Habari za Kitaifa

Kilio meli za watalii zikikosa kuvumisha uchumi Pwani

February 6th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

WAKAZI na wafanyabiashara katika Kaunti ya Mombasa na Pwani kwa jumla, wangali hawajaona manufaa makubwa kutoka kwa ongezeko la idadi ya meli za kifahari ambazo zimekuwa zikitia nanga katika Bandari ya Mombasa kwa karibu mwaka mmoja sasa.

Takriban miaka 10 iliyopita, Pwani na Kenya kwa jumla zilikuwa zikivuna kutokana na biashara ya meli za kitalii za kifahari ambapo watalii wangepata fursa kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo fuo za bahari, sehemu za kihistoria na hata mbuga za kitaifa za wanyamapori maeneo mbalimbali ya nchi.

Meli hizo zilikuwa zikikaa nchini kwa zaidi ya saa 24 ambapo watalii wangepata fursa ya kutalii maeneo.

Hata hivyo, imebainika changamoto mbalimbali kama vile gharama ya wageni kuingia Kenya, na mahitaji ya kiafya katika nchi nyingine ambazo wangependa kuzuru wakiondoka Kenya,zinawazuia wengi wanaotumia meli za kifahari kukaa ndani ya nchi kwa zaidi ya siku moja.

Mojawapo ya vikwazo ni kuwa, Shirika la Afya Duniani (WHO), huwa limeorodhesha Kenya kuwa miongoni mwa sehemu hatari ya kuambukizwa homa ya manjano.

Ziara ya hivi punde ilikuwa ni Februari 3, 2024, ambapo Kenya ilipokea wageni 3,500 kutoka meli ya kifahari ya MSC Poesia.

Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Dkt Alfred Mutua, aliungama kuwa Kenya inaweza kuvuna mapato mengi zaidi ya jinsi ilivyo sasa kutoka kwa utalii huo.

Alisema Kenya itafanya mazungumzo na WHO kuhusu suala la homa ya manjano.

“Meli itasalia Kenya kwa saa 12 pekee sababu ya mwongozo wa WHO,” alisema Dkt Mutua.

Kulingana na Wizara ya Utalii, mapato ambayo huletwa kutoka kwa kila meli ya kifahari ni karibu Sh50 milioni pekee ilhali Kenya inalenga kupata Sh2 bilioni kwa mwaka kutoka kwa aina hiyo ya utalii.

Tangu Novemba mwaka uliopita, meli nne zimetia nanga nchini zikiwa na wageni 8,480.

Hata hivyo, ni wachache tu kati yao ambao hutoka nje ya Bandari ya Mombasa kutembelea sehemu tofauti za Mombasa na wengine kuabiri ndege kuelekea mbuga za wanyama zilizo mbali, kabla kurudi saa chache baadaye kisha meli kuondoka.

Mtaalamu wa masuala ya utalii, Bw Mohammed Hersi, alisema endapo watalii wangezidisha saa 12, wangehitajika kudungwa chanjo dhidi ya homa ya manjano kabla waruhusiwe kuingia katika nchi nyingine ya kigeni.

“Wangelilala Kenya wangelazimika kuchanjwa pindi walipofika Durban ambapo walikuwa wakielekea ndio maana wengi wao waliamua kusalia kwenye meli,” alisema Bw Hersi.

“Wajua wengi wa watalii hao ni wazee waliona haina haja ya kujiweka kwenye hatari ya kulazimika kuchanjwa,” akaongeza.
Aliisihi Wizara ya Afya na Wizara ya Utalii kufanya bidii ili Kenya iondolewe kwenye orodha hiyo.

Kulingana naye, Kenya inaweza kunufaika sana kama kutapatikana mbinu za kuwashawishi watalii wa kigeni wanaowasili kwa meli za kifahari kukaa nchini kwa zaidi ya siku moja.

Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, alisema gharama na mfumo mgumu wa watalii wa kigeni kupata vibali vya kuingia nchini hata kwa siku chache pia ni changamoto inayofaa kutatuliwa.