Habari za Kitaifa

Ajali za bodaboda zakithiri Nairobi, wahudumu wamgeukia Mungu

Na FRIDAH OKACHI August 18th, 2024 2 min read

WAHUDUMU wa bodaboda jijini Nairobi walishiriki maombi katika eneo la Green Park ili kuombea wenzao zaidi ya 300 wakiwa na majeraha mabaya na wengine saba walioaga dunia Julai, 2024 katika ajali za barabara. 

Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa  Bodaboda Thomas Lesatin, amesema jijini Nairobi, sekta hiyo ina wahudumu wa bodaboda 3200 na wanazidi kupoteza vijana wenye umri kati ya miaka 20 na 30.

Bw Lesaatin alitoa wito kwa serikali kutoa mafunzo ya barabara kwa vijana wachanga ili kupunguza ajali hizo.

“Jumamosi asubuhi, Agosti 17, 2024, kwenye kundi letu, tulipokea taarifa nyingine ya kumpoteza mwezetu siku moja baada ya kumzika mwingine,” alisema. “Wahusika wengi ni wale ambao hufanyia mafunzo ya pikipiki katika bustani la uhuru Park. Akifanya siku mbili au tatu anaingia jijini kutafuta ajira.”

Katika mkutano huo, zaidi ya vijana 25 wanaouguza majeraha walihudhuria.

Kundi la wahumudu wa bodaboda wa Nairobi katika maombi. PICHA | FRIDAH OKACHI

Majeraha hayo yamesababisha mzigo mzito kwa wanachama wa bodaboda ambao hutoa msaada wa matibabu kwa wenzao. Walio na majeraha mengi wamelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Mtakatifu Maria, Lang’ata.

“Kuna viongozi wa bodaboda ambao wanaidhinisha vijana hao kuingia jijini baada ya kupewa hongo. Uchunguzi ambao tumefanya unaonyesha wapo kwenye vituo vya bodaboda na hapo kwenye ushirika. Tatizo likitokea, simu zote zinaelekezwa kwa wakuu wa miungano,” alilalama Bw Lesaatin.

Waliojeruhiwa wasimulia masaibu

Bw Calvince Okumu,32, bado anauguza majeraha kwenye sehemu ya uti wa mgogo na miguu baada ya ajali.

Bw Okumu anahitaji Sh 470,000, kugharamia matibabu ya upasuaji licha ya kufanyiwa mara mbili bila kupona.

Okumu alihusika kwenye ajali Mei, 2022 kwenye barabara ya Moi, jijini Nairobi.

“Mbele yangu niliona hatari na kukanyanga breki ya dharura na kuanguka chini. Hatua hiyo ilikuwa kuokoa maisha yangu japo nilibaki na majeraha,” alisimulia akiomba wenzake na dereva wa magari kuwa waangalifu.

“ Ukiona nimevalia mavazi haya ya kazi ni kuzuia nisipate maumivu mengine wakati ninafanya shughuli zangu za kazi. Sasa hivi ninapokanyanga breki kuna uchungu ambao nasikia kwenye sehemu zangu za mwili na hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji,” alisema Bw Okumu.

Mwanakamati wa Usafiri Salama Kaunti ya Nairobi, Bw Ken Onyango alisema sekta hiyo imeathiriwa huku wengi wakikiuka sheria za barabara.

Aliomba serikali kutoa pesa za bajeti ya mwaka 2024/2025 na kusambazwa kwenye miungano ya wahudumu hao ili kuwezesha mafunzo kabambe.

“Mwaka huu sekta yetu iliongoza kwa kusababisha ajali, ikifuatwa na watu wanaotembea kisha magari, serikali itoe pesa za mafunzo. Mpango wa usafiri salama umezindulia kwa sababu yetu,” alisema Bw Onyango.