Dimba

Hamkujituma, Ten Hag awazomea vijana wake Man U ikikabwa Uropa

Na MASHIRIKA September 26th, 2024 2 min read

MANCHESTER, Uingereza

Erik ten Hag amesikitishwa na vijana wake wa Manchester United kwa kukosa kujituma na kujitolea baada ya kutupa uongozi wakikabwa na FC Twente 1-1 kwenye Ligi ya Uropa, Jumatano.

Mashetani wekundu walipiga sare hiyo ya pili mfululizo siku nne baada ya kuokota sare tasa dhidi ya Crystal Palace ligini.

Ten Hag, ambaye bado anatiliwa shaka na waajiri wake kuhusu uwezo wake, aliwahi kuchezea na pia kuwa kocha wa Twente nchini Uholanzi kwa miaka 23.

Hapo Jumatano, United walichukua uongozi kupitia kwa Christian Eriksen dakika ya 35, lakini kiungo huyo alipokonywa mpira karibu na kisanduku chao na kuwezesha Twente kusawazisha kupitia kwa Sam Lammers dakika ya 68.

Eriksen alisema baada ya mechi kuwa Twente ilionyesha kiu zaidi ya kupata alama kuliko United na kuongeza kuwa hiyo si sawa.
Ten Hag naye alidai kuwa United ilishindwa kujituma asilimia 100.

“Ulijionea mwenyewe kuwa ilikuwa mechi yao ya kufa-kupona. Walijituma vilivyo na sisi hatukufanya hivyo,” akatanguliza Ten Hag kuhusu Twente.

“Hata asilimia 99 haitoshi, lazima ujitolee asilimia 100. Unafaa kumaliza mpinzani wako kabisa. Tuliongoza 1-0, lakini tukalegeza kamba badala ya kutafuta bao la pili na ushindi,” akachemka Ten Hag.

“Ukiona Twente walikuwa na moyo wa kupigania alama na hata baada ya kipenga cha mwisho walisherehekea vilivyo kwa sababu kilikuwa kitu kikubwa kwao,” akasema.

Kama timu, Ten Hag aliongeza kuwa wanafaa kuwa tayari kwa hali kama hiyo na hawakustahili kuwapa Twente fursa ya kusawazisha baada ya kuruhusu beki wa pembeni kulia kulisha chenga viungo bila ya kukabiliwa.

“Tunatamani vikombe, lakini ukiwa na tamaa hiyo lazima ujitume uwanjani kuthibitisha una uwezo. Leo, katika kipindi cha pili, nadhani tulilegea sana, hatukujituma. Hatukujitahidi kuzima wapinzani wetu na kama timu ni kitu tunajua tulifaa kufanya,” akasema.

Kiakili, Ten Hag alisema mara nyingi timu yake ina mtazamo mzuri.

“Nimeona katika michuano mingi bidii ya mchwa tuliyonayo na hiyo mara nyingi ni kitu kizuri sana. Hata hivyo, leo lazima niwakosoe. Hata hivyo, sio timu tu inafaa kujiangalia kwenye kioo tu, mimi pia ni sehemu yake. Tulifaa kufanya kazi tofauti, hasa katika kipindi cha pili. Tunafaa kumaliza mechi, hasa unapofahamu tuna matatizo katika ufungaji wa mabao na kuwa ukipata goli, unafaa kuwa na uimara katika mechi yako,” akasema.

Matokeo (Septemba 25): AZ Alkmaar 3-2 Elfsborg, Galatasaray 3-1 PAOK, Bodo/Glimt 3-2 Porto, Midtjylland 1-1 Hoffenheim, Manchester United 1-1 Twente, Dynamo Kiev 0-3 Lazio, Ludogorets 0-2 Slavia Prague, Nice 1-1 Real Sociedad, Anderlecht 2-1 Ferencvaros.