Dimba

Arteta agutuka baada ya Jesus kuumia, sasa atupia jicho mvamizi wa Juve Dusan Vlahovic

Na REUTERS, JOHN ASHIHUNDU January 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Mikel Arteta amelazimika kuingia sokoni katika kipindi hiki kifupi cha uhamaji wa wanasoka, akitarajiwa kusajili wachezaji kadhaa kwa lengo la kuimarisha kikosi chake ambacho kimeanza kuyumbayumba katika siku za hivi majuzi.

Kushindwa na Newcastle United katika kabumbu ya Carabao Cup na baadaye kubanduliwa na Manchester United katika FA Cup, raundi ya tatu, mnamo Jumapili, kumeibua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo wanaohofia pia majeruhi wengi kikosini.

Mjadala huu umeibuka wakati mashabiki hao wanasubiri kuona kikosi hicho kikabiliana na Tottenham Hotspur leo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuanzia saa tano usiku.

Jumanne, vyombo kadhaa vya habari nchini Uingereza viliripoti kuwa Arteta ameanza mikakati ya kumsajili mvamizi stadi wa Juventus ya Italia, Dusan Vlahovic.

Hata hivyo, ofa ya kwanza ya Arsenal kumsajili mwanasoka huyo raia wa Serbia kwa mkopo iligonga mwamba jana baada ya Juventus kudinda kuikubali.

Hata hivyo, jarida la soka la Football Transfers lilisema kuwa Arsenal ina nafasi kubwa ya kumpata mchezaji huyo iwapo itampa mkataba wa kudumu.

Jarida hilo linaongeza kuwa mpango wa Arsenal ni kumsajili Vlahovic kwa mkopo ikijiandaa kumchukua kwa mkataba wa kudumu mvamizi wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, baadaye mwaka huu.

Baadaye jana ripoti zilichipuka kuwa The Gunners walianza kusemezana na maskauti wa sogora wa PSG, Randal Kolo Muani.

Arteta analenga kuunda kikosi upya huku akidai jeraha linalomkabili nyota Gabriel Jesus ni la kutisha, hasa wakati huu ambapo tayari timu yake imepoteza Bukayo Saka vibaya aliyeumia wiki chache zilizopita.

Jesus aliumia dhidi ya Manchester United ambao waliibuka na ushindi wa mabao 5-3 kupitia kwa penalti katika mechi iliyomalizika kwa sare ya 1-1 katika muda wa kawaida na ziada.

Huku ripoti ya daktari kuhusu jeraha la Jesus ikisubiriwa kwa hamu, Arteta alisema kikosi chake kimelemaa kutokana na majeraha ya mara kwa mara kwa wachezaji muhimu.

Kuhusu debi ya kesho dhidi ya Tottenham Hotspur, huenda Arteta akakabiliwa na matatizo ya kuunda safu ya ushambuliaji ambayo haitakuwa na mastaa kadhaa wanaouguza majeraha.

Mshambuliaji mstaafu, Chris Sutton amesema Arsenal haihitaji sana mshambuliaji, lakini mchango wa kikosi kizima utakuwa muhimu zaidi.
Kabla ya Saka kuumia, Arsenal ilisumbuka kwa wiki kadhaa kutokana na kukosekana kwa kiungo mahiri Martin Odegaard alipojeruhiwa.

Washambuliaji wengine wanaofikiriwa kutua Emirates ni Matheus Cunha na Liam Delap, huku kukiwa na madai kwamba Arteta amekosa mtu wa kumshauri tangu mkurugenzi wa soka wa Arsenal, Eduardo Gasper (Edu) aondoke Novemba 2024.

Kuna uvumi kuwa klabu hiyo inapanga kumleta Thomas Roscky kujaza nafasi hiyo.

Sutton alisema Arsenal wanahitaji mshambuliaji stadi kama Victor Osimhen wa Nigeria anayechezea Galatasaray ya Uturuki kwa mkopo baada ya dili yake ya kujiunga na Chelsea kutibuka dakika ya mwisho.

Ratiba ya EPL, Jumatano:

Everton vs Aston Villa (22:30pm), Arsenal vs Tottenham (23pm), Newcastle United vs Wolves (22:30pm).