Habari za Kitaifa

DCI yafunga shule ya Hillside kutoa mili ya wanafunzi walioteketea


MAAFISA wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamefunga shule ya msingi ya Hillside Endarasha Academy, ambapo mkasa wa moto  uliua wanafunzi 18 Alhamisi.

Takriban wanafunzi wengine 13 wamelazwa katika hospitali mbalimbali kaunti ya Nyeri wakipokea matibabu.

Maafisa hao, wakiongozwa na afisa wa kitengo cha kuchunguza mauaji Bw Martin Nyuguto, walisema eneo hilo  limefungwa, hata kwa wanahabari.

Timu hiyo inayojumuisha wataalamu wa maiti ilifanya mkutano Jumamosi asubuhi ili kupanga shughuli za uchunguzi pamoja na kutoa mili kutoka eneo la mkasa.

Bw Nyuguto alisema walinuia kutumia eneo hilo kwa shughuli za uchunguzi na ingawa  hakutoa maelezo zaidi, kufika kwa wataalamu wa uchunguzi wa maiti kulionyesha kwamba mili ambayo ilinaswa katika bweni hilo ingeanza kutolewa.

“Ijumaa hatukuweza kufanya mengi kwa sababu tulikuwa tukishughulika na wazazi na familia,” Bw Nyuguto alisema.

Wanahabari walitakiwa kuondoka katika shule  hiyo ili kuruhusu wachunguzi kuanza kazi yao.

Maafisa wakuu wa serikali waliotarajiwa kusimamia shughuli walikuwa ni pamoja na Waziri wa Elimu Julius Ogamba, kulingana na ripoti.

Mnamo Ijumaa, wazazi waliofika katika taasisi hiyo waliruhusiwa kutazama eneo la uhalifu kujionea lilivyokuwa, na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya pia wanatarajiwa kuendeleza mchakato wa kuwaunganisha wanafunzi na wazazi wao.

Siku tatu za maombolezo

Rais William Ruto alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya wanafunzi waliofariki katika mkasa huo wa moto.

Dkt Ruto pia alitangaza kuwa katika kipindi hicho, kuanzia Jumatatu, Septemba 9, 2024 hadi Jumatano, Septemba 11, bendera ya Kenya na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitapeperushwa nusu mlingoti Ikulu, balozi zote za Kenya na majengo ya umma miongoni mwa maeneo mengine.

Aliapa kwamba wote waliohusika  watachukuliwa hatua ili kuhakikisha kuwa janga kama hilo halitokei tena.

“Kama Rais wenu, naahidi kwamba maswali magumu ambayo yameulizwa kama vile jinsi mkasa huu ulivyotokea yatajibiwa kikamilifu, kwa uwazi, na bila woga wala upendeleo,” Rais Ruto alihakikisha.

Imetafsiriwa na Benson Matheka