HabariHabari za Kitaifa

Azma ya Gideon Moi yavuruga hesabu za Ruto 2027

Na VITALIS KIMUTAI October 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

UAMUZI wa Kiongozi wa chama cha Kanu, Gideon Moi kuvunja kimya cha mwaka mmoja na kumshutumu Rais William Ruto kwa kutotekeleza makubaliano ya kisiasa umefungua ushindani mpya wa kudhibiti kura za Bonde la Ufa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Bw Gideon anadai Rais alisaliti makubaliano yaliyofikiwa Oktoba 10, 2025, katika makazi ya Kabarak ya aliyekuwa Rais Daniel arap Moi.

Alisema alikubali kufanya kazi na Dkt Ruto kwa heshima ya urais, licha ya upinzani kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake.

“Nilifanya hivyo bila kusita, licha ya upinzani kutoka kwa watu wangu,” akasema Bw Gideon, akiwataka wakazi wa Baringo wamsamehe kwa kumwamini Rais.

Makubaliano hayo yalionekana kuunganisha UDA na Kanu, lakini Gideon lakini aliarifiwa baadaye kuwa kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Oktoba 15, 2025, kilibadilisha mwelekeo wa makubaliano hayo.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Moses Kiyiapi alisema kifo cha Raila huenda kilimfanya Rais Ruto kudhani hahitaji tena ushawishi wa Gideon baada ya kuanza kujipenyeza kisiasa Nyanza.

“Uamuzi huo sasa unamrudia Rais miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu katika ngome yake ya kisiasa, ambako kila kura ni muhimu,” akasema Bw Kiyiapi.

Prof Prestone Chitere wa Chuo Kikuu cha Nairobi anasema hatua ya Bw Gideon kumkabili Rais hadharani inaweza kutatiza juhudi za Ruto kuimarisha uungwaji mkono Bonde la Ufa, hasa wakati uungwaji mkono katika maeneo mengine ya nchi haujahakikishwa.

Mvutano huo unaweza kuathiri kura katika kaunti za Kimasai, zikiwemo Narok na Kajiado, pamoja na maeneo ya Bonde la Ufa Kaskazini kama Baringo, Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi.

Viongozi wa Kanu wameunga mkono msimamo wa Bw Gideon, wakisema Rais lazima aonyeshe kuwa anaweza kutimiza makubaliano ya kisiasa.

“Kanu ina mizizi nchini kote, na huwezi kukidharau kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema aliyekuwa Mbunge wa Tiaty Asman Kamama.