Afya na JamiiMakala

Bei ghali ya chanjo inavyolemea wafugaji

Na SAMMY WAWERU August 20th, 2024 1 min read

WAFUGAJI wanalalamikia kupanda kwa bei ya chanjo ya wanyama nchini.

Huku wafugaji wakililia kuongezeka kwa gharama ya lishe ya mifugo, bei ghali inayoshuhudiwa ya chanjo inazidi kutia msumari moto kwenye kidonda kwani inapelekea wengi kushindwa kukabiliana na kudhibiti maradhi na minyoo kwa mifugo.

Mmoja wa wafugaji wa kondoo, Kaunti ya Nakuru, Murugi Mugane anasema imekuwa changamoto kupata chanjo ya mifugo miongoni mwa wakulima wadogowadogo kwani dawa zilizoko ni ghali.

“Chanjo ya mifugo imekuwa ghali. Kupata chanjo halisi na inayohitajika pia ni vigumu,” akasema mkulima huyo kutoka eneo la Molo, Mau Summit.

Murugi Mugane ambaye ni mfugaji wa kondoo Nakuru. PICHA|SAMMY WAWERU

Murugi, ambaye pia ni mwanzilishi wa Penzi Farm, amekuwa akifuga kondoo aina ya Dorper kwa kipindi cha karibu miaka miwili iliyopita sasa.

Kilio sawa na hicho kilitolewa na Fred Oloibe, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa na kondoo aina ya Dorper kutoka Cherangany, Kaunti ya Trans Nzoia.

“Kilimo cha mifugo ni mojawapo ya uwekezaji ambao hauwezi kufaulu bila chanjo kudhibiti minyoo na magonjwa. Bidhaa hiyo ni ghali na bei inapaswa kupunguzwa ili kuboresha sekta ya ufugaji,” akasema Bw Oloibe.

Kibebe, mwana wa kondoo kwenye zizi. PICHA|SAMMY WAWERU

Akiwa na zaidi ya kondoo 50, Murugi Mugane aliambia Taifa Dijitali wakati wa mahojiano ya kipekee kwamba kutafuta chanjo ni changamoto kubwa inayomkabili kila kukicha katika harakati zake za kujaribu kupanua ufugaji wake.

Kudhibiti minyoo na maradhi ni tatizo bayana miongoni mwa wakulima wengi, kwa mujibu wa wataalamu wa mifugo.

Dkt Maurice Msanya, mtaalamu na Meneja wa Mauzo kutoka shirika la Bimeda, anasema kwamba wafugaji wengi wanakosa ujuzi na ufahamu jinsi ya kukabiliana vilivyo na maradhi na minyoo.

Dkt Maurice Msanya, mtaalamu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mifugo. PICHA|SAMMY WAWERU

“Wanyama hupendwa sana na minyoo aina aina, hasa kwenye maeneo ya chemichemi. Ni vyema wafugaji kuwapa wanyama wao dawa za kuua minyoo mara kwa mara,” akasem Dkt Msanya.

Wakati wa msimu wa mvua, minyoo huvamia mifugo hivyo inawapasa wafugaji kuwa macho.

Imetafsiriwa na Kalume Kazungu