Junior Starlets, kuvaana na Japan
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya chini ya umri wa miaka 17, Junior Starlets, inatarajiwa kuvaana na Japan, mabingwa wa dunia wa mwaka 2014, leo katika mechi ya raundi ya 16 ya Kombe la Dunia katika uwanja wa Mohammed VI Football Complex, Sale, kuanzia saa tatu usiku saa za Kenya.
Hii ni mara ya kwanza kwa kikosi hicho kinachonolewa na Mildred Cheche kufuzu kwa hatua ya mwondoano katika historia yake ya mashindano hayo.
Starlets ni miongoni mwa timu nne za Afrika zilizofuzu kwa raundi hiyo, pamoja na wenyeji Morocco, Ghana na Nigeria. Zambia iliondolewa katika hatua ya makundi.
Kenya ilianza kampeni zake za Kundi E kwa kupoteza mabao 3-0 dhidi ya China kabla ya kuchapwa 6-1 na Marekani. Kiungo Lindey Weey alifunga bao la kufutia machozi katika dakika za nyongeza dhidi ya Wamarekani.
Huku matumaini ya kusonga mbele yakififia, Starlets ilihitaji ushindi mnono dhidi ya Samoa na matokeo mazuri katika mechi nyingine ili kuwania mojawapo ya nafasi nne za timu zilizomaliza nafasi ya tatu kwa matokeo bora.
Wasichana hao walijibu kwa kishindo kwa kuilaza Samoa mabao 4-0 na kujihakikishia tiketi ya raundi ya 16.
Mshambuliaji Mwanakombo Bakari alifungua ukurasa wa mabao dakika ya nne kabla ya Brenda Awuor kuongeza la pili dakika ya 44. Gaudencia Maloba alifunga la tatu dakika ya 62 huku Bakari akipachika bao lake la pili dakika mbili baadaye. Bakari alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa mechi.
Kenya ilimaliza ya tatu Kundi E ikiwa na alama tatu, nyuma ya China iliyopata tisa na Marekani iliyokuwa na sita. Samoa ilimaliza bila alama baada ya kufungwa mabao 28.
Katika mfumo wa mashindano ya mwaka huu, timu mbili za juu kutoka kila kundi zinafuzu moja kwa moja, huku timu nne bora zilizomaliza nafasi ya tatu zikikamilisha timu 16 za hatua ya mtoano.
Timu nyingine zilizofuzu kupitia nafasi hizo ni Poland kutoka Kundi B, Venezuela kutoka Kundi D na Morocco kutoka Kundi A.
Mafanikio hayo ni hatua kubwa kwa Kenya ikilinganishwa na mara yake ya kwanza kushiriki mwaka 2024 nchini Jamhuri ya Dominican. Wakati huo, Starlets ilimaliza ya tatu Kundi C ikiwa na alama tatu lakini haikusonga mbele.
Japan, ambayo inanolewa na Sadayoshi Shirai, ilimaliza kileleni mwa Kundi D kwa alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu, kufunga mabao tisa na kutoruhusu bao lolote.
Cheche alikiri kuwa haitakuwa rahisi kuikabili Japan, lakini akasisitiza kuwa kikosi chake kitajitahidi.
“Japan hatakuwa mpinzani rahisi, lakini tutajitahidi kadri tuwezavyo,” alisema baada ya ushindi dhidi ya Samoa.
Japan ilitwaa ubingwa wa dunia mwaka 2014 ilipoilaza Uhispania 2-0 nchini Costa Rica. Pia ilifika fainali mwaka 2016 lakini ikapoteza 5-4 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Korea Kaskazini baada ya sare tasa.
Timu hizo zitakutana kwa mara ya kwanza katika kiwango hiki, huku Starlets ikilenga kuendeleza historia yake kwa kutafuta tiketi ya robo-fainali.