Dimba

Equity Hawks wafuzu fainali ya mpira wa vikapu

Na TOTO AREGE October 9th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

EQUITY Hawks wamefuzu kwa fainali za Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu nchini (KBF) kwa wanawake baada ya kuilaza Stanbic Aces 82-64 katika mechi ya tano na ya mwisho ya nusu-fainali iliyochezwa Alhamisi jioni katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Ushindi huo uliwapa Hawks ushindi wa jumla wa mechi 3-2 katika mfululizo wa mechi tano, na sasa watamenyana na mabingwa watetezi Kenya Ports Authority (KPA) katika fainali zitakazochezwa kwa mfumo wa mechi tano.

Stanbic walikuwa wameanza vyema kwa kushinda mechi ya kwanza 66-60 na ya tatu 56-53, lakini Hawks walijikakamua na kushinda mechi ya pili 70-37 kabla ya kulazimisha mechi ya tano kwa ushindi wa 68-36 katika mechi ya nne.

Katika mechi ya Alhamisi, Stanbic walianza kwa kuongoza 12-9, lakini Hawks walijibu kwa kishindo na kumaliza robo ya kwanza wakiwa mbele kwa pointi 29-22.

Hawks waliendeleza makali yao katika robo ya pili, wakikusanya pointi 21 dhidi ya 13 za Aces na kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele 50-35.

Betty Kananu alikuwa nyota wa Hawks, akifunga alama 27. Taundeciah Peter alichangia alama 17, huku Melissa Akinyi akifunga  14 na Frida Yagomba akiongeza 11.

Kocha wa Hawks, Ben Oluoch, aliwasifia wcahezaji wake kutokana na nidhamu katika kunasa mipira, akisema vilikuwa vipengele muhimu vilivyowasaidia kushinda mechi hiyo yenye presha kubwa.

Hawks sasa wanajiandaa kukabiliana na KPA, ambao walifuzu kwa fainali baada ya kuwanyuka Swish 3-0.