Maoni

‘Bibi’ Netanyahu ni kiongozi mkaidi asiyeogopa lawama

Na DOUGLAS MUTUA August 2nd, 2024 3 min read

IKIWA umeshtuliwa na hatua ya Israeli kumuua kiongozi mkuu wa kisiasa wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh, basi jua kwamba huelewi kwamba taifa hilo la Kiyahudi linaongozwa na mtu wa aina gani!

Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin ‘Bibi’ Netanyahu, si kiongozi wa kawaida. Hana mfano wake duniani. Wala hajali maoni ya watu.

Na hatambui maelezo kwamba Haniyeh alikuwa kiongozi wa kisiasa, si kijeshi, wa Hamas. Kwa maoni ya ‘Bibi’, ukiua, au ukila njama kuua raia wa Israeli, kuzimu kunakuita! Ni siku yako tu ambayo haijatimia.

Si ajabu wanamgambo wa Hamas walipowashambulia raia wa Israeli, wakawaua baadhi yao na kuwateka nyara wengine mnamo Oktoba 7, 2023, ‘Bibi’ akiapa kulipiza kisasi alionya: “Haniyeh ni maiti anayetembea.”

SOMA PIA: Baada ya sarakasi za siasa za Kenya, uhondo sasa upo Amerika

‘Bibi’ binafsi amefaulu kukwamisha juhudi zozote za kutekelezwa kwa ‘suluhisho la mataifa mawili’ huru na yenye amani, Israeli na Palestina, ambalo limependekezwa na jamii ya kimataifa kwa muda mrefu.

La ziada ni kwamba, ndiye waziri mkuu aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi tangu taifa la sasa la Israeli liundwe mnamo 1947.

Amedumu mamlakani kwa muda mrefu – ila kuna vipindi vichache ambavyo alishindwa chaguzi – kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya maadui wa Israeli.

Kila wanapotaka kiongozi wa kuwapigania, asiyetaka amani kati yao na maadui zao, anayeasisi na kuhimiza kutwaliwa kwa ardhi ya Wapalestina na walowezi wa Kiyahudi, Waisraeli humchagua ‘Bibi’.

Baada ya nyakati tukizi mno ambapo ameshindwa chaguzi, ‘Bibi’ amefanya juu chini, wakati mwingine kuwatia woga Waisraeli, ili kuhakikisha aliyemshinda hadumu mamlakani. Na bahati ikisimama kila anapojaribisha.

Kwa raia wa Israel, ‘Bibi’ ni kiongozi shupavu aliye radhi kuwafuata na kuwaangamiza maadui wao kokote waliko bila kuogopa lawama zozote, ilhali kwa Wapalestina anawakilisha pepo wa mauti.

SOMA PIA: Hivi ndivyo Rais Ruto anavyopaswa kuongoza nchi

Mja mkaidi kama mkia wa mbuzi, ‘Bibi’ alionyesha ukaidi huo alipohutubia Bunge la Amerika wiki jana, nyakati nyingine akigonga meza kwa hasira, akaapa kuwaangamiza magaidi wote wanaoilenga Israeli, siku chache kabla ya Haniyeh kuuawa.

Akitoa hotuba hiyo, aliwapuuzilia mbali na kuwadhihaki mamia ya waandamaji waliokuwa wakifoka kauli-mbiu za matukano nje ya Bunge hilo, wakipinga harakati za kijeshi ambazo Israeli inaendeleza dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Ilikuwa ajabu sana kumwona mwandamanaji aliyetokea kimasomaso, huku kajitanda bendera ya kundi la wapiganaji wa Hamas, ambalo lilikwisha kutajwa na Amerika kuwa kundi la kigaidi, nje ya majengo ya bunge nchini Amerika!

Hali ilivyo sasa kwenye eneo zima la Mashariki ya Kati ni kuwa Waisraeli wanashangilia kwamba adui yao mkuu ameondolewa duniani, nao raia wengi wa mataifa jirani ya Israel wanaamini mwakilishi wa pepo wa mauti amefanya mambo yake. Amewatenda.

Kutokana na tukio hilo la hivi majuzi, watu wengi kote duniani wanatumbua macho yao kwenye runinga, kusikiliza redio, kusoma magazeti na kuvinjari mtandaoni wakiwa na hamu ya kujua kuuawa kwa Haniyeh kutakuwa na athari gani kidiplomasia.

Haniyeh alikuwa kiungo muhimu wa harakati za amani

Ukizingatia kwamba marehemu alikuwa kiungo muhimu katika harakati za kuleta amani kati ya Israeli na Hamas – na kukomesha vita vinavyoendelea kati yao – sasa ni sahihi kusema kuwa mustakabali wa vita hivyo haujulikani.

Ni kupitia gazeti hili ambapo nilimfahamu ‘Bibi’ Netanyahu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1996, yapata miaka 28 iliyopita.

Wakati huo nilikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Pili, na nilikumbana na picha ya ‘Bibi’ nilipokuwa nikipekua kurasa za gazeti hili ofisini mwa mwalimu wangu wa Kiswahili.

Mwanzo nilichangamkia picha hiyo sana kwa kuwa, kupitia hadithi nilizotambiwa na mamangu, nilimjua kakake, Yoni Netanyahu, aliyeuawa nchini Uganda akiwa katika harakati za kuwaokoa mateka walioshikiliwa na wanamgambo wa Palestina mnamo mwaka 1976.

Saa chache kabla ya kuuawa, ndege alimosafiria Yoni na wanajeshi wengine bingwa wa Israel ziliongezewa mafuta nchini Kenya kabla ya kuvamia Uganda, kulemaza jeshi la wanahewa la jirani yetu huyo, na kuwaokoa mateka wote kasoro mmoja.

Mamia ya raia wa Iran walipojitokeza kuhudhuria maandamano kabla ya mazishi ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh jijini Tehran, Iran Agosti Mosi, 2024. Picha|Reuters

Katika fikra zangu za kitoto, hasa baada ya mamangu kunieleza jinsi aliyekuwa dikteta wa Uganda, Iddi Amin Dada, alivyoshirikiana na magaidi hao kuwateka na kuwatesa Waisraeli, Yoni alikuwa shujaa.

Ukitilia maanani taswira ya Shujaa Yoni niliyojengewa akilini na mamangu, utaelewa kwa nini nilifurahi nilipojua ndugu yake, ‘Bibi’, alichaguliwa kuiongoza Israel.

Katika fikra zangu kama Mkenya mchanga wakati huo, nilifurahi sana kwamba raia wa Israel waliona umuhimu wa ‘kurudisha mkono’, yaani kulipa wema kwa wema.

Ni baada ya kukua ambapo nilielewa kwamba ‘Bibi’ haisaidii Israel, hakika anaikwaza zaidi, kwa kuhakikisha kwamba haiishi kwa amani na majirani zake.

SOMA PIA: Vijana kuandaa maandamano bila Raila kwafaa kumkosesha usingizi Ruto

Ushawishi wa ‘Bibi’ umeenea mbali na karibu. Amefaulu kuwagawa Waamerika kwa makundi mawili: viongozi wa chama cha Democrat wanaosisitiza kutekelezwa kwa ‘suluhisho la mataifa mawili’, na wale wa Republican wanaotambua Israel na kupuuzilia mbali Palestina.

Usione ajabu kwamba ‘Bibi’ ameagiza Haniyeh aangamizwe; aliwahi kuwaagiza majasusi wa Israel wanaoogopwa mno kote duniani, Mossad, wamuue aliyekuwa kiongozi mkuu wa Hamas, Khalid Mashal, miaka ya tisini.

Mashal, ambaye tayari alikuwa ameshambuliwa kwa sumu, aliokolewa dakika chache kabla ya kuondoka duniani pale aliyekuwa rais wa Amerika, Bill Clinton, alipomshinikiza ‘Bibi’ kughairi nia ya kumwangamiza.

Sawa na jinsi jaribio la kumuua Mashal lilivyozua mzozo mkubwa wa kidiplomasia kati ya Israel kwa upande mmoja, na Amerika na mataifa kadha ya Kiarabu kwa upande wa pili, mauaji ya Haniyeh yanatarajiwa kuvuruga mambo. Letu jicho!

[email protected]