Habari za Kitaifa

Baba wa kambo ashikwa kwa kumshambulia mtoto aliyedinda kumuita baba

Na DOMINIC OMBOK September 20th, 2024 2 min read

MTOTO wa miaka saba amelazwa katika hospitali moja ya Kisumu akiwa hali mahututi baada ya kudaiwa kushambuliwa na babake wa kambo kwa kukataa kumuita baba.

Mshukiwa aliyetambuliwa kwa jina Stephen Odhiambo, 29, alikamatwa na kuzuiliwa baada ya kumpeleka mtoto aliyejeruhiwa katika Hospitali ya Kaunti ndogo ya Kombewa kwa matibabu Ijumaa, Septemba 13, 2024.

Alidaiwa kumshambulia mvulana huyo mama yake akiwa katika hospitali moja akimhudumia mtoto wake mdogo.

Kulingana na mama huyo, mshukiwa huyo ana historia ya kuchukia watoto wake watatu, licha ya kuwa alikubali kuwachukua kama wake walipoamua kuoana miezi mitatu iliyopita.

“Nilipohamia kwake mara ya kwanza na watoto wangu wawili, mume wangu alisema ni sawa nimlete mwanangu mkubwa pia. Lakini mwezi Julai, alianza kumpiga mtoto kwa viboko mara kwa mara kabla ya kuendeleza ukatili huo kwa wale wadogo,” alisema.

Alieleza jinsi alivyogundua kuwa mwanawe alishambuliwa akiwa hospitalini.

“Nilisikia watu wakisema kuna mtu aliyekamatwa kwa kosa la kumpiga mtoto vibaya sana, nilipochungulia dirishani niliona ni mwanangu, usiku ule niliumia sana na kulia usiku mzima, alikuwa na majeraha katika mwili wake wote,” aliongeza.

Ripoti ya matibabu kutoka hospitali ilithibitisha kuwa mvulana huyo alipata majeraha kutokana na kipigo.

Kulingana na majirani, shambulio hilo lilianza baada ya mama wa watoto hao kuondoka kuelekea hospitalini na kuwaacha watoto wake wengine chini ya uangalizi wa Bw Odhiambo.

Mshukiwa huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Maseno Jumanne ambapo alikabiliwa na mashtaka mawili ya kumjeruhi mtoto mdogo na ukatili dhidi ya mtoto, kinyume na Kifungu cha 162(1)(A) cha Sheria ya Mtoto nambari 29 ya 2022.

Alikanusha mashtaka na akapewa dhamana ya pesa taslimu Sh20,000.

Hakuweza kupata kiasi hicho na mahakama ikaamuru Bw Odhiambo azuiliwe katika Gereza Kuu la Kodiaga.

Mtoto huyo baadaye aliokolewa na shirika la kijamii  linalohudumu eneo hilo, Compassionate Centre for Families (CCF), ambalo liliingilia kati kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto hao.

Sheila Otieno, Mkurugenzi Mkuu wa CCF, alieleza kuwa shirika hilo linalosaidia familia zilizo katika matatizo, linashirikiana na idara za serikali kuwalinda watoto hao.

“Kipaumbele chetu ni usalama wa watoto. Baada ya kuondoka hospitalini, tunapanga kumpeleka mama na watoto wake katika kituo chetu cha uokoaji kwa uangalizi na ulinzi zaidi,” Bi Otieno alisema.