Dimba

Junior Starlets waingia historia ya soka Afrika Mashariki

Na TOTO AREGE October 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

TIMU ya Kenya ya wanawake wasiozidi umri wa miaka 17, Junior Starlets, imeingia katika historia baada ya kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Starlets, wanaonolewa na Mildred Cheche, walipata tiketi hiyo baada ya kuichabanga Samoa 4-0 katika mechi yao ya mwisho ya Kundi E iliyochezwa Jumapili usiku katika uwanja wa Mohammed VI Football Academy, Salé, Morocco.

Ushindi huo unaifanya Kenya kuwa nchi ya pili Afrika Mashariki kufuzu kwa hatua ya mwondoano katika mashindano hayo baada ya Tanzania, iliyofanya hivyo mwaka 2022 nchini India iliposhiriki kwa mara ya kwanza.

Tanzania ilifika robo-fainali kabla ya kuondolewa na Colombia kwa kichapo cha mabao 3-0. Hata hivyo, haijafuzu tena kwa mashindano hayo tangu wakati huo.

Kenya ilianza kampeni yake ya mwaka huu kwa kupoteza 3-0 dhidi ya China na 6-1 dhidi ya Marekani, huku Lindey Weey akifunga bao pekee la Starlets dhidi ya Wamarekani.

Dhidi ya Samoa, mshambuliaji Mwanakombo Bakari alifungua ukurasa wa mabao dakika ya nne kabla ya Brenda Awuor kuongeza la pili dakika ya 44. Gaudencia Maloba alifunga la tatu dakika ya 62, kabla ya Bakari kukamilisha mabao yake mawili dakika mbili baadaye.

Kenya ilimaliza ya tatu kundini kwa pointi tatu na kufuzu kama mojawapo ya timu nne bora zilizomaliza nafasi hiyo katika makundi yao.

Kocha Cheche alisema wachezaji wake wamefanya vizuri, ingawa bado wana kazi kubwa mbele yao.

“Wasichana wamefanya vizuri. Kufuzu kwa hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza ni mafanikio makubwa. Tuna mengi ya kufanya, lakini kwa sasa tunafurahia wakati huu,” alisema.

Starlets sasa watakutana na Japan, mabingwa wa dunia mwaka 2014, katika mechi ya 16 bora Alhamisi hii, wakilenga kutinga robo-fainali.

Bakari, aliyetuzwa mchezaji bora wa mechi dhidi ya Samoa, alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi za timu kwa pamoja.

“Tulipambana kama timu, tukadumisha ari nzuri na kufanya kazi kwa bidii. Nina furaha kwa sababu tumeandika historia,” alisema.