Pambo

Aibu ilioje! Watu wazima kumdhalilisha mtoto anayelilia amani, afya ya akili

Na MARY WANGARI November 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

FATAKI  

SEHEMU kubwa wiki hii midahalo ilizagaa mitandaoni ambapo watu wazima, wanawake kwa wanaume, wengi wao ambao ni wazazi, waliungana kumdhalilisha mtoto. 

Endapo wewe ni mraibu wa mitandao ya kijamii, bila shaka ulikumbana na video au kusoma jumbe za watu wakimsawiri vibaya, kunuiza mambo ya soni na hata kumlaani mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14. 

Mtoto huyu ambaye kosa la pekee ni ujasiri wa kusimama kidete kutetea amani na afya yake ya akili pamoja na kaka yake mdogo alijipata taabani huku watu wazima wenye akili razini na waliopevuka kiumri wakimmiminia cheche za matusi. 

Kisa na maana? Alisisitiza kuendelea kuishi na baba yake wa kambo aliyewalea tangu utotoni pamoja na kaka yake mdogo baada ya wazazi wao kutengana na mama yao mzazi kufa baadaye. 

Licha ya kudhalilishwa na watu walioonekana kujawa na machungu ya kushangaza, binti huyo alisema bayana ni heri afe aungane na mama yake jongomeo kuliko kwenda kuishi na baba yake mzazi baada ya kushuhudia aliyompitishia mama yake. 

Ilistaajabisha sana kusikia na kusoma jumbe za watu wazima hasa kina mama ambao wangetarajiwa kufahamu uchungu wa mwana wakimuumbua mtoto huyo jinsi alivyopotoka na kubashiri atakavyoishia vibaya maishani. 

Wengine bila haya walinuiza kuwa msichana huyo tayari anashiriki unyumba na baba yake mlezi ndiposa hataki kwenda kuishi na baba yake mzazi licha ya kuwa tajiri na kupatiwa usimamizi na korti. 

Kanuni za utu, maadili na utamaduni wa Kiafrika unawaasa wazazi kutowasema vibaya watoto wa wenzao wakifahamu fika kwamba wao pia wanalea watoto. 

Inavunja moyo kuona jinsi baadhi ya wanajamii wamezoea na kukubali maovu kiasi kwamba mazuri yanapotokea wanayapinga vikali. 

Hawaamini mwanamke aliyekandamizwa na mumewe na kuachwa na watoto anaweza kumpata mwanamme atakayempenda pamoja na watoto wake na kumwoa kihalali.  

Wanakereketwa maini kuona kuwa inawezekana baba au mama wa kambo kuwapenda na kuwatunza watoto waliokataliwa na kutelekezwa na wazazi wao halisi. 

Wanaungulika kuwa baadhi ya watu hawapitii madhila waliyotarajia na wamesitirika kwa neema ya Maulana.