Habari za Kitaifa

Babake Monicah Kimani amsamehea ‘Jowie’

February 18th, 2024 1 min read

NA OMULO OKOTH

ASKOFU Paul Ngarama, babake Monicah Kimani, mwanamke aliyeuawa Septemba 19, 2018, amesema ameamua kumsamehe aliyemtendea mwanawe unyama huo.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Mahakama Kuu kumpata na hatia Joseph ‘Jowie’ Irungu ya kumuua Monica.

“Mahakama imefanya uamuzi wake, ambao si tofauti na nilivyotarajia mimi na familia yangu. Japo nimemsamehe Joseph Irungu, bado najiuliza ni kwa nini aliamua kumfanyia mwanangu hivyo,” Askofu Ngarama alisema.

Askofu huyo sasa anataka Irungu aombe msamaha, hatua anayosema kuwa itafanya roho yake itulie.

“Hii itamaliza kiwewe na maswali tuliyo nayo tangu 2018 wakati binti yangu wa pekee alichinjwa kama kuku,” Askofu Ngarama aliongeza.

“Biblia inatufunza kwamba sharti tuwasamehe waliotukosea bila masharti. Lakini asili ya kibinadamu na adabu pia inatupasa kuomba msamaha tunapokosea. Sijui kama anaweza kuomba msamaha,” Askofu Ngarama, 58, wa Kanisa la Rebuilding Apostolic Mission Church, lenye makao yake makuu Juba na Thika, aliongeza.

Mahakama Kuu ilimpata Irungu na hatia mnamo Februari 9, 2024, ya kumuua Monicah.