Dimba

Arsenal waomba muujiza Paris kesho nusu fainali ya Uefa

Na JOHN ASHIHUNDU May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

PARIS, UFARANSA

ARSENAL wana mlima mkubwa wa kukwea watakapokutana na PSG Jumatano usiku katika duru ya pili ya nusu fainali ya mechi za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA Champions League) baada ya kushindwa kwa bao 1-0 na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) katika duru ya kwanza ugani Emirates wiki jana.

Katika mechi ya kwanza, Arsenal walishindwa kutumia vyema nafasi nyingi walizopata kusawazisha bao hilo licha ya kufanya mashambulizi mara kwa mara langoni mwa wapinzani wao ambao walilemewa dakika za lala salama.

Gabriel Martinelli na Leandro Trossard ni miongoni mwa mastaa wa Arsenal waliopoteza nafasi za wazi.

Lakini huenda kikosi hicho cha Mikel Arteta kikapata nguvu zaidi kutokana na uwepo wa kiungo tegemeo Thomas Partey aliyekosa mechi iliyopita kutokana na marufuku baada ya kula kadi kadhaa za njano, huku wengi wakiamini kama raia huyo wa Ghana angekuwepo angemzuia mfungaji staa, Ousmane Dembele, raia wa Ufaransa kuipa PSG ushindi.

Partey, 31, ni kati ya wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Arteta ambapo uwepo wake utamfanya Mikel Merino arejeshwe kwenye nafasi yake ya mshambuliaji wa kati huku Declan Rice akicheza kama kiungo wa safu ya ulinzi, badala ya namba nane.

Arteta amesema kikosi chake kitashughulikia mechi hii kwa umakini mkubwa kama ilivyokuwa waliposafiri Madrid kucheza mkondo wa pili wa robo fainali wakijivunia uongozi wa 3-0.

Lazima twende Paris na mawazo ya kushinda. Tuna uwezo huo. Naamini tunaweza kufuzu fainali. Waliponea kwa sababu kipa wao Donnarumma alifanya kazi nzuri siku hiyo — Kocha wa Arsenal Mikel Arteta

Licha ya Arsenal kuvuma kwa kiasi fulani kwenye mechi hiyo, PSG chini ya kocha Luis Enrique waliumiliki mpira kwa kiasi asilimia 75% hasa katika dakika 15 za kwanza na kufunga bao la mapema dakika ya nne kupitia kwa Ousmane Dembele aliyepenya ngome ya Arsenal mara kwa mara.

Baada ya kupewa nafasi mwishoni mwa wiki dhidi ya Bournemouth, Partey alionekana kuwa katika kiwango kizuri na huenda akawa muhimu kwa kikosi cha Arsenal katika mechi ya Jumatano katika juhudi zao za kupindua matokeo na kufuzu kwa fainali ya UEFA.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi dhidi ya vijana wa PSG ambao hadi kufikia hatua hii ya nusu fainali tayari wameondoa timu mbili za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Aston Villa na Liverpool, baada ya awali kuchapa Manchester United katika hatua ya makundi.

Licha ya Jurrien Timber kuvutia mashabiki wengi msimu huu kutokana na udhabiti wake, raia huyo wa Uholanzi alipata kibarua kigumu kutoka kwa Khvicha Kvaratskhelia aliyekuwa mwiba kwenye ngome ya Arsenal.

Kvaratskhelia ndiye aliyetoa pasi ya bao lililofungwa na Dembele baada ya kupenya hadi ndani ya eneo la hatari kabla ya kumrudishia pasi Dembele alimimina wavuni bao hilo kutoka pembeni.

Katika mechi hiyo, Bukayo Saka alionekana mara kwa mara akirudi kumsaidia Timber kuvuruga juhudi za mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Georgia.