Dimba

Ishara Manchester United inafufuka

Na MASHIRIKA July 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHICAGO, Amerika

DALILI za kutia moyo mashetani wekundu wa Manchester United zinaendelea kujitokeza baada ya timu hiyo kucharaza Bournemouth 4-1 kwenye michuano ya kujiandaa kwa msimu mpya ya Premier League Summer Series, Alhamisi.

Rasmus Hojlund alifungua ukurasa wa mabao kupitia kichwa mapema katika mechi hiyo, Patrick Dorgu akaongeza la pili kabla ya mapumziko nao Amad Diallo na nguvu-mpya Ethan Williams wakaongeza mawili katika kipindi cha pili.

Matthijs de Ligt alijifunga dakika za lala-salama na kuwapa Bournemouth bao la kujifariji.

Licha ya kukosa huduma ya sajili wapya Bryan Mbeumo na Matheus Cunha, United walijenga juu ya ushindi wao wa 2-1 dhidi ya West Ham na bado wana nafasi ya kutwaa taji iwapo watapepeta Everton kwenye mechi yao ya mwisho saa sita usiku Jumatatu.

Zaidi ya yote, kocha Ruben Amorim aliona wachezaji wake wakianza kuzoea mbinu zake za kiufundi.

“Tulicheza kwa kasi na ukali, na tulimiliki mpira vizuri zaidi kuliko mechi iliyopita,” Amorim alinukuliwa na vyombo vya habari akisema.

“Kupata bao mapema kulifanya wachezaji kujiamini, na mabadiliko ya nafasi yanafanikiwa. Ni mechi ya maandalizi tu, lakini timu hii inaonekana tofauti.”

Kocha huyo Mreno alimsifu beki Luke Shaw kwa uimara wake wa ulinzi na mchango wa straika Hojlund.

“Si mabao pekee, uwezo wake wa kudhibiti mpira na kuunganisha mashambulizi unatusaidia sana. Nimefurahishwa na maendeleo yake,” akaongeza kuhusu Hojlund.

Amorim alisisitiza umuhimu wa maandalizi ya msimu baada ya United kumaliza ligi kwa rekodi yao mbaya zaidi msimu uliopita, wakikamata nafasi ya 16 na kukosa kushiriki michuano ya Ulaya.

Kwa shinikizo lililopo, ushindi dhidi ya Bournemouth umeibua matumaini ya kurejea kwenye ubora.

“Tulidhibiti mchezo vizuri na kupunguza makeke yao,” aliongeza Amorim.

“Wachezaji wale wale sasa wanaonekana kubadilika, na hiyo ni ishara nzuri.”

Uchezaji bora wa United na muundo ulioboreshwa unaonyesha mbinu za Amorim zinaanza kuzaa matunda, na matumaini yameongezeka kuwa anaweza kuirejesha timu kwenye mafanikio msimu ujao.