Hasimu wa Netanyahu, Gadi Eisenkot ateuliwa kuunda serikali
JERUSALEM, Israel:
RAIS wa Israel, Isaac Herzog, mnamo Jumamosi alimchagua Gadi Eisenkot, hasimu mkuu wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kujaribu kuunda serikali mpya, siku chache baada ya uchaguzi uliokumbwa na pingamizi kali uliowaacha viongozi wote wawili bila mkondo wazi wa mamlaka.
Netanyahu, kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini humo, anapigania kusalia mamlakani baada ya muungano wake wa ‘kambi ya kitaifa’ kupoteza idadi ya wengi katika uchaguzi wa Oktoba 27 lakini bado ukaibuka kama kambi kubwa zaidi bungeni.
Netanyahu ni mwanachama wa chama cha Likud ambacho ni cha mrengo wa kulia.
Eisenkot, aliyekuwa kiongozi wa jeshi amekataa kujiunga na vyama vya Waarabu ambavyo kama vingemuunga mkono, angepata idadi kubwa ya viti bungeni.
Lakini viongozi wa Waarabu, walioghadhabishwa na wanachoona kuwa sera za ubaguzi za Netanyahu na wandani wake wa mrengo wa kulia, bado walimteua Eisenkot kujaribu kuunda serikali kwanza – na kumuunga mkono zaidi.
“Rais Herzog amemwalika Gadi Eisenkot kwenye Makazi ya Rais, ambapo atatwikwa jukumu la kuunda serikali kesho,” alisema msemaji wa Rais Herzog, ambaye jukumu lake la usimamizi kwa sehemu kubwa linahusu kuteua mgombea kuunda muungano baada ya uchaguzi.
Kwenye ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X, Eisenkot aliandika, “Sasa ni wakati wa kuunda serikali ya dharura ya kitaifa. Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha tunastahili.”
Majuma kadhaa ya mazungumzo ya kina yanatarajiwa kufuata uteuzi wa Eisenkot.
Ana siku 28 kujaribu kubuni serikali ikiwemo uwezekano wa nyongeza ya siku 14.
Mbinu anazoweza kutumia zinajumuisha kujaribu kubuni serikali ya wachache kupitia kura za chama cha Waarabu kuhusiana na masuala nyeti, kubuni muungano na vyama vya mrengo kinzani ambavyo yeye na wandani wake wamevipuuza awali, au kubuni serikali ya muungano na Netanyahu.
Wachanganuzi wanasema mbinu zote hizo tatu huenda zisifanyike.
Endapo Eisenkot atafeli, mgombea mwingine anaweza kubuni serikali na ikiwa mgombea huyo atafeli, bunge linaweza kumteua mwingine.
Kuna makataa ya mchakato huo ya takriban siku 100.
Ikiwa hakuna atakayefanikiwa, uchaguzi mwingine utafanyika.
Likud alishinda idadi kubwa ya viti kwa chama kimoja akizoa 27 miongoni mwa viti 120 Knesset, lakini muungano mpana wa kidini na utaifa wa Netanyahu ukajitwalia 53 kwa jumla ikikosa viti 61 kufikisha idadi ya wengi.
Chama cha Eisenkot, Yashar, kiliibuka cha pili kikubwa Zaidi kikiwa na viti 21, huku muungano wake unaojumuisha mirengo minne ya kati na kushoto hadi vyama vinavyoongozwa na Wayahudi, ukishinda viti 48 pekee.
Vyama viwili vinavyowakilisha Waarabu walio wachache vilinyakua viti 19 ambavyo havikutarajiwa.
Eisenkot, 66, ambaye ni mwanawe mhamiaji kutoka Morocco atakuwa waziri mkuu wa taifa kutoka jamii ya Israeli ya Mizrahi, Wayahudi ambao chimbuko lao ni Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Eisenkot ambaye ni mtulivu na anayeambaa vyombo vya habari, alijitosa katika siasa 2022.
Alihudumu kwa muda mfupi kwenye baraza la wakati wa vita la Netanyahu kufuatia shambulizi la Hamas dhidi ya Israeli Oktoba 7, 2023, kabla ya kurejea katika upinzani.
Kutoka upinzani, alimkashifu hadharani Netanyahu kuhusu uongozi wake, ikiwemo usimamizi wa kampeni za kijeshi Gaza, na ameapa kuwa hatohudumu serikali pamoja naye.
Msimamo bayana wa Eisenkot vilevile umejifunga kwa gharama binafsi ambayo familia yake imelipia tangu 2023: mwana na wapwa wawili waliuawa wakipigana Gaza.