Mahakama yaamuru IG Kanja, DCI Amin kufikisha mwanaharakati Mwaipaya kortini
Mahakama Kuu imewaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin kumfikisha kortini mwanaharakati raia wa Tanzania Twaha Mwaipaya, akiwa hai au maiti,
Jaji Alexander Muteti alitoa agizo hilo Oktoba 30, kufuatia madai kwamba Mwaipaya alitekwa nyara eneo la Kamulu, Nairobi, Oktoba 25 na watu wasiojulikana.
Jaji pia aliwaagiza Kanja na Amin, au wawakilishi wao, kufika mahakamani Novemba 2 kueleza sababu za kukamatwa na kuzuiliwa kwa Mwaipaya na kwa nini asiachiliwe mara moja.
Shirika la Vocal Africa liliwasilisha kesi likitaka Mwaipaya afikishwe mahakamani likidai alipotea akiwa mikononi mwa polisi.
Shirika hilo linasema liliripoti kutoweka kwake katika Kituo cha Polisi cha Ruai siku aliyopotea, lakini juhudi za kumtafuta katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Nairobi hazikufua dafu.
Mahakama imeagiza polisi na DCI kuwasilisha majibu yao kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo Jumatatu.
Kwa mujibu wa shirika hilo, Mwaipaya ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Tanzania mwenye wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii.
Linaonya kuwa maisha yake yako hatarini iwapo atapelekwa kwa nguvu hadi Tanzania, ambako anaweza kuteswa au haki zake kukiukwa.
Shirika hilo pia lilieleza kuwa waliomteka walitumia magari yaliyokuwa na nambari bandia na yasiyokuwa na nambari, huku baadhi ya waliokuwa ndani wakiwa wamejifunika nyuso na kubeba bunduki.
Lilitaja visa vingine vya watu waliodaiwa kutekwa nchini Kenya, wakiwemo Macmillan Kiarie, Evans Otieno, Michael Oloo na Abdulaziz Duba, ambao hawajulikani waliko.
Vocal Africa ilisema inatia wasiwasi kuwa visa hivyo sasa vinahusisha hata raia wa kigeni.