Mabingwa Kenya Lionesses sasa jicho kwa duru ya 2 ya Challenger baada ya kutetemesha Cape Town
KENYA Lionesses wanatupia jicho kuendelea kutetemesha kwenye raga za Challenger Series baada ya kuanza msimu kwa kung’ata Argentina 17-12 katika fainali ya duru ya kwanza, jijini Cape Town, Afrika Kusini, mnamo Jumapili iliyopita.
Judith Okumu alikuwa fundi wa kuzamisha Argentina baada ya kutinga miguso miwili.
Nahodha Grace Okulu alipachika mguso mmoja na mkwaju katika ushindi huo wa kihistoria uliokuja baada ya Lionesses kuzidia maarifa mahasimu wao wa tangu jadi Afrika Kusini 19-15 katika nusu-fainali.
Katika fainali, vipusa wa kocha Dennis Mwanja waliongoza Argentina 7-5 wakati wa mapumziko kupitia alama za Okulu naye Marianela Escalante alifunga mguso bila mkwaju.

Okumu alipatia Kenya nafasi ya kupumua alipopachika mguso wake wa kwanza katika mchuano huo katika dakika ya 11 kabla ya kunyamazisha Argentina na mguso mwingine dakika ya 13.
Ingawa Argentina walipata mguso wa pili kupitia kwa Candela Delgado ulioandamana na mkwaju wa Sofia Gonzalez, muda wa kubadilisha mkondo wa mechi ulikuwa umekwisha.
Afrika Kusini waliridhika na nafasi ya tatu baada ya kulemea Colombia 29-0 katika mechi ya kutafuta nambari tatu.
Duru ya pili ya Challenger Series ni Machi 7-8 papo hapo jijini Cape Town ambapo Wakenya watavaana na Uganda na Ubelgiji katika Kundi A.
Mashindano haya ni ya kufuzu kushiriki Raga za Dunia 2025-2026.
Timu nne-bora kutoka Challenger baada ya duru tatu zitapepetana na nne za mwisho kutoka Raga za Dunia 2024-2025 kuamua nne zitakazoshiriki Raga za Dunia 2025-2026.