Kenya kuwakilishwa na 73 mashindano ya kuogelea ya Afrika
KENYA itawakilishwa na waogeleaji 73 wa Masters katika Makala ya 10 ya Afrika ya Kanda ya 3 (Africa Aquatics Zone 3) yatakayofanyika Oktoba 16–19 katika Bwawa la Kimataifa la Kasarani, Nairobi.
Mashindano hayo yatakutanisha zaidi ya mataifa 15 na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Shirikisho la Uogeleaji Afrika (Africa Aquatics), akiwemo Rais Diop Mohammed. Vitengo vitahusisha vijana, watu wazima na kundi la Masters, lenye waogeleaji wenye umri wa miaka 25 na kuendelea.
Miongoni mwa wakongwe watakaoshiriki ni Esther Kariuki (72), anayeonyesha kuwa umri si kikwazo. Wengine waliozidi miaka 50 ni Sally Ndiri, Wanja Michuki, Anthony Nge’no, Carol Mbutura, na ndugu Isaac na Samuel Litaba.
Kikosi hicho cha Kenya kitasimamiwa na Meneja Winnie Warui, Msaidizi Nasser Motha, huku Gedion Kioko akiwa Kocha Mkuu. Manahodha ni Su Kahumbu na Julian Kajwang (wanawake), pamoja na Leland Salano na Geoffrey Watene (wanaume).

Mkurugenzi wa Kiufundi Omar Ali Omari alisema kikosi hicho ndicho kikubwa zaidi cha Masters kuwahi kuwakilisha Kenya, akiongeza kuwa kinaashiria ukuaji mkubwa wa mchezo huo nchini. Alisisitiza umuhimu wa kuogelea katika kupambana na maradhi yasiyoambukiza, akisema ni mchezo unaojenga mwili wote bila majeraha makubwa.
Mashabiki wameombwa kujitokeza kwa wingi Kasarani kushangilia timu hiyo, huku mipango ikiendelea ya waogeleaji hao kukutana na Rais William Ruto kabla au baada ya mashindano. Baada ya Kasarani, ratiba ya Masters itaendelea Kiambu (Novemba 29) na Mombasa (Aprili 2026).