Harambee Stars yaangusha Morocco na kutinga robo fainali CHAN
TIMU ya taifa Harambee Stars Jumapili ilifuzu robo fainali ya kipute cha Kombe la Afrika kwa Wachezaji Wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024) baada ya kuipiga Morocco 1-0 katika uga wa MISC Kasarani.
Kenya iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani ilipata bao lake kipindi cha kwanza kupitia mvamizi wa Tusker Ryan Ogam. Kenya ilijipata matatani kipindi cha kwanza baada ya Chris Erambo kupewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mchezaji wa Morocco.
Ilikuwa mara ya kwanza ambapo Kenya ilikuwa ikipiga Morocco ambayo imeorodheshwa nambari moja Barani Afrika na nambari 12 duniani kulingana na viwango vya Fifa.
Kutokana na ushindi huo vijana wa nchi wanaongoza Kundi A kwa alama saba baada ya mechi tatu, huku Morocco ikiwa na alama tatu kwa kushinda Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) kwenye mechi yao ya kwanza.
Angola na Zambia zinatarajiwa kutifuana kwenye mechi nyingine baadaye.
Ushindi huo umehakikisha wanasoka wa Stars na benchi ya kiufundi wanapata Sh42 milioni. Kila mchezaji wa Harambee Stars sasa amejizolea Sh2.5 milioni baada ya kushinda mechi mbili na kupata sare moja (dhidi ya Angola Alhamisi iliyopita).
Rais William Ruto alikuwa ameahidi kuwa kwa kila ushindi kila mchezaji wa Harambee Stars atatunukiwa Sh1 milioni kwa ushindi kisha Sh500,000 kwa kupata sare
Habari zaidi kufuata