Akili MaliMakala

Alivyoanzisha kiwanda cha maziwa akiwa mwanafunzi

Na SAMMY WAWERU August 7th, 2024 2 min read

HISTORIA ya washirika waliofanikisha kuboresha sekta ndogo ya maziwa nchini ikiandikwa, majina ya Gabriel Mahindu bila shaka hayatakosa kwenye orodha.

Gabriel ni mjasirimali aliyewekeza kwenye biashara ya maziwa, shabaha yake ikiwa kuokoa wafugai wa ng’ombe wa maziwa.

Sawa na sekta zingine, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa pia Unapitia changamoto moto za hapa na pale – hasa za mabroka.

Barobaro huyu mkakamavu amejituma kuongeza maziwa thamani, kwa kuyasindika kuwa maziwa ya mtindi maarufu kama yoghurt.

Safari yake ni ya kuridhisha; kijana mwenye maono aliyoanza kupalilia akiwa shuleni.

Ni mmoja wa waanzilishi wa Comrades Dairy & Food Enterprises, kampuni ya kuunda yoghurt eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru.

“Biashara ya kuongeza maziwa thamani niliianzisha 2018, nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Egerton,” Gabriel anasema.

Gabriel Mahindu, mwasisi Comrades Dairy & Food Enterprises wakati wa Maonyesho ya Sankalp Barani Afrika 2024, Nairobi, akipanga maziwa ya mtindi. PICHA|SAMMY WAWERU

Pamoja na waasisi wenza, anaelezea kwamba hatua hiyo ilitokana na kuona wakulima – wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wakihangaika kupata soko.

Idadi kubwa ya wakulima wangali mateka wa mawakala, ikizingatiwa kuwa wao ndio hubeba gharama ya uzalishaji.

Ni kero na hasara bin hasara, gapu ambayo Gabriel anasema alilenga kuiangazia.

“Mabroka hupatikana wakati haja yao inawasukuma, na wanapokosekana mkulima anasalia akihangaika kupata soko,” asema.

Isitoshe, wanatumia jukwaa la mahangaiko yao kuwapunja “wakila kwa kijiko kahawa inapoiva”.

Akiwa mhitimu wa Digrii ya Masuala ya Kilimo and Ufugaji, Gabriel, hata hivyo anasema chuo alichosomea kiliegemea sana kutafiti jinsi ya kuongeza maziwa thamani na kukosa kuangazia pengo la soko.

Maziwa ya mtindi yanay0sindikwa na Comrades Dairy & Food Enterprises. PICHA|SAMMY WAWERU

Utamu wa kazi ni pesa, hivyo basi kilele cha biashara yoyote ile kama vile zaraa na ufugaji kinapaswa kuwa mkulima kutabasamu akielekea kwenye benki.

“Tulianza kwa kukusanya maziwa, kuyachemsha na kuyahifadhi tukiyatafutia wanunuzi,” Gabriel anadokeza.

Miaka sita baadaye, mjasirimali huyu ana kila sababu ya kutabasamu kutokana na hatua walizopiga.

Comrades Dairy & Food Enterprises, imegeuka kuwa mwokozi wa wafugaji Njoro ambapo maziwa inayokusanya ikiyaunda yoghurt hivyo basi kuteka soko lenye ushindani mkuu.

Comrades, ni jina tajika la lakabu nchini linalotumika na wanafunzi wa vyuo vikuu na vya anuwai kujitambua.

“Tunajivunia kuanzisha na kufanikisha wazo linalowafaa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa,” Gabriel anasema.

Kijana huyu ndiye aliibuka na wazo hilo la busara.

Gabriel Mahindu mwanzilishi wa Comrades Dairy & Food Enterprises akionyesha brandi aina Vanilla. PICHA|SAMMY WAWERU

Vanilla, Strawberry na Pro-biotic, ndizo brandi za maziwa ya mtindi ambayo kampuni yake hutengeneza chini ya nembo Prestige Dairy Brands.

Uundaji wake unaongozwa na vigezo vya Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) vya maziwa.

Ni kutokana na jitihada zake, alikuwa miongoni mwa wajasirimali waliopata fursa kushiriki Maonyesho ya Sankalp Barani Afrika 2024, makala ya 11 yaliyofanyika Jijini Nairobi.

Aidha, alishiriki kupitia ufadhili wa Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) na Scaling Up Nutrition Business Network (SBN).

Kauli mbiu ya maonyesho hayo ilikuwa ‘Kupiga jeki Ujasirimali Barani Afrika ili Kuwahi Maendeleo ya Kimataifa’, na Gabriel anasema mashirika hayo yamemsaidia kulainisha mikakati ya utendakazi, ikiwemo kuimarisha bidhaa na kuweka rekodi.

Aidha, Comrades Dairy imewekeza kwenye mitambo kama; ya kuchemsha maziwa, kuyapoesha, kusindika yoghurt na kuhifadhi, Gabriel akiomba wahisani kumpiga jeki kupata ile ya kisasa ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.

Ninaamini tukipata mashine za kisasa kampuni itapanuka na kuleta manufaa tele kwa wakulima, anasema.

Comrades Dairy & Food Enterprises ni kampuni iliyoanzishwa na Gabriel Mahindu eneo la Njoro, Nakuru kuunda yoghurt.