Dimba

Msihofu, mambo yatakuwa sawa hivi karibuni, asisitiza kocha wa Man Utd Erik ten Hag

Na GEOFFREY ANENE October 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MANCHESTER, Uingereza: Kocha Erik ten Hag ametaka mashabiki wa Manchester United wasiwe na hofu licha ya timu hiyo kuanza msimu kwa kushinda mechi mbili kati ya sita za kwanza kwenye Ligi Kuu akiahidi kuwa mambo yatakuwa sawa.

Ten Hag, ambaye kandarasi yake iliongezwa kabla ya msimu huu kuanza licha ya wamiliki kuaminika walikuwa wakitafuta kocha wa kujaza nafasi yake, anaendelea kumulikwa kwa sababu timu yake inakamata nafasi ya 13 baada ya kupepetwa 3-0 na Tottenham.

“Tutapata mafanikio msimu huu,” Mholanzi huyo alinukuliwa na vyombo vya habari nchini Uingereza.

“Hakuna kitu rahisi, lakini sioni kama hiki ni kitu cha kunipa wasiwasi. Tunaweza kutatua matatizo haya, timu hii inaweza kujinyanyua,” akasema Ten Hag.

Kocha huyo alisisitiza kuwa hana hofu kuhusu uwezekano wa kutimuliwa licha ya viichapo kutoka kwa Spurs na Liverpool kuibua ripoti kuwa ananing’inia pabaya akielekea michuano dhidi ya Porto (Ligi ya Uropa) na Aston Villa (ligini).

“Sifikirii hilo, sina tumbojoto,” alisema Ten Hag. “Tuliamua kuwa na mshikamano na wamiliki na viongozi kabla ya msimu kuanza. Tulifanya makubaliano na sote tuliyaunga mkono. Tunajua mpango mzuri nikuleta wachezaji chipukizi wakati wa mpito,” akaeleza Ten Hag.

Aliongeza, “Wanajua pia kuwa mwezi Mei katika misimu yangu sita iliyopita mimi huwa na mataji na hayo ndiyo tunalenga.”

Ten Hag aliongeza kuwa alifahamua kuwa United walikuwa katika kipindi cha mpito alipojiunga nao na kuwa amethibitisha anaweza kushinda mataji katikamisimu yake miwili ya kwanza baada ya kutwaa mataji ya Kombe la Carabao na Kombe la FA.

“Kutoka siku niliwasili hapa, tulijua kuwa lazima tufanye mambo tofauti. Tulikuwa na ulazima wa kuondoa baadhi ya wachezaji walio na umri mkubwa,” akasema.

Mpango wao, alisema, ni kuleta chipukizi na kuwa hiyo inachukua muda kupitisha ujumbe, kupata mfumo mzuri wa kucheza mechi na kuanzisha falsafa mpya. “Hii inachukua muda. Wakati hii inaendelea, lazima ushinde na nadhani tumethibitisha katika kipindi cha miaka miwili kuwa sisi hushinda. Nimethibisha katika safari yangu kuwa mimi hushinda kila mara. Katika miaka yangu sita imepita, nimezoa mataji manane,” akasema Ten Hag kabla ya kuvaana na Porto jana usiku.