Habari za Kitaifa

Aliyeiba mbolea aachiliwa kwa dhamana

Na RICHARD MUNGUTI September 2nd, 2024 1 min read

MFANYABIASHARA alishtakiwa Jumatatu, Septemba 2, 2024 na wizi wa mbolea ya thamani ya Sh2.2 milioni.

Benson Omondi Bonyo alikana mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina aliiba magunia 560 ya mbolea iliyokuwa inasafirishwa kutoka Mombasa hadi mabohari ya Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) ya Awendo, Kaunti ya Kisumu.

Bonyo, alikana kuiba mbolea hiyo mnamo Agosti 23, 2024 katika eneo la Mlolongo, Machakos.

Hakimu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka kwamba mbolea hiyo aina ya Urea yenye kiwango cha asilimia 46 cha Nitrojini, ilikuwa ya thamani ya Sh2, 268, 000 mali ya NCPB.
Mahakama ilifahamishwa kuwa mbolea hiyo ilikuwa inasafirishwa na lori nambari KBU 926A Mercedes iliyokuwa inaburura trela Nambari ZG 8186.

Mahakama ilielezwa kuwa mbolea hiyo ilikuwa imetolewa kwa bobari la kampuni ya Yara East Africa Ltd (K) Jomvu-Madafuni, Mombasa kusafirishwa hadi bohari la NCPB.

Bw Omondi aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “kosa analoshtakiwa nalo ni miongoni mwa kesi ambapo mmoja anaweza kuachiliwa kwa dhamana.”

Upande wa mashtaka haukupinga ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana ukisema ni haki yake.

Akitoa uamuzi wa ombi hilo, Bw Onyina alisema upande wa mashtaka haupingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Pia, hakimu alisema mshtakiwa hajadaiwa ni mkorofi na kwamba atatoroka akiachiliwa kwa dhamana.

“Nikitilia maanani mawasilisho ya upande wa mashtaka kwamba haupingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana, naamuru mshtakiwa alipe dhamana ya pesa taslimu Sh800, 000 afanye kesi akiwa nje,” Bw Onyina aliamuru.

Mshtakiwa pia alionywa dhidi ya kuvuruga mashahidi.

Bw Onyina aliagiza kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili, kutengewa siku ya kusikizwa na pia upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi.