Dimba

Arsenal kibogoyo ikiaga Carabao Cup

Na GEOFFREY ANENE February 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA Mikel Arteta alikiri masogora wake walikosa meno ya kung’ata Newcastle baada ya kubanduliwa kwenye Kombe la Carabao kwa jumla ya mabao 4-0, katika nusu-fainali Jumatano usiku.

Vijana wa Arteta sasa wamesalia katika mashindano mawili – Ligi Kuu (EPL) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Walipoteza 2-0 katika mkondo wa kwanza ugani Emirates mnamo Januari 7, na kupokea dozi sawa na hiyo katika mkondo wa pili kupitia mabao ya Jacob Murphy na Anthony Gordon uwanjani St James’ Park hapo Jumatano usiku.

Wanabunduki wa Arsenal pia walinyamazishwa 1-0 ligini Novemba 2024, kumaanisha wamepoteza mara tatu mfululizo mikononi mwa Newcastle, na pia wamepoteza mara nne katika mechi tano dhidi ya vijana wa kocha Eddie Howe.

Arsenal walifanya kila kitu dhidi ya Newcastle isipokuwa kufunga bao.

Walizidia Newcastle kwa umilikaji wa mpira (asilimia 69 kwa 31), makombora (11-10), pasi (423-203) na kona (13-1) wanazofahamika kufungia mabao, lakini wakaonyesha kuwa na matatizo yake ya zama ya kukosa makali langoni.

Newcastle walituma jumla ya makombora 17 kuelekea lango la upinzani huku Arsenal wakiwarushia 34 katika mikonndo yote miwili, lakini ni Gunners waliangukia pua katika kichapo hicho cha jumla cha 4-0.

Walijibwaga uwanjani St James’ Park wakilenga kufufua matumaini baada ya kuchabanga Manchester City 5-1 ligini nao Newcastle walikuwa wamepoteza 2-1 mikononi mwa Fulham.

Sasa wataelekea jijini Dubai katika Milki za Kiarabu (UAE) kwa kambi ya mazoezi ya majira ya joto kabla ya mchuano ujao dhidi ya Leicester ligini hapo Februari 15.

“Inauma kupoteza mchuano huu kwa sababu tulikuwa na matumaini makubwa. Tulifahamu kitakuwa kibarua kigumu baada ya kupoteza mkondo wa kwanza,” alitanguliza kocha Arteta.

“Sasa ni kulenga mbele kwa sababu ni uchungu. Tunaelekea Dubai tukitumai itatutasaidia kupata makali kwa sababu bado tuna mengi ya kupigania,” akaongeza Mhispania huyo ambaye vijana wake walibanduliwa na Manchester United kwenye Kombe la FA hapo Januari 12.

Arsenal wanakamata nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu kwa alama 50 kutokana na michuano 24, pointi sita nyuma ya Liverpool walio na mechi moja ya akiba.

Wako pia kwenye raundi ya 16 ya UEFA. Vijana wa Arteta wana kibarua kigumu kushinda mojawapo ya mashindano hayo mawili.

Nao Newcastle sasa wako pazuri kumaliza ukame wa miaka 70 bila taji nyumbani. Watakutana na mshindi kati ya Liverpool na Tottenham katika fainali ya Carabao.

Mara ya mwisho Newcastle walishinda taji nyumbani ni 1955 ambalo ni Kombe la FA. Taji la mwisho walishinda ni Inter-Cities Fairs Cup mwaka 1969 ambalo sasa ni Kombe la Europa League.