsalimia. Picha/ Sammy Waweru

Gitonga alikuwa mfyatuaji risasi hodari, na alipanda ngazi kuwa Kamanda wa kitengo cha Platuni.

“Miaka miwili na mitatu baadaye, nilipandishwa madaraka na kuwa Kapteni,” Mzee Gitonga asema.

Ni madaraka yaliyojiri kupitia mafunzo ya kipekee katika kikosi cha kijeshi, mitihani na mbinu za uongozi.

Hadi wakati wa kutoka kikosini, kwa kile Gitonga anataja kama kuchukua “staafu ya mapema”, alikuwa amekwea hadi wadhifa wa Luteni.

Ni kufuatia jitihada na bidii ambapo Gitonga aliteuliwa kuwa miongoni mwa maafisa wa kijeshi waliopata mwanya wa kipekee kukutana na Mzee Jomo Kenyatta, ambaye ndiye baba wa Rais wa sasa, Uhuru Muigai Kenyatta.

Baada ya vuguvu la Maumau kuondoa serikali ya Mbeberu, Mzee Jomo Kenyatta alihudumu kama Waziri Mkuu kati ya 1963 – 1964.

Aidha, kati ya 1964 hadi kufariki kwake mwaka wa 1978, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya.

“Mzee Jomo Kenyatta alipenda wafanyakazi wenye bidii na waliojotolea katika huduma walizopokezwa,” Gitonga aelezea, akikumbuka alivyokutana na Rais huyo mtangulizi wa Jamhuri ya Kenya.

Vilevile, Gitonga anamtaja Marehemu kama kiongozi aliyethamini amani, utangamano na umoja wa taifa, kando na kuwa Rais aliyetilia mkazo umuhimu wa elimu na kuondoa umaskini katika jamii.

“Alikuwa ameunga misuli, na wakati wa kukusalimia mikononi, ilikuwa ni lazima uwe imara na ngangari,” afisa huyo asema.

Gitonga pia alitangana na Mkuu wa Majeshi enzi hizo, Meja Jenerali Jackson Kimeu Mulinge.

Mkuu huyo wa majeshi pia alihudumu katika serikali ya Rais mstaafu, Daniel Arap Moi, ambaye kwa sasa ni marehemu.

Jenerali Mulinge alifariki mwaka wa 2014 akiwa na umri wa miaka 91.

“Jenerali Mulinge alisaidia kuokoa serikali wakati wa jaribio la kuipindua mwaka 1982,” Gitonga asema, akisisitiza kwamba afisa wa jeshi anapaswa kuwa mkakamavu, jasiri na mwenye bidii.

Mbali na kupandishwa madaraka, Gitonga pia alipata tuzo ainati, ikiwemo kombe la hadhi.

Ni mkazi wa Gilgil, Kaunti ya Nakuru, na baada ya kuondoka serikalini aliingilia shughuli za kilimo na ufugaji.

Isitoshe, ni mwanaharakati, mtetezi wa haki za wanyonge, ambapo anafichua si kesi moja, mbili au tatu amewasilisha kortini kutetea maslahi ya wananchi na pia vipande vya ardhi ya umma iliyonyakuliwa kuona kwamba ardhi hiyo inarejeshwa.

“Kuna baadhi ya kesi ambazo nimeshinda, na nyingine nyingi zingali zinaendelea kusikilizwa,” Mzee Gitonga asema.

SHINA LA UHAI: Hofu ya ongezeko la saratani ya mapafu nchini

Na PAULINE ONGAJI

MIAKA mitatu iliyopita, Jess*, mkazi wa mtaa wa Kayole jijini Nairobi, aligundulika kuugua saratani ya mapafu ikiwa katika awamu ya tatu.

Kabla ya utambuzi huo, binti huyu ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 28 pekee, aliteseka kwa muda mrefu huku akisaka matibabu kutoka kwa hospitali mbalimbali, bila kupata nafuu.

“Tatizo lilikuwa kwamba kila nilipoenda hospitalini, daktari alitambua maradhi tofauti hivyo kunibadilishia dawa,” aeleza.

Wakati huo asema, alionyesha ishara za maradhi tofauti.

“Nakumbuka kabla ya maradhi haya kugundulika, nilikuwa nakohoa damu na nilikumbwa na maumivu mengi. Aidha, wakati huo pia nilipatikana na Kifua Kikuu-TB, suala lililotatiza juhudi za madaktari kutambua nilichokuwa naugua haswa. Hata hivyo nilitibiwa TB na kukamilisha matibabu,” aeleza.

Lakini ajabu ni kwamba hakujulisha jamaa na marafiki kwamba amepatikana na saratani ya mapafu.

“Nilificha hali yangu kwa sababu wakati huo nilikuwa kiongozi wa vijana kanisani na nilichukulia maradhi haya kuwa ya aibu. Kumbuka kwamba ugonjwa huu mara nyingi huhusishwa na uvutaji sigara. Niliona iwapo ningetangaza hali yangu, basi ningetengwa,” aeleza.

Aidha, alihofia kwamba kutokana na sababu kuwa alikuwa anafanya kazi katika sekta ya utalii, angepoteza ajira.

Hata hivyo, kwa bahati nzuri mwaka wa 2019, alifanyiwa upasuaji ambapo pafu lake moja liliondolewa.

“Aidha, baada ya upasuaji huo, nilifanyiwa awamu sita za tibakemia, taratibu zilizochukua miezi minne kukamilisha. Kwa sasa bado naendelea na uchunguzi wa kimatibabu kuhakikisha kwamba kansa hiyo haitarejea,” aeleza.

Kulingana na ripoti ya utafiti iliyozinduliwa na Wizara ya Afya miezi miwili iliyopita, 39% ya vifo nchini 2020, vilitokana na maradhi yasiyosambaa ikilinganishwa na 27% mwaka wa 2014.

Aidha inatabiriwa kwamba vifo vinavyotokana na maradhi yasiyosambaa vitaongezeka kwa 55% kufikia 2030.

Kulingana na utafiti huo, maradhi yasiyosambaa yameonekana kuendelea kuongezeka nchini na sasa yanasemekana kusababisha 46% ya vifo vyote nchini, huku walio chini ya umri wa miaka 40 wakionekana kuathirika pakubwa.

Ongezeko hili linasemekana limetokana na mitindo duni ya kimaisha ikiwa ni pamoja na matumizi ya tumbaku, kutozingatia lishe bora, kutofanya mazoezi na unywaji pombe kupindukia.

Kwa upande wa kansa ya mapafu, utambuzi wake huwa kwa viwango sawa (11.6%) na vile vya kansa ya matiti.

Hata hivyo, kansa ya mapafu huua watu zaidi kwa mwaka ikilinganishwa na ile ya matiti, utumbo na tezi kibofu kwa jumla.

Kulingana na takwimu zilizochapishwa na Shirika la Afya Dunia – WHO – miaka mitatu iliyopita, vifo vinavyotokana na kansa ya mapafu nchini Kenya, vilifika 481 au 0.19% ya idadi yote ya vifo.

Aidha, viwango vya vifo ni 2.67 kwa kila idadi ya 100,000 ambapo Kenya imeorodheshwa nambari 152 miongoni mwa mataifa yaliyoathirika pakubwa duniani.

Makadirio ya kansa ya mapafu kutoka kwa WHO (GLOBOCAN) 2020, yanaonyesha kwamba mwaka jana, idadi ya wagonjwa wapya wa maradhi haya humu nchini ilikuwa 794.

Aidha, takwimu hizo zinaashiria kwamba wagonjwa 729 walifariki kutokana na maradhi hayaUlimwenguni, idadi ya vifo vinavyotokana na kansa hii, inatabiriwa kufikia milioni 2.45 kufikia mwaka wa 2030, ongezeko la asilimia 39 katika kipindi cha mwongo mmoja tu.

Kulingana na Prof Fredrick Chite Asiriwa, mtaalamu wa maradhi ya kansa na ya damu, japo sababu kuu zinazojulikana kusababisha maradhi haya hapa nchini ni uvutaji sigara na ukosefu wa hewa safi, asilimia kubwa ya wanaougua huwa ni kutokana na sababu zisizojulikana.

“Uvutaji sigara ndio hatari kubwa zaidi inayosababisha kansa ya mapafu huku ikichangia asilimia 80 ya visa vyote. Lakini mazingira na jeni pia huchangia. Kuwa wazi kwa asbesto, kemikali za radon aseniki, beryllium na urani, pia kumehusishwa na kansa ya mapafu,” asema.

Hatari

Aidha, hatari ya kukumbwa na aina hii ya saratani huongezeka ikiwa kuna historia ya kansa katika sehemu nyingine ya mwili, umri, historia ya kifamilia, kufanyiwa utaratibu wa mnururisho (radiation) katika sehemu ya kifua, na maradhi mengine ya mapafu kama vile Chronic Obstructive Pulmonary Disease (COPD).

Anadokeza ishara za kansa ya mapafu ni pamoja na mabadiliko ya kamasi, maumivu ya kifua au mgongo, kukohoa damu na ugumu wa kumeza chochote.

“Baadhi ya mbinu za uchunguzi zinazotumika katika utambuzi wa maradhi haya ni picha za eksirei, uchunguzi wa CT na PET scans, bronchoscopy (utaratibu ambapo njia za hewa mapafuni zinachunguzwa kwa kutumia mrija mwepesi kwa jina bronchoscope), needle biopsies (utaratibu ambapo sindano inatumika kuondoa seli, majimaji na tishu kutoka uvimbe unaoshukiwa kuwa na seli za kansa),” aeleza.

Prof Chite asema ni vigumu kudadisi takwimu kamili za maradhi haya kwani visa vingi vya kansa ya mapafu havitambuliwi kutokana na ukosefu wa uhamasishaji wa kutosha katika jamii na wahudumu wa kiafya.

“Aidha, kuna tatizo la violezi dhaifu vya utambuzi wa maradhi haya, ukosefu wa vifaa maalum vya utambuzi katika vituo vya kiafya nchini, huduma duni wakati na baada ya matibabu,” aongeza.

Kulingana na WHO, barani Afrika, ukosefu wa mbinu za utambuzi wa mapema, vilevile elimu muhimu na matibabu, ndio changamoto kubwa.

Mataifa maskini, Kenya ikiwemo, ambapo uwezekano wa kuishi ni chini ya viwango wastani, hunakili 15% pekee ya uwepo wa matibabu ya maradhi haya katika mifumo ya afya ya umma.

Hii ni tofauti sana ikilinganishwa na mataifa tajiri ambapo uwezekano wa kufikia huduma hizi ni 90%.

Ni udhaifu huu ambao umesababisha wagonjwa wengi wa kansa hii nchini kusaka huduma ng’ambo.

Inakadiriwa kwamba kati ya 25% na 30% ya waathiriwa humu nchini, husaka matibabu katika mataifa ya kigeni. Mara nyingi gharama ya matibabu ni ghali mno.

“Kansa ya mapafu sio ugonjwa mmoja na hutegemea na awamu ya maradhi hayo. Matibabu huhusisha taratibu kadhaa kama vile upasuaji, tibaredio, tibakemia n.k na pia huhusisha kikundi cha wataalamu. Gharama ya matibabu yaweza kuwa kati ya Sh1M na Sh5.5M,” aeleza Prof Chite.

Anasema kwamba wakati huu wa janga la corona, hali imekuwa mbaya hata zaidi kwa wanaougua maradhi haya.

“Hii ni kwa sababu wengi wanachelewa kupokea matibabu. Aidha ishara za Covid- 19 zinafanana na zile za kansa ya mapafu. Kwa mfano kushindwa kupumua, kukohoa na matatizo kifuani. Kuna baadhi ya wagonjwa ambao huenda wamefariki pasipo kusaka matibabu kutokana na marufuku ya usafiri kutoka sehemu moja au nyingine, vilevile hofu ya kushukiwa na jamaa zao kwamba huenda wanaugua corona badala ya maradhi haya,” aongeza.

Hata hivyo anasisitiza kwamba bado ni mapema kutambua iwapo corona imechangia kuongezeka kwa wagonjwa wa aina hii ya saratani.

“Kuna uwezekano kuwa wakati huu wa janga la corona mambo yamekuwa mabaya, lakini bado tunapokea wagonjwa wawili kila wiki sawa na awali. Tungali tunaendelea kudadisi hali ilivyo,” asema.

PATA USHAURI WA DKT FLO: Ukuvu mdomoni ni ishara ya HIV?

Mpendwa Daktari,

Hivi majuzi marafiki zangu waliniambia kwamba mojawapo ya mbinu ya kutambua iwapo mtu ana virusi vya HIV ni kwa kumuangalia mdomoni kuona iwapo ana ukuvu wa mdomoni (oral thrush).

Hiki ni kidokezi tosha cha kutambua iwapo mtu ana virusi hivi, au kuna matatizo mengine ya kiafya yanayosababisha hali hii?

George, Nairobi

Mpendwa George,

Mbinu pekee na ya uhakika kujua hali ya HIV ya mwenzako ni kwa kupimwa. Mtu anapoambukizwa virusi vya HIV anaweza dumu kwa kati ya miaka minane na kumi kabla ya kuanza kuonyesha ishara zozote.Aidha, wale wanaopokea matibabu na viwango vya virusi hivi mwilini viko chini, hawatakumbwa na maambukizi kama ukuvu wa mdomoni. Kumbuka kwamba maradhi yoyote yanayoathiri kingamwili ya mhusika yaweza mfanya mtu kukumbwa na ukuvu wa mdomoni. Hii ni pamoja na HIV, kisukari, maradhi ya figo, matatizo ya kihomoni, kansa, uzee, umri mdogo sana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli na za kutibu kansa.

Mpendwa Daktari,

Nina umri wa miaka 37 ambapo mimi ni mama wa watoto watatu. Wawili niliwazaa kupitia upasuaji. Pamoja na mume wangu tumekuwa tukifikiria kupata mtoto mwingine, lakini nakumbuka madaktari walinishauri nisifanyiwe upasuaji wa uzazi kwa mara nyingine. Hatari zipi ambazo huenda nikakumbana nazo ikiwa nitashika mimba tena?

Janet, Nairobi

Mpendwa Janet,

Baada ya kufanyiwa upasuaji mara mbili wakati wa kujifungua, unaweza shika mimba tena mradi usubiri kwa kati ya miezi 18 na 24 baada ya kupata mtoto wa mwisho.

Wakati wa kujifungua, utalazimika kufanya hivyo kupitia upasuaji, shughuli ambayo lazima ipangiwe.

Usijaribu kujifungua kupitia njia ya kawaida kwani kuna hatari ya uterasi kupasuka unapokumbwa na uchungu wa uzazi. Kuna uwezekano kwamba sehemu iliyokatwa wakati wa upasuaji imeacha gofu.

Ikiwa mji utajishikisha katika sehemu hii, huenda ukasababisha matatizo wakati wa ujauzito, japo sio jambo ambalo waweza dhibiti. Kutokana na sababu kuwa tayari una miaka 37, litakuwa jambo la busara ikiwa utashika mimba haraka iwezekanavyo, kutokana na hatari zinazohusishwa na umri mkubwa.

TAHARIRI: Ushuru zaidi ni mzigo usiofaa

KITENGO CHA UHARIRI

HATUA ya mahakama kuu kuharamisha sheria iliyonuia kuanzisha ushuru wa mapato wa asilimia moja ambao ungeshuhudia biashara na kampuni zikitozwa kodi hiyo hata wakati ambapo zimepata hasara, ni jambo la kujivunia.

Hatua hiyo ya mahakama inafaa kuizindua serikali kuhusu mipango yake ya kujiongezea mapato. Si vyema serikali kuongeza pato lake huku biashara hasa ndogondogo ambazo zingeipa hata ushuru zaidi zikianguka.

Je, biashara hizo zikishaanguka, serikali itatoza nani asilimia hiyo ya ushuru?

Naam, hamna serikali yoyote ulimwenguni inayoweza kuhudumu bila kutoza raia wake na mashirika ya kibiashara ushuru maadamu ni kutokana na kodi hiyo ambapo miradi ya maendeleo hufanikishwa mbali na watumishi wa umma kama vile walimu na madaktari kupata mishahara yao.

Ila pia hakuna taifa lililoendelea kiuchumi au kijamii kwa kuwatoza raia wake ushuru wa kupindukia kama huu ambao serikali ya taifa hili imekuwa ikipanga kuanzisha.

Hii ni kwa sababu unapowatoza raia ushuru mwingi, wanakosa uwezo wa kununua bidhaa mbalimbali jinsi ambavyo wangependa na hivyo basi biashara nyingi ambazo huwategemea raia hao kama wateja kukosa mapato.

Katika hali kama hiyo, watu wengi hukosa riziki na shughuli za kiuchumi kupungua, jambo linalodororesha viwango vya maisha.

Cha kusikitisha ni kuwa hata katika hali ambapo ushuru huu vinginevyo ungetumiwa kufadhili, kwa njia ya ruzuku, huduma nyingi za kimsingi, fedha nyingi zinazotokana na ushuru wa mwananchi huliwa kifisadi na Wakenya wachache walio katika nafasi zao.

Katika mataifa mengine ambapo ushuru mwingi hutozwa raia, huduma muhimu kama vile elimu, afya na hata usafiri huwa ni za hali ya juu mbali na kuwa nafuu zaidi.

Tatizo jingine kuu la kutoza ushuru mwingi ni kutoroka kwa wawekezaji wa kigeni ambao huhamia mataifa yaliyo na mazingira bora ya kufanyia biashara.

Kwa ufupi, utozaji ushuru usiokuwa na mipaka una athari nyingi hasi kuliko manufaa hasa kwa mataifa yanayostawi kama vile Kenya.

Covid-19: Majaribio kufanikisha utoaji chanjo kwa watoto wa kuanzia umri wa miaka mitano

Na MARY WANGARI

WATOTO kuanzia umri wa miaka mitano huenda wakaanza kupatiwa chanjo dhidi ya Covid-19 iwapo matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni ya Pfizer yataidhinishwa.

Kampuni ya Pfizer vilevile inasubiri kwa hamu matokeo ya utafiti kuhusu chanjo hiyo uliofanyiwa watoto wachanga wenye umri wa hadi miezi sita, katika hatua ambayo huenda ikavutia hisia kali kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Data kutoka kwa majaribio yaliyofanyiwa watoto wasiopungua 2,000 wenye umri kati ya miaka mitano na 11, iliashiria kinga imara ya mwili kutokana na kiwango cha chini cha chanjo hiyo bila athari zozote hasi, kulingana na utafiti huo uliochapishwa Jumatatu, Septemba 20.

Katika utafiti wake, Pfizer ilichunguza kiwango cha chembechembe za damu zinazopigana na ugonjwa huo ili kukadiria uwezo wake wa kutoa kinga ya mwili.

Utafiti huu ulitofautiana na ule wa awali ulioshirikisha watu wazima uliohusisha kulinganisha visa vya virusi vya corona miongoni mwa kundi moja na kundi la watu waliopokea chanjo hiyo.

Licha ya kuwepo kwa visa vya kutosha vya maambukizi miongoni mwa washiriki, Pfizer bado haijatangaza matokeo ya utafiti huo kuhusiana na ufaafu wa chanjo yake, kulingana na msemaji wa kampuni hiyo.

Iwapo itaidhinishwa na serikali ya Amerika ambayo kwa sasa inakagua chanjo hiyo, Pfizer itaweza kuanzisha mchakato wa kusambaza chanjo hiyo kwa watoto mwezi ujao Oktoba huku ikisubiri kibali kutoka kwa Uingereza na Uropa.

“Tuna furaha kujumuisha watoto katika ulinzi unaotolewa na chanjo punde tu tutakapopata kibali hasa tunapochunguza kusambaa kwa virusi aina ya Delta na tishio lake kwa watoto,”

“Visa vya Covid-19 miongoni mwa watoto Amerika vimeongezeka kwa karibu asilimia 240 tangu Julai na kuangazia haja ya utowaji chanjo,” alifafanua mkurugenzi wa Pfizer, Albert Bourla.

Haya yamejiri huku mjadala mkali ukitokota kuhusu kuwapa au kutowapa watoto chanjo ambapo Uingereza tayari imeanza mchakato wa kuwapa chanjo watoto wasio na virusi vya corona wenye umri wa kianzia miaka 12.

WANGARI: Elimu ya juu iwekeze zaidi katika ujuzi wa kiufundi na kitaaluma

Na MARY WANGARI

WATAHINIWA waliokamilisha mitihani yao ya Cheti cha Elimu ya Sekondari Nchini (KCSE) wataanza kujiunga na taasisi za elimu ya juu wiki hii.

Maelfu ya watahiniwa hao tayari wamepokea barua za mialiko kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali vya umma na vya kibinafsi, huku baadhi wakijiandaa kujiunga na taasisi za kiufundi kote nchini.

Kwa hakika, ni jambo la kufurahia na kuhuzunisha kwa pamoja hasa kwa kuzingatia mamia ya mahafali wanaozidi kutaabika kwa kukosa ajira hata baada ya kufuzu kwa shahada za digrii, uzamili na uzamifu.

Kisa cha hivi majuzi kuhusu Wakenya watatu wenye umri wa makamo kutoka Kaunti ya Homa Bay, waliolazimika kufundisha shule za chekechea licha ya kuwa na vyeti vya uzamifu, ni ithibati tosha ya uhalisia mchungu uliopo.

Viwango vya ajira vingali chini mno nchini licha ya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi zaidi kiuchumi barani Afrika.

Hali hii imewafanya mahafala wengi waliokuwa na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wao kukata tamaa huku baadhi yao wakijitosa katika uhalifu ili kupata riziki.

Kwa kuzingatia hilo, umuhimu wa kuwepo mfumo jumuishi unaotilia maanani ujuzi wa kiufundi na kitaaluma, hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Kwa miaka mingi, ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi umekuwa kero kuu ambayo imegharimu pakubwa mashirika ya umma na ya kibinafsi mamilioni ya fedha huku yakilazimika kusafirisha wataalamu kutoka mataifa ya kigeni nchini.

Ili kuziba pengo hilo, serikali inapaswa kushirikiana na wadau husika kuimarisha taasisi zinazotoa mafunzo na ujuzi wa kitaaluma utakaowezesha vijana kustawi nyanjani.

Taasisi hizo zitawezesha kuwepo kwa watu walio na ujuzi unaohitajika viwandani hivyo kufanya iwe rahisi kwao kupata ajira pindi wanapokamilisha mafunzo yao.

Ili Kenya iweze kufanikisha Ruwaza ya 2030 kuhusu ajira na maendeleo kiuchumi, ni sharti ihakikishe kuwepo kwa wafanyakazi walio na ujuzi unaohitajika katika taaluma husika.

Njia mojawapo ya kufanikisha hayo ni kwa kuwekeza katika taasisi zinazotoa mafunzo ya kiufundi ili kuhakikisha ukuaji na ustawi kiuchumi kwa jumla.

Serikali imejitahidi kuanzisha vituo vya kiufundi kote nchini ikiwemo kuwezesha wanafunzi kupata mikopo na ufadhili wa masomo kujiendeleza kielimu.

Masomo ya vyuo vikuu ni muhimu lakini ni sharti tuende na majira kwa kufanyia mageuzi mfumo wa elimu ya juu nchini.

Kando na kuwezesha vijana kupata ajira, mfumo unauopa kipaumbele ujuzi kiufundi na kitaaluma utaimarisha mustakabali wa Kenya kwa kubuni mikakati jumuishi ya ukuaji na ustawi kiuchumi.

mwnyambura@ke.nationmedia.com