Dimba

Mihic aanza kazi Gor Mahia kwa ushindi, Tusker, Police zikiambulia sare KPL

Na CECIL ODONGO, ABDULRAHMAN SHERIFF February 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA mpya wa Gor Mahia Sinisa Mihic Jumamosi alianza kazi kwa kishindo akiongoza klabu hiyo kushinda Mathare United 2-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu (KPL) iliyosakatwa uwanja wa Dandora Nairobi.

Ushindi huo ulisaidia K’Ogalo kupunguza uongozi wa Kenya Police na Tusker kileleni hadi kwa alama nne japo Gor bado ina mechi moja kibindoni.

Tusker na Kenya Police ziliumiza nyasi bure katika uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.

Kwenye mechi nyinginezo Nairobi City Stars ilitoka sare ya 1-1 na Bidco United katika mechi ya mapema  iliyosakatwa uga wa Kenyatta.

Bandari nayo ilitumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Mbaraki na kuipiga Sofapaka 1-0.

Uwanjani Dandora, mashabiki wa Gor Mahia walifika kwa idadi yao lakini wakapata pigo baada ya Mathare kuchukua uongozi mapema kipindi cha kwanza kupitia Elie Asieche.

Hata hivyo, Alphonce Omija alisawazishia vijana wa Mihic huku raia wa Ghana Enock Morrisson akifunga la pili kipindi cha pili na kuwahakikishia ushindi.

Gor bado ipo nambari tatu kwa alama 34 baada ya mechi 19 huku Kenya Police na Tusker zikiwa na alama 38 baada ya mechi 20.

“Kama kocha ni mpya wachezaji huwa wana ari ya kukuonyesha uzuri wao. Walifanya hivyo kwa dakika 20 za kwanza lakini wakalegea na mtindo waliokuwa wakicheza si ule niliowafunza mazoezini,” akasema Mihic.

“Katika kipindi cha pili walijizatiti na kulikuwa na shinikizo na hata baada ya kupata bao tulianza kulinda ngome yetu,” akaongeza mkufunzi huyo aliyepata ugumu wa kujieleza kwa kizungu.

Kule Mombasa Bandari ilijipatia bao lao la ushindi kwenye dakika ya 40 mfungaji akiwa Alfred Emoni aliyepokea pasi safi kutoka kwa William Gitama.

Kunako dakika ya 34, Emoni alipata pasi nzuri kutoka kwa Nyamawi Beja lakini akiwa amebakia yeye na kipa Evans Omondi akaupiga mpira ya kulenga ila ukatoka nje.

Ilimchukua dakika sita pekee  Emoni kulisahilisha kosa lake alipopokea pasi kutoka kwa William Gitama na kwa umakini akapiga mkwaju uliomshinda Omondi kuuzuia.

Bandari wapo nambari nne kwa alama 32 huku Sofapaka ikiwa ya tisa kwa alama 25 timu zote zikiwa zimecheza mechi 20

Victor Kunyuli na Gilbert Abadala nao walifungia Bidco United na Nairobi City Stars mtawalia.