Dimba

Man U yarusha sokoni wachezaji wote wakiwemo nyota watatu waliodhaniwa hawawezi kuuzwa

Na GEOFFREY ANENE January 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MANCHESTER United imewasilisha wachezaji wote sokoni wakiwemo nyota watatu wanaodhaniwa hawawezi kuuzwa.

Taarifa nchini Uingereza zinasema kuwa mashetani wekundu wa United wanasikiliza ofa kwa klabu zilizo tayari kununua mchezaji yeyote wake katika kipindi kifupi cha uhamisho mwezi huu wa Januari, huku mmiliki Sir Jim Ratcliffe akilenga kufanya mabadiliko makubwa kwa kikosi hicho kinachofanya vibaya kwenye Ligi Kuu msimu 2024-2025.

Ratcliffe amekuwa wazi kuhusu United kusaini wachezaji kiholela miaka ya hivi majuzi na anaamini wanafaa kubadilika.

United wanakamata nafasi ya 13 ligini na hawana ushindi mara nne mfululizo chini ya Ruben Amorim.

Kocha huyo Mreno tayari ameelezwa ana kiasi kidogo cha fedha za kutumia baada ya mtangulizi wake Erik ten Hag kumwaga Sh95.8 bilioni (Pauni 600 milioni) kusuka kikosi.

Inamaanisha kuwa Amorim hana nafasi ya kunyakua mshambulizi anayetaka sana Viktor Gyokeres mwezi huu kwa sababu Mswidi huyo anaruhusiwa kuondoka Sporting ikiwa United italipa ada ya uhamisho ya Sh12.7 bilioni (Yuro 80 milioni).

Mambo huenda yakawa mabaya zaidi ugani Old Trafford kwa sababu Amorim anaweza kupoteza baadhi ya wachezaji muhimu wakiwemo makinda kutoka akademia ya United, Kobbie Mainoo na Alejandro Garnacho, na Rasmus Hojlund.

Sajili wapya Leny Yoro, Noussair Mazraoui, Matthijs de Ligt, Manuel Ugarte na Joshua Zirkzee wanasemekana pia wanaweza kupigwa mnada miezi sita tu baada ya kujiunga na United ambayo imetumia Sh172.5 bilioni kununua wachezaji tangu mwaka 2015.