Habari

BBI: Mnara wa Babeli

December 1st, 2019 3 min read

Na WAANDISHI WETU

MGAWANYIKO mkubwa umezuka kuhusu mchakato unaofaa kutumiwa kutekeleza ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) ambayo ilizunduliwa Jumatano ya mwisho Novemba 2019.

Wanasiasa wanatoa kauli ambazo zinaashiria wazi kuwa wamegawanyika zaidi kuliko walivyokuwa kabla ya ripoti hiyo kuzinduliwa rasmi.

Chama cha ODM kimeshikilia kuwa hakitakubali mageuzi ya katiba yaliyopendekezwa kwenye ripoti hiyo ikiwa yataendeshwa kupitia bunge na wala sio kura ya maamuzi.

Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa wa chama hicho, Opiyo Wandayi, ambaye pia ni mbunge wa Ugunja alisema Jumamosi ingawa ODM inaunga mkono mapendekezo mengi katika ripoti hiyo, itahakikisha mageuzi yote yanatekelezwa kupitia kura ya maamuzi pekee.

“Ingawa tunakubali kuwa sheria inasema mapendekezo hayo sharti yapelekwe bungeni, tungetaka kufafanua kuwa mageuzi hayo yatafanikiwa tu kupitia kura ya maamuzi, na hatutakubali njia nyingine,” akasema.

Bw Wandayi alisema hayo wakati wa mazishi ya mwanahabari wa gazeti la ‘The Star’, Eric Oloo katika kijiji cha Uhor eneobunge lake la Ugunja, kaunti ya Siaya. Oloo aliuawa siku 10 zilizopita ndani ya nyumba ya mpeziwe ambaye ni Inspekta Mkuu katika kituo cha polisi cha Ugunja.

Bw Wandayi ambaye alikuwa ameandamana na Mbunge wa Ugenya David Ochieng aliwaambia wale ambao wanapinga kura ya maamuzi wajiandae kwa “mapambano makali siku zijazo.”

Kauli ya mbunge huyo wa ODM ilijiri saa chache baada ya Naibu Rais William Ruto kuwataja viongozi wanaoitisha kura ya maamuzi kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya BBI kama watu wanaotaka kuitumia kujipatia mamlaka kwa njia ya mkato.

Akiongea Jumamosi katika eneobunge la Kangundo, Kaunti ya Machakos Dkt Ruto alisema asilimia 99 ya mapendekezo ya ripoti ya BBI yanaweza kutekelezwa na asasi husika za serikali pamoja na bunge kupitia marekebisho ya sheria.

“Lakini kuna watu ambao hawataki ripoti hiyo kutekelezwa bila kuwagawanya Wakenya,” akasema alipofungua rasmi Chuo cha Mafunzo ya Matibabu cha Kangundo.

Nao takribani wabunge 40 kutoka eneo la Mlima Kenya wandani wa Dkt Ruto, wamepinga wazo la kutekelezwa kwa ripoti ya BBI kupitia kura ya maamuzi.

Wabunge hao kutoka kaunti 10 za jamii za Gema walitangaza Jumamosi kuwa wataunda kamati za wabunge kuongoza mchakato wa kutekeleza ripoti hiyo.

Kwenye taarifa iliyosomwa na Seneta wa Embu, Njeru Ndwiga baada ya mkutano huo wa siku mbili wa wabunge hao katika mkahawa wa Mountain Breeze, Embu, viongozi hao walisema watatenga bajeti ambayo itafadhili mpango wa kuhakikisha wananchi wanaelewa yaliyomo katika ripoti hiyo.

“Mapendekezo mengi katika ripoti ya BBI yanahitaji kutekelezwa kupitia sheria za kawaida wala sio mabadiliko ya kikatiba. Bunge ndio asasi ya kipekee yenye mamlaka ya kupitisha sheria kama hizo. Tunashikilia kuwa mageuzi yoyote ya kikatiba kuhusu ripoti ya BBI yaongozwe na bunge,” akasema Bw Ndwiga.

Miongoni mwa wabunge waliohudhuria mkutano huo ni; Maara Kareke Mbiuki,(Maara) Moses Kuria (Gatundu Kusini), Rigathi Gachagua (Mathira) John Muchiri (Manyatta), Kimani Ichung’wa (Kikuyu) Ndindi Nyoro (Kiharu), Wangui Ngirici (Mbunge Mwakilishi, Kirinyaga) Munene Wambugu (Kirinyaga ya Kati), Rahim Dawood (Imenti Kaskazini), Seneta wa Nakuru Susan Kihika, miongoni mwa wengine.

Mshirikishi wa mkutano huo alikuwa ni Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.

Wamsuta Ruto

Na wakiongea katika eneobunge la Bondo, Kaunti ya Siaya, wanasiasa kadha walimsuta Dkt Ruto kwa kuweka mtego wa kuangusha ripoti ya BBI kupitia bunge.

Gavana wa Machakos Alfred Mutua, mwenzake wa Siaya Cornel Rasanga, Seneta wa Siaya James Orengo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (Cotu-K) Francis Atwoli na wabunge kadha walitaja msukumo wa wafuasi wa Ruto kwamba marekebisho ya Katiba yafanywe kupitia bunge kama njama ya kuwapokonya Wakenya kila mazuri ambayo yamo katika ripoti hiyo.

“Inashangaza kuona watu ambao wamekuwa wakipinga mabadiliko ya Katiba sasa wamebadili msimamo na kuanza kupendekeza jinsi mchakato huo unavyopaswa kutekelezwa,” akasema Bw Orengo.

Akaongeza: “Mamlaka yote ambayo viongozi waliochaguliwa wanatumia wamepewa na Wakenya. Na hivyo hatuwezi kuacha mamlaka hayo ya wananchi kutumiwa vibaya na watu ambao haja yao ni kuendeleza masilahi yao.”

Naye Dkt Mutua alisema:“Hatuwezi kuwaacha wabunge wachache kuamua hatima ya Wakenya kwa kuongoza mpango wa marekebisho ya katiba. Wananchi ndio wenye mamlaka wala sio watu wachache.”

Kwa upande wake, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alipendekeza kamati ya kiufundi ibuniwe kuwaelekeza Wakenya katika uchambuzi wa ripoti ya BBI.

 

Waandishi: Dickens Wasonga, Benson Matheka, Charles Wanyoro, Victor Raballa, na Shaban Makokha