Habari za Kitaifa

CJ Koome aamuru mbakaji atumikie kifungo kizima cha miaka 20    


MAHAKAMA ya Upeo imeamuru mbakaji aliyekuwa amepunguziwa kifungo akae jela miaka 20.

Katika uamuzi wao, Jaji Mkuu Martha Koome na Majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaack Lenaola waliharamisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kupunguza kifungo dhidi ya Joshua Gichuki Mwangi hadi miaka 15.

Jaji Koome na wenzake wanne walikubaliana na teteSi za

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Igonga kwamba “Mahakama ya Rufaa ilikosea kupunguza kifungo alichohukumiwa Gichuki cha miaka 20.”

Majaji wa Mahakama ya Upeo (Mahakama ya juu zaidi nchini) walisema ubakaji ni hatia mbaya na kwamba wahusika wanastahili kuadhibiwa vikali.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote, tetesi za DPP tumeafikia uamuzi kwamba majaji wa Mahakama ya Rufaa walikosea kupunguza adhabu aliyopitishiwa Gichuki na mahakama ya Karatina,” walisema majaji hao.

Gichuki alisukumwa jela baada ya hakimu mkazi mahakama ya Karatina kumpata na hatia ya ubakaji kwa mujibu wa Kifungu nambari 8 (1) na 8 (3) za sheria za dhuluma za jinsia.

Gichuki alipatikana na hatia ya kumbaka msichana mdogo mnamo Machi 8, 2011 katika lokesheni ya Ngorano, Mathira Magharibi.

“Hii mahakama imekupata na hatia ya ubakaji na utatumikia kifungo cha miaka 20,” hakimu aliyesikiza kesi hiyo alisema akipitisha adhabu mnamo Oktoba 17,2011.

Gichuki alikata rufaa kupinga uamuzi huo katika Mahakama Kuu lakini ikakataliwa na kuagizwa atumikie kifungo chote.

Lakini majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa walibatilisha uamuzi huo na kuamuru mbakaji huyo atumikie kifungo cha miaka 15.

DPP alilalamika kwamba majaji wa rufaa walipuuza sheria walipopunguza adhabu hiyo kwa kuamuru Gichuki atumikie kifungo cha miaka 15.

DPP alisema ijapokuwa baadhi ya vipengee vya Katiba vinaruhusu kupunguzwa kwa adhabu, Mahakama ya Rufaa haikuzingatia mamlaka  iliyopewa Mahakama Kuu chini ya kifungu nambari 160 kinachoipa mahakama uwezo wa kupunguza ama kutoa adhabu iliyo na makali zaidi.

Mahakama ya Upeo iliamuru Gichuki akamatwe tena na kurudishwa jela kukamilisha kifungo hicho cha miaka 20.

“Baada ya kutathmini ushahidi na sheria kwa pamoja hii mahakama imeridhika Gichuki anastahili kutumikia kifungo cha miaka 20 kama alivyohukumiwa na mahakama ya Karatina 2011. Endapo ameachiliwa akamatwe na kurudishwa jela kukamilisha kifungo,” Jaji Koome na majaji Ibrahim, Wanjala, Njoki na Lenaola waliagiza.

[email protected]