Nyasi kuchanika na jasho kumwagika Liverpool na Chelsea wakivaana
WENYEJI na viongozi Liverpool wataalika nambari nne Chelsea katika mpepetano mkubwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wikendi hii unaoweza kuamuliwa na bao moja komboa ufe hapo Jumapili, Oktoba 20, 2024.
Katika mechi hiyo, itakuwa nyasi kuchanika na jasho kumwagika wavamizi matata Mohamed Salah (Liverpool) na Cole Palmer (Chelsea) wakiongoza klabu zao katika mechi hiyo ya raundi ya nane ambayo kila mmoja atalenga kuzidia mwingine ujanja ugani Anfield.
Ingawa takwimu za ana kwa ana zinawapa viongozi Liverpool asilimia kubwa ya kutamba (Reds wameshinda Chelsea mara 86, kutoka sare mara 46 na kupoteza mara 65), hautarajiwi kuwa mchuano rahisi kwa yeyote kutwaa ushindi.
Hiyo ni sababu Liverpool ya kocha Arne Slot na Chelsea yake mkufunzi Enzo Maresca zimeonyesha ziko sawa katika kila idara ikiwemo kumiminia wapinzani mabao.
Liverpool wanafukuzia ushindi wa sita mfululizo katika mashindano yote nao Chelsea hawajapoteza katika michuano saba ambapo wamezoa ushindi mara tano na kutoka sare mara mbili.
Motisha kubwa kambini mwa Liverpool itatokana na kuwa wako nyumbani na hawajapoteza mikononi mwa Blues mara tisa mfululizo (ushindi mara nne na sare mara tano) ugani Anfield.
Hata hivyo, ni mechi ambayo yeyote atatangulia kufunga bao la kwanza huenda akaibuka na ushindi na kudhihirisha ana uwezo kuwania vilivyo taji msimu huu.
Vikosi vitarajiwa: Liverpool – Kelleher; Alexander-Arnold, Konate, Van Dijk, Robertson; Jones, Gravenberch; Salah, Szoboszlai, Gakpo; Jota. Chelsea – Sanchez; Gusto, Tosin, Colwill, Veiga; Fernandez, Caicedo; Madueke, Palmer, Sancho; Jackson.