Habari Mseto

DCI – Raia wa Kichina Kenya wanavyotumia polisi kuteka nyara wenzao

January 21st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MAAFISA watatu wa kikosi cha kukabiliana na ghasia (GSU) wanazuiliwa kwa tuhuma za kutumiwa na raia wa Kichina wanaoishi Kenya kutekeleza utekaji nyara na kudai pesa kwa mabavu.

Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kupitia taarifa imesema kwamba Makonstebo Frederick Mwongela Mwololo, Samuel Mwiti na Kimwele Musyoki ambao ni maafisa wa GSU waliteka nyara Mchina mnamo Januari 8, 2024 katika Kaunti ya Machakos.

Huku tayari washukiwa hao wakiwa wameagizwa na mahakama ya Machakos watulie kama maji ya mtungi kizuizini ushahidi kufunguliwa mashtaka ukiendelea kuandaliwa, DCI ilisema “hawa ni washukiwa wa utundu miongoni mwetu kama polisi wanaotumiwa na Wachina katika njama zao za kuibiana”.

Taarifa hiyo ya DCI ilisema kwamba kinachochunguzwa ni mtandao wa kimataifa ulio na mizizi nchini China, ukilenga walio na ukwasi na ambao huishia kutekwa nyara na kuporwa.

“Katika njama hii, raia mmoja wa China aliyekuwa akielekea zake kazini akijibeba kwa gari lake alizubaishwa kwa kufungiwa barabara na magari mawili ya washukiwa katika barabara kuu kuelekea Mombasa kutoka Nairobi” taarifa hiyo inasema.

Soma pia: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/mwanamume-ashtakiwa-kwa-kumteka-nyara-mkewe

Washukiwa hao walimtia mbaroni Mchina huyo na kumweka pingu mikononi, kisha wakamsafirisha hadi milima ya Mua iliyoko Kaunti ya Machakos.

DCI inasema walipokezwa habari za kutoweka kwa raia huyo wa Kichina na wafanyakazi wenzake na pia jamaa na marafiki.

“Katika uchunguzi wetu tulibaini kwamba genge hilo lilijumuisha watu watano, wawili wengine wakiwa ni dereva wa teksi na pia ‘sonko’ mfadhili wa njama hiyo akiwa pia ni Mchina,” DCI ikasema.

Taarifa hiyo inaelezea kwamba mwathiriwa alishinikizwa kupiga simu nyumbani kwao China na aamrishe pesa ziwekwe kwenye akaunti ya benki nchini humo na baada ya kutii amri, akaachiliwa huru.

“Washirika wa njama hiyo wakiwa China walipiga simu katika danguro hilo la utekaji nyara na wakathibitisha kwamba pesa zilikuwa zimewekwa katika akaunti ya ujambazi huo,” DCI ikasema.

Magari mawili yanayoaminika yalitumika katika njama hiyo tayari yamenaswa, mshukiwa mkuu Mchina akiendelea kusakwa huku ushirika wa polisi duniani (Interpol) ukiwajibishwa jukumu la kusaka washukiwa wengine nchini China.

[email protected]