Dimba

AI yabashiri Arsenal itangoja sana kushinda Klabu Bingwa Ulaya

June 1st, 2024 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TEKNOLOJIA ya akili kama ya binadamu (AI) imebashiri kuwa Arsenal haitashinda Klabu Bingwa Ulaya kwa kipindi cha miaka 79 ijayo.

Huku fainali ya kombe hilo ya msimu 2023-2024 kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund ikiratibiwa kusakatwa Jumamosi usiku, AI imebashiri washindi wa makala ya Klabu Bingwa Ulaya hadi mwaka 2103.

Inasema Real Madrid wanachomoka na taji.

Cha kushangaza ni kuwa Arsenal, ambao nafasi nzuri wamemaliza katika mashindano hayo ya kiwango cha juu kabisa ya Ulaya ni nambari mbili msimu 2005-2006, hawapatikani katika orodha ya timu AI imebashiri zitanyakua taji.

Mabingwa wa 1968, 1999 na 2008 Manchester United wamepewa nafasi ya kuwa washindi wa mwaka 2025, ingawa hawakufuzu baada ya kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya nane msimu 2023-2024.

AI imebashiri kuwa wafalme wa mwaka 1974, 1975, 1976, 2001, 2013 na 2020 Bayern Munich wataibuka washindi mwaka 2026, huku washindi wa makala matatu yatakayofuata wakitoka Uingereza ambao ni Liverpool (2027) na Manchester City (2028 na 2029).

AC Milan watatawala mwaka 2030 nao washikilizi wa rekodi ya mataji mengi ya Klabu Bingwa Ulaya Real Madrid (14) watashinda makala ya 2031, 2032, 2053, 2054, 2094 hadi 2098 na 2011, Paris Saint Germain (2033, 2070, 2072 na 2093), Tottenham Hotspur (2034), Sporting Lisbon (2035), AS Roma (2036), Newcastle United (2037) na Liverpool (2038). Atletico Madrid watafagia mataji ya msimu 2039 hadi 2041.

Katika kipindi hicho cha miaka 79, Wolves wamebashiriwa kushinda mwaka 2042, Nottingham Forest na Rangers (mara mbili kila mojawapo) bila ya kusahau Leicester City, Celtic na Brentford.

Orodha ya washindi pia itakuwa na Malmo, Sheriff Tiraspol, Eintracht Frankfurt, Barcelona, Juventus, Chelsea, Torino, Lyon, Ajax, Feyenoord, Sevilla, Alaves, PSV Eindhoven, Besiktas, Galatasaray, Inter Milan na FC Porto, miongini mwa nyingine, lakini hakuna Arsenal popote.

Akili bandia ni nadharia na uundaji wa mifumo ya kompyuta yenye uwezo wa kutekeleza kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili ya kibinadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha.

Teknolojia hii ya akili mwigo inatumika kwa kiwango kikubwa viwandani, serikalini, na kwenye tafiti za kisayansi. Kama taaluma ya sayansi, AI ilianza rasmi mwaka 1956, ingawa imeanza kupata umaarufu miaka ya hivi majuzi.