Habari za Kitaifa

Agnes Kalekye ateuliwa Mkurugenzi Mkuu wa KBC kwa kipindi cha miaka mitatu

May 18th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Muungano wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOA) Agnes Kalekye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari Nchini (KBC).

Kupitia taarifa fupi kwa vyombo vya habari Ijumaa, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali Eliud Owalo, alisema Bi Kalekye ataanza kutekeleza majukumu ya afisi hiyo mara moja.

Afisa huyo ambaye, hadi uteuzi wake alihudumu kama Afisa Mkuu wa Operesheni katika Gazeti la The Star, atahudumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Tunamtakia Bi Kalekye heri njema katika wadhifa wake mpya katika wizara hii. Twamtarajia kufanya kazi kwa ushirikiano na Bodi ya Wakurugenzi katika kuimarisha utendakazi wa Shirika la Habari Nchini,” Bw Owalo akasema kwenye taarifa hiyo.

Wadhifa wa mkurugenzi mkuu wa KBC ulisalia wazi mnamo Desemba 19, 2024, baada ya waziri Owalo kumpiga kalamu Samuel Maina ambaye alikuwa akihudumu kama kaimu.

Baadaye alimteua Paul Macharia kama kaimu Mkurugenzi Mkuu kisha mchakato wa kujaza nafasi hiyo kikamilifu ukaanza.

Uteuzi wa Bw Kalekye unajiri mwezi mmoja baada ya Waziri Owalo kumteua aliyekuwa Mhariri Mkuu wa Shirika la Habari la Nation (NMG) Tom Mshindi kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa KBC.