Dimba

Manchester United wamshiba kabisa Ten Hag, wamwambia akanyage kubwa kubwa

Na GEOFFREY ANENE October 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MANCHESTER United wamemshiba Erik ten Hag na kumpiga teke baada ya mechi 10 za kwanza za msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza 2024-2025 ambapo klabu hiyo inasalia nje ya 10-bora.

Mholanzi huyo, ambaye atafidiwa Sh2, 680, 656, 000 kwa kufutwa kabla ya kandarasi kukamilika Juni 2026, amekuwa akining’inia pabaya kutokana na msururu wa matokeo mabovu.

Aliponea kufutwa kazi mwisho wa msimu 2023-2024 baada ya mashetani wekundu wa United kuingia Ligi ya Uropa kwa kushinda Kombe la FA.

Ten Hag, 54, ambaye aliongezwa kandarasi na wamiliki mwisho mwa msimu jana wakiamini anaweza kusaidia United kuimarisha matokeo, amepoteza kazi miaka miwili baada ya kutua ugani Old Trafford mnamo Aprili 2022.

Beki huyo wa zamani wa Twente, De Graafschap, Wallwijk na Utrecht alivutiwa na United baada ya kupata matokeo mazuri na Ajax nchini Uholanzi.

Nafasi ya baba huyo wa watoto watatu sasa imetwaliwa na Mholanzi mwenzake na shujaa wa zamani wa United, Ruud van Nistelrooy aliyekuwa naibu wake.

United inayomilikiwa na familia ya Glazer pamoja na Sir Jim Ratcliffe, imemtimua Ten Hag ikimwandikia kwaheri ya maneno 87.

Ten Hag aliongoza United katika mechi 128 akiwa usukani siku 850. Alishinda michuano 72.

Akiwa usukani, Ten Hag alishinda Kombe la Carabao msimu 2022-2023 na Kombe la FA msimu 2023-2024.

Katika miaka hiyo miwili, United ilitumia Sh100,524,600,000 kusuka kikosi, lakini matokeo yakawa ni yale yale mabovu.