Dimba

EPL: Shoka lasubiri Amorim Man United wakipigwa na Chelsea

Na GEOFFREY ANENE September 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MANCHESTER, Uingereza

HUENDA hatima ya kocha Ruben Amorim kambini mwa Manchester United ikaamuliwa katika mchuano mkali wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya wageni Chelsea, katika uwanja wa Old Trafford, Jumamosi.

Kocha huyo Mreno anaandamwa na presha kubwa kupata matokeo mazuri.

Amorim (kulia) baada ya mechi dhidi ya Manchester City uwanjani Etihad mnamo Septemba 14, 2025. PICHA | REUTERS

Mchanganuzi na staa wa zamani wa soka, Alan Shearer, ameonya kwamba Amorim anaweza “kufa na upanga wake” ikiwa hatabadilika, baada ya Red Devils wa Man United kuaibishwa 3-0 katika debi ya Manchester dhidi ya Manchester City wikendi iliyopita.

Matokeo hayo yamemfanya Amorim kuwa na asilimia ndogo zaidi ya ushindi kati ya makocha ambao wamewahi kunoa Red Devils tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, huku klabu hiyo ikiwa na mwanzo wake mbaya kabisa kwenye EPL katika kipindi cha miaka 33.

Amorim amesisitiza kwamba hataacha falsafa yake, akisema: “Nikihitaji kubadilisha falsafa yangu, nitabadilisha. Ikiwa sivyo, basi mtabadili mtu. Ninaamini njia yangu na nitaendelea nayo hadi pale nitakapoamua kubadilisha.”

Shearer alisema mchezo wa United ugani Etihad ulifichua mapengo makubwa katika uwezo, mfumo na mtazamo, licha ya klabu kumwaga Sh36.3 bilioni (Pauni 207.5 milioni) sokoni majuzi kusaini wachezaji mastaa wakiwemo washambulizi Bryan Mbeumo kutoka Brentford, Matheus Cunha (Wolves) na Benjamin Sesko (Leipzig).

Nico O’Reilly (kulia) wa Man City na Bryan Mbeumo wa Man United mechi yao ugani Etihad mnamo Septemba 14, 2025. PICHA | REUTERS

Aliongeza kuwa kipigo kingine kikubwa kitafanya nafasi ya Amorim kuwa maji yaliyomwagika; hayazoleki tena, huku United wakidumaa nje ya 10-bora katika jedwali la ligi hiyo ya klabu 20.

Majeruhi kwa wachezaji muhimu kama Cunha, Mason Mount na Diogo Dalot hayajasaidia lakini Shearer anasema bado hakuna dalili zozote kwamba timu imepiga hatua.

United wanapokutana na Blues ugani Old Trafford mfumo wa Amorim unazidi kugawanya maoni na hisia, na ingawa ameshikilia msimamo wake Shearer anaamini shinikizo zimefikia kiwango cha juu.

Ushindi Jumamosi unaweza kumpa Amorim muda zaidi, lakini kichapo kingine kikubwa kitalazimu uongozi wa klabu kuchukua hatua haraka.