Makala

Ajali: Watu 84 waaga dunia wiki ya kwanza ya mwaka

January 12th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WATU 84 wamepoteza maisha kupitia ajali za barabarani ndani ya muda wa wiki ya kwanza ya mwaka, kulingana na takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA).

Takwimu hizo za hadi kufikia Januari 7, 2024, zinaonyesha kuwa idadi ya vifo iliongezeka ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka 2023.

Kati ya Januari 1 na Januari 7, 2024, watu 84 waliangamia katika ajali za barabarani ikilinganishwa na 72 waliopoteza maisha yao wakati sawa na huo mwaka 2023.

Data za hivi punde kutoka NTSA zinaonyesha kuwa hadi kufikia Januari 7 jumla ya watu 508 walihusika katika ajali za barabarani. Watu 234 walijeruhiwa vibaya, 190 walipata majeraha mabaya na 84 wakafariki.

Miongoni mwa hao wahanga 84 waliopoteza maisha yao, wengi wao walikuwa ni watu wa kutembea kwa miguu, wakifuatwa na waendeshaji pikipiki, abiria, madereva wa magari na waendeshaji wa baiskeli.

Jumla ya watembeaji kwa miguu 31 walikufa katika ajali za barabarani, ikilinganishwa na 28 walioripotiwa mwaka jana huku waendeshaji pikipiki 23 wakifa ikilinganishwa na 24 waliokufa 2023.

Madereva saba waliangamia katika ajali za barabarani kati ya Januari 1 na Januari 7 ikilinganishwa na sita waliokufa katika kipindi sawa na hicho mwaka 2023.

NTSA, katika mpango wake wa kimkakati wa kati ya 2023-2027 inasema kuwa asasi kadha za serikali ya kitaifa na serikali za kaunti zilizotwikwa wajibu wa kudumisha usalama barabara zinakabiliwa na ukosefu wa fedha za kutosha kufadhili shughuli hizo.

Asasi hizo ni kama vile; NTSA, Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu (Kenha), polisi na idara za afya katika kaunti.

“Inakadiriwa kuwa ajali za barabara husababisha hasara ya kima cha zaidi ya Sh450 bilioni kwa uchumi wa nchi. Ipo haja ya ufadhili mkubwa kutolewa kwa mipango ya usalama barabarani nchini Kenya ndani ya miaka 10 ijayo,” NTSA.

Kulingana na NTSA, ajali nyingi hutokea katika barabara kuu ya kuelekea Kaskazini, ambazo huchangia ongezeko la idadi ya vifo.

Kwa mfano, barabara tano katika Kaunti ya Nairobi, zinazowakilisha asilimia mbili pekee ya mtandao wa barabara nchini, huchangia asilimia 36 ya vifo vyote kutokana na ajali barabarani katika kaunti hiyo.

Kulingana na NTSA asilimia 26 ya ajali zote Nairobi (sawa na asilimia 30 katika nchini nzima) hutokea kati ya saa moja usiku na saa nne usiku.

Mwaka 2023, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alisema hulka ya madereva kuendesha magari wakiwa walevi, uendeshaji kwa kasi kupita kiasi, kutotumia mikanda ya usalama na helmeti na kuvuka barabara bila uangalifu ndio huchangia pakubwa ajali barabarani.

Waziri wa Uchukuzi, Kipchumba Murkomen. PICHA | MAKTABA

Aidha, waziri alisema ajali nyingi haswa katika maeneo ya mijini, kutokea siku za Ijumaa jioni na Jumatatu asubuhi, hali ambayo inahusishwa na mwenendo wa madereva kuendesha magari wakiwa walevi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa zaidi ya watu 1.35 milioni duniani hufa kila mwaka kupitia ajali za barabarani.

Aidha, wengine 50 milioni hupata majeraha kutokana na ajali hizo.