Junior Stars wakabili Tanzania, Djibouti Kufuzu Afcon 17 2027
Timu ya Kenya ya wavulana wasiozidi umri wa miaka 17, Junior Stars, itakabiliana na Tanzania na Djibouti katika Kundi C la mashindano ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ukanda Baraza la Mashirisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Mashindano hayo yatafanyika Kigali, Rwanda, kuanzia Oktoba 10 hadi 19, huku mataifa 10 yakisaka tiketi mbili za kushiriki fainali za bara.
Mataifa mengine ni wenyeji Rwanda, Burundi, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda.
Kundi A lina Rwanda, Sudan, Somalia na Sudan Kusini, huku Kenya, Tanzania na Djibouti zikiwa Kundi C.
Timu itakayoongoza kila kundi itafuzu nusu-fainali pamoja na timu bora iliyomaliza nafasi ya pili. Watafika fainali ndio watakaowakilisha CECAFA AFCON nchini Morocco.
Kocha William Muluya Jumapili alitangaza kikosi cha wachezaji 23, huku timu hiyo ikiwa kambini tangu Septemba 24.
Nahodha Ian Nzisa, aliyerejea baada ya kuuguza jeraha, alisema kikosi kiko tayari kwa mashindano hayo.
“Tumeweka kambi kwa wiki mbili na tumejitayarisha vya kutosha. Kisaikolojia na kimwili tuko tayari. Tunawaahidi Wakenya kuwa tutafanya kila tuwezalo,” alisema Nzisa.
Msaidizi wa kocha Peter Okidi alisema Kenya itawakosa baadhi ya wachezaji muhimu kutokana na mitihani ya Gredi ya 10.
“Tunawakosa angalau wachezaji watatu muhimu, lakini tumepata wengine wenye uwezo,” alisema Okidi.
Kenya ilifika nusu-fainali mwaka uliopita na Okidi alisema safari hii wanalenga kufika fainali.
Stars wataanza kampeni dhidi ya Tanzania kabla ya kukutana na Djibouti.
Kikosi cha mwisho
Walinda lango
Georgian Omondi, Emmanuel Okinyi
Mabeki
Frankline Marango, Moses Ochola, Branton Odhiambo, Charles Okoth, Eugine Ochieng, Morgan Onyango, Yusuf Ahmed
Viungo wa kati
Lucksvien Ochiba, Rio Oyugi, Alvin Oloo, Emmanuel Mathiku, Carrilus Omware, Ian Nzisa
Washambuliaji
Byron Otieno, Myron Malcom, Tiffani Otieno, Nicholas Onyango, Daniel Ombati, Meloy Omondi, Caxton Atili, Brighton Omari, Timothy Okumu