Dimba

Chebet na Kipyegon watetemesha Amerika wakiweka rekodi za dunia za 5000m na 1500m mtawalia

Na GEOFFREY ANENE July 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA Beatrice Chebet na Faith Kipyegon waliandika historia kwa kuvunja rekodi za dunia katika mbio za mita 5,000 na 1,500m mtawalia, katika riadha za Diamond League zilizofanyika mjini Eugene nchini Amerika, Jumamosi, Julai 5, 2025.

Katika makala ya 50 ya Prefontaine Classic, bingwa wa Olimpiki wa 5,000m na 10,000m Chebet alikamilisha 5,000m kwa dakika 13:58.06 na kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kukimbia umbali huo chini ya dakika 14.

Alivunja rekodi ya dunia ya Gudaf Tsegay ya 14:00.21 iliyowekwa mwaka 2023 mjini Eugene.

Chebet alikimbia kwa kasi ya kuvutia, akiwa mbele ya Muethiopia Tsegay na Agnes Ngetich, na kuongezea kasi yake mita 200 za mwisho ili kumaliza kwa kishindo. Ngetich aliridhika na mafasi ya pili kwa 14:01.29, muda wa tatu bora katika historia, huku Tsegay akifunga tatu-bora kwa 14:04.41.

“Sikuwahi kufikiria nitakuwa wa kwanza kumaliza 5,000m chini ya dakika 14,” akasema Chebet.

“Baada ya Rome Diamond League nchini Italia (ambako alikimbia 14:03.69), nilijua nina uwezo. Nilijiambia, ‘ikiwa Faith anatafuta rekodi mjini Eugene, kwa nini mimi nisiitafute pia?” akauliza.

Karibu dakika 80 baada ya ulimwengu kushuhudia mwanamke wa kwanza kukamilisha 5,000m chini ya dakika 14, bingwa wa dunia na Olimpiki wa 1,500m Kipyegon naye aliandika historia katika 1,500m kwa kukimbia 3:48.68 na kuvunja rekodi yake ya dunia ya 3:49.04 aliyoweka Paris, Ufaransa mwaka jana kwa sekunde 0.36.

Kipyegon alikamilisha 400m za kwanza kwa 1:01.61 na 800m kwa 2:03.17, akiwa na Jessica Hull wa Australia unyo kwa unyo. Lakini Kipyegon aliongeza kasi katika mzunguko wa mwisho na kushinda kwa karibu sekunde tatu mbele ya Diribe Welteji wa Ethiopia (3:51.44) na Hull (3:52.67).

Katika 3,000m kuruka viunzi na maji, mzawa wa Kenya, Winfred Yavi wa Bahrain alikaribia kuvunja rekodi ya dunia kwa kukimbia 8:45.25, muda wa tatu bora katika historia.

Bingwa wa dunia na Olimpiki 3,000m kuruka viunzi na maji Yavi alimshinda bingwa wa zamani wa Olimpiki Peruth Chemutai wa Uganda katika hatua za mwisho, huku kinda Faith Cherotich akimaliza wa pili kwa 8:48.71 na Chemutai wa tatu kwa 8:51.77.

Hii ilikuwa mara ya kwanza Cherotich alipoteza msimu huu.