Dimba

Mwanaraga Ben Salem Adoyo apata dili ya nguvu nchini Amerika

Na GEOFFREY ANENE February 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NYOTA anayeinuka kwa haraka wa Kenya Shujaa, Benson Salem Adoyo amepata dili ya nguvu kuchezea klabu ya Austin Blacks nchini Amerika.

Adoyo, ambaye anafahamika kwa majina ya utani kama Jayues ama Magical Salem, ameelezea kufurahia kupiga hatua hiyo mpya.

“Nimesaini kandarasi ya miaka mitano na klabu ya raga ya Austin Blacks inayopatikana jimboni Texas. Imekuwa ndoto yangu kusaini kandarasi ya muda mrefu na klabu za kigeni. Naweza kusema ni ndoto imetimia, ingawa bado niko na ari ya kupata mafanikio zaidi,” Adoyo alieleza Taifa Leo kwa njia ya simu baada ya shughuli za kutafuta visa ya kusafiri. Anafaa kuelekea Amerika siku chache zijazo.

Ben Salem (aliye na mpira) akiwatoka wachezaji wa Zimbabwe wakati wa Safari Sevens 2024 mjini Machakos. PICHA | CHRIS OMOLLO

Adoyo, ambaye alizaliwa Agosti 7, 1999 na kulelewa katika mtaa wa mabanda wa Kibra mjini Nairobi, anafuata nyayo za wachezaji Monate Akuei aliyewahi kuchezea Kenya Simbas. Akuei aliye na asili ya Sudan Kusini alichezea Austin Blacks msimu uliopita.

“Kusaini kandarasi na Austin Blacks kutanifaidi sana. Kutaniwezesha kuimarisha mchezo wangu. Nimekuwa nacheza raga ya wachezaji saba kila upande sana na sasa naingilia raga ya wachezaji 15 kila upande,” akasema Adoyo aliyesomea shule ya msingi ya Ayany na kisha ile ya upili ya Dagoretti High.

Mara ya kwanza alijumuishwa katika timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ni wakati wa mashindano ya Safari Sevens mwaka 2021.

Akiwa nchini Kenya, Adoyo huchezea klabu ya Nondescripts. Alianzia uchezaji wake wa raga katika taasisi ya kukuza talanta ya Shamas baada ya kuvutiwa na shughuli za klabu hiyo kuwapa chakula wachezaji wenye umri mdogo wanaoanza kucheza.

Adoyo, ambaye shujaa wake katika raga ni Wakenya Collins Injera na Biko Adema na raia wa Tonga, Kurt Morath, aliwahi kuchezea Dallas Harlequins kwa kipindi kifupi mwaka 2023.