Dimba

Amorim pabaya dalili zote zikiashiria hana uwezo wa kufufua makali ya Man Utd

Na CHRIS ADUNGO September 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FOWADI na nahodha wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney, amedai kuwa kikosi hicho kwa sasa kinayumba na kusuasua zaidi chini ya kocha Ruben Amorim.

Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) walimpokeza Amorim mikoba yao mnamo Novemba 1, 2024 ili kujaza nafasi ya Erik ten Hag aliyetimuliwa.

Lakini zaidi ya miezi 10 baadaye, mkufunzi huyo raia wa Ureno ameshindwa kunyanyua waajiri wake huku dalili zote zikiashiria kwamba hana uwezo wa kufufua tena makali ya miamba hao wanaozidi kudidimia.

Man-United walikubali kichapo cha 3-0 kutoka kwa Manchester City katika gozi la EPL lililochezewa ugani Etihad mnamo Jumapili huku mashabiki wao wakiondoka uwanjani hata kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa pambano hilo kupulizwa.

“Nataka kutoa maoni yasiyoegemea kabisa upande wa kocha wala wachezaji. Ni vigumu sana kukaa hapa na kutarajia maendeleo. Sioni hata tumaini dogo la kikosi hiki kuanza kusajili matokeo bora katika siku za usoni,” akasema.

Rooney ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Man-United baada ya kupachika wavuni mabao 253 kati ya 2004 na 2017.

Mgongo wake unasomwa na majagina Sir Bobby Charlton (245), Denis Law (237) na Jack Rowley (190).

“Kulikuwa na tukio la mashabiki kuondoka ugani kuelekea mwisho wa mechi. Ungewasikia wakiimba jina la Amorim huku wakitaka refa akamilishe mchuano. Nadhani walikuwa wamekata tamaa na hawakufurahishwa na mchezo wa kikosi kizima. Hiyo ni taswira isiyokubalika kabisa,” akasema Rooney.

Chini ya Amorim, Man-United waliambulia nafasi ya 15 kwenye jedwali la EPL msimu uliopita wakiwa na pointi 42; hiyo ikiwa nafasi yao ya chini zaidi tangu 1989-90. Isitoshe, alama hizo walizojizolea ndizo chache zaidi kwao kuwahi kupata ligini tangu waliposhushwa daraja mara ya mwisho mnamo 1973-74.

Tangu Amorim atue ugani Old Trafford, Man-United wametumia takriban Sh43.5 bilioni kununua wachezaji wapya huku wakiagana pia na idadi kubwa ya wanasoka waliotofautiana na kocha huyo wa zamani wa Sporting CP ya Ureno.

Idadi kubwa ya masogora wa haiba ugani Old Trafford imemruhusu Amorim, 40, kutumia sana mfumo wa 3-4-3 ambao ameapa kutouacha baada ya kumvunia mafanikio tele alipoukumbatia kambini mwa Sporting.

“Nitafanya chochote ninachoweza kwa ajili ya ufufuo wa makali ya Man-United. Huo ndio ujumbe wangu wa kiapo changu kwa mashabiki wa kikosi hicho,” akaahidi Amorim ambaye kwa sasa ana presha ya kuchochea kuanza kusajili matokeo ya kuridhisha.

Baada ya kualika Chelsea wikendi hii, Man-United wameratibiwa kuvaana na Brentford, Sunderland, Liverpool, Brighton, Nottingham Forest, Tottenham Hotspur na Everton kwa usanjari huo.

Pamoja na kumweka Amorim katika hatari ya kupigwa kalamu, kichapo kutoka kwa Man-City pia kiliendeleza rekodi duni ya Man-United ambao wamejizolea alama nne kutokana na mechi nne za EPL kufikia sasa msimu huu.

Man-United walibanduliwa kwenye raundi ya pili ya Carabao Cup mwezi jana baada ya Grimsby Town kuwafunga penalti 12-11 kufuatia sare ya 2-2.

Mabao manne na alama nne kutokana na mechi nne za kwanza za EPL ndiyo matokeo duni zaidi ambayo Man-United wamewahi kusajili katika hatua hiyo ligini tangu 1992-93 wakiwa chini ya kocha Sir Alex Ferguson.

Kufikia wakati huo, hata hivyo, Ferguson tayari alikuwa amejizolea sifa tela baada ya kushindia waajiri wake Kombe la FA, League Cup na European Cup Winners’ Cup pamoja na kuwaongoza kuambulia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL mnamo 1987-88.

Kati ya timu 17 ambazo zimekuwa katika EPL tangu Amorim atue Old Trafford, Man-United ndiyo yenye rekodi rekodi mbaya zaidi pamoja na Spurs ambayo pia imejizolea alama 31 pekee kutokana na mechi 31.

Man-United wameshinda mechi nne pekee kati ya 26 zilizopita dhidi ya timu hizo zilizokuwa ligini kabla ya Leeds United, Burnley na Sunderland kupandishwa ngazi mwisho wa msimu jana.