Arsenal yavunja moyo mashabiki wa Man United kwa kubomoa Man City
ARSENAL wamekosesha mashabiki wa Manchester United amani baada ya kunyamazisha mabingwa watetezi Manchester City 5-1 ugani Emirates, Jumapili.
Mashabiki wa United waliunga mkono City baada ya kupoteza 2-0 mikononi mwa Crystal Palace wakitumai kuwa Arsenal wataangushwa wawe katika kapu moja la huzuni, lakini matumaini yao yakazimwa na mabao kutoka kwa Martin Odegaard dakika ya pili, Thomas Partey (56), Myles Lewis-Skelly (62), Kai Havertz (76) na Ethan Nwaneri (90+3).
Wanabunduki wa Arsenal sasa wamekamilisha mechi 14 bila kupoteza kwenye Ligi Kuu (EPL).
Arsenal, ambao mara ya mwisho walikuwa na rekodi kama hiyo ya michuano 14 bila kupoteza ligini ni wakiwa chini ya Unai Emery kati ya Agosti na Desemba 2018, walikuwa katika ligi tofauti dhidi ya mwalimu wa Arteta, Pep Guardiola.
Mfumaji matata Erling Haaland alisawazishia City 1-1 dakika ya 55, lakini baada ya Partey kurejesha Arsenal kifua mbele kupitia kombora la mbali, vijana wa Guardiola wakakosa majibu.
Ushindi huo mtamu unafikisha alama za vijana wa kocha Mikel Arteta kuwa 50 kutokana na mechi 24. Nambari mbili Arsenal wako alama sita nyuma ya viongozi Liverpool walio na mechi moja ya akiba.
Nottingham Forest wanapatikana katika nafasi ya tatu kwa alama 47. City na Newcastle wanafunga mduara wa tano-bora wakiwa na alama 41 kila mmoja katika usanjari huo.
Jumatatu itakuwa zamu ya Chelsea kualika West Ham ugani Stamford Bridge.
MATOKEO YA EPL JUMAPILI:
Manchester United 0-2 Crystal Palace
Brentford 0-2 Tottenham
Arsenal 3-1 Manchester City