Makala

Bodaboda wavuna pakubwa kufuatia barabara kukatika Gamba

May 28th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

KUKATIKA kwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen katika eneo la Gamba kumeletea wahudumu wa bodaboda eneo hilo tabasamu, biashara ya uchukuzi kwa kutumia pikipiki ikinoga.

Barabara hiyo ambayo ndio kiunganishi cha pekee kwa Lamu na maeneo mengine ya nchi, ilikatwa na mafuriko mapema Mei, hali iliyotumbukiza wasafiri kwenye mahangaiko ya kila siku.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo aidha ulibaini kuwa huku abiria wakiendelea kuhangaika kutokana na ongezeko la gharama ya nauli kusafiri kwenye barabara hiyo, kwa upande mwingine imekuwa kicheko kwa wanabodaboda, wachuuzi na wafanyabiashara wengine wadogowadogo Gamba kwani wamekuwa wakivuna pakubwa.

Bw Bakari Abdi, ambaye ni mhudumu wa bodaboda kutoka mjini Witu, anasema amekuwa akifika Gamba kila siku kutegea wateja wanaofika au kuvukishwa pale, ambapo huwachukua na kuwapeleka vijiji vya Witu na viunga vyake.

Usafiri wa pikipiki kutoka Gamba hadi Witu si chini ya Sh500.

Bw Abdi anasema kabla ya barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen kusombwa na mafuriko na kukatika eneo la Gamba, biashara ya bodaboda ilikuwa chini.

“Kabla ya Gamba kukatwa na mafuriko, kwa siku nilikuwa nikipata Sh1000 pekee baada ya kung’ang’ana mchana kutwa. Mahangaiko ya Gamba kwa upande mwingine yamenogesha biashara yetu ya uchukuzi wa wateja kwa pikipiki. Kwa siku bodaboda hawezi kukosa kati ya Sh2000 na Sh3000,” akasema Bw Abdi.

Bw Kahindi Masha, ambaye ni bodaboda wa upande wa Gamba kuelekea Minjila, pia alikiri kuvuna pakubwa tangu usafiri ulipolemazwa na mafuriko eneo hilo.

Kusafirisha abiria au mizigo kutoka Gamba hadi Minjila ni Sh400.

Bw Masha anasema kwa siku yeye husafirisha abiria kwa awamu karibu kumi, hivyo kupata kati ya Sh3000 na Sh4000.

Wasiwasi wake ni kwamba huenda biashara hiyo ya uchukuzi wa bodaboda ikadidimia punde ujenzi na kuunganishwa upya kwa barabara ya Lamu-Witu-Garsen utakapokamilika.

“Kama uonavyo, tayari wameanza kuiunganisha barabara kwenye sehemu iliyokatwa kupitia kujaza mawe na changarawe. Hiyo inamaanisha punde ujenzi utakapokamilika, safari za abiria wanaotoka Lamu kuelekea Mombasa au Mombasa kuelekea Lamu zitakuwa za moja kwa moja. Tutakosa biashara,” akasema Bw Masha.

Mbali na bodaboda, biashara nyingine zinazofanya vyema Gamba ni uchuuzi wa vyakula, ikiwemo matunda, mahindi changa ya kuchemsha au kuchoma, chai nakadhalika.

Baadhi ya wachuuzi na akina mama n’tililie hata wamejenga vibanda vinavyotumiwa na wasafiri kukata kiu na njaa kabla ya kuendelea na safari zao.

Bi Lucy Komora anasema waliafikia kujenga vibanda hivyo wanavyovitumia kama hoteli baada ya kuona mahangaiko ya wasafiri wanaofika Gamba na kukaa muda mrefu bila mlo.

Wasafiri wanapofika Gamba hulazimika kusubiri boti au mashua za kuwavukisha upande mwingine ili kuunganisha safari zao.

Wasafiri waking’ang’ania kuabiri boti na mashua eneo la Gamba. Usafiri wa majini ni miongoni mwa biashara zinazofanya vyema tangu mafuriko kuikata barabara ya Lamu-Witu-Garsen eneo la Gamba. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kuvukishwa kwa boti kwenye eneo hilo lililosombwa na mafuriko la Gamba ni Sh300.

Awali wasafiri, hasa wale wanaofika Gamba mapema au kuchelewa walikuwa wakivumilia njaa wakisubiri kupata boti au mashua za kuwavukisha upande mwingine.

“Hili lilitugusa na tukaamua kuanzisha hivi vibanda vya watu kula kabla ya kuendelea na safari zao. Tunapika sima kwa samaki, mchele na maharagwe, chai na vyakula vingine vingi hapa na biashara inafanya vyema,” akasem Bi Komora.

Vibanda vya chakula vikiwa vimeezekwa pembezoni mwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen eneo la Gamba. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Margaret Kimani ambaye ni mchuuzi wa mahindi changa ya kuchemsha eneo la Gamba pia alikiri kuvuna pakubwa tangu barabara kusombwa na mafuriko.

Anasema kabla ya mafuriko, biashara yake ilikuwa chini kwani kwa siku angeuza mahindi mahindi 50 pekee.

Yeye huuza mahindi yake kwa Sh30.

Anasema baada ya kufika Gamba kutegea wateja, amekuwa akiuza hadi mahindi 150 kwa siku, hivyo kujipatia fedha za kukimu karo ya watoto wake.

“Nyakati kabla ya mafuriko na barabara kukatika, mahindi yangu nilikuwa nikiyauza Sh20 pale mjini Minjila. Baada ya barabara kukatwa, nimekuwa nikitegea wapiti njia hapa Gamba, ambapo huwauzia mahindi kwa Sh30. Wateja ni wengi. Abiria, madereva, manahodha na mahamali, wote ni wateja wangu. Nauza mahindi kwa wingi msimu huu,” akasema Bi Kimani.

Manahodha wa boti na mashua, mahamali na madereva wa magari aina ya probox pia ni miongoni mwa waja wanaofaidi pakubwa na hali ilivyo ya mafuriko Gamba.

Hamali akibeba mizigo eneo la Gamba. Mahamali pia wanavuna pakubwa tangu barabara ilipokatwa eneo la Gamba, Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wasafiri waliohojiwa waliiomba serikali kuharakisha ujenzi na kuunganishwa kwa eneo lililokatwa na mafuriko la Gamba ili kuwapunguzia gharama ya usafiri.

Bw Hussein Ali, mkazi wa Lamu, anasema kabla ya barabara yao kukatika eneo la Gamba, usafiri kidogo ulikuwa wa afueni.

Kwa mfano, nauli ya kusafiri moja kwa moja kutoka Lamu hadi Mombasa ni Sh1,500 pekee hasa endapo utaabiri basi la usafiri wa umma.

“Hali ilivyo Gamba leo hii inafanya tunahitajika kulipa nauli ya Sh1000 kufika Gamba. Kisha unaabiri boti au mashua kuvukishwa upande wa pili kwa Sh300. Halafu unaabiri gari lingine la kuunganisha na kumalizia safari yako, ambapo huhitajika kulipa Sh1000 tena kufikishwa Mombasa. Gharama ya usafiri inatuumiza. Waharakishe ujenzi wa barabara yetu,” akasema Bw Ali.

Abiria pia walilalamika kwamba hali ilivyo Gamba imekuwa ikichangia kucheleweshwa kwa safari zao.

Bi Maryam Abubakar alisema walikuwa wakitumia masaa kati ya matatu au manne pekee kufika Malindi au Mombasa.

“Ni rahisi na haraka kusafiri moja kwa moja kutoka Lamu hadi Mombasa au kurudi. Kukatwa kwa barabara yetu eneo la Gamba kumeleta dhiki. Tunachelewa kufika tuendako. Badala ya muda wa saa tatu au nne, kwa sasa hutumia hadi muda wa saa saba barabarani. Serikali isikie kilio chetu na kujenga hii barabara haraka. Tunateseka,” akasema Bi Abubakar.