Hali si hali kwa Isak klabuni Newcastle uhamisho ukigongwa na visiki
MUSTAKABALI wa wanasoka Alexander Isak na Ademola Lookman kitaaluma huenda sasa ukavurugika baada ya juhudi zao za kutafuta klabu mpya kukumbana na visiki sugu.
Sawa na Isak, 25, aliyegomea Newcastle United ili kulazimisha uhamisho wake hadi Liverpool, Lookman amewasilisha ombi la kutaka Atalanta wamwachilie ili ajiunge na Inter Milan ambao ni washindani wakuu wa waajiri wake katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
Baada ya kukosa katika kikosi cha Newcastle ambacho kimekuwa kikijinoa barani Asia kwa minajili ya msimu ujao, Isak alielekea katika klabu yake ya zamani ya Real Sociedad mapema wiki jana kufanya mazoezi peke yake.
Alirejea Tyneside mwishoni mwa juma baada ya ofa ya Liverpool ya Sh18.7 bilioni kukataliwa na waajiri wake wanaotaka hela zisizopungua Sh25.5 bilioni.
Isak alijiunga na Newcastle kwa Sh10.2 bilioni kutoka Sociedad ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo 2022.
Nyota huyo raia wa Uswidi aliibuka mfungaji bora wa Magpies msimu uliopita kwa mabao 23 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Mbali na kuongoza Newcastle kufuzu soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), pia aliwashindia taji la Carabao Cup lililomaliza ukame wa miaka 70 bila taji.
Baada ya kukerwa na mwenendo wa Isak, wa kutaka kuondoka kwa lazima, kocha Eddie Howe sasa amechomoa kucha na kusisitiza kwamba sogora huyo lazima athibitishe kwamba anastahili kushiriki mazoezi na kikosi cha kwanza cha Newcastle.
“Sisi ni Newcastle United. Wachezaji wanafahamu majukumu yao na kila mmoja wao anajua kwamba hana uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza au hata kufanya mazoezi nasi,” alisema Howe, 47, mnamo Jumapili.
Newcastle wanawania saini ya mvamizi wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, ambaye pia anawindwa na Manchester United.
Wanakeshea pia mvamizi wa Brentford, Yoane Wissa.
Naye Lookman, 27, aliwasilisha ombi la kuagana na Atalanta baada ya kushutumu klabu hiyo kwa “kuvunja ahadi”.
Fowadi huyo wa Nigeria alisema alikubaliana na bodi kuwa angeondoka akipata ofa nzuri.
Hata hivyo, winga huyo mzaliwa wa Uingereza anasema Atalanta wamemkwamilia licha ya yeye kupokea ofa kulingana na kile anachoamini kilijadiliwa.
“Sina la kufanya ila kuzungumzia suala hili ambalo naamini ni haki yangu. Sielewi sababu ya Atalanta kunizuia kuhama.
Nimechoka na nimefika mwisho. Nathibitisha kuwa nimewasilisha ombi rasmi la kutaka kuondoka,” akaandika Lookman kwenye mtandao wa kijamii.
Nyota huyo alijiunga na Atalanta kutoka RB Leipzig ya Ujerumani mnamo 2022. Alifunga ‘hat trick’ yake ya kwanza kitaaluma katika fainali ya Europa League 2024 iliyoshuhudia Atalanta wakikomoa Bayer Leverkusen 3-0.
Amefungia Atalanta jumla ya mabao 52 kutokana na mechi 117.